Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Urusi yamwachia huru Mmarekani huku mjumbe wa Trump akikutana na Putin

Mmarekani huyo alikabiliwa na kesi nchini Urusi kwa tuhuma za kupigana kama mamluki upande wa Ukraine.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Beldeen Waliaula & Asha Juma

  1. Na kufikia hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu mubashara kwa leo. Kwaheri.

  2. Jeshi la Ujerumani laonya kuhusu tishio la hujuma za Urusi

    Jeshi la Ujerumani kwa mara ya kwanza limeainisha tishio la Urusi kufanya hujuma dhidi ya wanajeshi na vituo vyake kuwa “kubwa”, kiwango cha pili kwa juu katika mfumo wake wa ndani wa tathmini ya vitisho.

    Tathmini hiyo iliripotiwa Jumatano na vyombo vya habari vya WDR na Sueddeutsche Zeitung. Msemaji wa Wizara ya Ulinzi alithibitisha kuwa jeshi linakabiliwa na tishio kubwa la hujuma.

    Hatua hiyo imechochewa na kugunduliwa kwa ndege isiyo na rubani iliyokuwa imeanguka katikati ya Septemba ikiwa imebeba kopo lenye vilipuzi vyenye nguvu karibu na kituo cha kijeshi cha anga cha Wunstorf, katika jimbo la Lower Saxony.

    Kwa mujibu wa nyaraka za ndani za jeshi, Urusi imevuka “mstari mwekundu” kupitia matumizi ya ndege zisizo na rubani zilizobeba silaha, katika vitendo vinavyoweza kusababisha uharibifu wa kimwili au vifo dhidi ya Ujerumani na jeshi lake.

    Ndege iliyopatikana Wunstorf inafanana na ile iliyotumika katika jaribio la shambulio lililoshindwa katika uwanja wa ndege wa Leipzig/Halle mwezi Agosti. Hata hivyo, wachunguzi wanaamini kuwa ndege ya Wunstorf ililenga ndege za kijeshi, tofauti na tukio la Leipzig lililolenga ndege za mizigo za kiraia.

    Ujerumani imeilaumu Urusi kwa tukio la Leipzig, lakini Moscow imekanusha kuhusika na kukataa mara kwa mara madai ya kufanya hujuma barani Ulaya.

    Ripoti hiyo pia imetaja matukio yanayoshukiwa kuwa ya ujasusi wa Urusi, yakiwemo ndege zisizo na rubani kuruka juu ya eneo la mfumo wa ulinzi wa makombora wa Arrow 3 na kamera iliyofichwa iliyopatikana ikirekodi kituo muhimu cha reli mjini Minden.

    Vyombo vya ujasusi vinatarajia hali kuwa mbaya zaidi katika kipindi kifupi kijacho. Wizara ya Ulinzi imesema inaongeza doria za walinzi na kuimarisha usalama kwa kutumia kamera za infrared na mifumo ya ufuatiliaji wa uzio.

    Tathmini hiyo imekuja zaidi ya wiki moja baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Alexander Dobrindt, kusema Ujerumani inakabiliwa na “vita vya kivuli” na kutaka mamlaka ya vyombo vya ujasusi yaongezwe.

    Kansela Friedrich Merz alisema Jumatano kuwa taarifa potofu za Urusi na mashambulizi ya vita mseto ni vitisho vikubwa zaidi kwa Ujerumani.

    “Wananchi wetu bado wanadharau tishio hili kubwa kwa jamii yetu... Hili ni shambulio la msingi dhidi ya mfumo mzima wa kisiasa tulioujenga baada ya mwaka 1990,” alisema Merz.

  3. Marekani yatumia sheria adimu ya utesaji dhidi ya Maduro

    Nicolas Maduro, rais wa zamani wa Venezuela, ni miongoni mwa watu wachache walioshtakiwa nchini Marekani kwa kukiuka sheria inayoharamisha vitendo vya utesaji vinavyofanyika nje ya nchi, huku waendesha mashtaka wakipanua kesi dhidi yake na mkewe, Cilia Flores.

    Maduro, mwenye umri wa miaka 63, na Flores, 70, walikana mashtaka mapya wiki iliyopita ya kula njama ya kuwatesa wapinzani wa kisiasa ili kuendelea kushikilia madaraka. Mashtaka hayo yameongezwa kwenye yale ya awali ya biashara ya dawa za kulevya. Kesi yao inatarajiwa kuanza Juni 2027.

    Wawili hao walikamatwa Januari wakati wa operesheni ya kijeshi ya Marekani jijini Caracas iliyoagizwa na Rais Donald Trump, kisha kupelekwa New York.

    Kwa mujibu wa uchunguzi wa Reuters, Maduro na Flores ni watu wa saba na wa nane pekee waliotambuliwa kushtakiwa chini ya sheria ya mwaka 1994 inayoharamisha utesaji. Watu wanne wamepatikana na hatia chini ya sheria hiyo, huku wengine wakipata vifungo vya miaka 60 hadi 97 jela.

    Michel Paradis, wakili aliyewahi kuwawakilisha wafungwa wa Guantanamo Bay, amesema kesi ya Maduro ni ya kihistoria kwa kuwa ni mara ya kwanza Marekani kumshtaki mkuu wa nchi kwa madai ya kuidhinisha utesaji ndani ya nchi yake.

    Wataalamu wa sheria wanasema mashtaka ya utesaji yanaweza kuimarisha kesi ya upande wa mashtaka kwa kuonyesha jinsi Maduro anavyodaiwa kutumia ukandamizaji wa kisiasa na uhalifu mbalimbali ili kubaki madarakani.

    Katika tukio moja la mwaka 2018, waendesha mashtaka wanadai maafisa wa jeshi la Venezuela walimpiga mfungwa kwa panga na kumpulizia kemikali inayowasha mwili walipokuwa wakimhoji kuhusu mahali alipo mpinzani wa kisiasa wa Maduro.

    Watatu kati ya watu wanaodaiwa kuteswa ni raia wa Marekani, na ushahidi wao unaweza kuwa muhimu katika kesi hiyo.

    Mawakili wa Flores wamesema hana hatia na wanapanga kurekebisha ombi lao la kutaka kesi itupiliwe mbali kwa misingi ya kinga inayohusishwa na mkuu wa nchi huru.

    Chini ya sheria hiyo, kila shtaka la utesaji linaweza kuadhibiwa kwa kifungo cha hadi miaka 20 jela. Ikiwa mwathiriwa atafariki kutokana na utesaji, adhabu inaweza kuwa kifungo cha maisha au hukumu ya kifo.

    Hata hivyo, Maduro na Flores hawakabiliwi na hukumu ya kifo kwa sababu wameshtakiwa kwa kula njama ya utesaji, badala ya kutekeleza vitendo hivyo wenyewe.

    Soma Pia:

  4. China yaonya Ufilipino baada ya operesheni katika eneo tata

    Walinzi wa Pwani wa China (CCG) wamesema walifuatilia operesheni ya Ufilipino ya kupeleka mahitaji muhimu kwa meli iliyoko katika eneo la Second Thomas Shoal siku ya Jumatano, takriban mwezi mmoja baada ya Ufilipino kuishutumu Beijing kwa kuzuia operesheni kama hiyo katika Bahari ya Kusini ya China.

    CCG ilisema meli ya Ufilipino iliyopokea vifaa hivyo "ilikuwa huko kinyume cha sheria" katika eneo ambalo China inadai kuwa sehemu ya eneo lake, pamoja na sehemu kubwa ya Bahari ya Kusini ya China.

    Jeshi na Walinzi wa Pwani wa Ufilipino hawakutoa maoni ya haraka kuhusu taarifa hiyo.

    Madai ya China katika Bahari ya Kusini ya China yanakinzana na yale ya Brunei, Malaysia, Ufilipino, Taiwan na Vietnam, jambo ambalo limekuwa likichochea mivutano na migongano kati ya Beijing na Manila.

    Mnamo mwezi Septemba 25, Walinzi wa Pwani wa Ufilipino waliishutumu China kwa kuzuia operesheni ya kupeleka vifaa katika eneo la Second Thomas Shoal. Hata hivyo, China ilisema Ufilipino ilipuuzia maonyo ya Beijing, jambo lililosababisha kile ilichokiita "ufuatiliaji wa karibu" na maonyo ya maneno.

    Mwezi Septemba, meli ya Walinzi wa Pwani wa China ilidaiwa kugonga chombo cha Ufilipino kilichokuwa katika operesheni ya kupeleka mafuta karibu na eneo jingine lenye mzozo katika Bahari ya Kusini ya China. Ufilipino iliilaumu China kwa tukio hilo, huku Beijing ikiilaumu Ufilipino.

    Jumatatu, Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufilipino ilimwita balozi wa China kueleza "wasiwasi mkubwa na upinzani mkali" kuhusu kauli zake ambazo Ufilipino ilisema zilionyesha tishio la matumizi ya nguvu. Mwanadiplomasia huyo wa China alipinga madai hayo na kusema matamshi yake hayakuwa tishio kama ilivyodaiwa na Ufilipino.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Israel yalaani vikali makubaliano ya Libya na Uturuki

    Israel imesema kuwa “inalaani vikali” uamuzi wa bunge la mashariki mwa Libya kuidhinisha makubaliano ya mipaka ya baharini na Uturuki, hatua iliyokosolewa kwa haraka na Ugiriki, mshirika wa karibu wa Israel.

    Makubaliano hayo yaliyoidhinishwa Jumanne ni sehemu ya mgogoro wa muda mrefu kuhusu madai yanayokinzana ya mipaka ya bahari na haki za uchunguzi wa rasilimali za nishati katika eneo la mashariki mwa Bahari ya Mediterania.

    “Kwa masikitiko, kwa mara nyingine tunaona Uturuki ikifanya kazi za kudhoofisha utulivu wa eneo la mashariki mwa Mediterania,” Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel ilisema.

    Viongozi wa Israel na Uturuki wamekuwa wakibadilishana maneno makali katika miezi ya hivi karibuni kutokana na tofauti zao kuhusu Syria na vita vya Gaza.

    Ugiriki na Uturuki, ambazo zote ni wanachama wa muungano wa NATO lakini zimekuwa wapinzani wa muda mrefu, zimekuwa zikibishana kuhusu mipaka ya baharini katika Bahari ya Aegean na mashariki mwa Mediterania.

    Kwa muda mrefu, Ugiriki, Misri na Cyprus zimekuwa zikipinga makubaliano ya baharini kati ya Libya na Uturuki, zikidai kuwa yanakiuka madai yao ya maeneo ya baharini.

    Mwaka 2020, Athens na Cairo zilitia saini makubaliano yanayobainisha eneo lao maalum la kiuchumi katika mashariki mwa Mediterania, hatua ambayo Uturuki imekuwa ikiipinga.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Marekani yarejesha mamilioni ya Jammeh kuwafidia waathiriwa

    Gambia imethibitisha kupokea dola milioni 2.5 kutoka Marekani, fedha zilizotokana na mauzo ya jumba la aliyekuwa rais wa muda mrefu Yahya Jammeh.

    Serikali ya Gambia imesema fedha hizo zitatumika kuwasaidia waathirika wa utawala wake.

    Jammeh alitawala Gambia kwa zaidi ya miaka 20, kuanzia 1994 hadi 2017, kipindi kilichokumbwa na tuhuma za ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.

    Kiongozi huyo wa zamani pia anatuhumiwa kuhamisha mamilioni ya dola kutoka kwenye fedha za serikali kwa matumizi yake binafsi.

    Wizara ya Sheria nchini Marekani ilitangaza mwezi Septemba kuwa itarejesha Gambia fedha zilizopatikana kutokana na mauzo ya jumba la kifahari lililokuwa linamilikiwa na Jammeh.

    Wizara hiyo Ilisema kuwa kiongozi huyo wa zamani na mkewe walinunua jumba hilo katika kitongoji cha kifahari cha Potomac, jimbo la Maryland, karibu na Washington, kwa kutumia “mapato ya uhalifu na fedha za umma za Gambia zilizotwaliwa kinyume cha sheria”.

    Tume ya Fidia kwa Waathiriwa wa Gambia, iliyoanzishwa ili kuwafidia waathiriwa wa ukiukaji wa haki za binadamu uliofanyika wakati wa utawala wa Jammeh wa miaka 22, ilisema kwamba ina furaha kuwafahamisha waathiriwa, manusura na umma kwa jumla kuwa imepokea jumla ya dola za Marekani milioni mbili zilizopatikana kutokana na kutaifishwa na kuuzwa kwa jumba hilo.

    Tume hiyo iliongeza katika taarifa kuwa fedha hizo “zitatumika tu kulipa fidia kwa waathiriwa kupitia Tume hiyo”. Ilielezea kurejeshwa kwa fedha hizo kuwa “hatua muhimu” kuelekea malipo ya fidia yaliyoahidiwa katika sheria iliyopitishwa mwaka wa 2023.

    Aidha, wanasema kwamba Tume imejitolea kuhakikisha kuwa fedha hizo zinasimamiwa kwa uwajibikaji, uwazi na uadilifu, huku haki na mahitaji ya waathiriwa na manusura yakizingatiwa ipasavyo,.

    Jammeh kwa sasa anaishi nchini Equatorial Guinea, baada ya kulazimika kuondoka madarakani kufuatia shinikizo kutoka kwa nchi jirani za Afrika Magharibi, baada ya kushindwa katika uchaguzi wa mwaka 2016 dhidi ya rais wa sasa, Adama Barrow.

    Jammeh anatuhumiwa kuhusika na mauaji ya wapinzani wa kisiasa, kutoweshwa kwa watu kwa lazima, ubakaji na mateso.

    Tume ya uchunguzi ilikadiria kuwa kati ya watu 240 na 250 waliuawa na vikosi vyake katika taifa hilo, lenye wakazi milioni mbili.

  7. Mahama: Yeyote anayepambana na ugaidi anakaribishwa Afrika Magharibi

    Rais wa Ghana John Dramani Mahama amesema siku ya Jumatano kuwa hana wasiwasi kuhusu msaada wa kiusalama wa Urusi katika eneo la Sahel, akisisitiza kwamba yeyote aliyejitolea kupambana na ugaidi anakaribishwa katika eneo hilo.

    "Maoni yangu kuhusu hili ni kwamba yeyote aliyejitolea katika vita dhidi ya ugaidi anakaribishwa," Mahama alisema katika mkutano wa Financial Times Africa Summit uliofanyika London.

    Akizungumzia mpango wa kupeleka kikosi cha akiba cha Afrika Magharibi kusaidia kukabiliana na changamoto za usalama, Mahama alisema kucheleweshwa kwa hatua hiyo kunatokana na kukosekana kwa azimio la Umoja wa Mataifa ambalo lingesaidia kutoa fedha zinazohitajika kwa operesheni hiyo.

    Mahama pia alisema Ghana inalenga kupiga marufuku usafirishaji wa malighafi nje ya nchi ifikapo mwaka 2030 ili kuongeza thamani ya madini muhimu kabla ya kuuzwa nje.

    Alitaja madini hayo kuwa ni pamoja na lithiamu, manganizi, boksaiti na dhahabu.

    Rais huyo alisema kwa sasa asilimia 70 ya dhahabu ya Ghana huchakatwa ndani ya nchi kabla ya kusafirishwa nje, na akaongeza kuwa ana matumaini kwamba hivi karibuni nchi hiyo itakuwa ikisafisha asilimia 100 ya dhahabu yake.

    "Hilo litasaidia kuhamisha baadhi ya shughuli za uchakataji nchini na kuongeza nafasi za ajira kwa wananchi," alisema.

    Soma Zaidi:

  8. Urusi yamwachia huru raia wa Marekani Stephen Hubbard

    Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema Urusi imekubali kumwachilia raia wa Marekani aliyefungwa jela kwa tuhuma za kupigana upande wa Ukraine, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali ya Urusi.

    Putin amesema Stephen Hubbard amepelekwa katika Uwanja wa Ndege wa Pulkovo wakati wa mazungumzo yake na mjumbe wa Marekani Steve Witkoff mjini St Petersburg.

    Stephen Hubbard, mwalimu wa zamani kutoka Michigan, alihukumiwa kifungo cha karibu miaka saba katika koloni la adhabu nchini Urusi mwaka 2024.

    Moscow ilimtuhumu kupigana katika kikosi cha ulinzi cha Ukraine mjini Izyum kabla ya kukamatwa na majeshi ya Urusi.

    Marekani ilikuwa imemtaja kama aliyekuwa amezuiliwa isivyo halali, huku Rais Donald Trump akisema aliwasilisha suala lake kwa Vladimir Putin.

    "Mtaona kitakachotokea," Trump aliwaambia waandishi wa habari. "Tumekuwa tukifuatilia suala la Hubbard."

    CBS News, mshirika wa habari wa BBC nchini Marekani, iliripoti kuwa Hubbard alikuwa na matatizo ya afya na alitarajiwa kusafirishwa hadi jimbo la Texas kwa ajili ya matibabu.

    BBC imewasiliana na Ikulu ya White House kuomba maoni kuhusu suala hilo.

    Vyombo vya habari vya serikali ya Urusi viliripoti kuwa Witkoff alimshukuru Putin kwa kuachiliwa kwa Hubbard na pia, kwa niaba ya Trump, kwa makubaliano yaliyofikiwa na Washington mapema mwezi huu ya kuagiza dizeli kutoka Urusi.

    Putin alisema wakati wa mkutano huo kwamba shehena ya kwanza ya dizeli chini ya makubaliano hayo itaondoka Urusi ndani ya siku mbili hadi tatu zijazo, kwa mujibu wa shirika la habari la serikali la TASS.

    Makubaliano hayo ya dizeli yamemkasirisha Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky na yameendelea kuzorotesha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Kyiv na Washington.

    Wakati wa mkutano wa Jumatano mjini St Petersburg, Witkoff alionekana kwenye televisheni ya Urusi akisema kuwa makubaliano hayo ni mfano kwa Ukraine wa kile kinachoweza kupatikana kupitia ushirikiano.

    Soma Zaidi:

  9. Burudani tupu, mabao tele: Ligi ya Mabingwa yaweka rekodi mpya

    Tangu kuanzishwa kwa mfumo mpya wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mwanzoni mwa msimu wa 2024-25, mashindano hayo yamekuwa yakitoa kila kitu ambacho mashabiki wanakipenda. Lakini jambo linalojitokeza zaidi msimu huu ni ongezeko kubwa la mabao.

    Mabao 187 yamefungwa kufikia sasakatika michuano hiyo, wastani wa mabao 4.16 kwa kila mechi, kiwango cha juu zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya Ligi ya Mabingwa.

    "Angalia idadi ya mabao yanayofungwa, ni jambo la kushangaza," alisema winga wa zamani wa Manchester United na England, Ashley Young, kupitia BBC Radio 5 Live. "Washambuliaji wamekuwa makini sana mbele ya lango."

    Beki wa zamani wa Liverpool, Stephen Warnock, naye alieleza idadi hiyo ya mabao kuwa "ya ajabu". Lakini je, hali hii ni ya kipekee?

    Takwimu zafichua nini?

    Wastani wa sasa wa mabao kwa kila mechi si rekodi tu katika historia ya Ligi ya Mabingwa, bali pia ni wa tatu kwa ubora katika historia yote ya Kombe la Ulaya. Ni misimu miwili pekee, 1955-56 (4.38) na 1959-60 (4.19), iliyorekodi wastani mkubwa zaidi.

    Mabao yanaendelea kunyesha kwa kasi isiyo ya kawaida. Jumanne, mabao 40 yalifungwa katika mechi tisa pekee.

    Hata hivyo, siku ya kuvutia zaidi ilikuwa Jumatano iliyopita, ambapo mabao 46 yalifungwa, idadi ya tatu kwa ukubwa kuwahi kushuhudiwa ndani ya siku moja katika historia ya mashindano hayo.

    Kwa pamoja, mechi za Jumanne na Jumatano wiki iliyopita zilizalisha mabao 78, na kuifanya raundi ya pili ya mechi kuwa ya mabao mengi zaidi kuwahi kurekodiwa.

    Jumla hiyo ilikuwa mabao tisa zaidi ya yale 69 yaliyofungwa katika raundi ya kwanza ya msimu huu. Wakati huo, raundi hiyo ilikuwa tayari imeweka rekodi ya pili ya mabao mengi tangu kuanzishwa kwa mfumo mpya wa hatua ya ligi mwaka 2024-25.

    Swali ni je, rekodi nyingine itavunjwa tena wiki hii?

    Soma pia:

  10. Saudi Arabia yasema imedungua droni tano zilizokuwa zikielekea nchini humo

    Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia na unaounga mkono serikali ya Yemen, umesema wamedungua ndege tano zisizo na rubani zilizokuwa zikielekea katika eneo la Medina na mashariki mwa Saudi Arabia.

    Msemaji wa muungano huo, Turki al-Maliki, amesema kupitia taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa X, kuwa ndege tano zisizokuwa na rubani zilizokuwa zikielekea Saudi Arabia zilidunguliwa.

    Hata hivyo, msemaji huyo hakueleza ndege hizo zisizo na rubani zilitoka wapi wala ikiwa tukio hilo lilisababisha uharibifu wowote.

    Katika siku za hivi karibuni, mvutano kati ya Saudi Arabia na Wahouthi wa Yemen umeongezeka. Saudi Arabia imekuwa ikiishutumu kundi hilo kwa kufanya mashambulizi kwa kutumia ndege zisizo na rubani na makombora ya masafa marefu.

    Soma pia:

  11. Mjumbe wa Trump kukutana na Putin kujadili mpango wa kumaliza vita vya Ukraine

    Mjumbe maalum wa Marekani, Steve Witkoff, anatarajiwa kukutana na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, mjini St. Petersburg hii leo, ili kujadili mapendekezo ya kumaliza vita vya Urusi dhidi ya Ukraine ambavyo vimedumu kwa miaka kadhaa.

    Mazungumzo hayo yanafanyika siku moja baada ya Witkoff kukutana na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, mjini Oslo.

    Awali, Kyiv ilikuwa imeishutumu Marekani kwa kuinyima taarifa muhimu za ujasusi, madai ambayo Washington ilikanusha.

    Soma pia:

  12. Iran yajitolea kuwa mpatanishi kati ya Saudi Arabia na Wahouthi

    Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran, Abbas Araqchi, amesema kuwa Saudi Arabia na kundi la waasi la Wahouthi nchini Yemen bado hawajajibu pendekezo la Iran la kutaka kuwa mpatanishi kati ya pande hizo mbili ili kumaliza mapigano.

    Kulingana shirika la habari la Reuters, Araqchi alisema kuwa alikuwa amejitolea kusaidia kuanzisha mazungumzo ya kupata amani, baada ya mashambulizi ya Wahouthi dhidi ya Saudi Arabia kuongezeka mapema mwezi huu.

    Akizungumzia kuhusu taarifa ya Misri ya kuunga mkono Saudi Arabia katika vita dhidi ya Wahouthi, Waziri huyo alisema kuwa “uingiliaji wowote wa nje utachochea hali kuwa ngumu zaidi”

    Awali, Misri ilisema kuwa iko tayari kuipatia Saudi Arabia msaada wowote unaohitajika ili kulinda usalama wake.

    Soma pia:

  13. Tetesi za Soka: United, Arsenal na Liverpool zakoleza mbio za usajili

    Manchester United inapanga kufanya mageuzi makubwa katika safu yake ya ulinzi msimu ujao na inajiandaa kurejea kwa Lewis Hall wa Newcastle. Beki huyo wa England mwenye umri wa miaka 22 anaripotiwa kuwa tayari kuhamia Old Trafford. United pia inamuwinda beki wa Ufaransa Adrien Truffert (24) wa Bournemouth.( iNews)

    Real Madrid bado ina nia ya kumsajili beki wa Italia Riccardo Calafiori, lakini Arsenal imeweka wazi kuwa itahitaji ofa kubwa isiyo ya kawaida ili kumuuza mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24. (CaughtOffside)

    Liverpool na Arsenal zinamuwania beki kijana wa Hispania Xavi Espart (19), lakini Barcelona haitaki kumuachia na ina kipengele cha kuvunja mkataba wake kinachozidi pauni milioni 84. (Teamtalks)

    Newcastle United inafikiria kumsajili beki wa England Fikayo Tomori kutoka AC Milan mara tu atakapokuwa mchezaji huru mwishoni mwa msimu. (Football Insider)

    Arsenal pia inapanga kumsajili mshambuliaji wa Club Brugge, Nicolo Tresoldi (22), katika dirisha la Januari. Mjerumani huyo anatajwa kuwa na thamani ya pauni milioni 42. (Sun)

    Kiungo wa Argentina Emiliano Buendia yuko mbioni kuongeza mkataba wake na Aston Villa, huku mazungumzo ya mikataba mipya na Victor Lindelof pamoja na George Hemmings yakipiga hatua.

    Manchester United inaendelea kufuatilia hali ya winga wa Crystal Palace, Ismaila Sarr (28), ambaye pia anawindwa na Galatasaray. (Athletic)

    Beki wa Tottenham, Pedro Porro (27), anaripotiwa kuwa tayari kuzingatia nafasi ya kujiunga na Barcelona au Real Madrid iwapo ofa itawasilishwa. (Teamtalk)

    Wakati huo huo, beki wa Argentina Lisandro Martinez anatarajiwa kuondoka Manchester United mwishoni mwa msimu. (Mail)

    Soma pia:

  14. Trump: Amani au nguvu? Uamuzi wa mwisho kuhusu Iran ni wangu

    Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema hahitaji msaada wa nchi nyingine katika kukabiliana na Iran, akisisitiza kwamba Marekani ina uwezo wa kushinda mgogoro huo peke yake.

    Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari katika Ikulu ya White House Jumanne jioni, Trump alirudia madai yake kuhusu ubora wa Marekani katika mvutano unaoendelea na Iran.

    "Kama mnavyojua, tunaendelea vizuri sana kuhusu Iran. Kilichobaki ni kufanya uamuzi wa mwisho kuhusu namna tutakavyoshinda; je, tutafanya hivyo kwa njia ya amani au kwa njia kali?" alisema Trump.

    Aliongeza kuwa: "Kwa vyovyote vile, tunaendelea vizuri sana na hatuhitaji msaada wa mtu yeyote."

    Akizungumzia kupanda kwa bei ya mafuta kufuatia vikwazo vya usafiri katika Mlango wa Hormuz, Trump alisema wananchi wengi hawajaridhishwa na gharama za mafuta, lakini akaeleza kuwa hiyo ni gharama ndogo ikilinganishwa na hatari ya Iran kupata silaha za nyuklia.

    "Watu hawafurahishwi na bei ya mafuta. Hata hivyo, hiyo ni gharama ndogo kulipa ili kuzuia Iran kupata silaha za nyuklia," alisema.

    Trump pia alisema aliwasiliana na viongozi wa nchi mbalimbali ili kubaini kama wangekuwa tayari kuisaidia Marekani, lakini alidai kuwa wote walikataa.

    "Nilikuwa nawajaribu tu. Niliwapigia marais na mawaziri wakuu kadhaa kuwauliza kama wangependa kutusaidia, na wote walisema hapana," alisema.

    Hata hivyo, hakutaja viongozi aliowasiliana nao wala maelezo ya mazungumzo hayo.

    Kauli hizo zinakuja saa chache baada ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kuchapisha video ya mazungumzo yake ya simu na Trump. Katika video hiyo, Netanyahu anasikika akisema:

    "Donald, bado tuna kazi ambayo haijakamilika. Tutaikamilisha pamoja kwa sababu hakuna mwingine anayeweza kufanya hivyo."

    Wakati huo huo, Iran imeendelea kushinikiza kusitishwa kwa vitisho kutoka Marekani na Israel. Siku moja iliyopita, Tehran iliwasilisha barua kwa Umoja wa Mataifa ikitaka hatua zichukuliwe kukomesha vitisho hivyo.

    Maafisa waandamizi wa Iran pia walisisitiza katika mazungumzo yao na mkuu wa jeshi la Pakistan, Asim Munir, kwamba sharti la kuanza tena mazungumzo na Marekani ni Washington kuheshimu masharti yaliyofikiwa katika makubaliano ya Islamabad.

  15. Zaidi ya watu 300 wauawa katika mashambulizi ya droni nchini Sudan

    Jeshi la Sudan limetuhumiwa kutekeleza mashambulizi kadhaa ya ndege zisizo na rubani ambayo yameripotiwa kuwaua zaidi ya watu 300, wakiwemo watu kadhaa waliokuwa wakielekea kwenye mazishi.

    Vyanzo vimeiambia taasisi ya Sudan War Observatory, inayofuatilia mzozo uliozuka mwaka 2023 kati ya jeshi la Sudan na kikosi cha wanamgambo cha Rapid Support Forces (RSF), kuwa watu 150 waliuawa katika mashambulizi yaliyolenga maeneo mawili katika jimbo la West Kordofan, Jumapili jioni.

    Katika eneo la Abyei, linalozozaniwa na Sudan na Sudan Kusini, watu 153 waliuawa baada ya ndege zisizo na rubani kushambulia soko moja siku ya Jumatatu.

    Chanzo kimoja cha kijeshi kimeiambia BBC kuwa jeshi la Sudan lilitekeleza shambulizi hilo, kwa madai kuwa soko hilo lilikuwa kituo kinachosambaza mafuta kwa RSF.

    Shambulizi hilo limeongeza mvutano kati ya Sudan na Sudan Kusini, ambazo kwa pamoja zinasimamia eneo la Abyei. Nchi hizo zote mbili zinadai kumiliki eneo hilo lenye utajiri wa mafuta, katika mzozo ambao haujapata suluhu tangu Sudan Kusini ijitenge na Sudan mwaka wa 2011.

    Sudan Kusini imemwita balozi wa Sudan nchini humo ili kuwasilisha rasmi malalamishi yake kuhusu shambulizi hilo.

    Licha ya kuwepo kwa vikwazo vya usambazaji wa silaha kwa Sudan, mataifa ya kigeni yamekuwa yakiuza silaha ikiwemo ndege zisizo na rubani kwa pande zote mbili, jeshi la Sudan na RSF. Silaha hizo zinazidi kuwa miongoni mwa zinazotumiwa zaidi katika mzozo huo.

    Soma pia:

  16. Nigeria yathibitisha kisa cha Ebola kwa msafiri aliyetoka Afrika Mashariki

    Nigeria imeripoti kisa kimoja cha Ebola, kutoka kwa mgonjwa mmoja wa kike aliyesafiri kutoka Uganda, Afrika Mashariki, hadi mjini Abuja, nchini Nigeria.

    Waziri wa Afya wa taifa hilo, Muhammad Ali Pate, amesema kisa hicho kimethibitishwa kupitia vipimo vya maabara.

    Mgonjwa huyo kwa sasa ametengwa na anapokea matibabu katika hospitali moja mjini Abuja.

    Mamlaka za afya za Nigeria zimeanza kufuatilia watu waliokuwa karibu na mgonjwa huyo ili kuzuia kuenea zaidi kwa ugonjwa huo. Hadi kufikia sasa, watu 44 waliokuwa na mawasiliano ya karibu naye wametambuliwa.

    Nigeria ni nchi ya kwanza Afrika Magharibi kuripoti kisa kinachohusishwa na mlipuko wa sasa wa Ebola ambao umeenea Afrika Mashariki. Nchi hiyo ilifanikiwa kudhibiti mlipuko wa awali wa ugonjwa huo mwaka wa 2014.

    Soma pia:

  17. Zelensky akiri ushirikiano wa Marekani katika utoaji wa taarifa za kijasusi

    Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amesema kuwa ushirikiano wa Marekani na taifa lake katika kutoa taarifa za kijasusi kuhusu mashambulizi hatari ya makombora ya Urusi sasa umeanza kufanya kazi, baada ya kufanya mazungumzo na mjumbe maalum wa Rais Donald Trump, Steve Witkoff.

    Mkutano huo ulifanyika mjini Oslo, kufuatia tuhuma za Ukraine kwamba Washington ilikuwa imesitisha kutoa taarifa muhimu za kijasusi madai ambayo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, aliyakataa na kuyataja kuwa uongo.

    Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amesema mfumo huo umeanza tena kufanya kazi kwa ufanisi.

    "Tunashukuru kwamba mifumo ya ujasusi inafanya kazi. Ninazungumzia mifumo ya tahadhari ya mapema, ambayo ni muhimu sana kwa wananchi wetu, watoto, watu wazima na raia kwa ujumla, kwa sababu tunaweza kupata taarifa ya tahadhari wakati kombora la masafa marefu linapokuja. Ukraine inataka amani kuliko mtu mwingine yeyote. Na ni Urusi ndiyo iliyoanzisha vita hivi. Uamuzi wa kuendeleza mauaji ni wa Urusi, na Urusi pekee ndiyo inayopaswa kuwajibika kwa uamuzi huo.’’

    Rais wa Finland, Alexander Stubb, ambaye pia alishiriki katika mazungumzo hayo, alisema kuwa wamepiga hatua kuhusu mapendekezo ya kufikia amani, lakini hakutoa maelezo zaidi.

    Rais wa Urusi, Vladimir Putin, bado hajatoa maoni yake hadharani kuhusu mapendekezo hayo ya hivi karibuni.

    Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, amesema kuwa Kremlin itasikiliza mapendekezo ambayo Witkoff atawasilisha, huku akiondoa uwezekano wa “makubaliano yoyote ya kisiasa yanayohusisha kufanya mapatano kwa upande wa Urusi”.

    Soma pia:

  18. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja Jumatano ya leo