Tetesi za Soka: Kane kusalia Bayern, Man City kutema watano

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 2

Nahodha wa England, Harry Kane, 32, anatarajiwa kusaini mkataba mpya na Bayern Munich licha ya kuvutiwa na Barcelona. (Athletic)

Uteuzi wa Enzo Maresca kuwa kocha wa Manchester City unaweza kuanzisha mabadiliko makubwa ya kikosi, huku Rico Lewis, Nathan Aké, Nico González, Rúben Dias na Savinho wakitajwa kuwa miongoni mwa wachezaji wanaoweza kuuzwa. (Mail)

Manchester City wako tayari kutibua mipango ya Tottenham Hotspur ya kumsajili kiungo wa Newcastle United na Italia, Sandro Tonali, 26, licha ya kuwa tayari wamekubaliana kumsajili kiungo wa England, Elliot Anderson, 23, kutoka Nottingham Forest. (Marca)

AC Milan wako tayari kutoa dau la pauni milioni 21.5 kumsajili kiungo wa England, Mason Mount, 27, lakini Manchester United hawana mpango wa kumuuza. (Mail)

Hull City wanakaribia kumsajili kipa wa Rangers, Jack Butland, 33, huku kipa wa Croatia Ivor Pandur, 26, akielekea upande wa pili katika dili la kubadilishana wachezaji litakalomrejesha Butland Ligi Kuu England. (Sun)

Chelsea wanamuona beki wa kushoto wa Rayo Vallecano, Pep Chavarría, 28, kuwa mbadala wa Marc Cucurella, 27, anayetarajiwa kuuzwa kwenda Real Madrid. (Marca)

Kiungo wa Borussia Dortmund na Ujerumani, Felix Nmecha, 25, yuko tayari kukataa ofa kutoka Newcastle United kwa kuwa anatamani zaidi kuhamia Manchester United. (Bild via Sport Witness)

Winga wa Bayern Munich, Michael Olise, anafahamu kuwa klabu kadhaa, zikiwemo Real Madrid na Paris Saint-Germain, zinafuatilia kiwango chake akiwa na Ufaransa kwenye Kombe la Dunia. Mchezaji huyo mwenye miaka 24 anatarajiwa kukutana na Bayern baada ya mashindano hayo kujadili mustakabali wake. (AS)

RB Leipzig wamesema winga wa Ivory Coast, Yan Diomande, 19, atasalia klabuni hapo msimu ujao licha ya taarifa zinazoeleza kuwa amechagua kujiunga na Paris Saint-Germain. (Florian Plettenberg)