Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Maziko ya Mfalme Oyo wa Tooro Uganda yaanza huku mzozo wa urithi ukiendelea

Ibada ya Mazishi ya Mfalme Oyo Nyimba Kabamba Iguru Rukidi wa Nne, aliyewahi kuwa mtawala mwenye umri mdogo zaidi duniani, yafanyika katika kanisa kuu la dayosisi ya St.John Cathedral Uganda, Mfalme Oyo atazikwa leo katika makaburi ya kifalme ya Ufalme wa Tooro, magharibi mwa Uganda.

Moja kwa moja

Na Sarafina Robi & Mariam Mjahid

  1. Gazeti la Financial Times: Marekani yataka meli za mafuta zinazopita Hormuz kusafiri wakati maalum

    Gazeti la Financial Times limeripoti kuwa Marekani imezitaka meli za mafuta zinazopita kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz kusafiri wakati maalum pekee ili kuhakikisha zinapata ulinzi wa kijeshi.

    Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ombi hilo lilikuja baada ya Iran kuongeza mashambulizi dhidi ya meli zinazosafiri nyakati za usiku.

    Ripoti hiyo inaeleza kuwa tangu mwezi Mei, Marekani imekuwa ikitoa ulinzi wa anga kwa meli zinazojaribu kupita katika njia iliyo kando ya pwani ya Oman, upande wa kusini wa mlango-bahari huo.

    Financial Times iliripoti, ikinukuu barua pepe zilizotumwa na Kituo cha Uratibu cha Jeshi la Wanamaji la Marekani kwa washauri wa masuala ya majini, kuwa muda wa kuzilinda meli hizo ulipunguzwa na kuwa vipindi viwili maalum kwa siku mwanzoni mwa mwezi Septemba.

  2. Jeshi la Yemen ladai kusababisha hasara kubwa katika mashambulizi dhidi ya ngome za Wahouthi

    Msemaji wa jeshi la serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa ametangaza kuwa ngome za kundi la Wahouthi la Ansar Allah zimeshambuliwa katika maeneo ya Mokha na Dhubab, magharibi mwa Yemen.

    Msemaji wa jeshi, Majid al-Nuzili, alidai katika taarifa kwenye mtandao wa kijamii wa X kuwa mashambulizi hayo yaliharibu shabaha kadhaa katika maeneo ya Mokha na Dhubab.

    Kulingana na yeye, magari na silaha ziliharibiwa kabisa katika operesheni hizo, huku wapiganaji wa Kihouthi waliokuwa karibu na bandari ya Mokha pia wakiuawa.

    Aliongeza kuwa wanachama wengine wa kundi la Wahouthi walilengwa pia katika sehemu mbalimbali za mji huo wa pwani.

    Kwa mujibu wake, kundi kubwa la wapiganaji wa Kihouthi lilishambuliwa karibu na kituo cha biashara katika mji wa Mokha, na kusababisha kuangamizwa kabisa kwa watu waliokuwepo hapo.

  3. Maziko ya Mfalme Oyo: Binti Mfalme Ruth Nsemere Komuntale amuomboleza kakake kama mtu aliyekuwa mcheshi

    Katika hotuba yake ya mwisho ya kumuaga mdogo wake, Binti Mfalme Ruth Nsemere Komuntale alielezea miezi ya mwisho ya maisha ya Mfalme Oyo Nyimba Kabamba Iguru Rukidi III.

    Alieleza kwa ufupi namna saratani ya Mfalme Oyo ilivyogunduliwa. Alisema dalili za saratani hiyo zilianza kujitokeza katikati ya Oktoba 2025, kabla ya kugundulika kuwa alikuwa na Angiosarcoma, aina adimu na kali ya saratani inayotokea kwenye mishipa ya damu na mishipa ya limfu.

    Binti Mfalme alisema mdogo wake alitumia zaidi ya mwaka mmoja akitafuta matibabu nchini Uganda kutokana na baadhi ya dalili alizokuwa nazo, lakini saratani hiyo haikugunduliwa mapema.

    Baadaye, alipokuwa akipatiwa matibabu nchini Marekani, Mfalme Oyo aliomba hali yake ya kiafya iwekwe siri ili kuepusha hofu miongoni mwa watu wa ufalme.

    Katika kuhitimisha hotuba yake, Binti Mfalme aliwataka watu kuwa makini na afya zao, kusikiliza miili yao na kujitunza.

  4. Mkutano wa Delhi kuamua mustakabali wa muungano wa BRICS

    Viongozi wa dunia, akiwemo Rais wa Urusi Vladimir Putin, Rais wa China Xi Jinping, na Rais wa Iran Masoud Pezeshkian, wamekusanyika Delhi kwa ajili ya mkutano wa kilele wa BRICS.

    Kundi hilo liliundwa kwa lengo la kuwa na nguvu ya usawa dhidi ya Marekani na Ulaya Magharibi, lakini vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati vimeibua nyufa ndani yake.

    Mkutano huo ni fursa kwa BRICS kudhihirisha nafasi yake kama nguvu ya kisiasa na kiuchumi inayoweza kukabiliana na Magharibi, lakini pia ni jaribio kubwa kwa umoja wake.

    Migogoro ya kimataifa imefichua migawanyiko mikubwa, kwa mfano, Falme za Kiarabu zimekuwa zikilengwa na mashambulizi kadhaa ya ndege zisizo na rubani na makombora kutoka Iran mwaka huu.

    Mikutano ya BRICS katika kipindi cha miezi sita iliyopita haijazaa taarifa ya pamoja, jambo linalodaiwa kusababishwa na kutokubaliana sana kuhusu Iran na namna ya kushughulikia mizozo inayohusiana na Israel.

    Suala jingine ni Donald Trump, vitisho vyake vya ushuru wa biashara vinafanya iwe muhimu zaidi kwa wanachama wa BRICS kuungana ili kuleta uwiano, lakini wakati huo huo, kukabiliana naye kunaweza kuwa na gharama kubwa.

    Ikulu ya Marekani imeelezea baadhi ya mapendekezo ya BRICS kama yenye msimamo wa "kupinga Marekani," na nchi nyingi zitakuwa na tahadhari dhidi ya kumkasirisha rais huyo wa Marekani.

  5. Katika Picha: Ibada ya maziko ya Mfalme Oyo Nyimba katika kanisa la St John's Cathedral

    Ibada ya mazishi ya kumuaga Mfalme Oyo Nyimba yaanza rasmi katika kanisa la St. John's Cathedral nchini Uganda.

    Familia, jamaa na marafiki wamehudhuria katika ibada hiyo huku shughuli za misa zikianza rasmi.

    Maelfu ya waombolezaji walijipanga kando ya barabara wakati mwili wa Mfalme Oyo Nyimba Kabamba Iguru Rukidi wa Nne, Omukama wa Tooro, ukisafirishwa katika safari yake ya mwisho kuelekea Ikulu ya Karuziika.

    Sherehe za kimila ziliambatana na kila hatua ya msafara huo, kwa heshima ya utawala wake wa takriban miaka 31.

  6. Saudi Arabia yasitisha kwa tahadhari shughuli za bomba la mafuta la Mashariki-Magharibi

    Bomba la mafuta la Mashariki-Magharibi la Saudi Arabia, ambalo limekuwa likilengwa na mashambulizi ya droni kutoka Iraq, limezidi kuwa muhimu tangu kuzuka kwa vita Mashariki ya Kati kati ya Marekani na Israel upande mmoja na Iran upande mwingine.

    Bomba hilo la Petroline linaanzia katika maeneo ya mafuta ya Abqaiq, katika Mkoa wa Mashariki wa Saudi Arabia, hadi bandari ya Yanbu, magharibi mwa nchi hiyo. Lina urefu wa takriban kilomita 1,200 na ni njia kuu mbadala ya kusafirisha mafuta ya Saudi Arabia kwenda katika masoko ya dunia, bila kupitia Mlango wa Hormuz.

    Kwa mujibu wa kampuni za usafirishaji na wachambuzi, katika miezi michache iliyopita bomba hilo limekuwa likisafirisha mapipa milioni nne hadi tano ya mafuta kwa siku, sawa na asilimia nne hadi tano ya usambazaji wa mafuta duniani.

    Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Saudi Arabia (SPA), mabomba hayo yana uwezo wa kusafirisha takriban mapipa milioni saba ya mafuta kwa siku.

    Saudi Arabia imetangaza mara kadhaa katika miezi ya hivi karibuni kuwa maeneo yake, hususan miundombinu ya nishati, yamelengwa katika mashambulizi ambayo inasema yalifanywa na makundi nchini Iraq yenye uhusiano na Tehran.

  7. Tetesi za soka Ulaya: Richarlison bado anaweza kuondoka Spurs

    Klabu kadhaa bado zinamuwania mshambuliaji wa Brazil, Richarlison, mwenye umri wa miaka 29, baada ya mpango wake wa kuondoka Tottenham na kujiunga na Vasco da Gama kuvunjika. (UOL - in Portuguese)

    Philippe Coutinho, aliyewahi kuichezea Brazil, amekubali kutumia miezi mitatu katika klabu ya Santos. Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 34, aliyewahi kucheza Liverpool na Aston Villa, anatafakari iwapo ataendelea na soka baada ya kuwa mchezaji huru tangu Februari, alipoondoka Vasco da Gama. (Globo - in Portuguese)

    Manchester United inamfuatilia kwa karibu beki wa kushoto wa Bournemouth na timu ya taifa ya Ufaransa, Adrien Truffert, mwenye umri wa miaka 24, ambaye thamani yake inakadiriwa kuwa pauni milioni 60.(Teamtalk)

    Liverpool bado inamtaka kiungo wa Inter Milan, Aleksandar Stankovic, mwenye umri wa miaka 21, baada ya kuulizia uwezekano wa kumsajili katika dirisha la usajili la majira ya joto. (Teamtalk)

    Crystal Palace bado haijakata tamaa ya kumsajili beki wa kati wa Brest, Raphael Le Guen, mwenye umri wa miaka 20, ambaye ilijaribu kumsajili katika dirisha la usajili lililopita. (Ouest-France via SportWitness)

    Liverpool bado inamuwania winga wa Ufaransa, Michael Olise, mwenye umri wa miaka 24, lakini Bayern Munich haina mpango wa kumuuza katika dirisha la usajili la Januari. (Christian Falk)

    Lamine Camara sasa ameelekeza nguvu zake katika klabu ya Monaco baada ya mpango wa siku ya mwisho wa usajili wa kiungo huyo wa Senegal, mwenye umri wa miaka 22, kujiunga na Chelsea kuvunjika. Camara amesema, “Labda fursa nyingine zitajitokeza.” (ESPN)

    Jadon Sancho hatarajiwi kujiunga na klabu mpya hivi karibuni, huku winga huyo wa zamani wa England, mwenye umri wa miaka 26, akiendelea kutathmini chaguo zake baada ya kuondoka Manchester United mwezi Juni. (Football Insider)

    Lazio na Parma zimejiunga na Everton katika kuonyesha nia ya kumsajili mshambuliaji wa zamani wa Argentina, Mauro Icardi, mwenye umri wa miaka 33, ambaye ni mchezaji huru baada ya kuondoka Galatasaray mwishoni mwa msimu uliopita. (Corriere dello Sport - in Italian)

    Malaga inazingatia uwezekano wa kumsajili mshambuliaji wa zamani wa Manchester United na timu ya taifa ya Ufaransa, Anthony Martial, mwenye umri wa miaka 30, ambaye ni mchezaji huru baada ya kuondoka klabu ya Monterrey ya Mexico mwezi Juni. (Mundo Deportivo - in Spanish)

    Soma Zaidi Hapa:

  8. Maziko ya Mfalme Oyo wa Tooro Uganda yaanza huku mzozo wa urithi ukiendelea

    Mwili wa marehemu Mfalme Oyo Nyimba Kabamba Iguru Rukidi wa Nne, aliyefariki dunia mwezi uliopita akiwa na umri wa miaka 34, umesafirishwa kutoka Ikulu ya Karuzika hadi Kanisa Kuu la dayosisi ya St. John mjini Fort Portal.

    Maelfu ya waombolezaji,baadhi wakiwa wamevalia kanzu nyeupe na mavazi ya gome la mti, pamoja na viongozi wa taasisi za kitamaduni na watu mashuhuri wengine,wamekusanyika katika ikulu hiyo na kanisa kuu kuhudhuria shughuli ya kumuaga mfalme huyo kwa mara ya mwisho.

    Mfalme Oyo alifariki dunia nchini Marekani mwezi uliopita, ambako alikuwa akipatiwa matibabu ya saratani. Baadaye atazikwa leo Jumamosi katika eneo la makaburi ya kifalme huko Karambi.

  9. Hujambo na Karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja.