Namna pomboo wanavyotumika vitani dhidi ya adui

s

Chanzo cha picha, US Department of Defense

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Wakati wa vita vya pili vya dunia, pomboo walisemekana kutumika na Urusi kukusanya taarifa za ujasusi, kufanya mashambulizi na kutega mabomu ya baharini.

Ila sasa Iran inasemekana kutumia pomboo hao katika vita vya baharini vinavyoendelea.

Pomboo wana ufahamu mkubwa wa kiakili na uwezo wa kimwili, na wana uwezo wa kufuata maelekezo wakipewa mafunzo.

Wanyama hawa wakipekee wanaweza kutambua iwapo kuna kifaa kimetegwa chini ya bahari au sauti ya meli ya adui.

Pomboo wanatumikaje kwenye vita?

Picha ikionyesha pomboo

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Picha ikionyesha pomboo

Kuanzia miaka ya 1960 wanyama hawa wamekuwa wakitumika katika upelelezi na kudumisha usalama wa baharini.

Wanathaminiwa kwa akili zao zenye uwezo mkubwa, uwezo wao wa hali ya juu wa sona au kugundua vitu vilivyo chini ya bahari kutumia sauti ya mawimbi, na uwezo wa kuzama kwa kina kirefu zaidi kuliko wapiga mbizi au mashine.

Matumizi makuu ya kijeshi ya viumbe hawa wa baharini ni kama vile:

Kugundua na kuondoa mabomu yaliyoko chini ya bahari

Pomboo aina ya beluga wamefundishwa kugundua, kuweka , na wakati mwingine kusaidia kuondoa mabomu yaliyoko chini ya maji yanayotishia usalama wa meli.

Usalama wa bandari na kushika doria

Pomboo hutumiwa kugundua waogeleaji wa adui, wapiga mbizi, au watu wanaojaribu kuingia bandarini au kuweka vilipuzi kwenye meli za kijeshi.

Ukusanyaji wa taarifa za upelelezi

Kumekuwa na ripoti kuhusu pomboo aina ya beluga kama "Hvaldimir," wanaodhaniwa huenda walifundishwa na Urusi kufanya shughuli za upelelezi, mara nyingi wakionekana wakiwa na viunganishi vinavyoweza kubeba kamera au vifaa vya sensa.

Kutekeleza mashambulizi

Ripoti mbalimbali zimedai kuwa baadhi ya programu, kama zile zilizowahi kuendeshwa na Umoja wa Kisovieti na pia zinazodaiwa kutumiwa na Iran, ziliwafundisha pomboo kushambulia meli za adui kwa kutumia vilipuzi.

Je, ni kweli Iran inatumia Pomboo kwenye vita dhidi ya Marekani na Israel?

Katika mkutano na waandishi wa habari katika ofisi ya wizara ya ulinzi nchini Marekani, maarufu Pentagon, katika maswali yaliyoulizwa na waandishi wa habari, mojawapo ilikuwa "Je, Iran inatumia pomboo wa kujitoa mhanga?"

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth alijibu kwa kusema "Siwezi kuthibitisha wala kukanusha matumizi ya pomboo wa kujitoa mhanga, lakini naweza kuthibitisha kwamba hawana wanyama hao."

Jenerali Dan Caine pia alisema hajawahi kusikia ripoti kama hizo, na akauliza kama hii ni hadithi.

Kauli hizi zilikuwa zinarejelea makala ya Wall Street Journal yenye mada "Iran Inatafuta suluhisho la kukabiliana na kizuizi cha kijeshi"

Chapisho hilo liliandika kuwa vizuizi vya majini vya Marekani vimeonyesha mapungufu katika mkakati wao wa kudhibiti Mlango bahari wa Hormuz, na kwamba Iran inatafuta njia ya kutumia mwanya huo.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Taarifa ya wall street Journal pia inasema kuwa

"Maafisa wa Iran walisema Tehran inaweza kutumia silaha ambazo haijawahi kutumia hapo awali, kuanzia manowari, hadi pomboo wanaobeba mabomu ya kutegwa baharini, na kushambulia meli za kivita za Marekani. Jeshi la IRGC limetishia kuongeza mvutano huo kwa kukata nyaya za mawasiliano za fiber-optic katika Mlango bahari wa Hormuz, hatua ambayo inaweza kuvuruga mtandao wa intaneti duniani."

Ingawa matumizi ya kijeshi ya pomboo yanaweza kuonekana kama hadithi, zoezi hilo limekuwepo kwa miongo kadhaa.

Miaka 26 iliyopita, mwezi Machi tarehe 8, mwaka 2000, BBC iliripoti kwamba Iran ilinunua pomboo wa "kujitoa mhanga".

Ripoti hiyo ilisema kuwa pomboo hao waliopewa mafunzo na Jeshi la Wanamaji la Kisovieti waliuzwa kwa Iran, lakini wakati huo haikujulikana wazi wangefanya nini katika Ghuba ya Uajemi.

Wataalamu wa Urusi walikuwa wamewafundisha pomboo hao na wanyama wengine wa majini kushambulia meli za adui na wapiga mbizi, lakini kutokana na kupungua kwa ufadhili, wengi wao walihamishwa kwenda kwenye majumba ya makumbusho.

Boris Jurid, alikuwa mwalimu wa pomboo hizo na alianza kazi yake kama afisa wa manowari .

Wakati huo ilisemekana kuwa aliwauza wanyama hao wa majini kwa Iran baada ya kushindwa kugharamia chakula na matunzo yao.

Ripoti ya BBC wakati huo ilisema kwamba jumla ya wanyama 27, wakiwemo pomboo, simba wa baharini na nyangumi aina ya beluga, walisafirishwa kutoka Sevastopol katika Rasi ya Crimea kwenda Ghuba ya Uajemi kwa ndege ya mizigo.

Pomboo wanne aina ya beluga walikuwa wamefunzwa na Jurid katika kambi ya kijeshi la wanamaji katika Bahari ya Pacific kabla ya kuhamishiwa kutoka Crimea mwaka wa 1991.

Wanyama hao walifundishwa kushambulia wapiga mbizi wa adui kwa kutumia mikuki iliyofungwa mgongoni mwao au kuwavuta juu ya maji ili wakamatwe.

Mkufunzi wa wanyama wa Jeshi la Wanamaji la Marekani, Bud Bickford, akimsaidia pomboo wake mwenye umri wa miaka 33, Makai, kurudi kwenye bwawa baada ya kuogelea katika Bandari ya Umm Qasr,mwezi Aprili 29, 2003. Baada ya uvamizi wa Iraq, Jeshi la Wanamaji la Marekani lilitumia pomboo waliofunzwa kugundua na kuondoa mabomu ya baharini katika Ghuba ya Uajemi.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mkufunzi wa wanyama wa Jeshi la Wanamaji la Marekani, Bud Bickford, akimsaidia pomboo wake mwenye umri wa miaka 33, Makai, kurudi kwenye bwawa baada ya kuogelea katika Bandari ya Umm Qasr,mwezi Aprili 29, 2003. Baada ya uvamizi wa Iraq, Jeshi la Wanamaji la Marekani lilitumia pomboo waliofunzwa kugundua na kuondoa mabomu ya baharini katika Ghuba ya Uajemi.

Pomboo hao pia wangeweza kulenga meli za adui kwa kutekeleza mashambulizi ya kujitoa mhanga, wakibeba mabomu ya kutegwa ambayo yangelipuka yakigonga meli.

Inasemekana kwamba pomboo hao waliweza kutofautisha manowari za Kisovieti na za kigeni kwa sauti ya propela zao.

Mbali na Urusi, nchi nyingine pekee inayojulikana kufundisha pomboo kwa matumizi ya kijeshi ni Marekani, ambayo inaendesha programu ya wanyama wa baharini huko San Diego, California.

Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na ripoti zisizo rasmi za juhudi za baadhi ya nchi, zikiwemo Korea Kaskazini kuwafunza pomboo.

Tangu uvamizi wake wa Ukraine, Urusi inaripotiwa kuongeza matumizi ya pomboo za kijeshi katika bandari ya Sevastopol ili kukabiliana na wapiga mbizi wa adui na kulinda meli zake za kijeshi katika Bahari Nyeusi.

Picha ya mwaka 1973: Pomboo aliyefunzwa na Jeshi la Wanamaji la Marekani kugundua mabomu ya baharini na torpido.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Picha ya mwaka 1973: Pomboo aliyefunzwa na Jeshi la Wanamaji la Marekani kugundua mabomu ya baharini na torpido.

Akbar Hashemi Rafsanjani, katika kumbukumbu zake "Reforms in Crisis", aliandika kuhusu matukio ya Farvardin 2, 1990.

"Pomboo ni wanyama wenye akili na hutekeleza maagizo vizuri, isipokuwa inapofikia suala la muziki."