Hatima ya utawala wa kijeshi Mali baada ya shambulio la waasi ni ipi?

Kundi la wapiganaji wakiwa wamejificha wamesimama kuzunguka lori kwenye barabara ya vumbi. Mwanamume mmoja - amesimama kwenye gari - ameshikilia bunduki ya moja kwa moja juu. Upande wa kushoto wa picha ni miguu ya kahawia na ya njano ya sanamu.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Maelezo ya picha, Wapiganaji wanaotaka kujitenga wa Tuareg wameuteka mji wa Kidal baada ya wanajeshi wa Urusi na Mali kujiondoa.
    • Author, Makuochi Okafor
    • Nafasi, BBC Africa
    • Author, Mohamed Ibrahim
    • Nafasi, BBC Arabic
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Ukubwa wa mshtuko uliotikisa Mali na Afrika Magharibi ni vigumu kueleza kwa maneno. Katika mashambulizi yaliyopangwa kwa ustadi, washambuliaji waliweza kuingia mji mkuu wa Mali, Bamako, kumuua waziri wa ulinzi na kurejesha udhibiti wa maeneo ya kaskazini mwa nchi.

Wakazi katika miji tofauti nchini humo waliamka Jumamosi wakisikia milio ya risasi na milipuko. Muungano wa makundi mawili, Fronti ya Ukombozi ya Azawad (FLA) na kundi la JNIM lenye uhusiano na al Qaeda, ulisema ndio uliotekeleza mashambulizi hayo.

Ukubwa wa mashambulizi hayo na kujiondoa kwa majeshi ya Mali pamoja na vikosi vya Urusi kutoka mji wa Kidal kaskazini, ambao sasa uko chini ya udhibiti wa FLA, umeibua mashaka mapya kuhusu uimara wa serikali ya kijeshi inayoongozwa na Kanali Assimi Goita, aliyeingia madarakani kupitia mapinduzi ya Agosti 2020.

Imemchukua Goita siku kadhaa kujitokeza hadharani tangu shambulio hilo, jambo lililoongeza maswali kuhusu mustakabali wa utawala wake pamoja na nafasi ya vikosi vya Urusi vilivyotumwa Sahel kukabiliana na tishio la usalama.

Mwelekeo wa kwanza: Utawala wa kijeshi ubaki madarakani na kupambana

Wachambuzi wengi wanaamini huu ndio uwezekano mkubwa kwa muda mfupi, kwa kuwa jeshi bado linadhibiti miji mikuu, taasisi za serikali na maeneo muhimu ya nchi.

Hata hivyo, wanasema siku zijazo zitakuwa za maamuzi makubwa wakati jeshi likianza mashambulizi ya kujibu dhidi ya JNIM na FLA.

Mafanikio au kushindwa kwa operesheni hiyo, kwa mujibu wa mchambuzi Beverly Ochieng wa shirika la ushauri la Control Risks, yataamua muda ambao utawala wa kijeshi utaendelea kubaki madarakani.

Siku tatu baada ya mashambulizi, kurasa za urais mitandaoni zilichapisha picha za Goita akikutana na balozi wa Urusi nchini Mali, Igor Gromyko.

Pia kulikuwa na picha zake akiwatembelea majeruhi hospitalini.

Hata hivyo, bado hajatoa tamko rasmi kuhusu hali ilivyo, na wachambuzi wanasema kifo cha Waziri wa Ulinzi Sadio Camara kinaweza kudhoofisha uratibu wa kijeshi na kuathiri uwezo wa jeshi kujibu mashambulizi.

Camara alikuwa mmoja wa watu wenye ushawishi mkubwa zaidi ndani ya utawala huo na alichukuliwa kuwa kiungo kikuu kati ya Bamako na Moscow, pamoja na kuwa msanifu mkuu wa uwepo wa mamluki wa Urusi katika ukanda wa Sahel.

Balozi wa Urusi nchini Mali, Igor Gromyko, aliyeketi upande wa kushoto akiwa amevalia suti, na kiongozi wa Mali Kanali Assimi Goïta kulia akiwa amejificha.

Chanzo cha picha, @PresidenceMali

Maelezo ya picha, Urais wa Mali ulitoa picha hii ya mkutano kati ya Kanali Goïta na balozi wa Urusi
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wakati jeshi la Mali likisema linaendelea kupigania maeneo muhimu, linakabiliwa na changamoto kubwa kwani FLA tayari imeonyesha nia ya kusonga zaidi kusini kutoka Kidal.

Msemaji wa FLA Mohamed Elmaouloud Ramadane amesema ''tunataka kuudhibiti mji wa Gao, njia nyingi za kuingia mjini humo tayari zimedhibitiwa, isipokuwa kambi za jeshi''.

Pia ameiambia BBC mji wa kihistoria wa Timbuktu ni sehemu ya malengo yao yajayo."Itakuwa rahisi kuchukua hatamu tutakapowadhibiti kikamilifu Gao na Kidal."

Jeshi la serikali lilikuwa na uungwaji mkono wa watu wengi wakati lilipotwaa mamlaka karibu miaka sita iliyopita, na kuahidi kushughulikia mzozo wa muda mrefu wa usalama wa Mali.

Lakini tayari imelazimishwa katika nafasi ya ulinzi katika mwaka jana na kizuizi cha mafuta cha JNIM huku wapiganaji wakipanua uasi wao na kujumuisha vita vya kiuchumi.

Iwapo makundi hayo ya waasi yatafanikiwa kuendeleza mashambulizi yao, Mali inaweza kuingia katika mzozo wa muda mrefu utakaotikisa zaidi mustakabali wa utawala wa kijeshi.

Mwelekeo wa pili: Utawala wa kijeshi ubaki kwa msaada wa Urusi lakini watafute washirika wapya

Mashambulizi ya wikiendi iliyopita pia yamepunguza hadhi ya Urusi kama mshirika wa kuaminika wa usalama nchini Mali, Ochieng anasema.

Baada ya jeshi kuchukua madaraka mwanzoni mwa muongo huu, vikosi vya Ufaransa viliondolewa na nafasi yake kuchukuliwa na wapiganaji wa Urusi waliotumwa kusaidia kupambana na waasi.

Sasa sifa ya Urusi imepata pigo kubwa baada ya kushindwa kwa kikosi chake cha Africa Corps kulinda miji muhimu na kuzuia kuanguka kwa Kidal, anaelezea Laessing.

Magazeti katika stendi moja mjini Bamako yenye kichwa cha habari cha kumuomboleza waziri wa ulinzi aliyeuawa.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Magazeti ya Mali yamekuwa yakichapisha habari kuhusu waziri wa ulinzi aliyeuawa

Ingawa Mali inaweza kuendelea kushirikiana na Urusi, huenda sasa ikalazimika kupanua ushirikiano wake wa kijeshi.

Moja ya njia zinazotajwa ni kuimarisha uhusiano na Uturuki, ambayo imekuwa ikiongeza ushawishi wake barani Afrika.

Ochieng anasema kuwa kumekuwa na ripoti za mawasiliano ya usalama ya Uturuki kutumwa "kutoa mafunzo kwa walinzi wa rais" nchini Mali.

Tayari Uturuki ina uhusiano wa kijeshi na Mali na imekuwa ikiipatia ndege zisizo na rubani, ambazo ziliripotiwa kusaidia jeshi kurejesha Kidal mwaka 2024.

Mali pia imeonyesha dalili za kuanza kufufua uhusiano wake na Marekani baada ya miaka ya mvutano.

Mapema mwaka huu, afisa wa juu wa Marekani anayeshughulikia masuala ya Afrika alitembelea Bamako na kusisitiza heshima ya Marekani kwa mamlaka ya Mali pamoja na kueleza nia ya kuanzisha ukurasa mpya wa mahusiano.

Pia alisema kuwa Marekani inakusudia kufanya kazi kwa karibu zaidi na majirani na washirika wa Mali, Burkina Faso na Niger, katika masuala ya usalama wa pamoja na vipaumbele vya kiuchumi.

Bamako pia inaweza kutegemea zaidi Muungano wa Nchi za Sahel unaojumuisha Mali, Niger na Burkina Faso, ingawa hadi sasa muungano huo haujaonyesha nguvu kubwa ya pamoja vitani.

Kwa Urusi, swali kuu ni kama itaweza kudumisha ushawishi wake iwapo Mali itaanza kupanua ushirikiano wake wa usalama kwa washirika wengine.

Mgogoro huo pia unaweza kuwa kipimo cha mkakati wake mpana barani Afrika, ambapo Moscow imepanua ushawishi kupitia ushirikiano wa kijeshi.

Ikiwa vikosi vinavyoungwa mkono na Urusi vitaonekana kuwa haviwezi kuwalinda washirika wakuu, serikali zingine katika eneo hilo zinaweza kufikiria upya jinsi zinavyoitegemea Moscow.

Mwelekeo wa tatu: Shinikizo kuondoa utawala wa kijeshi lakini nani atachukua nafasi hiyo?

Mashambulizi ya Jumamosi yameunda changamoto kubwa zaidi kwa utawala wa kijeshi katika miaka ya karibuni.

Mashambulizi zaidi yanaweza kuongeza shinikizo kwa serikali ya kijeshi huku hasira ya umma ikiongezeka.

Mojawapo ya matokeo yanayowezekana ni mapinduzi mengine ya kijeshi, ambapo kundi tofauti la maafisa litachukua madaraka.

Njia nyingine ni muungano wa FLA na JNIM kuchukua nafasi ya serikali ya sasa, ingawa hilo litakabiliwa na mvutano mkubwa wa ndani.

FLA hujiona kama harakati ya kisiasa na ya utaifa, huku JNIM ikiwa kundi lenye silaha linalofuata msimamo mkali wa Kiislamu.

Makundi ya wanaotaka kujitenga na yale ya Kiislamu nchini Mali yamekuwa na uhusiano wa kubadilika tangu mwaka 2012, wakati uasi wa Watuaareg ulipotekwa na makundi ya Kiislamu.

Ingawa msemaji mmoja wa FLA aliwahi kuwaita wapiganaji wa JNIM "ndugu zao", kiongozi wa FLA Sayed Bin Bella alisisitiza baadaye kuwa hakuna muungano rasmi.

"tunapambana na adui mmoja, kwa hivyo lazima tuwe chini ya mwavuli mmoja".

Lakini kiongozi wa FLA, Sayed Bin Bella baadaye aliambia BBC kwamba "hakukuwa na uhusiano kama huo".

''Bendera wanazoinua ni zao wenyewe, si za al Qaeda, na ikiwa JNIM inataka kuungana nasi, lazima ivunje kwanza uhusiano wake na mtandao wa kimataifa wa al Qaeda'', alisema Sayed.

Wachambuzi wanasema tofauti hizi za kiitikadi zinaweza kufanya mgawanyo wa madaraka kuwa mgumu iwapo utawala wa sasa utaondolewa.

Ingawa JNIM katika miaka ya karibuni imepunguza kauli za wazi za jihadi ya kimataifa, anasema Ochieng.

Anasema uwezekano wa matokeo yanaweza kuwa hali ya aina ya Syria ambapo kundi ambalo lilikuwa na uhusiano na al-Qaeda linachukua madaraka.

Uongozi wa Syria umekosolewa na baadhi ya Waislam wenye misimamo mikali kwa kutokuwa na dini kupita kiasi.

Shutuma kama hizo tayari zinaelekezwa kwa JNIM kwa sababu ya ushirikiano wake na FLA, wachambuzi wanaofuatilia vituo vya habari vya wanajihadi wameripoti.

Hata hivyo, tofauti za itikadi kati ya JNIM na FLA zinaweza kuwa chanzo cha mvutano wa siku zijazo, isipokuwa wanaotaka kujitenga watapata udhibiti kamili wa kaskazini na kujiweka mbali na maendeleo kwingineko nchini.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid