Ufaransa inataka nini kipya Afrika?

Shugaban Faransa, Macron da shugaban Kenya Ruto

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Maelezo ya picha, Rais wa Ufaransa, Macron na Rais wa Kenya, William Ruto
    • Author, Akisa Wandera
    • Nafasi, BBC Africa
    • Akiripoti kutoka, Nairobi
    • Author, Hafsa Khalil
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Baada ya Ufaransa kushutumiwa kwa kuingilia masuala ya nchi za Afrika kwa mtindo unaofanana na ukoloni katika baadhi ya mataifa ambayo imekuwa na uhusiano nayo kwa muda mrefu, sasa nchi hiyo inajaribu kupanua ushirikiano wake kwa kuandaa mkutano wa kwanza kabisa wa viongozi wa Afrika nchini Kenya, huku lugha ya Kiingereza ikitumika kama lugha kuu ya mawasiliano.

Akizungumza katika Mkutano wa Maendeleo wa Afrika jijini Nairobi siku ya Jumatatu, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alitangaza uwekezaji wa dola bilioni 27 za Marekani barani Afrika katika sekta kama nishati, teknolojia, akili bandia (AI), uchumi wa bahari na kilimo.

Macron alisema:

"Afrika inaendelea kukua. Ni bara lenye idadi kubwa zaidi ya vijana duniani, na linahitaji mtaji ili liweze kujitegemea."

Aliongeza kuwa uwekezaji huo utasaidia kutengeneza ajira zipatazo 250,000 barani Afrika na nchini Ufaransa.

Pia alieleza kuwa Ufaransa haiji Afrika kwa lengo la kuwekeza pekee, bali pia inataka wafanyabiashara wakubwa wa Afrika wawekeze nchini Ufaransa.

Mkutano huo wa siku mbili ulilenga kupanua ushirikiano wa Paris na nchi za Afrika pamoja na kuunda makubaliano ya uwekezaji, katika kipindi ambacho chuki dhidi ya Ufaransa inaonekana kuongezeka katika baadhi ya nchi ilizowahi kuzitawala, hasa Afrika Magharibi.

Tangu nchi nyingi za Afrika zipate uhuru katika miaka ya 1960, Ufaransa imeendelea kuwa na uhusiano wa karibu wa kiuchumi, kisiasa na kiusalama na makoloni yake ya zamani, jambo ambalo limeifanya kushutumiwa kwa kuendelea kuzifungamanisha nchi hizo na ushawishi wake.

Mmchambuzi kutoka Senegal, Gilles Yabi, aliiambia BBC kuwa kizazi kipya cha Waafrika kinataka "kufunga ukurasa wa ukoloni na kipindi cha baada ya ukoloni."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Musalia Mudavadi, pia alisema mkutano huo ni fursa kwa Afrika kuanza kuzungumza kwa sauti moja.

Aliongeza kuwa kuandaa mkutano huo katika nchi ya Afrika ambayo haitumii Kifaransa ni ujumbe mkubwa unaoonyesha kuwa mawasiliano kati ya nchi hayapaswi kutegemea lugha pekee.

....

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Maelezo ya picha, Wengi walijitokeza kupiga picha na Rais wa Ufaransa, Macron
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mudavadi alisema huu ni "wakati muhimu" kwa Kenya na Ufaransa kushughulikia tatizo la tofauti za lugha lililosababishwa na mgawanyiko wa nchi za Afrika kuwa za Kiingereza, Kifaransa au Kireno, hali ambayo amesema inazuia mshikamano kamili wa bara hilo.

Aliongeza kuwa Kenya ni nchi muhimu katika diplomasia na mikutano ya kimataifa. Kwa mujibu wake, mkutano huo ulijikita katika masuala ya amani na usalama pamoja na kuangazia ushirikiano wa kiuchumi kati ya Afrika na mataifa mengine duniani, ikiwemo Ufaransa.

Viongozi wa kijeshi waliotwaa madaraka nchini Burkina Faso, Mali na Niger, ambazo zote ni makoloni ya zamani ya Ufaransa, waliwafukuza wanajeshi wa Ufaransa waliokuwa wakisaidia kupambana na waasi na wanajihadi katika eneo hilo, na badala yake wakageukia Urusi kwa msaada wa kiusalama.

Kabla ya mkutano huo, Rais Macron alitetea uamuzi wa kupunguza idadi ya wanajeshi wa Ufaransa barani Afrika, akisema kuondoka kwao hakukuwa "fedheha" bali ni hatua inayolingana na hali ya sasa.

Macron alisema:

"Tulipogundua kuwa uwepo wetu hauhitajiki tena baada ya mapinduzi ya kijeshi, tuliondoka."

Aliongeza kuwa anaamini nchi hizo na viongozi wake, hata wale waliofanya mapinduzi, wanapaswa kuruhusiwa kuchagua njia wanayotaka kufuata.

Hakuna viongozi kutoka Burkina Faso, Mali na Niger waliohudhuria mkutano huo.

Kwa sasa, Djibouti ndiyo nchi pekee yenye kambi ya kudumu ya kijeshi ya Ufaransa barani Afrika, iliyopo kandokando ya Bahari ya Shamu.

Mwanasiasa Gilles Yabi alisema kuwa kufanyika kwa mkutano huo nchini Kenya ni ishara ya mabadiliko katika uhusiano kati ya Afrika na Ufaransa.

Aliiambia kipindi cha BBC cha Newsday kwamba hili siyo tu jibu la Ufaransa kwa kuzorota kwa uhusiano wake na baadhi ya nchi za Afrika Magharibi, bali ni mkakati ambao imekuwa ikiujenga kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa Yabi, Ufaransa imegundua kuwa lazima itafute fursa mpya za uwekezaji nje ya makoloni yake ya zamani ya Afrika Magharibi na Afrika ya Kati.

Wakati Kenya na Ufaransa zote zikitarajia kupata faida za kiuchumi kutokana na kuandaa mkutano huo wa siku mbili Mei 11-12, Paris pia inajaribu kuonyesha kuwa bado ina ushawishi mkubwa barani Afrika, wakati ambapo mataifa kama China, Urusi na Uturuki yanaendelea kuongeza ushawishi wao katika bara hilo.

Akizungumza kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi siku ya Jumatatu, Rais Macron alisema Afrika inahitaji uwekezaji ili kufikia uhuru kamili na kujitegemea.

Alisema bara hilo "halihitaji kuendelea kutaka kusikia viongozi wa Ulaya wakiliambia linahitaji nini."

Macron pia alisema hataki Ufaransa kuendelea kuichukulia Afrika kama eneo maalum lililo chini ya ushawishi wake wa moja kwa moja, ambapo wafanyabiashara wa Kifaransa wanaamini wana haki ya kupata kandarasi kwa sababu tu nchi hizo zinatumia Kifaransa.

Zaidi ya viongozi 30 wa Afrika walihudhuria mkutano huo, pamoja wafanyabiashara wakubwa kutoka Afrika na wawakilishi wa makampuni makubwa ya Kifaransa.

Balozi wa Ufaransa nchini Kenya, Arnaud Suquet, alisema dunia inazidi kuwa na mgawanyiko na sintofahamu, hivyo kuna haja ya ushirikiano mkubwa zaidi kati ya nchi mbalimbali.

Pia alisema kuwa Ufaransa haianzi kuifahamu Kenya sasa, akibainisha kuwa tayari Ufaransa ni nchi ya nne kwa uwekezaji mkubwa nchini Kenya.

Katika jiji la Nairobi, maduka makubwa ya Carrefour yanaonyesha ushawishi wa Ufaransa, kwa kuuza bidhaa za Ufaransa, mvinyo, vipodozi na bidhaa za kuoka pamoja na bidhaa za nyumbani za Kenya.

Kwa vijana wengi wa Kenya, Ufaransa inaonekana zaidi kama nchi inayohusishwa na biashara na chakula kuliko siasa, tofauti na jinsi inavyoonekana katika baadhi ya makoloni yake ya zamani.

...

Chanzo cha picha, Bloomberg via Getty Images

Maelezo ya picha, Ufaransa imekuwa nchi ya nne kwa uwekezaji nchini Kenya.

Mchambuzi mwandamizi wa taasisi ya Control Risks, Beverly Ochieng, anasema Ufaransa inajaribu kubadili taswira yake barani Afrika na inapunguza namna ya kuonyesha nguvu ambayo ilikuwa imezoea hapo awali.

Alisema kuwa badala ya kutegemea nguvu za kijeshi pekee, sasa Ufaransa inatumia zaidi biashara, uwekezaji na diplomasia ili kudumisha ushawishi wake barani Afrika.

Kwa mujibu wa Ochieng, Ufaransa inatumia kampuni zake maarufu, ushawishi wake wa kitamaduni pamoja na nafasi yake ndani ya Umoja wa Ulaya kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na nchi za Afrika.

Kwa upande mwingine, serikali ya Kenya inatafuta uwekezaji katika sekta kama ujenzi, nishati na teknolojia. Kampuni za Kifaransa tayari zimeanza kufanya kazi katika sekta za usafiri, biashara na nishati nchini humo.

Pia kuna mazungumzo kuhusu ushirikiano katika sekta ya nishati ya nyuklia, wakati Kenya ikitafuta njia za kuongeza uwezo wake wa uzalishaji wa nishati siku zijazo.

Mwezi uliopita, Nairobi iliidhinisha makubaliano mapya ya usalama ya miaka mitano na Ufaransa, ambayo yanajumuisha ushirikiano wa kiintelijensia, usalama wa bahari katika Bahari ya Hindi pamoja na msaada wa dharura wakati wa majanga.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Musalia Mudavadi, alisema nchi hizo mbili pia zinajadili maeneo mapya ya ushirikiano, akisema kile kinachoitwa "Africa Forward Summit" ni maono ya siku zijazo, si kuangalia yaliyopita.