Mawaziri wa Marekani wawasili Ukraine kwa mazungumzo baada ya kukutana na Putin

Chanzo cha picha, Reuters
Wajumbe wawili wa Marekani wanatarajia kufanya "mazungumzo yenye tija" nchini Ukraine baada ya kukutana na Rais wa Urusi Vladimir Putin mjini Moscow kuhusu kumaliza vita.
Steve Witkoff na Jared Kushner waliwasili Kyiv Jumapili, baada ya "kujadili mipango madhubuti kuhusu hatua zinazofuata" na Putin Jumamosi, kwa mujibu wa Ikulu ya Marekani.
Haijafahamika bado mipango hiyo ni ipi, lakini tangazo linatarajiwa katika wiki zijazo huku juhudi za kumaliza vita nchini Ukraine zikiongezeka.
Hii itakuwa safari ya kwanza ya mazungumzo ya wajumbe wakuu wa Rais wa Marekani Donald Trump kwenda Kyiv. Putin na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky wamekubali kusitisha mashambulizi dhidi ya miji mikuu ya kila mmoja kwa siku tatu.
Mazungumzo ya Jumamosi mjini Moscow yalidumu kwa saa tatu na kufanyika kwa faragha katika makaazi rasmi ya Putin.
Mshauri wa Putin Yuri Ushakov alisema mazungumzo hayo yalikuwa "ya kujenga na ya wazi sana", huku akisema masuala ya kiuchumi na miradi inayoweza kunufaisha Urusi na Marekani pia yalijadiliwa.
Zelensky alisema yeye na timu yake wako "tayari kwa mazungumzo" na wanataka "kusogeza karibu mwisho wa vita".
Mazungumzo hayo yanafanyika wakati Urusi na Ukraine zikiwa zimeongeza mashambulizi ya anga katika miezi ya hivi karibuni.








