Wakenya wawili wahusishwa na ulaghai wa mikopo ya wanafunzi Marekani
Wizara ya Sheria ya Marekani imesema imebaini mtandao mkubwa wa ulaghai wa msaada wa fedha kwa wanafunzi, ambao unadaiwa kubadhirifu mamilioni ya dola zilizokusudiwa kuwasaidia wanafunzi wa Marekani kupitia mtandao wa ulaghai unaohusishwa na raia wa Kenya.
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Marekani, Colin McDonald, amesema Kitengo cha Kitaifa cha Utekelezaji wa Sheria dhidi ya Ulaghai, kwa kushirikiana na taasisi nyingine za serikali, kilifanya ziara nchini Kenya mwezi Septemba mwaka huu, na kukamata zaidi ya dola 750,000 za Marekani, sawa na shilingi milioni 97.44 za Kenya, kutoka katika akaunti ya sarafu za kidijitali ya cryptocurrency inayomilikiwa na raia wa Kenya anayedaiwa kuhusishwa na mtandao huo wa ulgahai.
"Hii ni mara ya kwanza katika historia ya Kitengo cha Kupambana na Ulaghai kukamata mali ya thamani ya aina hii nje ya Marekani," amesema.
McDonald amesema Wakenya wawili wanaoishi katika majimbo ya Nebraska na New Jersey ni miongoni mwa washukiwa watano wanaokabiliwa na mashtaka ya mtandao huo wa ulaghai, unaodaiwa kuhusisha uundaji wa akaunti za kughushi za maombi ya Shirikisho ya Msaada wa Kifedha kwa Wanafunzi (FAFSA), kwa kutumia taarifa za utambulisho zilizoibwa kutoka kwa raia wa Marekani.
"Wizara itawafungulia mashtaka washukiwa watano” McDonald amesema.Ameongeza kuwa, "Iwe uko Nebraska, New Jersey, Virginia au Nairobi, tutakufuatilia na kukupata."
Wizara hiyo imesema ulaghai huo ulibainika kupitia uchunguzi wa kitaifa uliopewa jina la Operation Ghostbusters, ambao ulifichua mtandao unaodaiwa kujihusisha na ulaghai kwa kutumia mfumo wa serikali wa kutoa misaada ya kifedha kwa wanafunzi tangu mwaka 2021.
Kwa mujibu wa Wizara ya Sheria, washukiwa hao waliiba taarifa za utambulisho za raia wa Marekani na kuzitumia kufungua akaunti za ghushi za FAFSA, huku wakisajili wanafunzi wasiokuwepo katika vyuo na taasisi za elimu ya juu.