Je, Manchester United hatarini kushushwa daraja EPL?

    • Author, Simon Stone
    • Nafasi, Mwandishi wa habari wa Manchester United
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

"Lazima tuendelee kupambana na kutafuta ushindi, hakuna njia nyingine," alisema Michael Carrick baada ya Manchester United kuchapwa mabao 2-0 na Chelsea Jumamosi.

Carrick anafahamu fika maumivu ya kushushwa daraja. Mwanzoni mwa maisha yake ya soka, alikuwepo katika kikosi cha West Ham kilichoshushwa daraja msimu wa 2002-03 licha ya kuwa na nyota kama David James, Joe Cole, Jermain Defoe na Trevor Sinclair.

Hata hivyo, West Ham ilimaliza katika nafasi ya tatu kutoka mkiani ikiwa na pointi 42, idadi ambayo hadi leo ndiyo kubwa zaidi kuwahi kuifanya timu kushuka daraja katika msimu wa mechi 38 wa Ligi Kuu ya England.

Kwa kuzingatia mwenendo wa sasa, pointi saba ambazo Manchester United imejikusanyia katika mechi tisa za kwanza zisingeifikisha hata pointi 30 kama kasi hiyo ingeendelea hadi mwisho wa msimu.

Hilo linaibua swali kubwa: Je, United inaweza kweli kujikuta ikipambana kuokoa nafasi yake katika Ligi Kuu yya England?

Mashabiki wachache sana wanaweza kukumbuka mara ya mwisho United iliposhuka daraja. Ni lazima uwe na umri wa karibu miaka 60 au zaidi kuwa na kumbukumbu za kipindi hicho.

Wengi hukumbuka simulizi la Denis Law kuichangia United kushuka daraja kwa bao la kisigino alilofunga akiwa Manchester City. Lakini ukweli ni kwamba kikosi hicho tayari kilikuwa kinaelekea kushuka chini ya kocha Tommy Docherty.

Tangu Novemba 1986, Manchester United haijawahi kujikuta katika eneo la kushuka daraja baada ya kucheza mechi tisa au zaidi za ligi. Wakati huo, Sir Alex Ferguson alikuwa ameanza kazi kwa pointi moja tu katika mechi zake mbili za kwanza baada ya Ron Atkinson kuondoka.

Nafasi mbaya zaidi ambayo United imewahi kuwa nayo katika hatua hiyo ya msimu tangu wakati huo ilikuwa ya 17 katika msimu wa 1989-90. Hivi sasa, imejikuta tena katika nafasi hiyo, ikisaidiwa zaidi na matokeo ya timu zilizo chini yake kuliko kiwango chake chenyewe.

Kikosi cha Carrick sasa kimecheza mechi tisa mfululizo bila ushindi katika mashindano yote, rekodi mbaya zaidi kushuhudiwa tangu msimu wa 1988-89. Ushindi wao pekee wa Ligi ya Premia msimu huu ulikuwa dhidi ya Ipswich mwezi Agosti, walipogeuza matokeo na kushinda wakiwa nyumbani.

Mashabiki wa United wamewahi tena kujipata katika hali kama hii. Chini ya kocha Ruben Amorim katika msimu wa 2024-25, timu hiyo ilikuwa nafasi ya 16 baada ya kucheza mechi 37 za ligi.

Tofauti kubwa ni kwamba wakati huo walikuwa pointi 14 mbele ya Leicester iliyokuwa nafasi ya tatu kutoka mkiani, hivyo hawakuwahi kuwa katika hatari halisi ya kushushwa daraja.

Hata hivyo, mfano wa Tottenham msimu uliopita unaonyesha jinsi mambo yanavyoweza kubadilika kwa haraka. Wakati mmoja walikuwa nafasi ya tatu kutoka mkiani na pointi mbili nyuma ya West Ham huku mechi nne pekee zikisalia.

Kwa hiyo, ingawa bado ni vigumu kuamini kwamba klabu inayotarajiwa kuingiza zaidi ya pauni milioni 700 kwa msimu inaweza kushuka daraja, uwezekano huo hauwezi kupuuzwa kabisa.

"Unaweza kuangalia umbali uliopo hadi eneo la kushuka daraja, au ukaangalia jinsi unavyoweza kupanda haraka kwenye msimamo kwa kushinda mechi," alisema Carrick.

"Hiyo ndiyo njia sahihi ya kulitazama suala hili."

Ili kujinasua katika hali hii, United inahitaji ushindi uwanjani.

Mechi yao inayofuata ni dhidi ya Aston Villa katika Uwanja wa Old Trafford tarehe 8 Novemba. Baada ya hapo wanakabiliwa na ratiba ngumu inayojumuisha safari za Liverpool, Newcastle na Arsenal.

Bado hakuna taarifa rasmi iliyotolewa kuhusu mustakabali wa Carrick, ingawa kabla ya kipigo dhidi ya Chelsea kulikuwa na matarajio kwamba angeiongoza timu katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Roma.

Kwa sasa hakuna anayejua kwa uhakika kitakachofuata. Kilicho wazi ni kwamba wachezaji wengi wanahitaji kuongeza juhudi zao uwanjani.

Mmoja wao ni Lisandro Martinez, ambaye hatakuwepo dhidi ya Aston Villa baada ya kutolewa kwa kadi nyekundu katika mechi dhidi ya Chelsea.

Mustakabali wa beki huyo katika Old Trafford pia unaendelea kuzua mijadala. Mkataba wake unakaribia kuingia mwaka wake wa mwisho, huku majeraha yake ya mara kwa mara yakiibua maswali ikiwa klabu inapaswa kumuongezea mkataba.

Athari za kifedha za kushushwa daraja ni zipi?

Manchester United imecheza mechi tisa mfululizo bila ushindi katika mashindano yote. Mara ya mwisho iliandikisha mfululizo wa matokeo mabaya zaidi ilikuwa mwaka 1984 ilipocheza mechi 10 bila kushinda.

Ingawa bado ni mapema kuzungumzia athari halisi za kushushwa daraja, madhara ya kifedha yanaweza kuwa makubwa sana.

Mchambuzi wa masuala ya fedha za soka Paul Quinn, anayefahamika kama The Esk, alikadiria kuwa Tottenham ingepoteza kati ya pauni milioni 197 na 235 iwapo ingeshuka daraja.

Kwa Manchester United, ambayo hupata sehemu kubwa ya mapato yake kupitia haki za matangazo ya televisheni, malipo yanayotolewa kwa timu zinazoshuka daraja yasingeweza kufidia hasara hiyo.

Zaidi ya hayo, klabu hiyo ina deni la pauni bilioni 1.15, linalojumuisha hati fungani, mikopo na malipo ya usajili ambayo bado hayajakamilika.

Wakati huohuo, viongozi wa klabu wanajiandaa kuanza mashauriano na mashabiki kuhusu mpango wa ujenzi wa uwanja mpya, huku mapendekezo ya mwisho yakitarajiwa kuwasilishwa mwishoni mwa 2027 au mwanzoni mwa 2028.

Mashabiki wa United walionyesha tena upinzani wao dhidi ya mpango huo wakati wa mchezo dhidi ya Chelsea katika Uwanja wa Stamford Bridge.

Kwa sasa, kushuka daraja bado linaonekana kuwa jambo lisilowezekana kwa Manchester United. Lakini ukweli kwamba mjadala huo umeanza kuibuka unaonyesha wazi namna kiwango cha timu hiyo kilivyoporomoka na kuiacha katika moja ya misimu yake migumu zaidi katika enzi za kisasa.

Imehaririwa na Ambia Hirsi