Nani analinda fedha za umma Tanzania?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Ukiona barabara mbovu, hospitali hakuna dawa, watoto wanakaa chini shuleni, wengi huuliza, zile trilioni zilizokusanywa za kodi na mikopo ziko wapi? au zinachotwa? mbona barabara hazitengenezwi? Maswali haya yanazunguka aina ya mijadala hii, inapofika kwenye fedha za umma.

Kwa wananchi, fedha za umma ni kitu kisichoonekana, lakini matokeo yake yanaonekana, anaipima kwa kuona barabara ya mtaani kwakwe ni nzuri inapitika, hospitali anaiona na huduma bora zipo, shule na huduma nyingine za kijamii zinazomzunguka. Lakini sio takwimu za fedha husika.

Sasa mjadala kuhusu usimamizi wa fedha za umma umeibuka tena upya Tanzania, baada ya kauli ya aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, kuhusu tuhuma za baadhi ya viongozi kujilimbikizia mali.

Serikali ya Tanzania ilipoulizwa tuhuma hizo, Msemaji wake Gerson Msigwa akasema "Nchi yetu inasheria, kama kuna mtu anafanya makosa kwenye rasilimali za taifa, anafikishwa mbele ya mikono ya sheria na anachukuliwa hatua".

Lakini nyuma ya kauli na majibu haya, kuna ukweli mpana zaidi wa kiuchumi na kifedha, kwamba fedha za umma ni rasilimali chache zinazotakiwa kugawanywa kwa mahitaji mengi yanayozidi uwezo wa nchi, na zinapaswa kulindwa zaidi.

Katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026 pekee, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilikusanya shilingi trilioni 28 (takribani dola bilioni 10), ikiwa ni zaidi ya lengo la shilingi trilioni 26.7, huku walipakodi wapya zaidi ya 900,000 wakisajiliwa katika kipindi hicho.

Lakini kadri trilioni zaidi zinavyoingia kwenye hazina ya nchi, ndivyo matarajio ya wananchi yanavyoongezeka na ndivyo hoja ya nani anazilinda fedha hizi, inapata mashiko.

Kwa nini kila shilingi ya umma ni muhimu?

"Ubadhirifu wa fedha za umma maana yake nini? Kwa lugha rahisi kabisa ni matumizi ya fedha za Umma zinazotumika kinyume na mipango iliyopangwa na matarajio," anasema Ndege Makula, mchambuzi wa masuala ya siasa na uchumi.

Makula anaongeza: "Katika uchumi kuna kitu kinaitwa efficiency (matumizi bora na yenye tija ya rasilimali zilizopo) , na scarcity (uhaba wa rasilimali). Kwa sababu rasilimali ni chache na mahitaji ni mengi, tunalazimika kupanga matumizi kwa umakini ili kila kilichopo kiweze kutumika kwa manufaa makubwa zaidi."

Kwa Tanzania, mapato ya Serikali yanatokana zaidi na kodi, mapato yasiyo ya kodi pamoja na mikopo ya ndani na nje. Fedha hizi huingia kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali kabla ya kugawanywa kwenye huduma za kijamii na miradi ya maendeleo.

Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Juma Mwenda, anasema mafanikio ya ongezeko la mapato yanayoonekana sasa Tanzania, yamechangiwa na ufanisi wa mifumo ya kodi na kuongezeka kwa utii wa sheria za mapato.

Makamu wa rais mstaafu Rais Dkt. Philip Mpango aliwahi kuonya muda mfupi kabla ya kustaafu: "Pamoja na kuanzishwa kwa mifumo ya kukusanyia mapato kama GePG, TAUSI na usajili wa mashine za POS, bado kuna upotevu mkubwa wa fedha za Serikali kama ambavyo ripoti za CAG za kila mwaka zinaonesha."

Kauli hiyo inaweka wazi mjadala muhimu unaoendelea kuhusu namna fedha za umma zinavyosimamiwa baada ya kukusanywa.

Ripoti za kila mwaka za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zinaonyesha changamoto mbalimbali ikiwemo matumizi yasiyo na tija, udhaifu katika usimamizi wa mikataba, na madeni ya muda mrefu katika baadhi ya taasisi za umma.

Ingawa sehemu kubwa ya bajeti hutumika kama ilivyopangwa, ipo sehemu ndogo inayonyooshewa kidole kuhusu ufanisi wa kila shilingi ya mlipa kodi.

Kwa mwananchi wa Kashenye (Kagera), Sirari (Tarime, Mara), au Horohoro (Mkinga, Tanga) yeye anatafsiri rahisi kwa lugha ya macho: mradi unaochelewa, huduma isiyo kamilika, au rasilimali inayoweza kutumika mahali pengine.

Imani ya wananchi kuhusu fedha zao

Oscar Mkude, mchambuzi wa siasa na uchumi, anasema changamoto si kuwepo kwa ripoti za ukusanyaji wa mapato au ukaguzi wa fedha za umma, bali hatua zinazochukuliwa baada ya ripoti hizo kutoka.

"Watanzania wanatamani kuona zaidi ya kinachotokea. Sasa hivi wanaona hakitoshi, imani yao inakuwa na mashaka," anasema. Kwa mtazamo wake, uwazi wa hatua za uwajibikaji ndio unaoweza kurejesha imani ya wananchi kwamba fedha zao zinasimamiwa ipasavyo.

Ingawa si mara zote, hatua zimewahi kuchukuliwa. Mwaka 2022, Rais Samia Suluhu Hassan alimsimamisha kazi aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Deusdedit Kakoko, kupisha uchunguzi baada ya Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kubaini ubadhirifu bandarini.

"Kuna ubadhirifu mkubwa Bandarini, naomba TAKUKURU ikafanye kazi. Nimeletewa ripoti ya ubadhirifu wa bilioni 3.6," alisema Rais Samia.

Hivi karibuni akiwa mkoani Singida, Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba alisema; "Nitashughulika na mchwa wanaokula fedha kwenye halmashauri zetu. Tunataka fedha za wananchi zitumike kujenga shule, vituo vya afya, barabara na miradi mingine ya maendeleo, si kugawanywa na wachache".

Kwa upande mwingine, Serikali imeendelea kusisitiza kuwa Tanzania ina mfumo wa sheria na taasisi za uwajibikaji, na kwamba kila anayehusishwa na matumizi mabaya ya rasilimali za umma huchunguzwa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria. Lakini wachambuzi wanasema uwajibikaji hauwezi kutegemea Serikali pekee.

Wakili wa kujitegemea Steven Msechu anasema bado kuna changamoto katika ushiriki wa wananchi. Kwa maoni yake, mwananchi hawezi kutoa taarifa kwa ufanisi kuhusu mali zinazodaiwa kutotangazwa na viongozi ikiwa hana fursa ya kuziona taarifa hizo. "Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma imenyimwa kupata taarifa za ukweli kutoka kwa wananchi. Kuna urahisi gani mwananchi kulifikia daftari la mali za viongozi ili aweze kusema kwamba kiongozi fulani hajazitaja mali zake?" anahoji.

Mtazamo huo unaendana na maoni ya wataalamu wa usimamizi wa fedha za umma Joseph Dalibon na Jean-Philippe Vion, wanaosema mfumo imara wa fedha za umma haujengwi na sheria pekee, bali pia na taasisi huru, ushiriki wa wananchi, mahakama zenye uhuru na matumizi ya teknolojia kuongeza uwazi. Dalibon anasema, "Mfumo imara wa fedha za umma unategemea sheria zilizo wazi zinazohakikisha uwazi, usawa na uwajibikaji. Bila hivyo, rasilimali za umma huathirika kupitia rushwa, uzembe na kuporomoka kwa imani ya wananchi."

Kwa Boniface Charles, dereva wa bodaboda jijini Dar es Salaam, mjadala wote kuhusu trilioni zinazokusanywa na Serikali unaishia kwenye huduma anazozipata yeye na familia yake.

"Mimi sihitaji kujua Serikali imekusanya trilioni ngapi. Nataka mtoto wangu akienda hospitali apate dawa. Hapo nitajua kodi yangu imefanya kazi," anasema.

Kauli yake inaakisi matarajio ya walipa kodi wengi nchini. Kwa Tanzania, ulinzi wa fedha za umma hauko kwenye taasisi moja pekee. Unajengwa na mfumo wa sheria unaotekelezwa na Serikali, unaokaguliwa na CAG, unaochunguzwa na vyombo vya uwajibikaji, na unakamilishwa na wananchi wanaohoji, kufuatilia na kudai matokeo.

Kwa sababu mwisho wa safari ya fedha za umma haupaswi kuonekana kwenye vitabu vya hesabu au rekodi za makusanyo pekee, bali kwenye dawa zinazopatikana hospitalini, madarasa yanayojengwa, barabara zinazopita na huduma zinazobadilisha maisha ya wananchi.