Iran: Marekani haitaamua namna au wakati vita vitakapomalizika
Tehran imeonya kuwa mzozo wowote mpya kati yake na Marekani unaweza kuwa wa muda mrefu zaidi na huenda ikavuka mipaka ya Iran, kufuatia tishio la Rais wa Marekani Donald Trump la kushambulia maeneo mengine nchini humo.
Msemaji wa jeshi la Iran, Mohammad Akrami Nia, alisema kuwa vita vyovyote vijavyo havitaamuliwa na Washington, akisisitiza kuwa Marekani haitakuwa na uwezo wa kuamua lini au kwa namna gani vita hivyo vitamalizika.
Wakati huo huo, Waziri wa Ulinzi wa Iran, Mehrdad Akhlaghi, amesema nchi yake itatoa jibu "la uwiano, thabiti na lenye ufanisi" endapo itakabiliwa na shambulio lolote. Kauli hiyo ilitangazwa kupitia televisheni ya taifa ya Iran.
Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema Iran ina nia ya kufikia makubaliano na Washington, akieleza: "Iran inaonyesha utayari wa kufanya makubaliano, na tutasubiri kuona iwapo hilo litatimia."
Akizungumzia uwezekano wa kurejea kwa mzozo wa kijeshi, Trump alisita kutoa msimamo wazi ikiwa Marekani itaanzisha tena operesheni za kijeshi dhidi ya Iran, akisema: "Sitawaambia."
Trump aidha, alidai kuwa Marekani imeharibu sehemu kubwa ya uwezo wa kijeshi wa Iran, lakini akadokeza kuwa bado kuna "eneo moja au mawili" ambayo Washington inahisi inahitaji kushughulikiwa.
Soma zaidi: