Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Urusi yaishambulia Ukraine licha ya kukubali kushiriki katika mazungumzo ya amani

Mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, umeshambuliwa kwa makombora saa chache baada ya Urusi kusema kuwa iko tayari kurejea katika meza ya mazungumzo ya amani.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Beldeen Waliaula

  1. Trump: Hakuna mazungumzo yanayoendelea na Iran,lakini tutapata suluhu hivi karibuni

    Katika taarifa yake ya hivi karibuni, Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa hakuna mazungumzo yanayoendelea na Iran.

    Alipoulizwa na wanahabari iwapo amekata tamaa ya kufanya mazungumzo na Iran, Trump alisema “hatufanyi mazungumzo na Wairani kwa sasa, lakini tutapata suluhisho,hilo litatokea hivi karibuni.”

    Rais huyo aliongezea kuwa “watu wengi wanafikiri kuwa hili litatokea baada ya uchaguzi.”

    Trump alikuwa akirejelea uchaguzi wa katikati ya muhula unaotarajiwa kufanyika nchini Marekani.

    Kauli za Trump kuhusu mazungumzo na Iran zinakuja wakati kiongozi mkuu wa kijeshi wa Pakistan Asim Munir, ambaye amekuwa mpatanishi mkuu katika mzozo wa hivi karibuni kati ya Marekani na Iran, alipozuru Tehran siku ya Jumanne.

    Soma pia:

  2. Serikali na kampuni zaharakisha kulinda tovuti zao baada ya kugunduliwa kwa dosari za kiusalama

    Serikali na baadhi ya kampuni kubwa zaidi duniani, zikiwemo Amazon, zinaharakisha kulinda mifumo yao baada ya kugunduliwa kwa dosari hatari za usalama wa mtandao.

    Dosari hizo zipo katika lugha ya programu iitwayo PHP, inayotumika kuendesha idadi kubwa ya tovuti. Kampuni ya usalama wa mtandao ya Wiz inakadiria kuwa takriban asilimia 70 ya intaneti imeathirika, ingawa BBC haijaweza kuthibitisha kwa njia huru makadirio hayo.

    Nchi kadhaa za Ulaya zimezima baadhi ya huduma za umma zinazopatikana mtandaoni kama tahadhari, huku Wikipedia pia ikiondoa baadhi ya sehemu za tovuti yake kwa muda.

    Hatua hizo zinaendana na ushauri uliotolewa na serikali mbalimbali, zikiwemo za Marekani, wa kuzima tovuti ikiwa dosari hizo haziwezi kurekebishwa mara moja.

    Kampuni ya Wiz, ambayo watafiti wake waligundua dosari hizo, imeitaja kuwa “dosari hatari zaidi kuwahi kugunduliwa na akili unde (AI).”

    Mashirika kadhaa ya usalama wa mtandao yamezitaka taasisi ambazo haziwezi kufanya marekebisho hayo kwa wakati kuzingatia kuzima tovuti zao kwa muda. Hatua hiyo imesababisha taasisi mbalimbali, zikiwemo serikali ya Finland, halmashauri ya Edinburgh na Shirika la Utangazaji la Uingereza BBC, kuziondoa baadhi ya kurasa zao mtandaoni.

    Ikulu ya Marekani imesema mashirika ya serikali yanashirikiana na maabara zinazoongoza katika utafiti wa akili unde ili kuharakisha upatikanaji wa suluhisho la tatizo hilo.

    Soma pia:

  3. Ndege zisizo na rubani zashambulia uwanja wa ndege Saudi Arabia

    Mtu mmoja ameuawa na wengine wanane kujeruhiwa katika shambulio lililotokea hapo jana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa King Fahd mjini Dammam, mashariki mwa Saudi Arabia, kulingana na Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya nchi hiyo

    Hata hivyo, Saudi Arabia haikutaja chanzo cha ndege isiyo na rubani iliyohusika katika shambulio hilo.

    Katika tukio jingine, Wizara ya Nishati ya Saudi Arabia imesema hapo jana kuwa watu wawili waliuawa na wengine wawili kujeruhiwa baada ya mabaki ya ndege isiyo na rubani kuanguka, kufuatia kunaswa kwa ndege hiyo iliyokuwa ikilenga kituo kimoja katika eneo la uchimbaji mafuta la Shaybah, katika jimbo la Mashariki lenye utajiri wa mafuta.

    Wizara hiyo imesema katika taarifa kuwa watu waliofariki walikuwa raia wa Ufilipino na Nepal, huku waliojeruhiwa wakiwa raia wa Pakistan na India. Hata hivyo, haikutaja chanzo cha ndege hiyo isiyo na rubani.

    Kwa upande wake, Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Marekani imewaagiza wafanyakazi wote wa ubalozi wake mjini Riyadh pamoja na familia zao kuondoka Saudi Arabia, kulingana na taarifa iliyochapishwa na shirika la habari la AFP.

    Chanzo hicho kilisema Washington pia imeamuru wanafamilia wa wafanyakazi wa balozi zake katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Jordan, Qatar na Bahrain kuondoka katika nchi hizo.

    Soma pia:

  4. Tetesi za Soka Ulaya: Arsenal tayari kumuuza Gyokeres?

    Arsenal inataka kurejesha pauni milioni 55 ilizotumia kumsajili mshambuliaji wa Uswidi mwenye miaka 28, Viktor Gyokeres, huku uhamisho wake ukitarajiwa zaidi mwishoni mwa msimu kuliko Januari. (Football Insider)

    Chelsea imejiunga na Galatasaray katika mbio za kumsajili kiungo wa Uswidi mwenye umri wa miaka 23 wa Brighton, Yasin Ayari. (Teamtalk)

    Liverpool haina haraka ya kuanza mazungumzo ya mkataba mpya na kiungo wa Argentina Alexis Mac Allister, 27, licha ya kupanda kwa kiwango chake msimu huu. (Telegraph)

    Manchester United ni miongoni mwa klabu kadhaa za Ulaya zinazomfuatilia beki wa Uholanzi mwenye miaka 18 wa FC Twente, Ruud Nijstad. (The Athletic)

    Barcelona na Real Madrid ni miongoni mwa klabu zinazomfuatilia kiungo wa Uswisi mwenye miaka 21 wa Aston Villa, Johan Manzambi, kufuatia mwanzo mzuri wa maisha yake katika klabu hiyo. (Football Insider)

    Sunderland inajiandaa kutoa ofa mpya dirisha la Januari kwa winga wa Msumbiji mwenye miaka 25 wa Sporting, Geny Catamo. (Teamtalk)Everton inamfuatilia Mshambuliaji wa Croatia mwenye miaka 24 wa Dinamo Zagreb, Dion Beljo, kama moja ya chaguo zake za usajili katika dirisha la Januari. (Football Insider)

    Liverpool, pamoja na klabu nyingine kubwa za Ulaya, zinavutiwa na kiungo wa Mexico mwenye miaka 18 wa Tijuana, Gilberto Mora. (Marca)

    Mshambuliaji wa Brazil Vinicius Jr, 26, aliwahi kuvutiwa sana kuhamia Arsenal wakati wa kiangazi, lakini sasa anatamani kuchezea Real Madrid kwa kipindi kilichosalia cha maisha yake ya soka. (Mail)

    Arsenal inaongoza mbio za klabu za Ligi Kuu England kuwania saini ya kiungo wa Uturuki mwenye miaka 20 wa Eintracht Frankfurt, Can Uzun. (The Daily Briefing)

    Pia unaweza kusoama:

  5. Papa Leo hatahitaji matibabu zaidi baada ya kufanyiwa upasuaji - Vatican

    Madaktari wa Papa Leo, wamesema hahitaji matibabu zaidi baada ya kufanyiwa upasuaji siku chache zilizopita, wa kuondoa uvimbe wa saratani kwenye mapafu yake.

    Matokeo ya vipimo vya tishu zilizotolewa wakati wa upasuaji yamethibitisha kuwa alikuwa na saratani ya mapafu aina ya adenocarcinoma, na kwamba ugonjwa huo ulikuwa umejikita katika eneo moja, kulingana na taarifa iliyotolewa na Vatican.

    “Uchunguzi wa baadaye wa saratani umethibitisha kuwa hakuna haja ya matibabu zaidi,” taarifa hiyo ilisema.

    Papa huyo mwenye umri wa miaka 71 aliruhusiwa kutoka hospitali ya Gemelli mjini Rome mwishoni mwa wiki iliyopita, siku nne baada ya kufanyiwa upasuaji.

    Habari hiyo ilitolewa saa chache baada ya Papa Leo kuongoza mkutano wake wa kwanza wa kawaida wa kila wiki katika uwanja wa Mtakatifu Petro tangu kuruhusiwa kutoka hospitalini.

    Papa huyo alifanyiwa upasuaji tarehe 13 mwezi Oktoba, ambapo sehemu ya chini ya pafu lake la kulia iliondolewa. Upasuaji huo ulidumu kwa dakika 90.

    Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki alikuwa ametangaza siku chache kabla, wakati wa sala yake ya Jumapili katika uwanja wa Mtakatifu Petro, kwamba alihitaji kufanyiwa upasuaji baada ya madaktari kugundua uvimbe kwenye pafu lake.

    Soma pia:

  6. Rais Macron awashtumu Trump na Netanyahu kwa kujinufaisha na ghasia zilizozuka Ufaransa

    Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, amewashutumu viongozi wa mataifa ya kigeni kwa kutumia maandamano yaliyozuka nchini humo kisiasa ili kujinufaisha katika uchaguzi unaokaribia katika mataifa yao.

    Bila kuwataja kwa majina, Macron alisema viongozi hao wanajipigia debe katika uchaguzi ujao “kwa gharama ya Ufaransa” kupitia kauli zao kuhusu ghasia hizo, zilizozuka wakati wa maandamano ya kupinga kupanda kwa gharama ya maisha.

    Akizungumza wakati wa ziara yake Mashariki ya Kati, Macron aliwarejelea kama “viongozi ambao wamejikita katika kampeni za uchaguzi, iwe katika eneo hili au upande mwingine wa Bahari ya Atlantiki.”

    Kauli hiyo inaonekana kuelekezwa kwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, anayekabiliwa na uchaguzi wa bunge wiki ijayo, pamoja na Rais wa Marekani, Donald Trump, ambaye nchi yake inatarajiwa kufanya uchaguzi wa katikati ya muhula mwezi ujao.

    Takriban watu 150 wamehukumiwa, huku zaidi ya watu 800 wakifikishwa mahakamani tangu kuzuka kwa ghasia zilizoikumba mji wa Paris na miji mingine, ikiwemo Lyon, Marseille na Nice.

    Soma pia:

  7. Marekani yapunguza 'kimyakimya' wanajeshi wake Mashariki ya Kati

    Shirika la habari la CBS, mshirika wa BBC nchini Marekani, limeripoti kuwa jeshi la Marekani linaendelea kupunguza kwa utaratibu na bila kutangaza wazi idadi ya wanajeshi wake katika baadhi ya kambi za kijeshi za Mashariki ya Kati, kufuatia vitisho vinavyoendelea kutoka kwa waasi wa Houthi na Iran.

    Taarifa hiyo, iliyochapishwa awali na NBC News siku ya Jumatano, ilimnukuu afisa wa serikali ya Marekani na afisa mwandamizi wa jeshi walioeleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya tathmini ya kiusalama inayoendelea katika eneo hilo.

    Akijibu taarifa hizo, msemaji wa Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM), Kapteni Tim Hawkins, alisema jeshi la Marekani hubadilisha mara kwa mara maeneo ya vikosi na vifaa vyake ili kuimarisha utayari wa operesheni zake. Hata hivyo, alikataa kutoa maelezo zaidi kwa sababu za kiusalama, akisisitiza kuwa majeshi ya Marekani bado yako tayari kulinda raia wake na maslahi ya nchi hiyo katika eneo lote.

    Wakati huo huo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imeagiza wafanyakazi wasio wa lazima katika ubalozi wake nchini Saudi Arabia pamoja na familia zao kuondoka nchini humo kutokana na vitisho vinavyotokana na waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran.

    CBS pia imeripoti kuwa balozi kadhaa za Marekani katika Mashariki ya Kati zimepunguza idadi ya wafanyakazi na kiwango cha huduma chini ya utaratibu wa uendeshaji wenye vikwazo (restricted operations).

    Hatua hiyo ilianzishwa mwezi Agosti wakati mvutano kati ya Marekani na Iran ulipozidi kuongezeka. Utaratibu huo huruhusu balozi kupunguza shughuli na wafanyakazi wake bila kusitisha kabisa huduma za kidiplomasia.

    Soma pia:

  8. Urusi yaishambulia Kyiv kwa makombora licha ya kukubali kushiriki katika mazungumzo ya amani

    Mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, umeshambuliwa kwa makombora saa chache baada ya Urusi kusema kuwa iko tayari kurejea katika meza ya mazungumzo ya amani, na hata Rais wa Marekani Donald Trump kusema kuwa dunia iko karibu kumaliza vita hivyo.

    Nyumba kadhaa zililengwa wakati wa shambulio hilo jana usiku, na kusababisha watu sita kujeruhiwa, kulingana na taarifa iliyotolewa na Meya wa Kyiv, Vitaliy Klitschko.

    Shambulio hilo la Urusi, limetokea wakati kumekuwa na juhudi mpya za kidiplomasia zinazoongozwa na wajumbe wa Donald Trump, Steve Witkoff na Jared Kushner.

    Witkoff alikutana na Rais wa Urusi Vladimir Putin mjini St Petersburg hapo jana, siku moja tu baada ya kukutana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky.

    Mazungumzo ya awali ya pande hizo tatu yalikuwa yamesitishwa mwezi Februari, na tangu wakati huo Urusi imekuwa ikiongenza mashambulizi yake huku Ukraine ikikabiliwa na upungufu wa makombora ya kuzuia mashambulizi yaliyokuwa yakitolewa na nchi za Magharibi.

    Haijabainika wazi ni mapendekezo gani hasa ambayo Witkoff aliwasilisha kwa Putin hapo jana.

    Hata hivyo, Mshauri wa Putin, Yuri Ushakov, alisema mapendekezo yaliyowasilishwa hayakuwa na manufaa makubwa.

    Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mazungumzo hayo hapo jana katika mji wa St Petersburg, Yuri Ushakov alisema kuwa duru nyingine ya mazungumzo inaweza kufanyika tarehe 10 mwezi Novemba mjini Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

    Soma pia:

  9. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja Alhamisi ya leo