Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwanini homoni ya testosterone ni kigezo cha kuwa mwanajeshi Marekani?
Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth, ametangaza kuwa jeshi la Marekani litafanya vipimo vya upungufu wa kichocheo cha testosterone kwa wanaume wenye umri wa miaka 30 na zaidi kama sehemu ya uchunguzi wa afya wa kila mwaka.
Katika video aliyochapisha kwenye mtandao wa X yenye kichwa "High-T Department", Hegseth alisema kuwa wanajeshi wameidhinishwa kufanyiwa uchunguzi ili kubaini kama wana viwango vya testosterone vinavyohitajika ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi wa hali ya juu.
Pia alisema kuwa wanajeshi watakaobainika kuwa na kiwango cha chini cha testosterone watapewa, kwa hiari yao, tiba ya uingizwaji wa homoni (Hormone Replacement Therapy – HRT).
Watu walio chini ya umri wa miaka 30 pia wanaweza kufanyiwa kipimo hicho iwapo wataona kinafaa kwao.
Bado haijabainika ikiwa vipimo hivyo vitafanywa pia kwa wanawake. Wanawake pia hupata upungufu wa kiwango cha testosterone wanavyozeeka.
Katika video hiyo, Hegseth alisema:
"Tunataka kuwapatia wapiganaji wetu huduma bora zaidi za matibabu duniani. Mpango huu unatimiza wajibu huo."
Je, tiba ya uingizwaji wa homoni ya testosterone itakuwa na manufaa?
Hegseth alisema kuwa kuzingatia afya ya muda mrefu kunalenga kuhakikisha wanajeshi wanabaki wenye nguvu na wana uwezo wa kufanya majukumu yao kwa ufanisi.
Alieleza kuwa jambo hili halihusu tu utendaji wao wanapokuwa kazini, bali pia maisha yao baada ya kustaafu jeshi, kwa kuwasaidia kubaki na afya njema na nguvu kwa muda mrefu baada ya kuacha kuvaa sare za kijeshi.
Pia alisisitiza kuwa katika jeshi kuna marufuku kali ya kutumia homoni ya testosterone bila agizo la daktari kwa lengo la kuongeza misuli.
Hegseth alisema kuwa mpango huo haukusudiwi kuongeza uwezo wa kimwili wa wanajeshi kwa njia isiyo ya kawaida, bali unalenga kushughulikia upungufu wa kichocheo cha testosterone kwa wale wanaouhitaji kitabibu.
Msemaji wa Pentagon, Sean Parnell, alisema katika taarifa kwamba kuanzia sasa, vipimo vya testosterone vitakuwa vya lazima kwa wanajeshi wote walioko katika utumishi wa kudumu na wa akiba wenye umri wa miaka 30 na zaidi.
"Vipimo hivi vinatoa taarifa muhimu na za msingi kuhusu afya ya wanajeshi.
Wale watakaobainika kuwa na uhitaji wa matibabu ya testosterone wanaweza kupewa tiba hiyo ili kujenga wanajeshi wenye afya, uwezo na nguvu," alisema.
Pentagon haikutoa majibu kuhusu iwapo vipimo hivyo vitafanywa kwa wanaume na wanawake wote, wala kama itazingatia kutoa tiba za vichocheo vya estrojeni kwa wanawake wanaoingia katika kipindi cha ukomo wa hedhi wa awali (perimenopause).
Seneta wa Chama cha Democratic kutoka Illinois, Tammy Duckworth, ambaye ni mkongwe wa Vita vya Iraq na mjumbe wa Kamati ya Huduma za Kijeshi, alisema anaamini vipimo vya homoni vinapaswa kupatikana kwa wanaume na wanawake wote.
Kwa upande mwingine, Mbunge wa Chama cha Democratic kutoka Pennsylvania, Chrissy Houlahan, alilaani kauli ya Hegseth.
Kurahisisha upatikanaji wa matibabu ya testosterone
Dkt. Mohit Khera ameiambia BBC kwamba wanaume wote wenye umri wa miaka 30 na zaidi wanapaswa kupimwa kiwango cha kichocheo cha testosterone. Mwaka jana aliongoza jopo la wataalamu la Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Marekani (FDA) lililojadili matumizi na upimaji wa testosterone katika jeshi la Marekani. Alisema vipimo hivyo ni muhimu katika kutathmini afya ya mtu kwa sasa na katika siku zijazo.
"Vijana wengi wa kiume wana viwango vya chini vya testosterone. Hali hii husababisha kupungua kwa nguvu za misuli na uwezo wa kufanya kazi nzito. Hilo linaweza kuwa tatizo katika uwanja wa vita," alisema Khera, ambaye ni profesa wa magonjwa ya njia ya mkojo katika Chuo cha Tiba cha Baylor.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa tiba ya uingizwaji wa kichocheo cha testosterone (TRT) inapaswa kutolewa tu ikiwa mtu ana dalili zinazostahili matibabu, na kwamba tahadhari kubwa inapaswa kuchukuliwa kabla ya kuanza tiba hiyo.
Alisema tiba hiyo inaweza kuwa na manufaa kama vile:
- Kuongeza nguvu za misuli.
- Kupunguza mafuta mwilini.
- Kupunguza hatari ya msongo wa mawazo
- Kuimarisha mifupa kwa muda mrefu
Hata hivyo, alifafanua kuwa tiba hiyo haifai kwa kila mtu.
"Iwapo vijana wa kiume watatumia testosterone, inaweza kupunguza uwezo wao wa kupata watoto. Wanaume walio katika umri wa kuzaa wanapaswa kufahamishwa jambo hili mapema. Pia inaweza kuongeza kwa kiwango kidogo hatari ya kupata magonjwa ya moyo," alisema.
Tangazo la Hegseth limekuja wakati Waziri wa Afya wa Marekani, Robert F. Kennedy Jr., pamoja na maafisa wengine, wanajaribu kuondoa vikwazo vinavyowazuia madaktari kuandika dawa za testosterone kwa wanaume.
Waziri huyo wa Afya amesema hatua hiyo ni sehemu ya suluhisho la kukabiliana na mgogoro wa kitaifa wa kupungua kwa uwezo wa kupata watoto nchini Marekani.
Mwezi uliopita, FDA ilipendekeza kuondoa baadhi ya maonyo kuhusu usalama na ufanisi kutoka kwenye nembo za dawa za tiba ya uingizwaji wa testosterone na pia kulegeza zaidi kanuni zinazodhibiti utoaji wa dawa hizo kwa wagonjwa.