Kwa nini dunia inazidi kupendelea China kuliko Marekani?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Kulingana na utafiti mpya wa Kituo cha Utafiti cha Pew nchini Marekani, China sasa inaonekana kwa mtazamo chanya zaidi kuliko Marekani katika nchi nyingi duniani.

Hii ni mara ya kwanza kwa shirika hilo kurekodi matokeo kama haya.

Matokeo ya utafiti huo yanaonyesha kuwa maoni chanya kuhusu China yamefikia viwango vya juu zaidi kuwahi kurekodiwa katika nchi nyingi, huku mtazamo kuhusu Marekani ukiendelea kuwa mbaya zaidi.

Watu walioshiriki katika utafiti huo walisema kuwa hawana imani kubwa na Rais wa Marekani Donald Trump wala Rais wa China Xi Jinping, ingawa Xi alipata kiwango cha juu cha uungwaji mkono kuliko Trump.

Ingawa Marekani bado inaonekana kuheshimu uhuru wa mtu binafsi zaidi kuliko China, China inaonekana kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine kwa kiwango cha chini ikilinganishwa na Marekani.

Kituo cha Utafiti cha Pew kilifanya utafiti huo kwa kuwahoji zaidi ya watu 42,000 katika nchi 36 kati ya mwezi Februari na Mei.

Katika nchi 25 kati ya 36 zilizofanyiwa utafiti, watu wengi walikuwa na mtazamo chanya kuhusu China kuliko walivyokuwa nao kuhusu Marekani.

Hii ni mara ya kwanza kwa kituo hicho, ambacho kimekuwa kikifuatilia maoni ya watu duniani kuhusu mataifa yenye nguvu tangu mwaka wa 2002, kurekodi matokeo ya aina hii kulingana na Jonathan Schulman, ambaye ni mmoja wa watafiti walioandaa ripoti hiyo.

Miongoni mwa nchi zilizoshuhudia mabadiliko makubwa zaidi katika kuanza kuipendelea China ni Hispania, Indonesia, Italia, Ugiriki na Canada.

Ni nchi sita pekee katika utafiti wa mwaka huu ambazo bado zina mtazamo chanya zaidi kuhusu Marekani. Nyingi kati ya hizo ni washirika wa karibu wa Marekani ambao ni Poland, Ufilipino, Korea Kusini, India, Japani na Israel.

Aidha, kituo hicho cha utafiti kiligundua kuwa kiwango cha wastani cha kukubalika kwa Marekani katika nchi 20 kimekuwa kikishuka kwa miaka ya hivi karibuni, huku kiwango cha wastani cha kukubalika kwa China kikiendelea kuongezeka.

Watafiti pia walibaini kuwa maoni chanya kuhusu China yameongezeka katika zaidi ya theluthi moja ya nchi zilizofanyiwa utafiti katika miaka ya karibuni, kwa kutumia data iliyopanuliwa ya takwimu iliyojumuisha pia Marekani.

Maoni chanya kuhusu China yamefikia viwango vya juu zaidi kuwahi kurekodiwa katika baadhi ya maeneo yaliyofanyiwa utafiti mwaka huu, yakiwemo Italia, Hispania, Colombia, Mexico, Indonesia, Malaysia, Nigeria na Uturuki.

Kwa ujumla, watafiti waligundua kuwa nchi zenye kipato cha kati zilikuwa na mtazamo chanya zaidi kuhusu China, ilhali nchi tajiri zilikuwa na mtazamo hasi zaidi.

Xi Jinping na Donald Trump

Utafiti huo pia uliwauliza walioshiriki ikiwa wana imani na uwezo wa Rais wa China Xi Jinping na Rais wa Marekani Donald Trump kufanya maamuzi sahihi kuhusu masuala ya kimataifa.

Kwa ujumla, viwango vya imani kwa viongozi hao wawili vilikuwa vya chini ya asilimia 50. Hata hivyo, katika nchi nyingi zilizofanyiwa utafiti, watu walionyesha kumwamini Xi zaidi kuliko Trump.

Xi Jinping alipata kiwango cha juu zaidi cha imani nchini Pakistan, ambapo asilimia 83 ya washiriki walisema wanamwamini, huku kiwango cha chini zaidi kikiwa nchini Japani, ambapo ni asilimia 7 pekee waliomwamini.

Kwa upande wa Donald Trump, kiwango cha juu zaidi cha imani kilirekodiwa nchini Ufilipino kwa asilimia 68, wakati kiwango cha chini zaidi kilikuwa asilimia 4 katika Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki.

'Kukosekana kwa utulivu Marekani kunasababisha wasiwasi kwa watu wengi'

Taasisi ya utafiti wa maoni ya umma ya Gallup ilibaini kuwa China iliipita Marekani katika viwango vya kuungwa mkono duniani mwaka uliopita, huku kukiwa na pengo kubwa zaidi la kuipendelea China katika kipindi cha miaka 20.

Hata hivyo, uchunguzi wa kila mwaka wa Maoni ya Umma juu ya Uchina unaofanywa na taasisi ya utafiti ya Marekani ya Jumuiya ya Asia unaonyesha kuwa taswira ya China, ambayo ilidorora wakati wa janga la corona, imeimarika kwa kiwango kidogo tangu huo.

Chong Ja Ian, mwanazuoni asiye mkazi katika Taasisi ya Carnegie China, alisema kwamba matokeo ya hivi karibuni ya Pew hayakuwa ya kushangaza.

"Kukosekana kwa utulivu katika sera za Marekani, ikiwa ni pamoja na matumizi ya nguvu na madhara ya kiuchumi yanayotokana na hilo, kumesababisha wasiwasi mkubwa," alisisitiza.

Utafiti wa Pew ulianza muda mfupi baada ya Trump kuzidisha propaganda zake kuhusu kutaka Marekani kuchukua eneo la Greenland na baada ya Marekani kumkamata kiongozi wa Venezuela Nicolas Maduro. Marekani pia ilianzisha vita na Iran kipindi ambacho utafiti huo ulikuwa ukiendelea.

Dk. Chong aliongeza kuwa "ikiwa China inafurahia uungwaji mkono wa watu wengi kweli bado ni swali linaloendelea kufuatiliwa, lakini kwa sasa inaonekana kuwa nchi inayotabirika zaidi. Beijing pia inaendelea kufanya juhudi kuboresha taswira yake," hasa katika nchi zinazoendelea.

Kuhusu tofauti kati ya viwango vya juu vya upendeleo kwa Uchina na viwango vya chini vya uaminifu kwa Xi Jinping, Dk. Chong anasema kuwa, wakati China "inaweza kutabirika zaidi na kwa hivyo kupendelewa na wengine, hilo halibadilishi ukweli kwamba Xi ni mtu mwenye msimamo wa kiimla zaidi."

Alieleza kuwa chini ya uongozi wa Xi, China "imechukua misimamo yenye ujasiri zaidi na kauli za uthubutu, ikiwa ni pamoja na kusisitiza zaidi kwa nchi nyingine kuendana na mtazamo wake wa dunia" — huku maswali yakiendelea kuwepo kuhusu namna makabila madogo yanavyoshughulikiwa ndani ya nchi hiyo.

"Nadhani watu wanahusisha sera za kulazimisha na zisizo na ufanisi zaidi kiuchumi kwa Xi Jinping binafsi, lakini wanahusisha mambo chanya zaidi, kama vile maendeleo ya kiteknolojia, na China kwa ujumla."