Kombe la Dunia 2026: Kwa nini kuna wachezaji wengi wanaochezea mataifa ambayo hawakuzaliwa?

    • Author, Fernando Duarte
    • Nafasi, BBC World Service
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Kwa dakika 25 tarehe 13 Juni, Morocco iliweka historia ya Kombe la Dunia wakati wa sare yao ya 1-1 na Brazil – kwa kutokuwa na mchezaji hata mmoja aliyezaliwa Morocco.

Kombe la Dunia la Wanaume la Fifa la 2026 lina idadi kubwa ya wachezaji wanaowakilisha nchi ambazo hawakuzaliwa - karibu robo ya wachezaji wote wanaoshiriki.

Tayari mashindano hayo yameshuhudia mchezaji akifunga dhidi ya taifa lake la kuzaliwa, wakati Ibrahim Mbaye, mzaliwa wa Ufaransa, alipoifungia Senegal bao katika ushindi wao wa 3-1 dhidi ya Les Bleus Juni 16.

Mwaka 2022, mshambuliaji wa Uswisi Breel Embolo, aliyezaliwa nchini Cameroon, alikuwa mchezaji wa kwanza katika historia ya zaidi ya miaka 90 ya mashindano hayo kufunga bao dhidi ya taifa lake la kuzaliwa.

Badala ya kurukaruka kwa ushindi na furaha, aliinua mikono yake kwa muda mfupi ishara ya kuomba msamaha.

"Nilijua kwamba kama ningefunga nisingeshangilia bao hilo, kuonesha heshima. Hata hivyo, hilo halikumaanisha kuwa sikuwa na furaha na bao hilo," Embolo aliwaambia waandishi wa habari wakati huo.

Katika Kombe la Dunia la 2026, ni timu nane tu kati ya 48 hazina mchezaji aliyezaliwa nje ya nchi, kulingana na orodha rasmi za vikosi zilizowasilishwa kwa shirikisho linaloongoza la soka duniani Fifa.

Curacao, timu inayoshiriki Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza, ina mchezaji mmoja tu aliyezaliwa katika kisiwa cha Karibi kama sehemu ya kikosi chao cha wachezaji 26. Nchi hiyo ni sehemu ya Ufalme wa Uholanzi na wengi wa wachezaji wake wamezaliwa Uholanzi.

Wakati huo huo Qatar imeleta wachezaji kutoka mataifa 10, kuanzia Afrika hadi Ulaya na Amerika Kusini.

Mabadiliko kama hayo yameunda mgawanyiko wa kifamilia.

Ndugu wanne wanawakilisha timu tofauti: Desire na Guela Doue (Ufaransa na Ivory Coast), Nico na Iñaki Williams (Hispania na Ghana), Harry na John Souttar (Australia na Scotland) na kaka wa kambo Derrick Luckassen na Brian Brobbey (Ghana na Uholanzi).

Kabla ya 2026, hili lilitokea mara mbili tu - wakati kaka wa kambo Jerome na Kevin Prince Boateng walipocheza katika Kombe mbili za Dunia (2010 na 2014) wakiwakilisha Ujerumani na Ghana. Walikabiliana uwanjani mara zote mbili.

Profesa Gijsbert Oonk, mwanahistoria wa Uholanzi na mtaalamu wa masomo ya uhamiaji na utambulisho katika Chuo Kikuu cha Erasmus nchini Uholanzi, anasema mwelekeo huo ni kielelezo cha mabadiliko ya ulimwengu.

"Karibu 4% ya idadi ya watu duniani wanaishi katika nchi ambayo hawakuzaliwa. Ikijumuisha wafanyakazi na wana michezo," anaelezea. "Ni kielelezo cha maisha ya uhamaji."

Mabadiliko ya Ulimwengu

Idadi ya wachezaji waliozaliwa katika nchi nyingine katika timu za Kombe la Dunia imeongezeka na kushuka.

Kulingana na utafiti kutoka Kitivo cha Uhamiaji, Sera na Jamii cha Chuo Kikuu cha Oxford (COMPAS), asilimia ilibaki kati ya 2 na 14 hadi mashindano mawili ya mwisho kabla ya kuongezeka na kufikia 16.5% nchini Qatar 2022.

Kiwango hicho kimeongezeka zaidi hadi 23% mwaka 2026 - huku jumla ya wachezaji waliozaliwa katika nchi nyingine ikifikia 289 kati ya 1,248, huku idadi ya timu zinazoshindana zikiongezeka kutoka 32 hadi 48.

Fifa iliundwa mwaka 1904, lakini ilianzisha sheria rasmi za utaifa katika miaka ya 1960. Hadi wakati huo, wachezaji wangeweza kuchezea nchi yoyote waliyochagua.

Mfano maarufu zaidi ni Luis Monti. Kiungo wa kati wa Argentina aliiwakilisha nchi yake katika Kombe la Dunia la 1930, ambapo timu yake ya Amerika Kusini ilimaliza wa pili. Kisha akabadilisha utaifa na kujiunga na Italia kwa mashindano ya 1934, akishinda kombe pamoja nao.

Monti anasalia kuwa mtu pekee aliyecheza fainali za Kombe la Dunia kwa mataifa mawili tofauti.

1962, Fifa ilitoa vigezo, ikiamuru wachezaji lazima wawe na uraia wa nchi wanayotaka kuichezea, na hawawezi tena kuwakilisha zaidi ya taifa moja.

Isipokuwa kwa wachezaji ambao uraia wao ulibadilika bila hiari, kama vile wachezaji kutoka USSR ya zamani na Yugoslavia.

Mabadiliko zaidi yalikuja mwaka 2004, wakati Fifa ilipoanza kuruhusu wachezaji kuwakilisha nchi moja katika ngazi ya vijana na kuhamia nyingine katika ngazi ya wakubwa.

Hata hivyo, pia ilieleza kwamba mchezaji anapaswa kuwa na "uhusiano wa wazi" na nchi - angalau mzazi mmoja au babu au bibi aliyezaliwa nchini humo, au awe mkazi kwa angalau miaka miwili.

Tangu wakati huo, sharti la makazi limeongezeka hadi miaka mitano, huku wachezaji sasa wakiruhusiwa kubadili timu ikiwa wamecheza mechi tatu au chache za kimataifa za wakubwa kabla ya umri wa miaka 21.

Watazame Simba wa Atlas

Mabadiliko haya ya sheria yamekuwa habari njema kwa mataifa yanayoitwa yenye wachezaji waliozaliwa nje, ambapo sehemu kubwa ya raia wao wameenea kote ulimwenguni - kama Morocco.

Katika miaka ya 2010, katika harakati za kuboresha ubora wa soka lake, nchi hiyo iliweka wafuatiliaji katika nchi za Ulaya zenye jumuiya kubwa za Morocco, kama vile Ufaransa, Uholanzi na Ubelgiji.

Kuongezeka kwa vipaji kutoka kwa wachezaji waliozaliwa nje ni moja ya sababu zilizochangia ubora wa soka ya Morocco: kuwa taifa la kwanza la Afrika kufikia nusu fainali ya Kombe la Dunia, huko Qatar 2022.

Wachezaji wawili kati ya watatu wa Morocco waliofunga wakati wa mikwaju ya penalti ya robo fainali hawakuzaliwa Morocco - Hakim Ziyech mzaliwa wa Uholanzi, na Achraf Hakimi, ambaye alifunga dhidi ya taifa lake la kuzaliwa, Uhispania.

"Hii ni hadithi ya nchi ambayo imejifunza kuwathamini watu wake walio nje ya nchi, kuwa ni sehemu muhimu ya mfumo wake wa soka wa kitaifa," anasema Dkt. Myriam Cherti, mtafiti wa COMPAS.

Uamuzi 'kutoka moyoni'

Dkt. Cherti anasema chaguo za wachezaji wa mpira wa miguu zinaweza kuchochewa na "taaluma, hisia na siasa", ikiwa ni pamoja na matarajio ya kifamilia au fursa za kimataifa.

Kwa mfano, Ibrahim Mbaye aliwahi kuichezea Ufaransa katika ngazi zote za vijana, lakini alitangaza mwaka jana, akiwa na umri wa miaka 17, kwamba ataichezea Senegal, nchi ya kuzaliwa ya mama yake.

"Sitajuta kamwe kuchagua kuichezea Senegal kwa sababu ilikuwa uamuzi kutoka moyoni," alimwambia mtangazaji wa Senegal RTS wakati huo.

Wengine, kama vile beki wa zamani wa Real Madrid, Pepe, walichagua kuiwakilisha nchi ambayo wamepewa uraia.

Kulingana na vyombo vya habari vya Brazil vinavyomnukuu baba yake, Pepe alikataa kuiwakilisha Brazil mwaka 2006 na badala yake akachagua Ureno, ambapo amekuwa akiishi na kucheza tangu mwaka 2001.

Aliishia kukutana na nchi yake ya kuzaliwa katika mechi kali ya hatua ya makundi kwenye Kombe la Dunia la 2010.

"Sikujutia kamwe uamuzi wangu wa kuwa Mreno," alisema katika mkutano na waandishi wa habari wakati huo.

Wakati mwingine kuajiriwa. 2018, Roberto Lopes mzaliwa wa Dublin, ambaye baba yake anatoka Cape Verde, alipokea ujumbe kutoka kwa meneja wa nchi hiyo Rui Aguas kupitia LinkedIn, akiuliza kama angependa kuichezea timu ya taifa.

Lopes, ambaye anachezea Shamrock Rovers ya Ireland, alipuuza ujumbe huo kwa miezi kadhaa akidhani ni uongo, kabla ya kutambua kosa lake. "Nilijiona mkorofi," Lopes aliambia BBC Sport.

Beki huyo aliendelea kuwa mmoja wa mashujaa wa sare ya bila bila kati ya Cape Verde na mabingwa wa Ulaya, Uhispania tarehe 15 Juni.

Utata na mgawanyiko

Hata hivyo, kile kinachoitwa "kuchagua bendera" hakiji bila utata.

Sepp Blatter, rais wa Fifa kuanzia 1998 hadi 2015, alionya mwaka 2007 kwamba Kombe la Dunia linalotawaliwa na timu "zilizojaa wachezaji wa Brazil" ni "hatari.”

Mshambuliaji wa Uhispania aliyezaliwa Brazil, Diego Costa, alizomewa na umati wa watu katika Kombe la Dunia la 2014 - ilipochezwa Brazil - kwa kuchagua kuwakilisha Ulaya.

Profesa Gijsbert Oonk, anayefundisha wanafunzi wa mataifa mbalimbali, anasema suala hilo linaleta mgawanyiko kila wakati linapoibuliwa katika mihadhara yake.

Baadhi wanasema mashabiki "hawawezi kujitambulisha na nchi zao tena" ikiwa timu inategemea wachezaji waliozaliwa nje, anasema. "Lakini wengine huchukua mtazamo wa haki za binadamu na kusema 'waacheni, ni kazi yao, mapato yao'," anaongeza.

Kwa Dkt. Cherti, mpira wa miguu hauwezi kubaki bila mabadiliko ya kijamii: "Timu ya taifa si kielelezo tu cha idadi ya watu wa ndani. Ni kielelezo cha uhamiaji, historia na safari za kimataifa."