Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, EU na Nato zaionya Urusi baada ya taifa hilo 'kuanzisha' mgogoro mpya dhidi ya Ujerumani

Wakuu wa Nato na Tume ya Ulaya wameonya kwamba Urusi inazidisha uchokozi wake na wameapa kuikabili iwapo itaendelea.

Muhtasari

  • Trump aweka sura yake katika sarafu ya dola 1 ya Marekani
  • Shambulio la Iran dhidi ya meli ya mafuta ya Saudia laua mabaharia wawili wa Ufilipino - Saudia
  • EU na Nato zaionya Urusi baada ya taifa hilo 'kuanzisha' mgogoro mpya dhidi ya Ujerumani

Moja kwa moja

Abdalla Seif Dzungu

  1. Trump aweka sura yake katika sarafu ya dola 1 ya Marekani

    Picha ya Donald Trump imeingia kwenye sarafu ya Marekani – ikiwa mara ya kwanza kwa rais aliye hai kuonekana kwenye sarafu ya Marekani katika karne moja.

    Siku ya Jumatano, Kampuni ya Marekani ya Mint ilizindua sarafu ya ukumbusho ya $1 yenye picha ya Trump pamoja na maneno "Kwa Mungu tunamwamini", kusherehekea maadhimisho ya miaka 250 ya Marekani.

    Sarafu ya toleo maalum ina "roho, fahari, na urithi wa taifa linalokaribia maadhimisho yake muhimu", Kampuni ya Marekani ya Mint ilisema.

    Sarafu hizo - zenye bei ya $61 (£45) kwa roll ya 25 na mfuko wa 100 kwa $154.50 - "hazikuwepo kwa sasa" kwenye tovuti ya Kampuni ya Marekani ya Mint ndani ya saa chache baada ya kuanza kuuzwa.

    BBC imewasiliana na Kampuni ya Marekani ya Mint, Hazina na Ikulu kwa maelezo zaidi.

    Sarafu hiyo "imeundwa kusherehekea hatua hii muhimu ya kitaifa" kwa "muundo wa maadhimisho ya kizazi kimoja unaokusudiwa kuwa nyongeza bora kwa sarafu za kisasa," Kampuni ya Marekani ya Mint ilisema.

    Pia zinauzwa katika mashine za kuuza bidhaa katika duka la US Mint huko Washington DC.

    Ingawa sarafu hizo zina rangi ya dhahabu hazina dhahabu yoyote halisi. Kulingana na US Mint, sarafu hizo zinasharikisha 88.5% ya shaba huku asilimia iliosalia ikiundwa na zinki, manganese na nikeli.

  2. Israel yafichua "mipango iliyoandaliwa" ya kuwafukuza Wapalestina kutoka Ukanda wa Gaza

    Waziri wa Ulinzi wa Israeli Yisrael Katz amefichua kwamba Israeli ina mipango tayari ya kuwaondoa Wapalestina kutoka Ukanda wa Gaza, lakini inasubiri Marekani kufikia makubaliano kuhusu wapi Wagaza watahamishiwa.

    Katika mkutano na waandishi wa habari Jumatano, Katz alisema: "Hatimaye hakuna suluhisho halisi kwa Gaza bila uhamiaji huu," akiongeza kuwa serikali ya Israeli "imepanga na iko tayari kuwaondoa, kwa njia ya baharini, kwa njia ya anga, na kwa kila njia inayowezekana."

    Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu amesema kwamba nchi yake haina mpango wa kujiondoa kutoka eneo lolote lililo chini ya udhibiti wa kijeshi katika Ukanda wa Gaza, akisisitiza udhibiti wa Israeli juu ya eneo hilo.

    Netanyahu alitoa matamshi hayo wakati wa ziara yake Jumatano kwa vikosi vya Israeli huko Gaza.

    Hii ilikuwa ziara ya kwanza ya uwanjani ya Netanyahu tangu makubaliano ya kusitisha mapigano yatangazwe Oktoba iliyopita.

  3. Shambulio la Iran dhidi ya meli ya mafuta ya Saudia laua mabaharia wawili wa Ufilipino - Saudia

    Saudi Arabia imelaani kile ilichosema ni shambulio la Iran dhidi ya meli kubwa ya mafuta inayomilikiwa na Saudi Arabia Jumatatu usiku na kuwaua mabaharia wawili wa Ufilipino.

    Kampuni ya kitaifa ya meli ya Saudi Arabia, Bahri, ilithibitisha Jumatano kwamba meli yake ya Sidr "ilihusika katika tukio la utovu wa usalama wakati ikipitia Mlango-Bahari wa Hormuz".

    Sidr ilipigwa na makombora kaskazini mwa rasi ya Musandam ya Oman, kulingana na makampuni ya usalama wa baharini.

    Meli kubwa ya mafuta inayomilikiwa na Korea Kusini, Senegal Prosperity, iliripotiwa kupigwa mashariki mwa Musandam wakati huo huo.

    Iran haijajibu madai ya Saudi Arabia. Lakini ilisema mapema kwamba meli mbili za mafuta zilishika moto baada ya kugonga mabomu zikitumia njia isiyoidhinishwa kupitia mlango-bahari.

    Habari za vifo vya mabaharia hao zilikuja baada ya jeshi la Marekani kutekeleza wimbi la mashambulizi ya angani dhidi ya Iran na vikosi vya Iran kulenga kambi za Marekani katika nchi jirani za Kiarabu kwa makombora na ndege zisizo na rubani katika ufyatulianaji wao mkubwa wa risasi tangu Julai.

    Siku ya Jumatano waziri wa afya wa Iran alisema watu 18 waliuawa na 108 kujeruhiwa katika mashambulizi ya Marekani.

    Iran imeishutumu Marekani kwa "uhalifu wa kivita" kutokana na shambulio liliowaua watu wanne wakiwemo watoto wawili kwenye sherehe ya harusi katika mji wa kusini wa Sirik. Jeshi la Marekani lilisema linachunguza ripoti hizo.

    Taarifa ya kampuni ya meli Bahri ilisema "tukio la usalama" ambalo halijatajwa lililoathiri Sidr lilitokea katika Mlango-Bahari wa Hormuz yapata saa 23:40 kwa saa za huko (19:40 GMT) Jumatatu.

    "Ni kwa huzuni kubwa kwamba Bahri inathibitisha kufariki kwa mabaharia wake wawili wa Ufilipino kutokana na tukio hilo," iliongeza.

    "Kampuni inatoa rambirambi zake za dhati na salamu za rambirambi kwa familia zao, wapendwa wao, na wafanyakazi wenzao wakati huu mgumu."

  4. EU na Nato zaionya Urusi baada ya taifa hilo 'kuanzisha' mgogoro mpya dhidi ya Ujerumani

    Wakuu wa Nato na Tume ya Ulaya wameonya kwamba Urusi inazidisha uchokozi wake na wameapa kuikabili iwapo itaendelea.

    "Shambulio la Leipzig linaashiria uchokozi mpya katika ardhi ya Umoja wa Ulaya unaohusishwa moja kwa moja na Urusi," alisema Rais wa Tume hiyo Ursula von der Leyen, siku moja baada ya Ujerumani kulaumu Urusi kwa shambulio la ndege isiyo na rubani mwezi uliopita kwenye uwanja wa ndege wa Leipzig.

    "Lazima tuchukue hatua na hiyo ina maana kujibu uzembe wa Urusi haraka na kwa njia bora zaidi," von der Leyen alisema.

    Katibu Mkuu wa Nato Mark Rutte amesema muungano mzima, ambao unajumuisha Marekani, unasimama "kwa mshikamano kamili na Ujerumani".

    Urusi imekataa shutuma za Ujerumani kwamba ndege isiyo na rubani iliyobeba vilipuzi ililenga ndege ya mizigo ya Ukraine kwa makusudi mnamo tarehe 4 Agosti.

    Ndege hiyo iliharibiwa na roboti katika uwanja wa ndege wa Leipzig/Halle na ndege ya pili isiyo na rubani inadhaniwa kugongana na ndege nyingine ya mizigo.

    Ndege ya tatu isiyo na rubani iliripotiwa kupatikana siku 10 baadaye katika uwanja wa ndege, ambao ni kitovu muhimu cha Nato na hutumiwa mara kwa mara na ndege ya usafiri ya Antonov ya Ukraine.

    Ni hadi Jumanne ambapo serikali ya Ujerumani ilisema uchunguzi wa polisi na uchunguzi wa kijasusi umethibitisha kwamba Urusi ilihusika na matukio hayo.

    Waziri wa mambo ya ndani alisema kwamba umbo la ndege isiyo na rubani, vipengele vyake, vilipuzi na kifyatulio chake , vyote vilijulikana kutoka Urusi.

  5. Natumai hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja