Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Kila nilichosomea hakina thamani': AI inavyobadili ajira
- Author, Dalia Haidar
- Akiripoti kutoka, BBC News Arabic
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Miaka mitatu iliyopita, Mwingereza Kyle Palmer alifanya uamuzi ambao wengi waliuona kuwa wa pupa. Aliamua kuifunga kampuni yake ya masoko ya kidijitali licha ya kuwa na mikataba yenye faida na wateja wengi. Sasa anasema aliona biashara yake ikikabiliwa na tishio kutokana na huduma alizokuwa akitoa kuanza kupatikana kwa urahisi kupitia mifumo ya akili unde.
Palmer anasema, "GPT 4 ilipoanza kutumika, nilitambua kuwa huduma nyingi tulizokuwa tukitoa zingepoteza thamani. Wateja walianza kuulizia kuhusu akili unde na kutaka tupunguze gharama za huduma zetu."
Miezi kadhaa baadaye, aliamua kuifunga kampuni hiyo. Aliona kuwa ingezidi kuwa vigumu kuwashawishi wateja kulipia huduma ambazo mifumo ya akili unde ilikuwa tayari inaweza kutekeleza sehemu kubwa ya kazi zake.
"Nilikuwa najifunza kutumia mifumo ya akili unde, ndipo nilipotambua kuwa miaka yote niliyotumia kusoma, kupata mafunzo na kukuza ujuzi wangu ilikuwa kama imepotea bure," anasema kwa kejeli.
"Sasa kuna mfumo unaomwezesha mtu yeyote duniani kupata matokeo ya kiwango hicho kwa dola 20 pekee kwa mwezi," anasema, akirejelea gharama ya wastani ya kupata huduma za juu za mifumo hiyo.
Simulizi la Palmer si la kipekee. Kila kampuni kubwa inapotangaza kupunguza wafanyakazi, swali lilelile huibuka: Je, akili unde imekuwa sababu halisi ya watu kupoteza ajira, au kampuni zinaitumia kama kisingizio cha kufanya mageuzi ya kiutendaji na kupunguza gharama?
Wimbi la kupunguzwa kwa wafanyakazi
Mnamo Julai 2026, Microsoft ilitangaza mpango wa kuwaachisha kazi takribani wafanyakazi 4,800, sawa na asilimia 2.1 ya wafanyakazi wake wote. Hatua hiyo ilitangazwa wakati kampuni ikiendelea kuwekeza katika miundombinu ya akili unde na bidhaa zake za Copilot.
Oracle nayo iliendelea na mageuzi makubwa ya kiutendaji yaliyohusisha kupunguza takribani ajira 21,000. Kampuni hiyo ilisema hatua hiyo inalenga kupunguza gharama zinazotokana na upanuzi wa vituo vya kuhifadhi na kuchakata data pamoja na uwekezaji katika teknolojia za akili unde.
Amazon pia ilipunguza wafanyakazi katika idara zake za usafirishaji na huduma kwa wauzaji, huku ikiendelea kupanua matumizi ya mifumo ya kiotomatiki na akili unde katika maghala na shughuli zake za kila siku.
Mwelekeo huo haukuishia katika sekta ya teknolojia. Benki za Uingereza, zikiwemo Barclays na NatWest, nazo zilitangaza kupunguza wafanyakazi wakati matumizi ya teknolojia za akili unde yakiongezeka, kwa mujibu wa Reuters.
Kampuni ya BT Group pia ilieleza kuwa akili unde inaweza kuharakisha upunguzaji wa wafanyakazi katika mpango wake wa kuondoa ajira kati ya 40,000 na 55,000 ifikapo mwaka 2030.
Katika miezi ya hivi karibuni, kampuni kadhaa kubwa duniani zimetangaza mipango ya kupunguza idadi ya wafanyakazi huku zikielekeza mabilioni ya dola katika akili unde, mifumo ya kiotomatiki na miundombinu ya kidijitali.
Hali hiyo imeshuhudiwa zaidi katika kampuni kubwa za teknolojia, ambazo zimekuwa zikifanya mageuzi makubwa ya kiutendaji sambamba na uwekezaji mkubwa katika uundaji wa mifumo ya akili unde na ujenzi wa vituo vya kuhifadhi na kuchakata data.
Je, akili unde ni kisingizio cha kuficha udhaifu wa kampuni?
Hata hivyo, wataalamu hawakubaliani kikamilifu kuhusu iwapo akili unde ndiyo sababu kuu ya kampuni nyingi kupunguza wafanyakazi.
Hamoud Al Mahmoud, mhariri mkuu wa Harvard Business Review Arabia, anaamini kuwa sehemu ya tatizo ilianza baada ya janga la COVID 19.
Anasema kampuni nyingi ziliajiri idadi kubwa ya wafanyakazi kutokana na matarajio makubwa ya ukuaji wa biashara za kidijitali, lakini baadaye zikagundua kuwa zilikuwa zimeajiri watu wengi kuliko mahitaji ya shughuli zao.
Anaongeza kuwa baadhi ya kampuni hutumia akili unde kama kisingizio cha kueleza maamuzi ya kupunguza wafanyakazi. Hata hivyo, anakiri kuwa teknolojia hiyo ina athari halisi ambazo tayari zimeanza kujitokeza, ingawa kasi ya mabadiliko hayo ni ndogo kuliko ilivyotarajiwa na baadhi ya kampuni.
Takwimu zinaunga mkono hoja hiyo kwa kiasi fulani. Nchini Marekani, takwimu za mwaka 2025 zilizochapishwa na kampuni ya Challenger Gray & Christmas, inayotoa huduma za ushauri kuhusu ajira na mabadiliko ya taaluma, zilionyesha kuwa ni ajira zaidi ya 54,000 pekee kati ya zaidi ya milioni 1.2 zilizotangazwa kuondolewa zilizohusishwa na akili unde. Hiyo ni takribani asilimia 4.5 ya jumla ya ajira zilizotajwa.
Kwa upande wake, Nader Ghazal, rais wa Mtandao wa Kimataifa wa Akili Unde yenye Maadili, anasema kuwa upunguzaji mwingi wa wafanyakazi umetokana na sababu nyingine, zikiwemo mageuzi ya kiutendaji, matumizi ya teknolojia za kidijitali na shinikizo la kiuchumi.
Anasema, "Si suala la akili unde kuchukua nafasi za binadamu pekee. Hali halisi ni tata zaidi ya hapo."
Ghazal anaamini kuwa kinachotokea sasa si kuondolewa kwa taaluma nzima, bali ni mabadiliko ya majukumu na namna kazi zinavyotekelezwa.
Katika sekta ya viwanda, anasema roboti na mifumo ya kiotomatiki zinaweza kutekeleza kazi za kawaida na zinazojirudia kwa ufanisi mkubwa. Hata hivyo, bado zinahitaji usimamizi na uingiliaji wa binadamu zinapokabiliwa na hali tata, hitilafu za kiufundi au majukumu yanayohitaji uamuzi na uzoefu wa kufanya kazi katika mazingira halisi.
Kwa upande wa kazi za ofisini, anaamini kuwa ujuzi muhimu zaidi katika siku zijazo utakuwa uwezo wa kutumia mifumo ya akili unde katika kutekeleza majukumu, badala ya kushindana nayo.
"Hakuna shaka kuwa akili unde itahatarisha ajira za watu ambao hawatakuwa tayari kubadilika," anasema.
"Kazi nyingi zitabadilika namna zinavyotekelezwa badala ya kutoweka kabisa."
"Timu ya wataalamu mfukoni mwako"
Baadhi ya makadirio yanaashiria kuwa mabadiliko hayo yanaweza pia kufungua fursa mpya za ajira.
Kampuni ya utafiti na ushauri wa biashara ya Gartner imependekeza kuwa takribani asilimia 30 ya wafanyakazi watakaopoteza ajira kutokana na matumizi ya teknolojia za akili unde wanaweza kurejea katika soko la ajira ifikapo mwaka 2029, iwapo kampuni zitafikiria upya mikakati yao ya kuajiri na kutumia wafanyakazi.
Hamoud Al Mahmoud anaamini kuwa baadhi ya kampuni zilizoharakisha kupunguza wafanyakazi tangu mwaka 2024 zinaanza kutambua kuwa mabadiliko kuelekea matumizi ya akili unde yatachukua muda mrefu kuliko zilivyotarajia.
Anasema, "Ni kweli kuwa akili unde itachukua nafasi ya baadhi ya kazi, lakini haifanyi hivyo kwa kasi ambayo wengi walidhani."
Kwa Kyle Palmer, suluhisho lilikuwa kuendana na hali mpya badala ya kupinga mabadiliko hayo.
Baada ya kuifunga kampuni yake, alielekeza nguvu zake katika kutoa mafunzo kwa wajasiriamali na watu wanaojiajiri kuhusu namna ya kutumia mifumo ya akili unde kuboresha na kukuza biashara zao.
Anaeleza sababu ya uamuzi huo akisema, "Niliona jinsi akili unde ilivyobadilisha kazi yangu na kuwasaidia watu walionizunguka. Ndipo nilipoamua kuwa miongoni mwa wale wanaojifunza namna ya kunufaika na teknolojia hiyo."
Anaongeza kuwa sasa anawasaidia watu kuanzisha biashara zao au kubuni vyanzo vipya vya mapato kwa kutumia mifumo hiyo.
Anaelezea teknolojia hiyo kuwa sawa na kuwa na "timu ya wataalamu mfukoni mwako" kwa gharama ndogo ya kila mwezi.
Hata hivyo, Palmer anakiri kuwa hakuna uhakika kuhusu mustakabali wa teknolojia hiyo. Anasema inabadilika kwa kasi kiasi kwamba ni vigumu kutabiri kitakachotokea katika kipindi cha miaka mitano au kumi ijayo.
Anasema, "Ni muhimu kukumbuka kuwa ChatGPT imekuwepo kwa miaka michache tu. Huo ni muda mfupi sana ukizingatia athari ambayo tayari imekuwa nayo."
Anaongeza: "Iwe mustakabali huo utakuwa mzuri au wenye changamoto kubwa, kuna uwezekano mkubwa tukapitia kipindi kigumu na chenye mabadiliko mengi yasiyotabirika katika miongo miwili ijayo, hadi tutakapoelewa namna teknolojia inavyoingiliana na jamii zetu."
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid