Rais wa zamani wa Korea Kusini aliyeko gerezani ahukumiwa miaka 30 zaidi kwa kutuma droni Korea Kaskazini
Mahakama nchini Korea Kusini imemhukumu rais wa zamani, Yoon Suk Yeol, kifungo cha miaka 30 jela kwa kuhusika na operesheni ya kutuma droni ndani ya Korea Kaskazini.
Waendesha mashtaka walidai kuwa Yoon aliamuru operesheni hiyo mwezi Oktoba 2024 kwa lengo la kuichokoza Pyongyang na kuunda mazingira ya dharura ambayo yangetoa sababu ya kutangaza sheria ya kijeshi baadaye mwaka huo.
Yoon alipotangaza sheria ya kijeshi tarehe 3 Desemba, alidai kuwa alikuwa akilinda nchi dhidi ya "vikosi vinavyopinga taifa" ambavyo vinaunga mkono Korea Kaskazini.
Hata hivyo, baadaye ilibainika kuwa hatua hiyo ilichochewa zaidi na matatizo ya kisiasa ya ndani, na alilazimika kufuta amri hiyo baada ya maandamano makubwa ya wananchi.
Yoon tayari alikuwa ameondolewa madarakani kupitia mchakato wa kura ya kutokuwa na imani naye na alikuwa akitumikia kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya uasi kufuatia jaribio lake la kutangaza sheria ya kijeshi.
Mawakili wa Yoon Suk Yeol walidai kwamba hatua zake zilikuwa "halali" na zilikuwa jibu la uchokozi wa Korea Kaskazini kupitia kile walichokiita "maputo ya taka".
Hii ilikuwa ikirejelea tukio la mwaka 2024 ambapo Korea Kaskazini ilirusha mamia ya maputo kuvuka mpaka kuelekea Korea Kusini.
Baadaye iligundulika kuwa maputo hayo yalikuwa yamebeba taka, uchafu mbalimbali na kinyesi.
Nchi hizi mbili zimekuwa zikitumia mbinu ya "maputo ya propaganda" tangu wakati wa Vita vya Korea, ambapo ujumbe wa kisiasa au propaganda huwekwa ndani ya maputo hayo na kurushwa kuvuka mpaka kuelekea upande mwingine.
Kwa miaka mingi, maputo hayo yametumiwa kusambaza ujumbe wa kisiasa, vipeperushi, habari na propaganda kati ya Korea Kaskazini na Korea Kusini kama sehemu ya vita vya kisaikolojia kati ya nchi hizo mbili.
Unaweza kusoma;