Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, Shahed zimepata mrithi? Kombora jipya la Urusi la Filin
Kurugenzi Kuu ya Ujasusi ya Wizara ya Ulinzi ya Ukraine (GUR) inaripoti kuwa Urusi ilianza kutumia kombora jipya la masafa marefu aina ya Filin mwishoni mwa msimu huu wa kiangazi.
Hili ni toleo jipya la silaha zisizo na rubani za vizazi vilivyotangulia, zinazozinduliwa kutoka ardhini badala ya kwenye ndege. Silaha hizi zina kichwa cha kivita chenye uzito mdogo kuliko makombora ya kawaida ya masafa marefu.
Makombora haya mapya yanayofanana na ndege zisizo na rubani yataweza kufika maeneo ya ndani zaidi ya Ukraine, kwa kuwa masafa yake ya kuruka yanatajwa kufikia kilomita 1,200. Kwa upande mwingine, ndege zisizo na rubani za Shahed zinazotumia injini za jeti, katika matoleo yake mbalimbali ya sasa, zina masafa mafupi zaidi.
Kwa mujibu wa GUR, kombora hilo limetengenezwa na kampuni ya JSC NPO Molniya, ambayo ni sehemu ya Shirika la Silaha za Makombora za Kimbinu la Urusi.
Idara hiyo ya ujasusi inasema Filin ni mwendelezo wa juhudi za sekta ya kijeshi na viwanda ya Urusi kutengeneza silaha za mashambulizi ya angani zenye injini za jeti, zinazozinduliwa kutoka ardhini na ambazo gharama zake za uzalishaji ni nafuu kwa kulinganisha.
Kwa mujibu wa idara hiyo, kombora hilo lina mwili uliotengenezwa kwa mchanganyiko wa nyuzinyuzi za kaboni na nyuzinyuzi za kioo (fibreglass). Lina urefu wa mita 3.5 na upana wa mabawa wa mita 3.
Baadhi ya vipengele vyake hutengenezwa kwa kutumia teknolojia ya uchapishaji wa vitu kwa 3D.
Kasi ya juu inayotajwa ya Filin ni hadi kilomita 800 kwa saa, huku masafa yake ya kuruka yakifikia kilomita 1,200.
Kombora hilo linaweza kuruka katika miinuko ya chini sana au kufikia urefu wa hadi kilomita 6. Kuna matoleo yenye vichwa vya kivita vyenye uzito wa kilo 50 na kilo 100.
Kwa mwonekano, linafanana kwa kiasi fulani na Geran-5, toleo la hivi karibuni la ndege isiyo na rubani ya Urusi yenye injini ya jeti, lakini Filin huruka kwa kasi ndogo zaidi.
Kombora hilo huzinduliwa kutoka kwenye kifaa maalumu kilichowekwa ardhini kwa kutumia kichocheo cha baruti.
GUR pia imebaini kuwa vifaa vya kielektroniki vinavyotumika ndani ya Filin vinatengenezwa na kampuni ya Urusi ya PLAZ LLC, inayohusika pia na uzalishaji wa ndege zisizo na rubani aina ya Harpy.
Kwa mujibu wa idara hiyo ya ujasusi, vipande vya vifaa vya kielektroniki vya bidhaa hizo mbili vina mpangilio na alama zinazofanana.
Kombora hilo huelekezwa kwenye shabaha kwa kutumia mfumo wa urambazaji wa ndani usiotegemea mawimbi ya nje, uliotengenezwa China, pamoja na mfumo wa Comet wenye antena 16 za kupokea mawimbi ya satelaiti.
Wakati huohuo, uchambuzi wa vipengele vilivyotumika katika utengenezaji wake umeonyesha ongezeko la sehemu zinazotengenezwa China ikilinganishwa na makombora na ndege nyingine zisizo na rubani za Urusi.
GUR inasema injini ya Filin imetengenezwa nchini Urusi. Ni injini aina ya R500 inayozalishwa na kampuni ya Reynolds LLC.
Injini inayofanana na hiyo iliwahi kubainika kutumika katika makombora ya masafa marefu ya S-71K Kover na S-71M Monochrome.
Tishio jipya mbadala wa Shahed
Siku moja kabla ya taarifa hiyo, Waziri wa Ulinzi wa Ukraine, Yevheniy Khmara, alisema wizara yake inafanya kazi kuhakikisha Ukraine inapata ndege zisizo na rubani za kuzuia mashambulizi, ndege za kivita na risasi zake, mifumo ya makombora na mizinga ya kujihami dhidi ya mashambulizi ya angani, mifumo ya silaha za kujilinda, pamoja na vifaa vya vita vya kielektroniki na suluhisho nyingine za kuimarisha ulinzi wa anga.
"Tunajua pia aina ya silaha ambazo Urusi inatengeneza. Hii inahusu ndege zisizo na rubani zenye injini za jeti zinazoweza kufikia kasi ya kilomita 800 kwa saa. Sisi pia tunatafuta njia za kukabiliana na kizazi kijacho cha vitisho," alisema Khmara.
Aliongeza kuwa watengenezaji wa silaha na kampuni za sekta ya ulinzi wamepewa jukumu la kuwasilisha mapendekezo na mifano ya awali ya suluhisho hizo.
Kwa mujibu wa vyanzo vya BBC ndani ya Wizara ya Ulinzi ya Ukraine, Khmara alikuwa akirejelea kombora la Filin.
Makombora, ndege zisizo na rubani zinazotumika kama makombora, au silaha zinazoweza kuzunguka eneo la shabaha kabla ya kushambulia, zinapofikia kasi ya kilomita 800 hadi 900 kwa saa, huwa vigumu zaidi kuzitungua kwa kutumia ndege zisizo na rubani za kuzuia mashambulizi. Hali hiyo inalinganishwa na makombora ya kawaida na vizazi vya kwanza vya makombora yanayotumia injini za jeti.
Yevheniy Khmara pia aliwaambia waandishi wa habari kuwa Ukraine tayari imepata mafanikio katika kutumia ndege zisizo na rubani za kuzuia mashambulizi dhidi ya ndege zisizo na rubani zinazotumia injini za jeti.
"Kikosi kimoja, wakati wa operesheni ya kijeshi, kilitumia ndege tano za kuzuia mashambulizi aina ya Bars na kuharibu shabaha zote tano za angani. Hiyo ina maana ya ufanisi wa asilimia 100," alisema waziri huyo.
Kwa mujibu wake, mojawapo ya njia zenye ufanisi mkubwa zaidi katika kukabiliana na ndege zisizo na rubani zinazotumia injini za jeti ni matumizi ya ndege za kivita.
Awali, BBC iliandika kuwa kipindi cha kutumia ndege za kawaida zisizo na rubani kuzuia mashambulizi ya Shahed na matoleo ya kwanza ya Shahed yenye injini za jeti kinaelekea ukingoni.
Kwa kuibuka kwa matoleo mapya ya silaha hizo yanayoweza kufikia kasi ya kilomita 800 hadi 900 kwa saa, kunahitajika mifumo mipya ya kuzitungua.
Hili litahitaji ndege za kuzuia mashambulizi zenye kasi kubwa na injini za jeti, ambazo kwa sasa Ukraine haina kwa kiwango kinachohitajika.