Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Iran yaanzisha mashambulizi mapya Bahrain, Jordan, Erbil

Iran imetekeleza mashambulizi kwa kutumia ndege zisizo na rubani dhidi ya Kuwait,Bahrain na Jordan huku safari za ndege zikisitishwa kwa muda katika uwanja wa ndege wa Erbil nchini Iraq.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Lizzy Masinga & Beldeen Waliaula

  1. Maelfu ya watu wakimbia moto wa nyika Ufaransa na Uhispania

    Maelfu ya watu wamekimbia moto mkubwa wa nyika magharibi mwa Ufaransa kwa kutumia magari na boti,huku Uhispania ikitangaza hali ya dharura ya kitaifa kutokana na moto uliotokea nje ya mji mkuu wa Madrid.

    Mamlaka za Ufaransa ziliamuru kuhamishwa kwa watu wote kutoka rasi ya Cap Ferret, eneo maarufu la utalii katika pwani ya Atlantiki.

    Mataifa yote mawili yameomba msaada kutoka Umoja wa Ulaya baada ya moto huo kuathiri uwezo wa vikosi vya wazima moto na watoa huduma za dharura.

    Soma pia:

  2. UN yataka mabaharia waliokwama katika Mlango bahari wa Hormuz warejeshwe nyumbani

    Umoja wa Mataifa umetaka nchi zinazohusika katika vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati kushirikiana kuhakikisha mabaharia wapatao 6,000 waliokwama katika Mlango bahari wa Hormuz wanaondolewa kwa njia salama na kurejeshwa makwao.

    Kamishna mkuu wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu, Volker Türk, ametoa wito wa hatua za haraka kuchukuliwa ilikushughulikia hali ya maelfu ya mabaharia hao, akisema wanakabiliwa na "mgogoro mkubwa wa kibinadamu” katika eneo hilo la bahari.

    Awali, kabla ya kuzuka upya kwa mapigano kati ya Iran na Marekani, Shirika la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Bahari (IMO) lilitangaza kuwa angalau mabaharia 6,000 waliokuwa ndani ya mamia ya meli walikuwa wamekwama katika Mlango bahari wa Hormuz.

    Mabaharia hao bado hawajaweza kuondoka eneo hilo wala kurejea makwao, hali ambayo imeendelea kuzua wasiwasi wa kibinadamu.

    Soma pia:

  3. Mahakama yasitisha kwa muda mchakato wa kumuondoa Ramaphosa madarakani

    Mahakama Kuu ya Western Cape nchini Afrika Kusini imempa afueni Rais Cyril Ramaphosa, kwa kusitisha kwa muda mchakato wa kamati ya bunge, ya kumuondoa madarakani.

    Mahakama hiyo imesema kesi ya Ramaphosa ya kupinga uhalali wa ripoti iliyobaini kuwa anaweza kuwa na mashtaka ya kujibu kuhusu mwenendo wake, lazima isikilizwe kwanza mwezi Septemba kabla ya mchakato wa kumuondoa madarakni kuendelea.

    Kesi hiyo inahusu namna Rais Ramaphosa alivyoshughulikia wizi wa takriban dola 580,000 za Marekani uliotokea mwaka 2020 katika shamba lake la Phala Phala

    Jopo la majaji watatu lilisikiliza kesi hiyo. Majaji wawili waliunga mkono ombi la Ramaphosa la kusitisha kwa muda shughuli za kamati ya bunge, huku jaji mmoja akitaka ombi hilo litupiliwe mbali.

    Kutokana na uamuzi wa wengi, mchakato wa uchunguzi wa bunge kuhusu uwezekano wa kumuondoa rais huyo madarakani hautaendelea, hadi kesi yake nyingine itakapomalizika.

    Ramaphosa amekuwa akikanusha mara kwa mara kufanya kosa lolote na amesisitiza kwamba hatajiuzulu kutokana na sakata hilo maarufu kama ‘Farm Gate’, tangu ilipobainika kuwa alikuwa na kiasi hicho cha fedha za kigeni, ambazo hakuwa ametangaza rasmi, na baadaye zikaibiwa katika shamba lake mwaka wa 2020.

    Rais huyo alijitetea kuwa dola 580,000 za Marekani zilizokuwa zimefichwa katika nyumba yake ya kifahari kwenye shamba la Phala Phala, mkoani Limpopo, kaskazini mwa Afrika Kusini, zilikuwa mapato yaliyotokana na mauzo ya nyati.

    Soma pia:

  4. Wakimbizi raia wa DRC wanoishi Burundi wakumbwa na uhaba wa chakula

    Na Robert Kiptoo

    BBC Nairobi

    Zaidi ya wakimbizi laki moja na thelathini walioko nchini Burundi, wengi wao waliokimbia machafuko na mapigano mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wanakabiliwa na hatari ya ukosefu wa chakula katika miezi ijayo

    Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, limeonya kuwa linahitaji dola milioni 35 za Marekani ili kuendelea kuwapatia chakula na huduma za lishe wakimbizi hao hadi Agosti mwaka ujao.

    WFP imesema kuwa maelfu ya wakimbizi hao wanaoishi katika kambi za muda nchini Burundi kwa sasa wanaishi kwa lishe moja kwa siku huku baadhi wakikosa chakula.

    WFP imesema kuwa bila ufadhili mpya, ugawaji wa chakula unaweza kusitishwa kabisa kuanzia mwezi Oktoba mwaka huu.

    Wengi wa wakimbizi hao walifika Burundi wakitafuta usalama, mlo wa siku na mahali pa kuishi. Lakini sasa msaada huo ambao umekuwa tegemeo lao kuu uko hatarini kutoweka kabisa.

    Tayari upungufu wa fedha umeilazimu shirika hilo la WFP kupunguza mgao wa chakula kwa wakimbizi wengi. Shirika hilo linaonya kuwa ikiwa msaada utasitishwa kabisa, njaa itaongezeka, utapiamlo utakuwa mkubwa zaidi miongoni mwa wakimbizi hao hasa watoto na kina mama.

    Mwishoni mwa mwaka uliopita, kuongezeka kwa mapigano mashariki mwa Congo kulisababisha zaidi ya watu laki moja kukimbilia Burundi.

    Soma pia:

  5. Jurgen Klopp ateuliwa kuwa kocha mkuu wa Ujerumani

    Baada ya timu ya taifa ya Ujerumani kushindwa katika Kombe la Dunia baada ya kufungwa na Paraguay kwa mikwaju ya penalty, kocha mkuu wa timu hiyo Julian Nagelsmann alijiuzulu.

    Wiki tatu tu baadaye, Jurgen Klopp ametwikwa jukumu la kurejesha timu ya Ujerumani katika hadhi yake ya awali.

    Klopp ametia Saini mkataba wa miaka minne wa kuwa kocha mkuu wa timu ya Ujerumani kwa miaka minne.

    Kocha huyo ataiongoza timu hiyo katika fainali za Euro 2028 na Kombe la Dunia la 2030, huku mechi yake ya kwanza akiwa kocha wa Ujerumani ikitarajiwa kuwa dhidi ya Uholanzi tarehe 24 mwezi Septemba.

    Klopp, ambaye ametwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na Ligi Kuu ya England akiwa na Liverpool, pamoja na mataji mawili ya Bundesliga akiwa na Borussia Dortmund, tayari anahesabiwa kuwa mmoja wa makocha bora zaidi katika historia ya soka la Ujerumani.

    Soma pia:

  6. Iran yaishambulia Kuwait, Jordan na Bahrain

    Iran imesema imeshambulia vituo vya kijeshi vya Marekani vilivyoko Mashariki ya Kati kwa kutumia ndege zisizo na rubani.

    Iran imesema mashambulizi hayo ni ya kulipiza kisasa mashambulizi ya Marekani dhidi ya taifa hilo ambayo yamedumu sasa kwa siku 13 mfululizo.

    Awali milipuko iliripotiwa katika maeneo ya pwani ya Ghuba ya Uajemi nchini Iran, pamoja na maeneo ya magharibi, kaskazini na katikati mwa nchi hiyo. Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali ya Iran, watu wanne wameuawa na wengine watano kujeruhiwa katika shambulio lililotokea kusini magharibi mwa taifa hilo.

    Kwa kujibu shambulio hilo Iran ilianzisha mashambulizi dhidi ya Kuwait, mshirika wa Marekani, huku ving'ora vya tahadhari vikisikika nchini Bahrain na Jordan. Safari za ndege pia zilisitishwa katika uwanja mkubwa wa ndege nchini Iraq kufuatia taarifa za kuanguka kwa droni karibu na eneo hilo.

    Hatua ya Iran imejiri wakati taifa hilo imekuwa ikilaani mpango wa Marekani wa kutumia mali za Iran zilizozuiliwa kufidia uharibifu uliosababishwa na vita, jambo linaloashiria kuongezeka kwa mvutano kati ya mataifa hayo mawili.

    Hapo jana, Rais wa Marekani Donald Trump alisema kuwa fidia ya uharibifu uliosababishwa kwa meli za mizigo katika Mlango bahari wa Hormuz italipwa kwa kutumia "fedha za Iran ambazo zinadhibitiwa na Marekani."

    "Uharibifu huu unaweza kuwa mkubwa sana, lakini huo ndio utaratibu wa haki na usawa," Trump aliandika kwenye mtandao wake wa Truth Social.

    Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran, Abbas Araghchi, alijibu kwa kusema kuwa, kunyakua mali za taifa lingine ili kulipia madai yasiyohusiana ni "kuchochea migogoro zaidi."

    Soma pia:

  7. Uingereza imesemema iko tayari kujilinda baada ya Iran kusema kuwa kambi zake ni ‘maeneo halali' kushambuliwa

    Serikali ya Uingereza imesema iko tayari kujilinda saa 24 kwa siku, baada ya Iran kutangaza kuwa kambi za kijeshi za Uingereza zinazotumiwa na Marekani ni malengo halali ya kushambuliwa.

    Uingereza imeiruhusu Marekani kutumia vituo vya kijeshi vya Uingereza vinavyohifadhi wanajeshi na ndege za Marekani kwa shughuli ilizozieleza kuwa za kujilinda, huku ikikataa kushiriki katika mashambulizi ya moja kwa moja dhidi ya Iran.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeituhumu Uingereza kuwa mshirika wa Marekani katika vita hivyo, huku Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kikisema kuwa nchi yoyote itakayoiunga mkono Marekani kijeshi itabeba matokeo ya hatua hizo.

    Kauli hiyo imekuja wakati Marekani ikiendelea na usiku wa 13 mfululizo wa mashambulizi dhidi ya malengo mbalimbali nchini Iran.

    Rais wa Marekani Donald Trump amekuwa akiikosoa serikali ya Uingereza na aliyekuwa Waziri Mkuu Sir Keir Starmer, akidai hawajaunga mkono vya kutosha kampeni ya kijeshi ya Marekani.

    Hata hivyo, Iran imeendelea kuichukulia Uingereza kama sehemu ya operesheni hiyo ya kijeshi.

    Mwezi Machi, wakati wa siku za mwanzo za vita vinavyoongozwa na Marekani na Israel dhidi ya Iran, Uingereza iliruhusu Marekani kutumia vituo vya kijeshi vya RAF Fairford na Diego Garcia kushambulia miundombinu ya kijeshi ya Iran iliyodaiwa kutumika kushambulia mataifa ya Ghuba na meli katika Mlango bahari wa Hormuz.

    Kwa mujibu wa taarifa, sera hiyo imeendelea hata baada ya Andy Burnham kuwa Waziri Mkuu mpya wa Uingereza, kufuatia uamuzi wa kuongeza muda wa makubaliano hayo na Marekani.

    Katika taarifa iliyochapishwa na shirika la habari la Tasnim, linalohusishwa na IRGC, kundi hilo lilidai kuwa ndege za Marekani ziliondoka katika kambi ya RAF Fairford siku mbili kabla kutekeleza mashambulizi dhidi ya Iran.

    Unaweza kusoma;

  8. Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dodoma akabiliwa na shtaka la ugaidi

    Sakata la kisheria linalomkabili mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Melkisedeki Kaijage, limechukua mkondo mpya baada ya upande wa mashtaka kubadilisha shtaka lake na kumfungulia kesi ya ugaidi, The Citizen limeripoti.

    Bw. Kaijage amekuwa akishikiliwa na polisi tangu Julai 8, 2026, baada ya kukamatwa kwa tuhuma za kuchochea maandamano ya umma, kosa ambalo awali halikuruhusu dhamana.

    Kutokana na hali hiyo, Chama cha Wafanyakazi wa Taaluma cha UDOM (UDOMASA) kiliwasilisha maombi ya kumtaka apewe dhamana, ambayo yalisikilizwa Jumanne, Julai 21, 2026.

    Baada ya mahakama kutoa mwongozo uliowezesha mchakato wa dhamana kufuatia shtaka la awali la uchochezi, mawakili wa utetezi pamoja na viongozi wa UDOMASA walipoanza kukamilisha taratibu za kuachiwa kwake, mamlaka zilibadilisha shtaka hilo.

    Mwenyekiti wa UDOMASA, Dk. Gerald Shija, alisema Bw. Kaijage sasa anakabiliwa na shtaka la ugaidi, ambalo halina dhamana, na amehamishwa kutoka mahabusu ya polisi kwenda Gereza la Isanga.

    "Jana tulipata taarifa kwamba Bw. Kaijage amepelekwa mahakamani. Tulipofika, tulibaini tayari alikuwa amewekwa rumande kwa shtaka jipya la ugaidi," alisema Dk. Shija.

    Shtaka hilo jipya linaweka vikwazo vikubwa vya kisheria kwa familia yake na wenzake katika jitihada za kumtoa kwa dhamana.

    Kwa mujibu wa wenzake, Bw. Kaijage anafahamika kama mhadhiri anayependwa na wanafunzi na mwenye uhusiano mzuri nao, hali ambayo wanaieleza kuwa inatokana na mbinu zake za ufundishaji zinazowavutia wanafunzi, badala ya shughuli za uhamasishaji wa kisiasa.

  9. Watatu wahukumiwa kifungo cha maisha jela kwa utekaji wa wanafunzi Nigeria

    Wanaume watatu nchini Nigeria wamehukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kukiri makosa yanayohusiana na utekaji wa makumi ya wanafunzi na walimu katika jimbo la Oyo, kusini-magharibi mwa nchi.

    Watuhumiwa hao walikiri kuficha taarifa kuhusu watu waliohusika na mashambulizi hayo, na pia kukubali kuwa wanachama wa kundi linalohusishwa na Boko Haram.

    Hukumu hiyo imekuja karibu wiki mbili baada ya mamlaka kutangaza kuwa wanafunzi na walimu 44 waliotekwa nyara katika mashambulizi ya kuratibiwa dhidi ya shule tatu wilayani Oriire mwezi Mei waliokolewa.

    Matukio hayo ya utekaji yalisababisha maandamano kutoka kwa wazazi, vyama vya walimu na mashirika ya kutetea haki za binadamu, ambayo yalitaka serikali kuimarisha usalama wa shule.

    Katika miaka ya hivi karibuni, utekaji wa watu kwa ajili ya kudai fidia umekuwa ukiongezeka nchini Nigeria, huku makundi yenye silaha yakilenga maeneo yenye ulinzi hafifu kama vile shule, makanisa, misikiti na vijiji vya mbali.

    Nigeria inaendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali za kiusalama, zikiwemo magenge ya wahalifu yanayojulikana kama "bandits", ambayo hujihusisha na uporaji na utekaji wa watu kwa ajili ya kudai fidia.

    Nchi hiyo pia inakabiliwa na uasi wa makundi ya wanamgambo wa Kiislamu, migogoro ya ardhi kati ya jamii mbalimbali, pamoja na machafuko yanayochochewa na makundi yanayotaka kujitenga katika baadhi ya maeneo ya nchi.

  10. Trump: 'Tutagharamia uharibifu wa meli kwa kutumia mali za Iran zilizozuiliwa nchini Marekani'

    Rais wa Marekani Donald Trump aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa Truth Social siku ya Alhamisi jioni: "Taarifa hii ichukuliwe kuwa tangazo rasmi hadi hapo taarifa nyingine itakapotolewa kwamba, kuanzia sasa na kuendelea, uharibifu wowote kwa meli, mizigo, au chochote kinachohusiana navyo, utalipwa kwa kutumia mali za Iran zinazomilikiwa na kudhibitiwa na Marekani.

    Uharibifu huo unaweza kuwa mkubwa sana, lakini hata hivyo, huu ndio uamuzi wa haki na usawa zaidi."

    Hata hivyo, matumizi ya mali za Iran zilizopo Marekani yanahitaji idhini ya mamlaka za kisheria na mahakama.

    Katika kesi zilizopita, kama vile maombi kutoka kwa manusura wa mashambulizi ya kigaidi ambayo Iran iliyaunga mkono au kuhusika nayo, mahakama za Marekani mara kwa mara zimeamua dhidi ya Iran na kusema kuwa haina haki ya kisheria ya kuamua kesi za aina hiyo.

    Bw. Trump pia aliwaambia waandishi wa habari siku ya Alhamisi kuwa huenda akaamuru shambulio kubwa sana dhidi ya Iran siku ya Ijumaa asubuhi, shambulio ambalo rais huyo wa Marekani alilielezea kuwa "lisiloweza kulinganishwa" na mashambulizi ya awali.

  11. Marekani yatoza ushuru kwa mataifa kadhaa ya washirika wa biashara

    Marekani imetangaza ushuru mpya kwa washirika wake 60 wa kibiashara, wanaowakilisha sehemu kubwa ya bidhaa zinazoingizwa nchini humo, kwa madai kwamba hawajachukua hatua za kutosha kukomesha ajira za kulazimishwa.

    Ushuru huo, unaoanzia asilimia 10 hadi 12.5, unazihusu nchi na maeneo muhimu ya kiuchumi, ikiwemo Uingereza, China, Umoja wa Ulaya, Canada, Japan na India.

    Unaanza kufanya kazi Ijumaa, baada ya ushuru wa muda wa asilimia 10 uliowekwa mapema mwaka huu kumalizika.

    Hatua hiyo ni mwendelezo wa mvutano wa vita vya kibiashara uliochochewa tena na Rais wa Marekani Donald Trump baada ya kurejea madarakani mwaka jana.

    Mapema mwaka huu, Mahakama Kuu ya Marekani iliamua kuwa ushuru mwingi uliowekwa duniani chini ya mamlaka ya dharura ulikuwa umeanzishwa kinyume cha sheria.

    Tangu uamuzi huo, Trump amekuwa akitafuta njia nyingine za kutekeleza sera yake kuu ya biashara.

    Mwezi uliopita, Ikulu ya Marekani ilipendekeza ushuru wa asilimia 10 hadi 12.5 kwa bidhaa kutoka mataifa kadhaa, ikidai hayafanyi juhudi za kutosha kukabiliana na ajira ya kulazimishwa.

    Siku ya Alhamisi, Mwakilishi wa Biashara wa Marekani, Jamieson Greer, alisema ushuru huo utaanza kutekelezwa kwa maelekezo ya Rais Trump.

    Katika taarifa yake alisema hatua hiyo italenga kurekebisha ukiukwaji wa haki za binadamu na biashara isiyo ya haki, huku ikilenga kuboresha ustawi wa wafanyakazi duniani.

    Ushuru huo mpya utawahusu washirika 60 wakuu wa biashara wa Marekani, ambao kwa pamoja wanachangia asilimia 99.4 ya bidhaa zote zinazoingizwa nchini humo, kwa mujibu wa mamlaka za Marekani.

    Ofisi ya Mwakilishi wa Biashara wa Marekani ilisema kuwa Rais Donald Trump ameifanya marufuku ya uagizaji wa bidhaa zinazozalishwa kwa kutumia ajira ya kulazimishwa kuwa sehemu muhimu ya makubaliano ya biashara ya pande mbili na mataifa mengine.

    Kwa mujibu wa ofisi hiyo, hadi sasa washirika 10 wa kibiashara wamekubali kuweka marufuku hiyo katika makubaliano yao na Marekani, huku mataifa mengine yakichukua hatua kama hizo kufuatia uchunguzi uliofanywa katika wiki za hivi karibuni.

    Mataifa ambayo yameahidi kutunga na kutekeleza kikamilifu marufuku ya bidhaa zinazotokana na ajira ya kulazimishwa yatatozwa ushuru wa asilimia 10. Nchi ambazo hazijatoa ahadi hiyo zitatozwa ushuru wa juu zaidi wa asilimia 12.5.

    Mwakilishi wa Biashara wa Marekani, Jamieson Greer, alisema ameridhishwa na hatua za haraka zilizochukuliwa na baadhi ya washirika wa biashara kupiga marufuku bidhaa zinazozalishwa kwa ajira ya kulazimishwa, na akaeleza kuwa anatarajia kuhakikisha hatua hizo zinatekelezwa ipasavyo.

    Unaweza kusoma;

  12. Mlinzi wa J.D. Vance asimamishwa kazi kwa kuvujisha taarifa nyeti

    Shirika la Ulinzi wa Viongozi wa Marekani (US Secret Service) limetangaza kuwa mmoja wa maafisa wa kikosi cha ulinzi cha Makamu wa Rais J.D. Vance amesimamishwa kazi na anachunguzwa kwa madai ya kuvujisha taarifa nyeti.

    Maelezo kuhusu taarifa hizo zinazodaiwa kuvujishwa hayajawekwa wazi, lakini Anthony Guglielmi, msemaji wa shirika hilo, alisema afisa huyo anakabiliwa na uwezekano wa uchunguzi wa kijinai kuhusiana na madai ya kuhatarisha usalama wa operesheni na taarifa.

    "Tabia yoyote inayoweza kuhatarisha usalama wa mtu anayelindwa haitavumiliwa," aliongeza. Ikulu ya Marekani imekataa kutoa maoni kuhusu uchunguzi huo.

    Hata hivyo, mtandao wa MS Now uliripoti wiki iliyopita, ukirejelea vyanzo vinavyofahamu suala hilo, kwamba baadhi ya wanachama wa kikosi cha ulinzi cha Bw. Vance hawakuridhishwa na safari za familia yake. CNN iliripoti kuwa kusimamishwa kazi kwa afisa huyo kulihusiana na kuchapishwa kwa ripoti hiyo.

    Kulingana na MS Now, baadhi ya maafisa walikuwa wameonyesha kutoridhika katika majadiliano ya ndani kuhusu mipango ya safari za familia ya J.D. Vance, ikiwa ni pamoja na safari iliyopangwa ya helikopta ya kijeshi kumpeleka mtoto mdogo wa Makamu wa Rais kwenye mazoezi ya gofu, pamoja na safari za familia yake kutafuta nyumba katika eneo la Washington, D.C. BBC bado haijaweza kuthibitisha ripoti hizi kwa njia huru.

  13. Mataifa ya Kiarabu yapinga kuingia msikiti Al Aqsa kwa waziri wa Israel mwenye msimamo mkali

    Nchi nane za Kiarabu na Kiislamu zimelaani vikali kuingia kwa waziri wa Israel na walowezi katika Msikiti wa Al-Aqsa kupitia taarifa ya pamoja.

    Mawaziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia, Falme za Kiarabu (UAE), Jordan, Misri, Qatar, Uturuki, Pakistan, na Indonesia walitoa taarifa ya pamoja wakilaani vikali kitendo cha Itamar Ben-Gvir, Waziri wa Usalama wa Taifa wa Israel, na walowezi wa Israel kuingia katika Msikiti wa Al-Aqsa.

    Taarifa hiyo, iliyotolewa jioni ya Alhamisi, Agosti 2, ilieleza kuwa kitendo hiki ni ukiukaji wa wazi wa hali ya kihistoria na kisheria ya Msikiti wa Al-Aqsa na uchokozi usiokubalika ambao unaweza kusababisha kuongezeka kwa mivutano katika eneo hilo.

    Nchi hizo nane pia zilisisitiza yafuatayo:

    Haja ya kuheshimu mamlaka ya usimamizi ya Jordan juu ya maeneo matakatifu ya Kiislamu na Kikristo mjini Jerusalem;

    Kupinga jaribio lolote la kubadilisha hadhi ya kihistoria na kisheria ya Msikiti wa Al-Aqsa;

    Haja ya kusitisha vitendo vya uchokozi na vya upande mmoja ambavyo vinaweza kuhatarisha usalama na utulivu wa eneo hilo;

    Kuzingatia sheria za kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa kuhusu Jerusalem. Taarifa hiyo ilitolewa baada ya Itamar Ben-Gvir kuingia katika eneo la Msikiti wa Al-Aqsa akiwa na mamia ya walowezi wa Israel, kitendo ambacho kimelaaniwa vikali na Wapalestina, Jordan, pamoja na nchi kadhaa za Kiarabu na Kiislamu.

  14. Mashambulizi ya Wahouthi yazua hofu ya mzozo mpana zaidi Mashariki ya Kati na uharibifu wa uchumi duniani

    Wapiganaji wa kundi la Houthi nchini Yemen wanadai kushambulia meli katika Bahari ya Shamu, hatua inayotishia kuzidisha hali tete tayari iliyopo Mashariki ya Kati.

    Kwa kulazimisha meli kurejea nyuma kutoka kwenye mlango mwembamba wa bahari wa Bab el-Mandeb, wametishia kukatiza njia kuu ya usafiri wa baharini inayounganisha Ulaya na Asia.

    Haya yanajiri huku mashambulizi kati ya Marekani na Iran yakiendelea, na wakati ambapo makubaliano ya kuendeleza sekta ya nyuklia ya Saudi Arabia yakizua hofu ya mbio za silaha.

    Kwa sasa, mwaka wa 2026 unadhihirika kwa masikitiko kuwa mmoja wa miaka yenye vurugu na machafuko makubwa kwa baadhi ya maeneo ya Mashariki ya Kati.

    Kwa usiku 13 mfululizo, Kamandi Kuu ya Marekani (Centcom) imefanya mashambulizi ya anga dhidi ya Iran.

    "Vituo vya amri ya kijeshi vya Iran, ghala za kuhifadhia ndege zisizo na rubani (drones), mitandao ya mawasiliano, vituo vya ufuatiliaji wa pwani, na uwezo wa kijeshi wa baharini ili kudhoofisha zaidi tishio linaloletwa na Iran kwa mabaharia raia na meli za kibiashara zinazopita katika Mlango-Bahari wa Hormuz," ilisema Centcom katika taarifa yake usiku wa Alhamisi.

    Nchi za Kiarabu za Ghuba ambazo kwa kawaida ni maeneo tulivu yenye uhalifu mdogo na kodi nafuu sasa zinapaswa kujifunza kuishi huku zikikabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa jirani yao mwenye silaha nyingi ng'ambo ya bahari: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

  15. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja