Kylie Jenner azua mjadala baada ya kuvaa sidiria yenye thamani ya dola milioni 50
Nyota wa vipindi vya uhalisia, Kylie Jenner, amezua hisia mseto baada ya kushiriki kwa mara ya kwanza katika maonyesho ya mitindo ya Victoria’s Secret, akiwa amevalia sidiria yenye thamani ya dola milioni 50, sawa na takriban pauni milioni 37.
Mjasiriamali huyo wa vipodozi aliwashangaza watazamaji katika maonyesho ya kila mwaka ya kampuni hiyo ya nguo za ndani siku ya Jumapili, alipovaa sidiria maarufu ya Fantasy Bra, iliyotengenezwa kwa dhahabu ya karati 18 na almasi 4,410, kwa mujibu wa mbunifu wake.
Kwa miaka mingi, Fantasy Bra imekuwa sehemu muhimu ya maonyesho hayo, huku kuchaguliwa kuivaa kukichukuliwa kama heshima kubwa na hatua muhimu katika taaluma ya mwanamitindo.
Baadhi ya mashabiki walifurahia kuchaguliwa kwa Jenner, mwenye umri wa miaka 29 na nyota wa kipindi cha The Kardashians. Hata hivyo, wengine waliikosoa kampuni hiyo kwa kutompa fursa mwanamitindo mkongwe.
Mtaalamu wa mitandao ya kijamii na masoko, Joel Marlinarson, amesema hatua hiyo ilipangwa kwa makini na kuzua mjadala mkubwa kuhusu mustakabali wa uanamitindo na mitandao ya kijamii.
Ameiambia BBC Newsbeat kuwa Jenner anawakilisha kizazi kipya cha umaarufu, ambapo kampuni zinatanguliza watu wanaoweza kuvutia watazamaji wengi badala ya kuzingatia vigezo vya kawaida vya mwanamitindo.
Marlinarson amesema watazamaji vijana wanajihisi kuwa karibu na Jenner kwa sababu wamekua wakimfuatilia kwenye mitandao ya kijamii na kupitia kipindi chake cha uhalisia pamoja na dada zake wa familia ya Kardashian.
Hata hivyo, amesema baadhi ya watazamaji wanaokumbuka enzi ya mwanamitindo maarufu Naomi Campbell wanaweza kuona kupewa kwa Jenner fursa hiyo kuwa ni usaliti wa kile walichokizoea katika ulimwengu wa mitindo.