Moja kwa moja, Marekani na Iran zaanzisha mashambulizi mapya huku mazungumzo yakikwama
Mashambulizi ya hivi karibuni yanatokea baada ya mazungumzo kuhusu makubaliano ya kukomesha vita vyao vya miezi kadhaa kushindwa kuendelea mwishoni mwa juma.
Muhtasari
Marekani yawawekea vikwazo waasi wanaohusishwa na serikali ya DRC na Rwanda
Muswada wa kuongeza muda wa rais wa Zimbabwe wapita hatua ya kwanza ya usomaji bungeni
Chanzo cha picha, Getty Images
Muswada tata
ambao unaweza kuongeza muda wa urais nchini Zimbabwe umepita hatua yake ya
kwanza ya usomaji bungeni.
Sheria hiyo
inayopendekezwa inalenga kurekebisha katiba ili kuongeza muda wa muhula wa rais
na wabunge kutoka miaka mitano hadi saba.
Pia unalenga
kubadilisha mfumo wa uchaguzi wa rais, ambapo badala ya kura ya moja kwa moja
ya wananchi, bunge litakuwa na mamlaka ya kumchagua kiongozi wa nchi.
Utasomwa mara ya pili Jumatano wakati wabunge
watakapojadili uhalali wa marekebisho zaidi ya kumi.
Ibara zenye utata zaidi zinapendekeza kuruhusu Rais
Mnangagwa na wabunge kusalia ofisini hadi 2030 na kubadilisha kura ya urais
kutoka kwa mchakato wa umma hadi wa bunge.
Marekebisho yaliyopendekezwa yamesababisha ghadhabu kwa
wananchi na yanakabiliwa na changamoto kadhaa za kisheria.
Wakosoaji wakiwemo Chama cha Wanasheria nchini humo
wanasema mapendekezo hayo yanadhoofisha taasisi za kidemokrasia na kulimbikiza
madaraka kwa rais.
Makanisa makubwa na mashirika ya haki za binadamu
wanasema mabadiliko hayo ni kinyume na katiba na yanahitaji kura ya maoni.
Mswada huo utahitaji angalau theluthi mbili ya kura
katika Mabunge yote mawili ili kupitishwa.
Marekani yawawekea vikwazo waasi wanaohusishwa na serikali ya DRC na Rwanda
Chanzo cha picha, Reuters
Marekani imewawekea vikwazo makamanda wawili wa makundi
yenye silaha wanaotuhumiwa kuchochea ghasia na ukosefu wa utulivu mashariki mwa
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Katika taarifa iliyotolewa siku ya Jumanne, Ofisi ya
Idara ya Hazina ya Marekani ya Udhibiti wa Mali za Kigeni (OFAC) iilimwekea
vikwazo Gustave Kubwayo, iliyemtambua kama kamanda wa kitengo cha kijasusi na
operesheni maalum cha Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR).
Wakati huo huo, John Imani Nzenze, aliyesemekana kuwa
kamanda na mkuu wa upelelezi wa kundi la waasi la M23 pia aliwekewa vikwazo.
"FDLR na M23 wameteka maeneo kwa kutumia nguvu na
kuua raia mashariki mwa DRC," taarifa kutoka Idara hiyo ilisema.
Iliongeza kuwa: "Kutokana na hatua ya leo, mali na
maslahi yote katika mali ya watu waliotambuliwa au waliozuiwa walioelezwa hapo
juu ambazo ziko Marekani au katika milki au udhibiti wa watu wa Marekani zimezuiwa."
Rwanda inaishutumu serikali ya DRC kwa kuunga mkono FDLR,
kundi lenye silaha lililoundwa na wanajeshi wa zamani wa Rwanda na watu wenye
itikadi kali ambao walikimbilia mashariki mwa Congo wakati wa mauaji ya kimbari
ya 1994. Kigali inawachukulia waasi hao kuwa tishio.
Kwa upande mwingine, mamlaka ya Congo na waangalizi
wengine wa kimataifa wameishutumu Rwanda kwa kuunga mkono kundi la M23, kundi
lenye silaha ambalo limeteka maeneo mengi kutoka kwa serikali ya DRC katika kipindi
cha mwaka uliopita.
"Ghasia zinazoendelea kufanywa na makundi yenye
silaha zinazidisha mzozo mbaya wa kibinadamu na ni tishio kwa maslahi ya
Marekani katika eneo hilo," Waziri wa Fedha wa Marekani Scott Bessent
alisema.
"Vikwazo vya leo vinaunga mkono azimio la amani na
kukomesha umwagaji damu," aliongeza, akizitaka DRC na Rwanda kusitisha
uungaji mkono wao kwa makundi yenye silaha yaliyoidhinishwa kama ilivyoainishwa
na mikataba ya amani inayoongozwa na Marekani iliyotiwa saini mwezi Desemba
mwaka jana.
Hii si mara ya kwanza kwa wanachama wa makundi yenye
silaha nchini DRC kuwekewa vikwazo. Lakini hatua hizo zimeshindwa kukomesha
mapigano katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo lenye machafuko.
Tetesi za Soka Ulaya: Aston Villa haina mpango wa kumuuza Rogers
Chanzo cha picha, Getty Images
Aston Villa haina mpango wa kumuuza Morgan Rogers
huku klabu kadhaa zikiwa na nia ya kumsajili kiungo huyo mshambuliaji,
Barcelona bado wana hamu ya kumsajili Marcus Rashford kutoka Manchester
United na Real Madrid wanafanya mazungumzo na beki wa kulia wa Inter Milan
Denzel Dumfries.
Aston Villa wanajua kuwa kuna nia ya kumsajili kiungo
mshambuliaji Morgan Rogers kutoka klabu kadhaa, ikiwemo Arsenal, lakini
hawana mpango wa kumuuza mchezaji huyo wa kimataifa wa Uingereza mwenye umri wa
miaka 23. (Telegraph - subscription required)
Beki wa pembeni wa Eintracht Frankfurt, Nathaniel
Brown, mwenye umri wa miaka 22, ndiye anayewindwa na Bayern Munich na Arsenal.
(The Athletic - subscription required)
Manchester City na Chelsea wanamtaka beki wa
pembeni wa Juventus Andrea Cambiaso, 26, huku Barcelona pia
ikifuatilia hali ya mchezaji huyo wa kimataifa wa Italia. (Gazzetta dello
Sport - in Italian)
Chanzo cha picha, Getty Images
Liverpool na Paris St-Germain huenda zote zikamtaka winga wa RB Leipzig Yan Diomande lakini klabu hiyo ya Ujerumani haitikiswi na hali hiyo kwani inaamini mchezaji huyo wa miaka 19 hataendelea kuwa nao kwa mwaka mwingine tu bali pia atasaini mkataba mpya ulioboreshwa. (Sky Sports Germany)
Kocha wa Barcelona Hansi Flick, mkurugenzi wa michezo
Deco na rais Joan Laporta bado wana hamu ya kumsajili mshambuliaji wa
Manchester United Marcus Rashford kwa mkataba wa kudumu huku Bayern
Munich, Newcastle, Tottenham na Aston Villa wakimtaka
mchezaji huyo wa kimataifa wa Uingereza mwenye umri wa miaka 28. (The I)
Juventus wanaangalia uwezekano wa kumsajili
mshambuliaji wa Bournemouth na Uholanzi Justin Kluivert mwenye umri
wa miaka 27 kama mbadala wa mchezaji wa Real Madrid mwenye umri wa
miaka 26 wa Morocco Brahim Diaz. (Gazzetta dello Sport - in Italian)
Manchester United wamemfuatilia mlinzi wa Juventus na
Ufaransa Pierre Kalulu na klabu ya Turin huenda ikalazimika kumuuza mchezaji
huyo wa miaka 25 ili kusawazisha masuala ya miamala baada ya kushindwa kufuzu
kwa Ligi ya Mabingwa. (Corriere dello Sport - in Italian)
Kiungo wa kati wa Ureno Mateus Fernandes, 21, ameruhusiwa
kuondoka West Ham baada ya mawasiliano kutoka Manchester United na Arsenal, huku Liverpool na Paris
St-Germain pia zikimfuatilia. (Teamtalk)
Aston Villa, Atletico Madrid na Borussia
Dortmund zinamtaka mshambuliaji wa Club Brugge, Mjerumani Nicolo
Tresoldi, 21, baada ya msimu mzuri Ubelgiji. (The Athletic - subscription
required)
Real Madrid wamefanya mazungumzo na mlinzi wa Inter
Milan Denzel Dumfries, ambaye kima chake cha kuuza ni pauni milioni 21.6,
huku wakimwona mchezaji huyo wa kimataifa wa Uholanzi mwenye umri wa miaka 30
kama shabaha yao kuu ya kuimarisha safu yao ya beki wa kulia. (Athletic)
Israeli imeendelea
na mashambulizi yake kusini mwa Lebanon siku ya Jumanne, lakini haikushambulia
Beirut kufuatia makubaliano ya kusitisha mapigano kwa kiasi fulani na kundi la
Hezbollah linaloungwa mkono na Iran.
Lebanon
ilisema kwamba, chini ya makubaliano yaliyotangazwa na Rais wa Marekani Donald
Trump usiku wa Jumatatu, vikosi vya Israeli havitashambulia mji mkuu kwa mabomu
nayo Hezbollah haitashambulia Israeli.
Hii ilitokea
baada ya Iran kusema kwamba hatua ya Israeli nchini Lebanon inahatarisha
mazungumzo kuhusu makubaliano ya kukomesha vita vyake na Marekani.
Kufuatia
tangazo la kusitisha mapigano, jeshi la Israeli lilisema limezuia makombora
mawili yaliyorushwa kaskazini mwa Israeli.
Hezbollah
ilisema imeshambulia vikosi vya Israeli kusini mwa Lebanon, ambapo maafisa
waliripoti mashambulizi mabaya ya Israeli.
Marekani na Iran zaanzisha mashambulizi mapya huku mazungumzo ya kusitisha mapigano yakikwama
Chanzo cha picha, X/US Central Command
Jeshi la
Marekani linasema limeanzisha mashambulizi ya "kujilinda" dhidi ya
Iran na kudungua makombora ya masafa marefu na ndege zisizo na rubani kwenye
meli na nchi za Ghuba.
Mashambulizi
hayo kwenye Kisiwa cha Qeshm, katika Mlango-Bahari wa Hormuz, yalikuwa
"kujibu majaribio ya mashambulizi ya Iran kote Mashariki ya Kati",
Kamandi Kuu ya Marekani (Centcom) ilisema.
Iran ilisema
imeshambulia kambi na helikopta za Marekani katika "nchi ya kikanda"
kwa kutumia makombora na ndege zisizo na rubani kama kulipiza kisasi.
Centcom
ilisema Tehran imerusha makombora mawili dhidi ya Kuwait na matatu dhidi ya
Bahrain, ambayo yote yalivunjika vipande vipande au kuzuiliwa.
Mashambulizi
ya hivi karibuni yanatokea huku mazungumzo ya kusitisha mapigano yakikwama,
baada ya mazungumzo kuhusu makubaliano ya kukomesha vita vyao vya miezi kadhaa
kushindwa kuendelea mwishoni mwa juma.
Centcom
iliongeza kuwa shambulio hilo katika Kisiwa cha Qeshm lilikuwa limelenga kituo
cha udhibiti wa ardhini cha jeshi la Iran, na kwamba jeshi la Marekani pia
lilidungua ndege tatu zisizo na rubani ambazo zilikuwa zimerushwa na Iran
kuelekea kwa "mabaharia raia waliokuwa wakipitia maji ya kikanda kihalali".
IRGC ilisema
"kuvuruga usalama wa Mlango-Bahari wa Hormuz kutakuwa na gharama kubwa kwa
jeshi la Marekani lenye uchokozi".
Iran imekuwa
ikishambulia mara kwa mara maeneo ya Bahrain na Kuwait, ambapo kambi za kijeshi
za Marekani zipo.
Hapo awali,
Centcom ilisema imeishambulia na kuiharibu meli ya mafuta isiyo na mizigo
iliyokuwa ikielekea Iran, kama sehemu ya kizuizi cha majini cha Washington
kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz.