Marekani yaonya kuhusu uwezekano wa vita kati ya Ethiopia na Eritrea
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amewataka viongozi wa Ethiopia na Eritrea kujizuia na kuepuka hatua zinazoweza kuongeza mvutano wa kijeshi mpakani mwa nchi hizo, akionya kuwa hali hiyo inaweza kusababisha vita.
Rubio amesema ana wasiwasi mkubwa kuhusu taarifa za kuongezeka kwa harakati za wanajeshi katika mpaka wa Ethiopia na Eritrea. Ameonya kuwa kuendelea kupeleka na kukusanya wanajeshi mpakani kunaongeza hatari ya kuzuka kwa vita.
Wakati wa vita vya mwaka 2020 hadi 2022 kati ya jeshi la serikali ya Ethiopia na vikosi vya Tigray, jeshi la Eritrea liliunga mkono jeshi la serikali ya shirikisho na kushiriki katika mapigano dhidi ya vikosi vya Tigray.
Hata hivyo, baada ya vita hivyo kumalizika kupitia Mkataba wa Pretoria, tofauti zilianza kujitokeza kati ya serikali za Ethiopia na Eritrea.
Maafisa kadhaa waandamizi wa Ethiopia, akiwemo Waziri Mkuu Abiy Ahmed, wamekuwa wakisema wazi kuwa nchi hiyo inahitaji bandari. Abiy amesisitiza kuwa Ethiopia, yenye wakazi takribani milioni 130 na uchumi unaokua, haiwezi kuendelea kukosa njia ya moja kwa moja ya kufikia bahari.
Kwa upande wa Ethiopia, Eritrea inatuhumiwa kushirikiana na chama cha TPLF na makundi mengine yenye silaha nchini humo kwa lengo la kuigawa Ethiopia.
Nchi hizo mbili zimekuwa katika mvutano wa kidiplomasia huku hali ya kijeshi mpakani ikiendelea kuibua wasiwasi.
Baada ya vikosi vya Tigray vilivyokuwa vimeelekea kusini mwa eneo hilo kurejea upande wa mpaka wa Eritrea, kumekuwa na ongezeko la wanajeshi wa Eritrea na wa serikali ya shirikisho la Ethiopia katika maeneo ya mpakani.
Akizungumza na waandishi wa habari, Rubio alisema:
“Unaona wanajeshi wakielekea mpakani kutoka pande zote mbili. Katika hali kama hii, unapowaona wanajeshi wa pande zote mbili wakikusanyika mpakani, huwa na wasiwasi kwamba hali hiyo inaweza kugeuka na kuwa mzozo mkubwa zaidi.”
Aliongeza kuwa dunia haihitaji vita nyingine kwa sasa.
Soma pia: