Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Samora Machel: Miaka 40 tangu kifo chake bado Afrika yamlilia
- Author, Florian Kaijage
- Nafasi, BBC Swahili
- Akiripoti kutoka, Dar es Salaam
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Leo Oktoba 19, 2026 imetimia miaka 40 tangu Rais wa kwanza wa Msumbiji, Samora Machel alipofariki dunia mwaka 1986 katika ajali ya ndege iliyotokea katika Milima ya Lebombo Jirani na kijiji cha Mbuzini, nchini Afrika Kusini.
Ndege ya rais Machel aina ya Tupolev Tu-134 ilitumbukia na kuanguka ndani ya ardhi ya Afrika Kusini, jirani sana na mipaka ya Msumbiji na Eswatini ya sasa-Zamani Swaziland, ikitokea katika mkutano wa viongozi wa Afrika nchini Zambia.
Kati ya watu 44 waliokuwemo kwenye ndege hiyo, watu 33 walipoteza maisha akiwemo Rais Machel aliyekuwa na umri wa mika 53, na wajumbe wa msafara wake, marubani, na waandishi wa habari, huku 10 pekee wakinusurika.
Ripoti rasmi za awali za mahakama nchini Afrika Kusini mnamo 1987 zilipeleka kwa marubani kuwa lilikuwa kosa la kibinadamu. Lakini kulikuwa na madai na dhana kubwa kuwa serikali ya sera ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini ilihusika kwa kutumia mfumo wa mawimbi bandia ya redio (false beacon) kuipotosha ndege hiyo njia.
Serikali na mamlaka mbalimbali zimeendelea kupitia upya au kufungua upya uchunguzi wa tukio hilo baada ya kuibuka kwa ushahidi mpya unaodai uingiliaji wa vyombo vya usalama vya wakati huo, kufuatia taarifa kama zile zilizoripotiwa.
Eneo la ajali huko Mbuzini Afrika Kusini limejengwa mnara na makumbusho Samora Samora Machel kwa ajili ya kuadhimisha kumbukumbu ya shujaa huyo na wenzake na kuhimiza mshikamano wa kitaifa.
Mwalimu Julius Nyerere ambaye alikuwa mwenyekiti wa nchi zilizo mstari wa mbele katika ukombozi wa kusini mwa Afrika hakuamini kabisa kuwa ajali hiyo ilikuwa ya kawaida. Katika kauli zake, aliuhtumu waziwazi utawala wa kibaguzi wa rangi wa Afrika Kusini kwa kuhusika na kifo cha Samora Machel. Nyerere alieleza kuwa Samora alikuwa tishio kubwa kwa utawala wa makaburu kutokana na msimamo wake thabiti wa kuwasaidia wapigania uhuru wa ANC ya Afrika Kusini) na ZANU PF ya Zimbabwe.
Samora Machel ni nani?
Samora Moisés Machel alikuwa mwanamapinduzi, mpigania uhuru na mwanasiasa wa Msumbiji aliyeliongoza taifa hilo kupata uhuru kutoka kwa utawala wa kikoloni wa Ureno na kuwa rais wake wa kwanza baada ya uhuru mwaka 1975. Hadi wa leo, anakumbukwa kama mmoja wa viongozi mashuhuri zaidi wa harakati za ukombozi barani Afrika.
Kutoka muuguzi hadi mpigania uhuru
Machel alizaliwa tarehe 29 Septemba 1933 katika Mkoa wa Gaza, uliokuwa sehemu ya Msumbiji iliyotawaliwa na Ureno. Baada ya kupata elimu yake ya awali, alifanya kazi ya uuguzi, ambako alishuhudia ubaguzi wa rangi na hali ngumu zilizowakabili Waafrika chini ya utawala wa kikoloni. Uzoefu huo ulimhamasisha kujiunga na harakati za kupigania uhuru.
Katika miaka ya 1960, alijiunga na FRELIMO (Front for the Liberation of Mozambique), vuguvugu lililoongoza mapambano dhidi ya utawala wa Kireno. Baada ya kuuawa kwa kiongozi wa FRELIMO, Eduardo Mondlane, mwaka 1969, Machel alichukua uongozi wa harakati hizo na kuimarisha mapambano ya ukombozi.
Rais wa kwanza wa Msumbiji huru
Baada ya Msumbiji kupata uhuru tarehe 25 Juni 1975, Machel aliapishwa kuwa rais wa kwanza wa taifa hilo.
Akiwa madarakani, alitekeleza sera za ujamaa, akapanua huduma za afya na elimu, na kuhimiza umoja wa kitaifa. Aliamini kuwa maendeleo ya taifa yalihitaji wananchi kujiona kwanza kama Wamsumbiji badala ya kutanguliza tofauti za kikabila au kikanda.
Rais aliyetaka kujenga taifa jipya
Uhuru wa Msumbiji ulikuwa ushindi mkubwa kwa Machel na FRELIMO, lakini pia ulikuwa mwanzo wa changamoto mpya.
Serikali yake ilirithi nchi iliyokabiliwa na uhaba wa wataalamu, miundombinu duni na tofauti kubwa za kijamii na kiuchumi zilizochochewa na ukoloni.
Machel alitaka kubadilisha hali hiyo kupitia sera zilizosisitiza usawa wa kijamii, elimu, huduma za afya na ushiriki wa wananchi katika maendeleo. Serikali yake ilipanua huduma za umma na kuweka mkazo katika kuongeza fursa za elimu kwa wananchi waliokuwa wametengwa kwa muda mrefu.
Kisiasa na kiuchumi, Machel alifuata mfumo wa ujamaa, akiamini kuwa taifa jipya lilihitaji kujinasua si tu kutoka katika utawala wa kikoloni, bali pia kutoka katika mifumo ya kiuchumi aliyodhani ingeendeleza ukosefu wa usawa.
Hata hivyo, utawala wake haukukosa changamoto. FRELIMO ilijenga mfumo wa chama kimoja, huku serikali ikikabiliwa na ukosoaji kuhusu namna ilivyoshughulikia upinzani wa kisiasa na uhuru wa wananchi.
Aidha, vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoikumba Msumbiji vilikwamisha juhudi za maendeleo na kuongeza gharama za kiuchumi na kibinadamu.
Kwa hiyo, urithi wa Machel hauwezi kueleweka kikamilifu bila kuzingatia mafanikio ya serikali yake pamoja na mapungufu ya mfumo wa kisiasa aliouongoza.
Kwa nini alikuwa mwiba kwa utawala wa apartheid?
Machel hakuwa kiongozi wa Msumbiji pekee. Alikuwa pia mmoja wa viongozi muhimu wa nchi zilizojulikana kama Nchi za Mstari wa Mbele, zilizoshirikiana kupinga ukoloni na ubaguzi wa rangi katika kusini mwa Afrika.
Chini ya uongozi wake, Msumbiji iliunga mkono harakati za African National Congress (ANC), zilizopigania kumalizika kwa utawala wa wachache weupe nchini Afrika Kusini. Pia iliunga mkono mapambano ya ukombozi katika eneo hilo, ikiwemo yale yaliyosaidia Zimbabwe kupata uhuru mwaka 1980.
Msimamo huo uliiweka serikali ya Machel katika mvutano na utawala wa apartheid nchini Afrika Kusini.
Ingawa makubaliano ya Nkomati ya mwaka 1984 yalilenga kuboresha uhusiano kati ya nchi hizo mbili na kuzuia kila upande kuunga mkono wapinzani wa upande mwingine, uhasama haukumalizika.
Wakati huo huo, Msumbiji ilikabiliwa na vita dhidi ya RENAMO, kundi lililopata uungwaji mkono kutoka kwa utawala wa Rhodesia na baadaye Afrika Kusini. Vita hivyo vilichangia uharibifu wa miundombinu, kuyumba kwa uchumi na mateso makubwa kwa raia.
Katika mazingira hayo, Machel alionekana na wafuasi wa ukombozi wa Afrika kama mshirika muhimu. Kwa utawala wa apartheid, sera zake za kikanda zilikuwa changamoto kwa juhudi za kuzuia kuenea kwa harakati za ukombozi.
Ajali ya ndege iliyoacha maswali mengi
Usiku wa tarehe 19 Oktoba 1986, Machel alikuwa akirejea nyumbani kutoka Lusaka, Zambia, ambako alikuwa amehudhuria mkutano wa viongozi wa kikanda.
Ndege ya rais ilianguka katika eneo la milima karibu na Mbuzini, nchini Afrika Kusini, karibu na mipaka ya Msumbiji na Swaziland ya wakati huo.
Mwaka 1987, tume ya uchunguzi ya Afrika Kusini iliyoongozwa na jaji Cecil Margo ilihitimisha kuwa ajali hiyo ilisababishwa na makosa ya marubani, ambao hawakufuata taratibu za usalama wakati wa kushusha ndege na walishindwa kudumisha mwinuko salama.
Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na wataalamu wa Sovieti ulipendekeza kuwa mawimbi ya redio yaliyotengenezwa kwa udanganyifu huenda yaliipotosha ndege hiyo kutoka njia yake sahihi na kuielekeza milimani.
Tofauti hizo zilichochea madai kwamba huenda ndege ilielekezwa kwa makusudi nje ya njia yake na kwamba utawala wa apartheid ulihusika katika ajali hiyo.
Tume ya Ukweli na Maridhiano ya Afrika Kusini ilichunguza suala hilo baadaye, lakini haikupata ushahidi wa kutosha kuthibitisha kwa uhakika hitimisho la tume ya Margo au maelezo ya wataalamu wa Sovieti.
Hata hivyo, uchunguzi huo uliibua maswali kuhusu baadhi ya vipengele vya uchunguzi wa awali. Hali hiyo imechangia kuendelea kwa mjadala kuhusu uwezekano wa hujuma.
Kwa hiyo, ingawa madai ya kuhusika kwa utawala wa apartheid yameendelea kutajwa katika mijadala kuhusu kifo cha Machel, hayajathibitishwa kuwa ndiyo sababu ya ajali hiyo.
Hilo ndilo linalofanya kifo chake kuendelea kuwa mojawapo ya matukio yenye utata katika historia ya kusini mwa Afrika.
Urithi unaovuka mipaka ya Msumbiji
Kwa miongo kadhaa, Machel amekumbukwa na viongozi na wapigania ukombozi wa Afrika kama ishara ya mshikamano wa bara hilo.
Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi zilizosaidia harakati za ukombozi wa Msumbiji na nchi nyingine za kusini mwa Afrika. Uhusiano wa Machel na viongozi kama Julius Nyerere uliakisi ushirikiano wa kikanda uliokuwa muhimu katika mapambano dhidi ya ukoloni na apartheid.
Kwa wananchi wengi wa Msumbiji, Machel bado ni alama ya uhuru na mwanzo wa taifa lililojitawala. Kwa wapigania ukombozi wa Afrika Kusini na Zimbabwe, anakumbukwa kwa mchango wake katika kipindi ambacho viongozi wa Afrika walishirikiana kupinga mifumo ya utawala wa kikoloni na kibaguzi.
Eneo la Mbuzini, ambako ndege yake ilianguka, limehifadhiwa kama eneo la kumbukumbu ya kihistoria. Mnara na makumbusho vilivyojengwa hapo vinawaenzi Machel na wenzake waliopoteza maisha, na kukumbusha uhusiano wa kihistoria kati ya Msumbiji na Afrika Kusini.
Miaka 40 baada ya kifo chake, urithi wa Machel unaendelea kuibua tafakari kuhusu maana ya uhuru, uongozi na mshikamano wa Afrika.
Alikuwa kiongozi aliyesaidia kuikomboa nchi yake kutoka kwa ukoloni na aliyekuwa na nafasi muhimu katika mapambano ya kikanda, lakini pia aliongoza mfumo wa chama kimoja uliokuwa na mapungufu ya kisiasa.
Historia yake, kwa hiyo, ni zaidi ya simulizi la shujaa aliyefariki katika ajali yenye utata. Ni simulizi la kiongozi aliyesaidia kubadilisha historia ya Afrika, na ambaye mafanikio yake, maamuzi yake na mazingira ya kifo chake bado yanaendelea kujadiliwa na vizazi vinavyoendelea.