'Mlo ulioniacha na vimelea 38 kwenye ubongo'

Lowri anasema anamshukuru Mungu kuwa hai na mwenye afya njema baada ya masaibu yaliyomkuta.
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Mara ya kwanza Lowri Denman alipojua anakabiliwa na changamoto za kiafya ni wakati alipoona mnyoo wa urefu wa mita moja wakati akijisaidia.

"Ilikuwa na muonekano mbaya sana, kama utepe mwembamba unaonata na wenye matuta madogo," alisema mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 42 kutoka Wales.

Ilikuwa dalili ya kwanza ya neurocysticercosis, ambayo ilimwacha Lowri na vimelea 38 kwenye ubongo wake, na kusababisha maumivu makali ya kichwa, kifafa, na psychosis.

Yeye ni mmoja wa watu wachache nchini Uingereza wanaopatikana na maambukizi haya ya ubongo kila mwaka, yanayosababishwa na mabuu ya minyoo.

Baada ya miaka kadha ya tiba na kupona, Lowri anataka kuhamasisha watu kuhusu ugonjwa huu.

Safari ya ndoto yangu

Lowri anasema safari yake ya India mwaka wa 2007 ilikuwa ya kushangaza

Chanzo cha picha, Lowri Denman

Maelezo ya picha, Lowri anasema safari yake ya India mwaka wa 2007 ilikuwa ya kushangaza

Lowri alizuru India kwa miezi mitatu mwaka 2007.

Hapo ndipo daktari wake, Dk. Brendan Healy, mshauri wa magonjwa ya kuambukiza na microbiolojia, anaamini alipata maambukizi.

Lowri alikuwa amekata shauri ya kutokula nyama akiwa safarini, akitarajia kuepuka changamoto ya kuharibikiwa na chakula, lakini Dkt. Healy anaamini kwamba alikula nyama ya nguruwe ambayo ilikuwa na mayai ya minyoo kwa bahati mbaya.

Alikuja kujua miaka mitatu baadaye, mwaka wa 2010, kwamba ana minyoo.

Alienda kumuona daktari wa familia, lakini vipimo vya kinyesi vilitoa matokeo ya kuridhisha na alijihisi vizuri, hivyo maisha yake yaliendelea kama kawaida.

Baada ya mwaka mmoja, alianza kukailiwa na maumivu makali ya kichwa. Mnamo 2011, alipata kifafa kwa mara ya kwanza.

"Nilianza kuwa na matatizo ya kuzungumza," alisema. "Ghafla, nilipata fahamu na nilikuwa kwenye gari la wagonjwa. Nikajiuliza, 'Hii ilitokeaje? Kwa nini?'

Kutafuta majibu

.

Chanzo cha picha, Lowri Denman

Baada ya kulazwa hospitalini, alifanyiwa vipimo vya CT scan na MRI, na Lowri alitakiwa kuja kuchukua majibu.

"Daktari alinikalisha chini na kuniambia, 'Tumepitia picha zako na kupata vimelea 38 kwenye ubongo wako," Lowri alisimulia.

"Mimi na mama yangu tulikosa la kusema, tulijipata tukijiuliza, 'Hi ni nini jamani?'

Mara ya kwanza walifikiri kuwa ni toxoplasmosis, maambukizi yanayotokana na kinyesi cha paka kilicho na viini vilivyombukizwa.

Mamake Lowri aliuliza ikiwa kifafa chake kina uhusiana woowte na minyoo aliyogunduliwa kuwa nao mwaka mmoja uliopita.

Baada ya vipimo zaidi, hatimaye alibainika kuwa ana neurocysticercosis -maambukizi ya vimelea katika ubongo na uti wa mgongo yanayosababishwa na minyoo.

"Wakati huo, maswali mengi yanaibuka, kwa sababu haujui ni nini kitakachojitokeza siku zijazo linapokuja suala la afya yako," Lowri alisema.

Taenia solium

.

Chanzo cha picha, Lowri Denma

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Minyoo wanaofahamika kama Taenia solium, wanapatikana kila mahali duniani.

Hata hivyo, maambukizi ni ya kawaida hasa katika sehemu za Amerika Kusini na Kusini-mashariki mwa Asia, na Afrika katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Kulingana na Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa vya Marekani (CDC), uchafu uhusababisha kuenea kwa vimelea hivyo, ambavyo ni vya kawaida zaidi katika maeneo ambayo watu wanaishi kwa karibu na nguruwe.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa takribani watu milioni 8.3 duniani wanaugua ugonjwa wa neurocysticercosis.

Ni mojawapo ya sababu kuu zinazoweza kuzuilika za kifafa katika maeneo ambapo ugonjwa huu ni wa kawaida.

Watu wanaweza kupata minyoo kwa kula nyama mbichi ya nguruwe au ambayo haijaiva vizuri. Hata hivyo, hii haisababishi moja kwa moja neurocysticercosis.

Mtu aliyebeba vimelea anaweza kuwa na mayai yake madogo kwenye kinyesi chake.

Usipoosha mikono yako vizuri baada ya kutumia choo, mayai yanaweza kuchafua chakula au maji wanayogusa na kumezwa na mtu mwingine.

Ndani ya mwili, mayai huanguliwa na kuwa mabuu ambayo yanaweza kuunda uvimbe katika viungo mbalimbali, kama vile misuli, moyo, na macho.

Hii inajulikana kama cysticercosis. Wakati uvimbe unapojitokeza kwenye ubongo au uti wa mgongo, huitwa neurocysticercosis, aina kali zaidi ya ugonjwa.

Lowri alilazwa hospitalini kwa wiki mbili, ambapo alipokea tiba na dawa za kuzuia vimelea na steroid. Kwa muda, matibabu yalionekana kufanya kazi.

Kwa miaka kadhaa, alihisi kwamba afya yake ilikuwa imeimarika, lakini siku moja alizimia kazini.

Picha za CT zilibaini uvimbe mkubwa katika ubongo wake karibu na vimelea hivyo.

Baada ya kuzimia, alihisi kuchanganyikiwa na kushikwa na ganzi na kuumwa na mwilini. Aliishia kuacha kazi yake na kuhamia kwa baba yake.

Aliapewa dawa za steroid zilizobadilisha mwonekano wake, na maisha yake yalipozidi kuwa magumu, alianza kuhisi mfadhaiko hadi afya yake ya akili ikasambaratika.

"Nilikuwa na wasiwasi mkubwa, na kuingiwa na hofu," alisema Lowri, ambaye alilazwa kwa wiki sita katika hospitali ya watu walio na magonjwa ya akili.

"Familia yangu ilikuwa na tamaa kadri mambo yalivyozidi kuwa mabaya."

Kurejesha hali yake ya afya ilivyokuwa hapo awali imekuwa safari ndefu tangu wakati huo, na hatimaye alirudi kazini mwaka wa 2022.

Hali ya "kipekee''

Dr. Healy stated that Lowri's case had been analyzed by leading experts from the UK and the US.

Healy alibainisha kuwa Lowri alikuwa mgonjwa wa kipekee na hali yake ilikuwa imechunguzwa na wataalamu wengi mashuhuri nchini Uingereza na Marekani.

"Baadhi ya wataalamu wa magonjwa ya kuambukiza nchini wanendeleza taaluma yao bila kukabiliana na hali kama hii; ni nadra sana," alisema.

Baada ya miaka mingi ya kusumbuliwa na matatizo ya kiafya, vimelea hivyo viliganda na kuwa kama mawe (calcified) katika ubongo wa Lowri.

"Sijafanyiwa upasuaji wa kuviondoa," alieleza.

Dkt. Healy alibainisha kuwa Lowri alipata matibabu ya "kuangamiza mayai yote na, kwa bahati nzuri, anaonekana kuushinda ugonjwa huo."

Hajapata kifafa tangu mwaka 2017, lakini atalazimika kuendelea kutumia dawa za kifafa maisha yake yote.

Lowri alionyesha azma yake ya kuhakikisha kuwa uzoefu wake unaleta matokeo chanya.

"Sasa nataka kuendelea na maisha yangu na kutoa elimu kuhusu ugonjwa huu," alisema.

"Ninafurahi kuwa hai, mwenye afya na nguvu tena, na kamwe silichukulii jambo hili kuwa lakawaida."

Imetafsiri na Ambia Hirsi