Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kombe la Dunia 2026: Jinsi Brazil mpya inavyoimarika na umuhimu wa Cunha
- Author, Lucas Leiva
- Nafasi, BBC
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Kombe la Dunia linazidi kusonga mbele - na nafurahi kusema timu ya Brazil pia inazidi kuimarika. Inaonekana Carlo Ancelotti amepata kikosi bora na tumeimarika katika kila mchezo wa hatua ya makundi.
Brazil inacheza na Japan katika hatua ya 32, huku Matheus Cunha akionekana kuwa ndiye ufunguo wa kiwango kizuri cha Brazil.
Ni jambo la kustaajabisha kidogo, kwa sababu kwa kawaida umma wa Brazil unatarajia mchezaji nambari tisa kuongoza mashambulizi yetu, na Cunha ni tofauti na kile ambacho mashabiki wamekizoea.
Ni mchezaji anayeweza kucheza kama namba tisa, namba kumi na pia kutengeneza nafasi kwa wengine. Na anaweza pia kufunga mabao - ana matatu hadi sasa katika mashindano haya. Na anaipa timu kitu ambacho Brazil hawajawahi kuwa nacho hapo awali.
Nani nambari tisa bora?
Kwa namna fulani, Cunha hunikumbusha mwenzangu wa zamani wa Liverpool, Roberto Firmino kwa jinsi anavyoingia golini, na kumpa mlinzi mashaka kuhusu la kufanya.
Ikiwa mlinzi atamfuata, inawapa nafasi na uhuru Vinicius Jr na Rayan. Ikiwa mlinzi ataondoka na kumwacha Cunha, basi hupanda na mpira na kutoa pasi au kufunga.
Ilikuwa ajabu sana kwa Brazil kuingia katika Kombe la Dunia bila kujua ni nani nambari tisa wetu bora.
Hata wakati wa mchezo na Scotland, hakuna aliyejua nani atakuwa chaguo la kwanza la kuwa mshambuliaji wa kati.
Sidhani kama Ancelotti alijua kabla ya mashindano pia, kwa sababu aliwajaribu Cunha, Igor Thiago, Endrick, Joao Pedro na Richarlison.
Na wakati mwingine majeraha humsaidia meneja kufanya maamuzi. Raphinha ni mchezaji mzuri, lakini anapenda kuzunguka-zunguka sana. Katika mchezo wa kwanza, dhidi ya Morocco, alicheza kama 10 nyuma ya Thiago, na pia anaweza kucheza kwenye winga zote mbili.
Lakini, alipoumia katika misuli ya paja dhidi ya Morocco, nafasi yake ilichukuliwa na Rayan ambaye ni mchezaji anayebaki upande wa kulia.
Kwa hivyo, kuwa na Vini upande mmoja na Rayan upande mwingine kunatoa nafasi zaidi kwa Cunha kuingia katika maeneo anayopenda. Yuko peke yake katikati, na kwa mtindo wake wa uchezaji, hilo linamfaa.
Mambo yanaweza kubadilika. Jambo muhimu ni kwamba Ancelotti ana machaguo mengi na tunasubiri kuona atafanya nini baadaye. Hata hivyo, Brazil watu wengi wanafikiri Cunha ndiye jibu.
'Utambulisho wa Brazil ni kubadilika’
Kila kitu ambacho nimezungumzia hadi sasa ni jukumu la meneja. Jambo bora zaidi kuhusu Ancelotti ni kwamba anaweza kubadilika kulingana na hali.
Amefanya kazi katika ligi nyingi akiwa na vilabu vingi na wachezaji tofauti na kila mara hushinda. Kila mtu huzungumzia kuhusu usimamizi wake na jinsi anavyowapa watu matokeo bora kwa njia hiyo, lakini nadhani wakati mwingine husahau kwamba yeye pia ni mzuri sana kimbinu.
Mojawapo ya mambo niliyoyaona kuhusu Brazil ya Ancelotti ni kwamba hawana wasiwasi kuhusu kumpa mpira mpinzani wao. Sisi si timu inayohitaji kuwa na umiliki wa 70% wakati wote.
Wakati mwingine, ukiipa timu nyingine mpira inakuwa tatizo kwao. Na, ukifika katika nafasi sahihi na kutoa presha kwa wakati unaofaa, na kwa nguvu inayofaa, unaweza kuwaadhibu.
Hilo lilifanya kazi dhidi ya Scotland, kwa bao la kwanza na la pili ambalo lilikataliwa. Na tulifunga mabao kama hayo kabla ya Kombe la Dunia, katika michezo ya kujiandaa, dhidi ya Panama na Misri.
Dhidi ya Scotland tuliwapa mpira na tulikuwa tunawapeleka wachezaji wao mahali tulipotaka wawe.
Hatukuwa na mpira lakini tulikuwa na udhibiti kwa wakati unaofaa, na tulitoa presha. Ni sehemu ya mpango wa Ancelotti kuweka mtego, na ilifanya kazi.
Kama una watu ambao wanaweza kubadilika kama sisi, kwa nini tusibadilike kama timu?
'Hii ni Brazil mpya’
Hii ni Brazil mpya na nadhani tunahitaji kuwa tofauti na timu zetu za zamani.
Simaanishi tunawarudisha watu nyuma, tukilinda na sio kufunga, lakini hii ni Kombe la Dunia la kwanza ambapo hatuna mabeki wa pembeni wanaoshambulia na wanaokwenda mbele sana. Ni tofauti na ilivyokuwa kwa Roberto Carlos, Cafu, Maicon, Marcelo au Dani Alves!
Douglas Santos na Roger Ibanez au Danilo, hubaki sana nyuma, lakini hiyo ni sababu nyingine ambayo Vini inaweza kumfanya kubaki mbele zaidi tunaposhambulia.
Wachezaji wanne wa nyuma wanaonekana imara sana.
Tumehama kutoka mfumo wa 4-2-3-1 hadi 4-3-3. Kwa hivyo, kuna sababu nyingi za kuwa na matumaini mema – kwani katika ulinzi tumeruhusu bao moja pekee hadi sasa, na pia katika mashambulizi tumefunga saba - lakini mwishowe kinachohitajika ni kuendelea kushinda.
Hilo ndilo linalowafanya Brazil watabasamu hadharani, na kwa sasa, wanatabasamu. Kabla ya mchezo wa kwanza kulikuwa na wasiwasi. Hata hivyo, baada ya michezo mitatu, kila mtu ana furaha sana.