Catherine Nyongesa: Daktari aliyeweka rehani utajiri wake kuokoa wagonjwa wa saratani Kenya

    • Author, Isabella Mwagodi
    • Nafasi, Mwandishi BBC Swahili
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Unapoingia benki kuomba mkopo wa shilingi milioni 100 sawa na ($77,333), matarajio ya maofisa wa mikopo ni kusikia mpango wa biashara utakaozalisha faida kwa haraka.

Lakini Dkt. Catherine Nyongesa alipowaeleza kuwa alihitaji fedha hizo kujenga hospitali ya kuwahudumia wagonjwa wa saratani, wengi wao hawakuona mantiki ya uwekezaji huo.

Kwao, hospitali inayolenga kuwahudumia wagonjwa wengi wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za matibabu haikuonekana kuwa mradi wenye faida.

"Labda kama ungekuwa mradi mwingine wa biashara, lakini si wa kuokoa maisha," walimwambia.

Huo haukuwa mwisho wa safari yake.

Baada ya kukataliwa na benki kadhaa, Dkt. Nyongesa hakukata tamaa. Alitafuta ushauri wa kitaalamu kuhusu biashara, akaboresha mpango wake wa uwekezaji na kuendelea kugonga milango mingine hadi alipofanikiwa kupata mkopo aliouhitaji.

Uamuzi huo wa kuthubutu kuchukua mkopo wa shilingi milioni 100 ndio uliozaa Texas Cancer Centre jijini Nairobi, hospitali ambayo leo imekuwa moja ya vituo vinavyotoa huduma za matibabu ya saratani nchini Kenya.

Hatua hiyo pia ilimweka kwenye historia kama mwanamke wa kwanza nchini Kenya kuwa Daktari Bingwa wa Saratani.

Anapokumbuka siku ya kwanza hospitali hiyo ilipoanza kupokea vifaa na samani, bado hujawa na hisia.

"Nilikuwa natembea kwenye ushoroba wa hospitali nikijibana kidogo mwilini ili nijihakikishie kama kweli ilikuwa ni hali halisi au ndoto. Nikajiambia, 'Catherine, kweli ndoto yako imetimia.''

Kutoka kwenye umaskini hadi ndoto kubwa

Ili kuelewa ni kwa nini Dkt. Nyongesa alikuwa tayari kuchukua hatari ya mkopo wa shilingi milioni 100 sawa na ($77,333), inabidi urudi nyuma katika maisha yake ya utoto.

Hakulelewa katika mazingira ya neema. Elimu yake ilikumbwa na changamoto kubwa za kifedha kiasi kwamba hata kumaliza shule ya sekondari kulionekana kuwa ndoto isiyowezekana.

"Mama yangu alikuwa akiuza pombe ya kienyeji ili tupate chakula na kulipa ada, lakini fedha hazikuwahi kutosha," anakumbuka.

Wakati matumaini ya kuendelea na masomo yalipoanza kufifia, wanafunzi wenzake waliinuka na kumchangia ada kupitia harambee ndogo iliyomwezesha kuhitimu masomo yake.

Nilipomuuliza wale wanafunzi wenzake wanajihisi vipi leo wanapomwona alivyoingia kwenye vitabu vya historia ya tiba nchini, alitabasamu kwa furaha: "Wanajivunia sana! Wanaona matunda ya mbegu ndogo waliyoipanda miaka hiyo."

"Wanafurahi sana. Wanaona matunda ya mbegu waliyoipanda miaka mingi iliyopita."

Kutokana na uzoefu huo, anaamini watu unaojizunguka nao wana mchango mkubwa katika mustakabali wa maisha.

"Zungukweni na marafiki wenye maono, si wale wa kukimbizana na sherehe kila wikiendi!" anasema huku akicheka. "Msiogope kuota ndoto kubwa. Hata mambo yanapokuwa magumu vipi, daima kuna njia ya kutokea."

Maumivu ya familia yaliyozaa dhamira

Mbali na changamoto za kifedha, familia yake ilikumbwa na pigo jingine lililobadili kabisa mwelekeo wa maisha yake.

Dada yake aligundulika kuwa na saratani ya ovari wakati huduma za matibabu ya ugonjwa huo nchini zilikuwa chache na gharama zake zilikuwa kubwa mno.

"Nilikuwa naumia sana kumtafutia hospitali, daktari na dawa. Hapo ndipo nilipoamua kwamba siku moja ningejenga hospitali ya saratani."

Miaka zaidi ya 20 baadaye, simulizi hiyo imegeuka kuwa ushuhuda wa matumaini.

Dada yake sasa amepona maumivu ya saratani na bado anaendelea kupata huduma chini ya uangalizi wa Dkt. Nyongesa katika hospitali ambayo aliijenga kwa ndoto na ujasiri wake mwenyewe.

Kuokoa maisha kuliko kutafuta faida

Kwa Dkt. Nyongesa, kila mgonjwa anayevuka mlango wa Texas Cancer Centre si mteja wa biashara pekee.

Ni fursa ya kutimiza ahadi aliyojiwekea baada ya kushuhudia mateso ya dada yake, kwamba wagonjwa wa saratani wanapaswa kupata huduma kwa wakati na kwa gharama zinazowezekana.

Anasema licha ya vifaa na dawa za kutibu saratani kuwa na gharama kubwa, lengo lake si kuongeza faida, bali kuhakikisha huduma zinawafikia watu wengi zaidi.

"Kupitia Mamlaka ya Afya ya Jamii, SHA, gharama ambazo wagonjwa walikuwa wakitoa kutoka mifukoni mwao zimepungua kwa kiasi kikubwa."

Anaeleza kuwa hospitali inalenga kupata mapato yatakayowezesha kulipa mishahara ya wafanyakazi, gharama za uendeshaji na kuhakikisha huduma zinaendelea kupatikana.

"Kinachotupa nguvu ni kuona wagonjwa wengi wanapata matibabu. Hata kama faida si kubwa, thamani ya kuokoa maisha ya binadamu ni kubwa zaidi."

Mfano wa kuigwa na Waridi wa kweli

Kutoka kwa msichana aliyesomeshwa kwa michango ya wanafunzi wenzake hadi kuwa daktari aliyethubutu kukopa shilingi milioni 100 sawa na ($77,333), kujenga hospitali ya saratani, simulizi ya Dkt. Catherine Nyongesa ni ushahidi kwamba ndoto kubwa zinaweza kutimia hata zinapoonekana kutowezekana.

Dkt. Catherine Nyongesa ni Waridi wa BBC anayeonyesha ujasiri wa kipekee.

Ni simulizi ya mwanamke ambaye aligeuza maumivu ya familia kuwa matumaini kwa maelfu ya wagonjwa.

Na pengine, somo kubwa zaidi analoliacha ni kwamba unapokuwa na dhamira ya kubadili maisha ya wengine, hata milango inayofungwa leo inaweza kufunguka kesho.

Imehaririwa na Mariam Mjahid