Wahouthi wasonga kwa kasi Tihama, wakiteka kilomita 130 za pwani ya Yemen
Kusonga kwa kasi kwa Wahouthi katika eneo kubwa la tambarare ya pwani ya Tihama, kusini mwa Yemen, kunaonekana kuwashangaza wachunguzi wengi.
Tihama ni eneo kame la tambarare ya pwani nchini Yemen. Hadi hivi karibuni, muungano unaopinga Wahouthi unaojulikana kama ‘National Resistance’ ulikuwa ukidhibiti eneo kubwa kando ya pwani ya Bahari ya Shamu, lakini ndani ya siku chache, sehemu kubwa ya eneo hilo imeangukia mikononi mwa Wahouthi.
Kwa mujibu wa baadhi ya makadirio, vikosi vya Wahouthi vinavyoungwa mkono na Iran vimetwaa hadi kilomita 130 za pwani ya Yemen yenye umuhimu wa kimkakati.
Hii ni mafanikio makubwa zaidi ya kijeshi ya Wahouthi katika miaka ya hivi karibuni, yakionyesha kuwa licha ya miaka 12 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, mashambulizi makali ya anga ya Saudi Arabia, pamoja na mashambulizi ya Marekani, Israel na Uingereza, Wahouthi bado ni nguvu inayopaswa kuzingatiwa.
“Kwa kuwa sasa wamefika huko, wataimarisha udhibiti wao, na itakuwa gharama kubwa zaidi kuwaondoa,” Hisham al-Ameisi, mchambuzi mwandamizi katika Taasisi ya Ulaya ya Amani yenye makao yake Brussels, aliiambia BBC.
Afisa mmoja aliambia mashirika ya habari ya Reuters na AFP kuwa boti zilizobeba wapiganaji wenye silaha wa Houthi zilifika katika Kisiwa cha Baryim/Miyun,ambacho hugawanya mlango bahari huo katika njia mbili za meli, baada ya vikosi vya serikali kuondoka eneo hilo siku ya Alhamisi.
Afisa huyo, aliyeomba kutotajwa jina, aliongeza, "Wahouthi wametwaa udhibiti kamili wa eneo la Bab al-Mandab na Kisiwa cha Miyun kilicho katikati ya mlango bahari huo."
Shahidi mmoja alisema kuwa wanamgambo wa Houthi "wamesambaa kando ya pwani ya Bab al-Mandab, na wanazunguka kwa kutumia magari ya kijeshi."
Pia unaweza kusoma: