Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

‘Tukifika 2029 tayari tutakuwa na Katiba mpya’ – Samia Suluhu Hassan

Rais wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa, kwa sasa wapo katika hatua za mwisho za kuunda tume ya maridhiano itakayohusika na kuunda katiba mpya.

Muhtasari

Moja kwa moja

Faidha Ngaga & Beldeen Waliaula

  1. Kufikia hapo tunatamatisha matangazo yetu ya moja kwa moja. Kwaheri.

  2. Vikosi vya Iraq vyaingia Baghdad, kwenye ngome inayoungwa mkono na Iran

    Vikosi vya Iraq vimeripotiwa kuingia kusini mwa Baghdad ambako kwa muda mrefu imekuwa chini ya udhibiti wa kundi la wanamgambo linaloungwa mkono na Iran, Kataib Hezbollah.

    Kwa mujibu wa msemaji wa jeshi la Iraq, wanajeshi waliingia katika mji wa Jurf al-Sakhar hii leo kwa amri ya Waziri Mkuu Ali al-Zaidi.

    Msafara wa magari ya kijeshi ya Iraq yaliyokuwa yakipeperusha bendera ya taifa uliingia Jurf al-Sakhar hii leo, huku wanajeshi wakichukua nafasi mbalimbali za ulinzi na kuuzunguka mji huo.

    Maafisa wa usalama wanasema operesheni hiyo pia inahusisha vikosi vinavyosimamia ulinzi wa miundombinu ya mafuta na nishati.

    Hata hivyo serikali ya Iraq, inalishutumu Kataib Hezbollah kwa kuendesha mtandao wa magendo ya mafuta ambao umelitia taifa hilo hasara ya mamia ya mamilioni ya dola katika mapato.

    Takribani miaka kumi iliyopita kundi hilo limekuwa likidhibiti mji huo tangu uliporejeshwa kutoka kwa wanamgambo wa Islamic State (IS).

    Iraq inakabiliwa na shinikizo kutoka Marekani la kuyapokonya silaha makundi yanayoungwa mkono na Iran, ambayo yanatuhumiwa kutekeleza mashambulizi dhidi ya vikosi vya Marekani katika eneo hilo.

    Soma pia:

  3. ‘Tukifika 2029 tayari tutakuwa na Katiba mpya’ – Samia Suluhu Hassan

    Rais wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa, kwa sasa wapo katika hatua za mwisho za kuunda tume ya maridhiano itakayohusika na kuunda katiba mpya.

    “Kama tulivyoahidi kwenye Ilani, tukifika 2028, 2029 tayari tutakuwa na Katiba iliyorekebishwa, au jina lolote mnalopenda kuiita, Katiba mpya, Katiba iliyorekebishwa, tutakuwa tayari tuko nayo mikononi,” amesema Rais Samia.

    Akizungumza hii leo, Novemba 20, 2026, akiwa Kilimanjaro Tanzania rais Samia alisema licha ya changamoto za kiusalama zilizojitokeza kufuatia matukio ya Oktoba 29, hali ya usalama imerejea katika utulivu, huku Serikali ikiendelea kutekeleza mapendekezo ya tume iliyoundwa kuchunguza matukio hayo.

    Rais huyo mesema serikali ya nchi hiyo ipo katika hatua za mwisho za maandalizi ya kuunda tume ya maridhiano ya kitaifa, ambayo inatarajiwa kutangazwa hivi karibuni kwa lengo la kuimarisha umoja wa taifa na kuweka msingi wa mchakato wa mabadiliko ya Katiba nchini.

    ‘Kwanini tume ya maridhiano? tunafanya tume ya maridhiano ili kulirudisha taifa pamoja,kujua hoja gani na nini kibadilike kwenye Katiba yetu’ ameelezea rais Samia.

    Kiongozi huyo amesisitiza kuwa serikali yake imeanza mashauriano na makundi mbalimbali, yakiwemo viongozi wa dini, vyama vya siasa na taasisi za kiraia, ili kupata wawakilishi watakaoshiriki katika tume ya maridhiano

    “Kama mnavyojua tulikumbwa na msukosuko mwaka wa 2025, ila hali ya usalama nchini imeimarika.Kutokana na hayo tuliunda tume kuchunguza yaliyotokea,na tayari tumeanza kutekeleza mapendekezo ya tume hiyo. Kinachofuata sasa ni kuunda tume ya maridhiano kuelekea uundaji wa katiba” amesema Rais Suluhu.

    Rais huyo amesema kuwa tume hiyo itatangazwa hivi karibuni, na tayari amekuatana na makundi mbalimbali ikiwemo ya kidini, taasisi za kiraia na wanasiasa ambao watashiriki katika tume hiyo na kuchangia kuleta mabadiliko kwenye katiba ya nchi hiyo.

    Rais Suluhu ameahidi kuwa ifikiapo mwaka wa 2028-2029 Tanzania itakuwa na katiba mpya

  4. Urusi yarusha kombora Poland wakati wanajeshi wanafanya mazoezi

    Poland imesema kuwa kombora la Urusi aina ya cruise lilikuwa miongoni mwa vitu vitatu vilivyoingia katika anga yake mapema leo, huku Waziri Mkuu Donald Tusk akisema tukio hilo halionekani kuwa la bahati mbaya, kwani mazoezi ya kijeshi ya mataifa ya Magharibi yalikuwa yakiendelea katika eneo hilo.

    Hakuna mtu aliyejeruhiwa wala uharibifu wowote ulioripotiwa, lakini Poland imelielezea tukio hilo kuwa ni "uchokozi" kutoka Moscow.

    Urusi bado haijatoa maoni kuhusu ukiukaji huo wa anga ya Poland, uliotokea wakati wa mashambulizi makubwa zaidi ya anga ya Urusi dhidi ya Ukraine tangu mwaka 2022.

    Waziri wa Ulinzi wa Poland, Wladyslaw Kosiniak-Kamysz, amesema kombora hilo aina ya Kh-101 lilianguka katika eneo la mashambani la Nowy Lipowiec, kusini mashariki mwa Poland, umbali wa takriban kilomita 50 kutoka mpaka wa Ukraine.

    Katibu Mkuu wa NATO, Mark Rutte, amelaani kile alichokitaja kuwa "ukiukaji mkubwa wa anga ya Poland" na kusema ndege za kivita za NATO zilitumwa kukabiliana na hali hiyo.

    "Tukio hili ni hatari waziwazi na ni matokeo ya vita vinavyoendelea vya Urusi dhidi ya Ukraine," amesema Rutte.

    Soma pia:

  5. Takriban wanawake 600 waliuawa Afrika Kusini ndani ya miezi mitatu

    Takriban wanawake 600 wameuawa nchini Afrika Kusini kati ya mwezi Julai na Septemba mwaka huu, kulingana na takwimu za hivi karibuni za uhalifu nchini humo.

    Idadi hiyo inajumuisha wanawake 13 ambao miili yao, ikiwa na majeraha, ilipatikana imetupwa katika maeneo yaliyokaribu na mji wa Johannesburg.

    Mauaji hayo yalisababisha hasira kubwa nchini humo huku polisi wakikabiliwa na shinikizo la kuwatafuta waliohusika.

    Afrika Kusini ni miongoni mwa nchi zenye viwango vya juu zaidi duniani vya ukatili wa kijinsia na mauaji.

    Katika tukio jingine la hivi karibuni, wanawake watano na mtoto mmoja mdogo walipigwa risasi na kuuawa katika jimbo la Free State mapema wiki hii.

    Takwimu mpya za uhalifu ambazo zimezotolewa hii leo zimeonyesha kuwa wanawake 581 waliuawa nchini humo kati ya Julai na Septemba, wakiwemo 131 katika jimbo la Gauteng, linalojumuisha mji wa Johannesburg.

    Soma pia:

  6. Wahouthi waishtumu Saudi Arabia kwa kulenga boti na kuua raia

    Waasi wa Wahouthi nchini Yemen wameishutumu Saudi Arabia kwa kushambulia boti iliyokuwa imebeba raia na kuua watu 19, huku vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Yemen vikianza tena baada ya kipindi cha utulivu.

    Msemaji wa Wizara ya Afya ya Wahouthi, Anis Asaby, amelaani shambulizi hilo lililotokea hii leo akisema: "Ndege za nchi hiyo zililenga boti ya kiraia iliyokuwa imebeba wakimbizi zaidi ya 25, na kusababisha vifo vya raia 19 huku wengine wanne wakijeruhiwa."

    "Kuwalenga raia na wakimbizi ni uhalifu wa kivita wa kiwango cha juu na ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu."

    Msemaji huyo wa Wizara ya Afya ya Wahouthi pia ametangaza kupitia mtandao wa kijamii wa X kuwa boti hiyo ilikuwa ikisafiri kutoka eneo la Ras al-Ara kuelekea mji wa Hays, kusini mwa Yemen.

    Soma pia:

  7. Nigeria yapendekeza matibabu badala ya adhabu kwa wanaojaribu kujiua

    Rais wa Nigeria, Bola Tinubu, ameiomba bunge la taifa hilo kuondoa adhabu za jinai kwa watu wanaojaribu kujiua lakini wakashindwa, akipendekeza badala yake wapewe msaada wa kimatibabu.

    Pendekezo hilo linalenga kubadili msimamo wa Nigeria kuhusu jaribio la kujiua, kutoka kwenye kuwaadhibu wahusika kisheria hadi kuwapatia matibabu na huduma za kuwawezesha kurejea katika maisha ya kawaida.

    Hatua hiyo inafuatia miaka kadhaa ya wito wa mageuzi kutoka kwa wataalamu wa afya ya akili. Mswada mwingine unaolenga kuondoa uhalifu wa jaribio la kujiua tayari umepitishwa katika hatua ya pili ya usomaji katika Seneti.

    Chini ya sheria za Nigeria, kujaribu kujiua ni kosa la jinai, ambapo mtu anayepatikana na hatia anaweza kuhukumiwa kifungo cha hadi mwaka mmoja jela, kutozwa faini au adhabu zote mbili.

    Mswada huo wa Seneti pia unapendekeza kubadilisha adhabu za jinai kwa watu wanaojaribu kujiua na badala yake kuwapatia matibabu, huduma za urekebishaji na msaada mwingine.

    Mswada huo ambao umedhaminiwa na Seneta Asuquo Ekpenyong, ambaye amesema kuwafungulia mashtaka watu wanaonusurika baada ya kujaribu kujiua kunaweza kuwakatisha tamaa watu wenye mawazo ya kujiua kutafuta msaada.

    Pia ameonya kuwa familia zinaweza kuficha matukio hayo kwa kuhofia kufunguliwa mashtaka pamoja na unyanyapaa wa kijamii.

    Amesisitiza kuwa lengo la mswada huo si kuhalalisha au kuhamasisha watu kujaribu kujiua, bali ni kuwalinda wale wanaonusurika na kuwapa msaada wanaohitaji.

    Soma pia:

  8. Urusi yashambulia madaraja Kyiv, watu wanane wauawa

    Urusi imeshambulia madaraja katika mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, na kuua watu wanane katika mojawapo ya mashambulizi makubwa zaidi ya anga tangu kuanza kwa vita hivyo.

    Shambulio hili linakuja siku chache baada ya Ukraine kuharibu vibaya daraja la Crimea, linaounganisha eneo la Crimea na Urusi.

    Watu wawili waliuawa katika mashambulizi hayo ya Urusi yaliyolenga kituo cha reli katika mji wa Lviv, magharibi mwa Ukraine.

    Aidha,makombora ya balistiki yalilenga madaraja matatu yanayovuka Mto Dnipro, ambayo ni njia muhimu zinazotumiwa na wakazi wa Kyiv kusafiri ndani ya mji huo. Watu sita wamethibitishwa kufariki.

    Rais wa Urusi Vladimir Putin alikuwa ametishia kulipiza kisasi kufuatia shambulizi la Ukraine lililolenga Daraja la Crimea.

    Meya wa Kyiv, Vitali Klitschko, amewataka wakazi kuepuka kuingia mjini kwa kutumia magari binafsi isipokuwa pale ambapo inawalazimu kabisa.

    Soma pia:

  9. Bernie Sanders: Sababu za Marekani kuipiga Iran ni za uongo

    Seneta mashuhuri wa Marekani wa Vermont, Bernie Sanders, amesema: "Vita vya Vietnam vilianzishwa kwa msingi wa uongo. Vita vya Iraq vilianzishwa kwa msingi wa uongo. Vita dhidi ya Iran navyo vimeanzishwa kwa msingi wa uongo."

    Sanders ametoa kauli hiyo katika mahojiano kwenye podikasti ya The Diary of a CEO, iliyorushwa Alhamisi, Novemba 19.

    Akifafanua madai yake kuwa sababu zilizotolewa za kuanzisha vita dhidi ya Iran ni za uongo, Sanders amesema katika podikasti hiyo: "Madai kwamba serikali ya Iran ilikuwa tayari kutushambulia ni ya uongo... Ninaamini kuwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amekuwa akijaribu kuivuta Marekani katika vita dhidi ya Iran kwa miaka 40 iliyopita, kwa lengo la kuidhoofisha na kuvuruga uthabiti wake."

    Unaweza pia kusoma:

  10. Ripoti yaonya kuwa kupunguzwa zaidi kwa wafanyakazi BBC kutaathiri watazamaji na wasikilizaji

    Ripoti mpya imeonya kuwa mipango ya kupunguza wafanyakazi na kusitisha vipindi zaidi katika Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) itakuwa na athari kubwa zaidi kwa watazamaji na wasikilizaji kuliko hatua za awali za kupunguza matumizi.

    BBC ilitangaza mapema mwaka huu mipango ya kupunguza karibu ajira 1,800 na kusitisha baadhi ya vipindi na huduma zake.

    Hata hivyo, shirika hilo bado linahitaji kupunguza zaidi matumizi ili kufikia lengo lake la kuokoa pauni milioni 500.

    Ripoti ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi ya Uingereza (NAO) imetabiri kuwa awamu inayofuata ya kupunguza matumizi katika BBC itakuwa kali zaidi kuliko iliyopita, na athari zake zitaonekana zaidi kwa wasikilizaji na watazamaji.

    BBC imeikaribisha ripoti hiyo, ikisema kwa muda mrefu imekuwa ikieleza kuwa mfumo wa sasa wa ufadhili wa shirika hilo hauwezi kuendelea kwa namna endelevu na unahitaji kufanyiwa marekebisho.

    Ripoti ya NAO pia imesema hatua za sasa zinatarajiwa kupunguza idadi ya wafanyakazi wa BBC kwa asilimia 11 ndani ya miaka mitatu.

    Mkuu wa NAO, Gareth Davies, amesema: "Kwa kuwa BBC imebakiza chini ya mwaka mmoja na nusu kabla ya kufanya upya hati yake ya uendeshaji, hakuna shaka kuwa inakabiliwa na maamuzi magumu."

    Hali ya kifedha ya BBC imeendelea kuwa mbaya katika miaka ya hivi karibuni kutokana na kupungua kwa mapato yatokanayo na ada ya leseni ya televisheni na kuongezeka kwa gharama za utayarishaji wa vipindi.

    NAO imesema hadi sasa BBC imepunguza matumizi kwa kupunguza idadi ya wafanyakazi, kupunguza mali na miundombinu inayosimamia, kuboresha teknolojia, kurahisisha taratibu za kazi pamoja na kubadilisha aina na wigo wa vipindi na huduma inazotoa.

    BBC tayari imetangaza mipango ya kupunguza matumizi yake kwa takribani asilimia 10. Hatua hizo zinajumuisha kupunguza wafanyakazi katika idara zake za habari, huduma za kitaifa na kikanda nchini Uingereza pamoja na idara nyingine zinazozalisha vipindi.

    Unaweza pia kusoma:

  11. Ikulu ya White House yamfuta kazi mkuu wa usalama wa mtandao baada ya hitilafu kubwa za mifumo

    Mkuu wa usalama wa mtandao wa Marekani, Sean Cairncross, amefutwa kazi yake, chanzo kilicho karibu na Ikulu ya White House kimeiambia AFP siku ya Alhamisi, kufuatia hitilafu kubwa za mifumo na kuongezeka kwa wasiwasi kuhusu vitisho vinavyotokana na akili mnemba (AI).

    Rais wa Marekani Donald Trump aliunga mkono kikamilifu uamuzi huo kwa madai kuwa Cairncross hakuwa na sifa stahiki za kutekeleza majukumu ya nafasi hiyo, chanzo hicho kimesema.

    Majukumu yake yatatekelezwa kwa muda na Kirsten Davies, ambaye kwa sasa ni Afisa Mkuu wa Teknolojia ya Habari katika Wizara ya Ulinzi. Chanzo hicho kimesema Davies ana sifa zinazofaa zaidi kwa nafasi hiyo na tayari amethibitishwa na Seneti.

    Katika siku na wiki za hivi karibuni, hitilafu kubwa za mifumo nchini Marekani zimeathiri usafiri, mawasiliano na biashara za mtandaoni kwa watumiaji wengi. Hitilafu hizo pia ziliathiri mtandao wa ndani wa mawasiliano wa siri za juu katika Shirika la Usalama wa Taifa (NSA).

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, alimpongeza Davies kupitia mtandao wa X, akiandika: "Hongera kwa Mkurugenzi mpya wa Usalama wa Mtandao wa Taifa, Kirsten Davies. Natarajia kufanya kazi pamoja naye kuimarisha usalama wa mtandao wa Marekani."

    Kabla ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Usalama wa Mtandao wa Taifa, Cairncross alihudumu katika nyadhifa mbalimbali ndani ya Ikulu ya White House wakati wa muhula wa kwanza wa utawala wa Trump.

    Unaweza pia kusoma:

  12. Pakistan inatarajiwa kuwa nchi yenye idadi kubwa zaidi ya Waislamu duniani ifikapo mwaka 2070

    Utafiti mpya uliofanywa na Kituo cha Utafiti cha Pew (Pew Research Center) umeonesha kuwa idadi ya Waislamu duniani inaweza kuizidi ile ya Wakristo.

    Utafiti huo unatabiri kuwa ifikapo mwaka 2070, Pakistan inaweza kuipiku Indonesia na kuwa nchi yenye idadi kubwa zaidi ya Waislamu duniani, huku India ikishika nafasi ya pili. Aidha, idadi ya Wakristo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) inaweza kuizidi ile ya Marekani.

    Makadirio ya Pew yanaashiria mabadiliko makubwa katika mgawanyo wa idadi ya watu na dini katika eneo la Asia Kusini.

    Pakistan inatarajiwa kuipiku Indonesia kwa idadi ya Waislamu, huku India ikifuata katika nafasi ya pili. Bangladesh nayo inatarajiwa kushuhudia ongezeko kubwa la idadi ya Waislamu.

    Utafiti huo unatoa makadirio ya namna dini mbalimbali duniani zinavyoweza kuwa katika kipindi cha miaka 50 ijayo. Unategemea takwimu zilizokusanywa kutoka nchi na maeneo 201, zinazojumuisha karibu watu wote duniani.

    Unaweza pia kusoma:

  13. Kiboko maarufu zaidi duniani, Fiona, afariki baada ya kumeza kofia iliyosokotwa kwa nyuzi

    Fiona, kiboko ambaye alikuwa maarufu zaidi duniani tangu kuzaliwa kwake mwaka 2017, amefariki kwa huzuni katika Bustani ya Wanyama ya Cincinnati nchini Marekani baada ya kumeza kofia iliyosokotwa kwa nyuzi (knitted hat) ya mmoja wa wageni iliyokuwa imepeperushwa kwa bahati mbaya na upepo na kuingia kwenye eneo lake.

    "Tunashiriki habari hizi za kusikitisha kwa huzuni kubwa. Fiona hakuweza kuokolewa licha ya juhudi kubwa za timu yetu ya madaktari wa mifugo na wahudumu wa wanyama," bustani hiyo ilisema katika taarifa yake siku ya Alhamisi.

    Fiona alimeza kofia hiyo siku 10 kabla ya kufariki kwake, lakini mwanzoni hakukuwa na dalili zozote zilizoashiria kwamba angepata madhara makubwa kiasi hicho.

    "Tumeshtuka sana kwa sasa. Hatukutarajia hili. Alipambana hadi dakika ya mwisho," alisema mkurugenzi wa bustani hiyo, Dave Jenaik.

    Fiona alizaliwa Januari 2017 akiwa njiti sana, akiwa na uzito wa kilo 13 pekee, ambao ni takribani theluthi moja ya uzito wa kawaida wa mtoto wa kiboko.

    Wahudumu wa bustani hiyo walianza kusimulia hatua kwa hatua maisha ya Fiona kupitia mitandao ya kijamii, wakionesha jinsi alivyopambana kuishi, kukua, kuogelea na kucheza. Jambo hilo lilimfanya kuwa maarufu duniani kote.

    Umaarufu wake ulifikia hatua ya ladha ya aiskrimu kupewa jina lake, huku picha yake pia ikitumika katika onesho la ballet la The Nutcracker lililoandaliwa na kikundi cha sanaa cha eneo la Cincinnati.

    Kifo chake pia kimekuja kabla ya wakati wake, kwani kwa mujibu wa wataalamu wa Bustani ya Wanyama ya Cincinnati, viboko wanaweza kuishi hadi miaka 50 wanapotunzwa kwenye mazingira ya kifungoni.

    Unaweza pia kusoma:

  14. Baraza la Ushirikiano wa Ghuba laitetea UAE, lakosoa serikali ya Somalia

    Katibu Mkuu wa Baraza la Ushirikiano wa Ghuba (GCC), Jassim Mohamed Al-Budeywi, amelaani kile alichokitaja kuwa kauli zisizowajibika na kampeni ya vyombo vya habari inayolenga Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), inayodaiwa kuendeshwa na maafisa wa serikali ya shirikisho la Somalia.

    Katika taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti rasmi ya Baraza hilo, Al-Budeywi amesema UAE ina mchango mkubwa katika kuimarisha usalama na utulivu pamoja na kuhamasisha mazungumzo kati ya mataifa.

    Ametolea mfano wa UAE kuandaa duru ya hivi karibuni ya mazungumzo kati ya Urusi na Ukraine, akisema hatua hiyo inaonesha nafasi ya nchi hiyo katika kutafuta amani na utulivu katika ngazi za kikanda na kimataifa.

    Ameongeza kuwa tuhuma zinazoelekezwa dhidi ya UAE zinadhoofisha juhudi za nchi hiyo za kuimarisha mazungumzo na ushirikiano ndani ya ukanda huo na kimataifa.

    Katibu Mkuu huyo amesema nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano wa Ghuba zitaendelea na juhudi za kuimarisha usalama, utulivu na maendeleo, huku zikipinga vikali kampeni yoyote ya vyombo vya habari inayolenga kuharibu sifa ya nchi mwanachama.

    Kwa upande wake, Umoja wa Falme za Kiarabu umekosoa uamuzi wa Somalia wa kumfukuza balozi wake nchini humo, ukiutaja kuwa hatua isiyo na uhalali na yenye uhasama.

    Rais wa Somalia ameituhumu UAE kwa kuunga mkono tawala za kikanda zinazopinga serikali ya shirikisho iliyoko Mogadishu.

    Unaweza pia kusoma:

  15. Wall Street Journal: Mkuu wa Mossad ataka mashambulizi mapya ya pamoja dhidi ya Iran

    Gazeti la Marekani la The Wall Street Journal limeripoti kuwa mkuu wa shirika la ujasusi la Israel, Mossad, Roman Goffman, alitoa wito wa kuanzishwa tena kwa mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel dhidi ya Iran wakati wa ziara yake nchini Marekani wiki iliyopita.

    Gazeti hilo lilisema kuwa watu wanaofahamu mazungumzo hayo waliliambia kuwa pendekezo hilo lilitolewa wakati Rais wa Marekani, Donald Trump, akiripotiwa kutafakari hatua anazoweza kuchukua dhidi ya Tehran.

    Roman Goffman, mkuu wa Mossad na mshirika wa karibu wa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alikutana na maafisa wa utawala wa Trump mjini Washington siku ya Ijumaa. Miongoni mwa maafisa aliokutana nao ni John Ratcliffe, mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA).

    Kwa mujibu wa vyanzo vilivyonukuliwa na The Wall Street Journal, Goffman aliwasilisha taarifa za kijasusi kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran ambazo Israel ilikuwa imezipata.

    Vyanzo hivyo viliongeza kuwa mkuu huyo wa Mossad alitoa wito wa kuanzishwa kwa kampeni mpya ya mashambulizi ya anga dhidi ya Iran, ambayo ingedumu kwa siku kadhaa.

    Iran imeonya dhidi ya kuanzishwa kwa vita vingine.

    Maafisa wa kisiasa na kijeshi nchini humo, akiwemo Mohsen Rezaei, katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, wamesema kuwa iwapo vita vitaanza tena, Iran itapanua wigo wa mapigano na kuyafanya yahusishe eneo zima la Mashariki ya Kati.

    Unaweza pia kusoma:

  16. Pentagon: Gharama ya vita dhidi ya Iran yazidi dola bilioni 48

    Afisa wa Pentagon ametangaza Alhamisi kuwa gharama za vita dhidi ya Iran zimezidi dola bilioni 48 tangu mzozo huo ulipoanza mwishoni mwa Februari.

    “Makadirio hayo yanajumuisha gharama za risasi, vifaa vinavyohitaji kubadilishwa na gharama za uendeshaji,” Naibu Mkuu wa Fedha wa Pentagon, Arthur Miller, alisema katika kikao cha Seneti kilicholenga kuchunguza sifa zake za kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Navy anayeshughulikia usimamizi wa fedha.

    Kiasi hicho hakijajumuisha uharibifu wa kambi za kijeshi za Marekani Mashariki ya Kati wala silaha za kijeshi zilizoharibiwa katika maeneo hayo, ambazo baadhi zimeathiriwa pakubwa na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na makombora ya Iran.

    Hii ni taarifa ya kwanza kuhusu gharama za vita tangu katikati ya Oktoba, wakati makadirio ya Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) yaliyopatikana na CBS News, mshirika wa BBC nchini Marekani, yalipokadiria gharama hizo kuwa dola bilioni 47.1.

    Kwa mujibu wa makadirio ya awali, sehemu kubwa ya gharama hizo, takriban dola bilioni 29, ilihusishwa na kubadilisha silaha na risasi zilizotumika. Vifaa vilivyopotea, vikiwemo ndege na ndege zisizo na rubani, vilichangia pia takriban dola bilioni 6 za gharama hizo.

    Unaweza pia kusoma:

  17. Denmark: Mwanamke wa miaka 112 afichuliwa kuwa alikuwa kiongozi wa Wanazi

    Mwanamke mwenye umri mkubwa zaidi kuwahi kurekodiwa nchini Denmark amefichuliwa kuwa aliwahi kuwa kiongozi wa tawi la chama cha Nazi katika eneo aliloishi wakati wa uvamizi wa Ujerumani.

    Mwezi uliopita, raia wa Denmark walimpongeza Kirsten Schwalbe alipotimiza umri wa miaka 112 na siku 218, na hivyo kuwa mtu mwenye umri mkubwa zaidi kuwahi kurekodiwa nchini humo.

    Hata hivyo, siku mbili tu baada ya kutangazwa kuvunja rekodi hiyo, ilibainika kuwa aliwahi kuwa kiongozi wa chama cha Nazi katika eneo lake wakati wa uvamizi wa Ujerumani.

    Kumbukumbu zinaonesha kuwa Schwalbe alijiunga na chama cha mrengo mkali wa kulia cha Danish National Socialist Workers Party mwezi Agosti 1941, na baadaye kupanda vyeo hadi kuwa kiongozi wa muda katika mji wa Holstebro, kuanzia Agosti 1943 hadi Julai 1944.

    Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya ndani, pia aliongoza kundi la wanawake la chama hicho, huku mumewe aliyefariki akiwa na nafasi ya uongozi ndani ya chama hicho.

    Awali, Schwalbe alikanusha kuwahi kuwa mwanachama wa chama cha Nazi, kabla ya kupuuzia suala hilo kwa kudai kuwa hakufahamu vizuri itikadi ya chama hicho.

    Alisisitiza kuwa haikuwa haki kuchunguzwa kuhusu matendo yake wakati wa vita, akidai kuwa wakati huo wake hawakujihusisha na masuala hayo bali waliyaachia wanaume.

    “Mume wangu aliniomba, nami nikamwambia kuwa sikujali. Sikuwa na shauku na siasa, kwa hiyo nilifanya tu kile alichoona kinafaa,” alisema.

    Hata hivyo, wanahistoria waliochunguza kumbukumbu hizo walisema Schwalbe alikuwa na nafasi kubwa zaidi ndani ya chama hicho kuliko alivyokiri.

    Claus Bundgaard Christensen, mwanahistoria wa Denmark, alisema: “Hakuwa mwanachama wa kawaida tu. Alikuwa na nafasi kubwa zaidi ya kuwa mwanaharakati.”

    Chama cha Nazi nchini Denmark kilikuwa vuguvugu kubwa zaidi la kifashisti nchini humo, likiwa na mfumo uliofanana na chama cha Adolf Hitler nchini Ujerumani.

    Schwalbe alijiunga na chama hicho baada ya Ujerumani kuivamia Denmark mwaka 1940. Wakati huo, Wanazi wa Denmark walishirikiana na vikosi vya Wajerumani waliokuwa wakiikalia nchi hiyo, huku raia wa Denmark wakishawishiwa kujiunga na jeshi la Waffen-SS.

    Ukweli huo ulifichuliwa mwezi uliopita na gazeti la Denmark la Kristeligt Dagblad, lililomfanyia uchunguzi Schwalbe baada ya kuchapishwa kwa kitabu cha wasifu wake kilichoitwa We Need Something to Laugh About, ambacho hakikutaja historia yake ya uhusiano na chama cha Nazi.

    Familia ya Schwalbe iliambia vyombo vya habari vya ndani kuwa amekuwa “akiathirika sana” kutokana na taarifa hizo za vyombo vya habari, na kukataa kutoa maoni zaidi.

    Unaweza pia kusoma:

  18. Mchungaji amekutwa na hatia ya kuhusika na mauaji ya Rais wa Haiti

    Mchungaji mmoja kutoka jimbo la Florida nchini Marekani amepatikana na hatia ya makosa kadhaa yanayohusiana na mauaji ya aliyekuwa Rais wa Haiti, Jovenel Moïse.

    Christian Emmanuel Sanon, raia mwenye uraia wa Marekani na Haiti, amepatikana na hatia ya mashtaka yote manane yaliyokuwa yakimkabili, yakiwemo ya kula njama ya kumuua au kumteka nyara mtu. Anakabiliwa na uwezekano wa kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.

    Sanon, mwenye umri wa miaka 67, alishtakiwa kwa kuhusika katika mpango wa kumuondoa madarakani Moïse na kujichukua nafasi ya urais wa Haiti mwaka 2021. Inadaiwa kuwa alikusudia kufanya hivyo ili baada ya kushika madaraka, aweze kutoa mikataba yenye thamani kubwa kwa kampuni ya ulinzi yenye makao yake Florida.

    Mauaji ya Moïse yameiacha Haiti bila kiongozi kwa kipindi cha miaka mitano. Pengo hilo la uongozi limechangia kuongezeka kwa machafuko yanayosababishwa na magenge ya uhalifu katika taifa hilo maskini la eneo la Caribbean.

    Uchaguzi wa rais umepangwa kufanyika mwaka ujao, huku mke wa Moïse, Martine, ambaye alijeruhiwa katika shambulio lililomuua mumewe, akitangaza wiki hii kuwa anakusudia kugombea urais.

    Kwa mujibu wa CBS, mshirika wa BBC nchini Marekani, Sanon alipatikana na hatia siku ya Jumatano baada ya kesi iliyodumu kwa wiki nane katika mahakama ya shirikisho mjini Miami.

    Wakili wake amesema Sanon bado anasisitiza kuwa hana hatia na anakusudia kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.

    Waendesha mashtaka wamesema Sanon alikuwa na "matamanio ya kisiasa" nchini Haiti na kwamba mwezi Aprili 2021 alikutana na washirika wengine wa njama hiyo kupanga mpango wa kumuondoa Moïse madarakani kupitia shambulio la kutumia silaha katika kasri la rais mjini Port-au-Prince, mji mkuu wa nchi hiyo.

    Miongoni mwa washirika hao walikuwa wakuu wa kampuni za Counter Terrorist Unit Federal Academy na Counter Terrorist Unit Security, ambazo kwa pamoja zilijulikana kama CTU.

    Kampuni hizo zilitarajiwa kufadhili mapinduzi hayo kwa kubadilishana na kupata mikataba ya serikali ya kutekeleza miradi ya miundombinu, pamoja na kutoa vikosi vya ulinzi na vifaa vya usalama.

    Unaweza pia kusoma:

  19. Mwanamke aliyedungwa dawa na kubakwa na mumewe pamoja na wanaume wengine azungumza

    Mwanamke aliyedungwa dawa, kubakwa na kutangazwa mtandaoni kwa ajili ya ngono na mumewe amesema "hatawahi kujisikia salama kabisa" baada ya wanaume wanne kupatikana na hatia ya kumfanyia unyanyasaji wa kingono, katika kesi ya kwanza ya aina hiyo nchini England.

    Joanne Young, ambaye ameamua kuondoa haki yake ya kutotajwa jina, amesema: "Mtu niliyemwamini zaidi duniani alinigeuka na kunisaliti kwa njia ya kutisha zaidi."

    Philip Young, mwenye umri wa miaka 50, tayari alikuwa amekiri makosa mbalimbali ya kumdunga dawa na kumbaka mkewe kwa kipindi cha miaka 13 katika nyumba yao mjini Swindon, Wiltshire. Aliwaalika wanaume kupitia tovuti na programu kama Craigslist, Grindr na Fab Swingers kwenda nyumbani kwao bila mkewe kujua.

    Siku ya Alhamisi, Norman Macksoni, 48, Richard Wilkins, 62, Connor Sanderson-Doyle, 32, na Mohammed Hassan, 38, walipatikana na hatia ya makosa mbalimbali ya kingono na jopo la majaji katika Mahakama ya Winchester Crown. Wilkins na Macksoni kila mmoja alipatikana na hatia ya kosa moja la ubakaji.

    Joanne Young, ambaye alitalikiana na Philip Young mwaka jana, amesema unyanyasaji huo "umeninyang'anya maisha yangu kama nilivyokuwa nikiyafahamu".

    Akizungumza nje ya mahakama, alisema: "Kilichonitokea hakikuwa kitendo cha mtu mmoja pekee, wengine walialikwa kushiriki na wao wakachagua kufanya hivyo."

    Joanne Young amesema uhalifu uliofanywa dhidi yake umekuwa na "athari kubwa na ya kutisha kwa maisha yangu na ya watoto wangu".

    Alisema: "Ninaishi na maumivu ambayo ni vigumu kuyaelezea kwa maneno, na jambo hili litaathiri maisha yetu milele. Inatisha kufikiria kuwa jambo hili linaweza kumtokea mtu yeyote."

    Unaweza pia kusoma:

  20. Ulaya yataka kushiriki mazungumzo ya amani Ukraine, Putin aweka masharti

    Viongozi wa Ulaya wamesema wako tayari kufanya mazungumzo na Urusi kuhusu kumaliza vita vya Ukraine, katika ishara kubwa ya kuunga mkono Kyiv.

    "Ulaya ina msimamo wa wazi, thabiti na wa pamoja katika mazungumzo," amesema Waziri Mkuu wa Uingereza, Andy Burnham, huku Kansela wa Ujerumani, Friedrich Merz, akisisitiza kuwa "madai ya Moscow ya kutaka mambo mengi kupita kiasi si ya kweli".

    Viongozi hao walikuwa wakizungumza katika mkutano wa Berlin wa washirika wa Ukraine, unaojulikana kama Coalition of the Willing.

    Jared Kushner, mkwe wa Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye ni mmoja wa wajumbe wawili wa Marekani waliokuwa Berlin, amesema rais huyo anataka kufikia makubaliano na Moscow "akiwa na Ulaya upande wake". Hata hivyo, Rais wa Russia Vladimir Putin amekuwa akikataa hadi sasa Ulaya kushiriki katika mazungumzo ya amani yanayoongozwa na Marekani.

    Trump awali alifanya mazungumzo ya kihistoria ya pande tatu mjini Shenzhen, kusini-mashariki mwa China, na Putin pamoja na Rais wa China Xi Jinping, na baadaye alishiriki kwa njia ya simu katika mkutano wa Berlin akiwa ndani ya ndege ya Air Force One.

    Katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofuata mazungumzo hayo na Trump pamoja na Xi, Putin alizungumzia suala la mazungumzo ya amani yanayohusisha mataifa mbalimbali, akisema Marekani imekuwa ikiitaka Russia "kwa msisitizo" kuruhusu mataifa ya Ulaya kushiriki.

    Putin alidai Urusi haipingi wazo hilo, lakini alisema Moscow inataka kufahamu "Ulaya italeta nini katika mazungumzo hayo".

    "Ndiyo maana, kupitia njia za kidiplomasia, tumewaalika mataifa ya Ulaya kuja Moscow ili kubainisha misimamo yao. Baada ya hapo, tutaamua ni kwa mfumo gani tutaendeleza mazungumzo na Ukraine," alisema.

    Unaweza pia kusoma: