Saudi Arabia lazima iitambue Israel - Trump

    • Author, Robert Greenall
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Rais Donald Trump amesema kuwa makubaliano kati ya Marekani na Saudi Arabia ya kuisaidia nchi hiyo ya Ghuba kuendeleza nishati ya nyuklia yanategemea Riyadh kuitambua Israel.

"Makubaliano ya Nishati ya Nyuklia kwa Matumizi ya Kiraia (Hakutakuwa na urutubishaji wa nyenzo!)... ambayo yanahusu matumizi yasiyo ya kijeshi pekee... yataidhinishwa, lakini sharti lake kuu ni Saudi Arabia kujiunga na Makubaliano ya Abraham yanayoheshimika na kufanikiwa sana," Trump alisema kwenye mtandao wa Truth Social.

Haijabainika ikiwa sharti la kujiunga na makubaliano hayo liliainishwa katika maandishi ya makubaliano ya nyuklia — ambayo hayajachapishwa — au ikiwa Saudi Arabia ilikubaliana na sharti hilo.

Mpaka sasa, Saudi Arabia haijatoa maoni yoyote kuhusiana na kauli hizo za Trump.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani Karoline Leavitt siku ya Alhamisi alisema kwambaTrump alikuwa amejadili sharti hilo na viongozi wa Saudi Arabia mara kadhaa hapo awali.

"Amesema kwamba wasipojiunga na Makubaliano ya Abraham, mpango huo hautafanyika," alisema. "Kwa hivyo, tutaendelea na mazungumzo hayo na wenzetu wa Saudi Arabia huko mbeleni."

Kauli za Trump zinakuja kufuatia ukosoaji kutoka kwa wataalamu kwamba makubaliano kati ya Marekani na Saudi Arabia yaliyotangazwa siku ya Jumatano yanaweza kuleta hatari ya kuenea kwa silaha za nyuklia hapo baadaye katika eneo ambalo tayari halina utulivu.

Baadhi ya wabunge wa Republican na Democratic walitilia shaka makubaliano hayo, ingawa Chama cha Republican cha Trump kinadhibiti mabunge yote mawili (la juu na la chini) na wapinzani wa makubaliano hayo wanaonekana kutokuwa na kura za kutosha kuzuia utekelezaji wake.

Kulingana na Wizara ya Nishati ya Marekani, makubaliano hayo yanajumuisha "makubaliano ya ushirikiano wa nyuklia kwa madhumuni ya amani" na "makubaliano ya pande mbili kuhusu hatua za usalama na udhibiti".

"Kwa pamoja, makubaliano haya mawili yanaweka msingi wa kisheria kwa ushirikiano wa miongo kadhaa na wenye thamani ya mabilioni ya dola, ambao unakuza malengo kadhaa muhimu ya kiuchumi na kimkakati, ikiwa ni pamoja na kuzuia kuenea kwa silaha za nyuklia," ilisema taarifa kutoka wizara hiyo.

Ilisema kuwa makubaliano hayo yatawasilishwa kwa Bunge la Marekani ili yafanyiwe tathmini.

Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) lilisema siku ya Alhamisi kuwa linafahamu mipango ya Marekani na Saudi Arabia kuhusu "makubaliano ya pande mbili ya ushirikiano wa nyuklia kwa matumizi ya kiraia na mpango wa kuiomba IAEA kutekeleza hatua za uhakiki kuhusiana na jambo hili".

"Tunatarajia kupokea ombi la uhakiki huo na kushirikiana na Marekani pamoja na KSA [Ufalme wa Saudi Arabia] katika kuhakikisha utekelezaji wa hatua hizo."

Wakati wa muhula wa kwanza wa Trump kama rais wa Marekani, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Bahrain zilitia saini Makubaliano ya Abraham, hatua iliyopelekea kurejeshwa kwa uhusiano wa kawaida kati ya Israel na mataifa hayo mawili ya Kiarabu—tukio la kwanza la aina hiyo katika miongo kadhaa.

Tangu wakati huo, Sudan, Morocco na Kazakhstan nazo pia zimetia saini makubaliano hayo.

Saudi Arabia hapo awali ilisema haitafanya hivyo bila kuanzishwa kwa taifa la Palestina, lakini Ikulu ya Marekani ilisema makubaliano hayo hayatatekelezwa Riyadh isipojiunga nayo.

Israel imekaribisha kauli hiyo ya Trump.

Katika ujumbe kwenye mtandao wa X, ofisi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ilisema kuwa Saudi Arabia kujiunga na makubaliano hayo "itakuwa hatua kubwa ya kihistoria kuelekea amani Mashariki ya Kati".

Taarifa hiyo haikutaja makubaliano ya nyuklia. Hata hivyo, Waziri wa Uchumi wa Israel, Nir Barkat, alisema hapo awali kuwa nchi yake "inaweza kukabiliana na hali hiyo" iwapo Saudi Arabia ingekuwa na uwezo wa nyuklia kwa ajili ya matumizi ya amani.

Wengine walionyesha wlipinga vikali. Waziri wa zamani wa ulinzi wa Israel, Avigdor Lieberman, aliliambia gazeti hilo: "Kila mpango wa kijeshi wa nyuklia huanzia na mpango wa kiraia."

Israel yenyewe inaaminika kuwa na silaha za nyuklia, lakini haijawahi kuthibitisha wala kukanusha hilo.

Makubaliano hayo kati ya Marekani na Saudi Arabia yanaelezwa na Wizara ya Nishati ya Marekani kama "makubaliano ya ushirikiano wa nyuklia kwa ajili ya amani" ambayo yataziwezesha "kampuni za Marekani kupata fursa kubwa katika mpango wa nishati ya nyuklia wa Saudi Arabia".

Suala la nyuklia limekuwa kiini cha mzozo wa miezi kadhaa kati ya Marekani na Israel kwa upande mmoja na Iran kwa upande mwingine; Iran imekuwa ikikanusha kwa miaka mingi madai ya mataifa ya Magharibi kwamba inalenga kumiliki silaha za nyuklia.

Mtawala wa Saudi Arabia, mrithi wa ufalme Mohammed bin Salman, aliambia shirika la habari la CBSbmwaka wa 2018 kwamba taifa lake halikuwa na mpango wa kumiliki silaha za nyuklia, lakini kwamba "bila shaka yoyote, iwapo Iran ingetengeneza bomu la nyuklia, nasi tungefanya vivyo hivyo haraka iwezekanavyo".

Awali, ripoti za vyombo vya habari vya Marekani ziliashiria kuwa makubaliano hayo yangeiruhusu Saudi Arabia kurutubisha urani hapo baadaye—jambo linaloweza kutumika kama nishati kwa mitambo ya kuzalisha umeme, lakini pia linaweza kutumika kutengeneza mabomu ya nyuklia. Hata hivyo, kauli za Trump zinaonekana kupinga jambo hilo.

Rosemary Kelanic, mkurugenzi wa mpango wa Mashariki ya Kati katika taasisi ya uchambuzi ya Defense Priorities yenye makao yake nchini Marekani, alisema ingekuwa jambo la "kushangaza sana" Marekani ingeiruhusu Saudi Arabia kuwa na mitambo ya kurutubisha urani.

"Marekani haijawahi kufanya hivyo hapo awali. Hatujawahi kusaidia nchi nyingine kurutubisha urani katika ardhi yake," alisema, huku akiongeza kuwa hii ni kwa sababu "ikiwa unaweza kuzalisha nishati yako mwenyewe ya nyuklia, huenda ukaamua" kutengeneza silaha za nyuklia.