Moja kwa moja, Marekani yamuwekea vikwazo Kabila kwa tuhuma za kuunga mkono makundi ya waasi DR Congo

Washington inadai Kabila alitoa msaada wa kifedha kwa AFC, kuhamasisha wanajeshi kuasi kutoka jeshi la Congo, na kupanga mashambulizi dhidi ya vikosi vya serikali.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Ambia Hirsi & Beldeen Waliaula

  1. Iran yawasilisha pendekezo jipya la mazungumzo kwa Marekani

    Picha ya mwanamke akiwa amebeba bendera ya Iran

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Picha ya mwanamke akiwa amebeba bendera ya Iran

    Tehran imewasilisha pendekezo jipya la mazungumzo na Marekani kupitia mpatanishi, Pakistan, shirika la habari la serikali ya Iran (IRNA) limeripoti.

    Hii imeonekana kama hatua ya kujaribu kumaliza mvutano uliopo kati ya Marekani na Iran.

    Shirika la habari la IRNA halijatoa maelezo Zaidi kuhusu pendekezo hilo, lakini bei za mafuta duniani, ambayo ilikuwa imepanda maradufu, imeshuka baada ya Iran kuwasilisha pendekezo hilo.

    “Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imewasilisha mapendekezo yake ya hivi karibuni kwa Pakistan, kama mpatanishi katika mazungumzo na Marekani, usiku wa Alhamisi,” Shirika la habari la IRNA limeandika.

    Baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano kuanza kutekelezwa tarehe 8 mwezi Aprili, Islamabad iliandaa mazungumzo kati ya wajumbe wa Tehran na Washington, ikilenga kuafikia makubaliano ya kumaliza vita vilivyoanza baada ya shambulio la Marekani na Israel dhidi ya Iran tarehe 28 mwezi Februari.

    Mazungumzo hayo yalitibuka bila maafikiano yoyote.

    Pia unaweza kusoma:

  2. Rais wa Kenya atangaza nyongeza ya mishahara kwa wafanyikazi wa kawaida na sekta ya kilimo

    Rais wa Kenya William Ruto

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Rais wa Kenya William Ruto

    Rais wa Kenya William Ruto, ametangaza ongezeko la 12% wa mshahara wa wafanyikazi wa kiwango cha chini na nyongeza ya 15% kwa wafanyikazi wa sekta ya kilimo.

    Ruto alitoa tangazo hilo wakati wa maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani yaliyofanyika magharibi mwa Kenya.

    Rais alisema serikali yake imeongeza mishahara kufuatia ombi la wafanyakazi kupitia muungano wa wafanyikazo nchini humo.

    “Hatimaye, kwa kutambua kujitolea, uvumilivu na mchango mkubwa wa wafanyakazi wetu katika ukuaji wa uchumi wetu, ninafuraha kutangaza ongezeko la 12% ya mishahara ya jumla na 15% kwa mishahara ya wanaohudumu katika sekta ya kilimo,” alisema Ruto.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Israel yawaachilia wanaharakati waliokamatwa baada ya msafara wao wa kuelekea Gaza kuzuiliwa

    Picha kutoka kwa video ikionyesha wanaharakati wakiinua mikono yao wakiwa ndani ya moja ya meli zilizozuiwa na majeshi ya Israel

    Chanzo cha picha, Global Sumud Flotilla/Handout via REUTERS

    Maelezo ya picha, Picha kutoka kwa video ikionyesha wanaharakati wakiinua mikono yao wakiwa ndani ya moja ya meli zilizozuiwa na majeshi ya Israel

    Wanaharakati wote isipokuwa wawili, waliokuwa wamekamatwa na majeshi ya Israel baada ya msafara wao uliokuwa ukielekea Gaza kuzuiwa,wameachiliwa huru nchini Ugiriki.

    Hapo jana takriban wanaharakati 175 waliokuwa ndani ya boti 22 zilizobeba misaada kuelekea Gaza, walikamatwa karibu na kisiwa cha Crete.

    Waandaaji wa msafara huo wa Flotilla walilaani hatua hiyo wakiuita “uharamia,” wakisema wanachama wao walikamatwa kinyume cha sheria zaidi ya kilomita 965 kutoka Gaza, katika maji ya kimataifa.

    Wizara ya mambo ya kigeni ya Israel, kwa upande wake, iliuita msafara huo kuwa “mbinu ya kujipatia umaarufu.”

    Wanaharakati wote waliokamatwa wameachiliwa huru katika kisiwa cha Crete, isipokuwa wanaume wawili ambao wamesafirishwa hadi nchini Israel “kwa ajili ya kuhojiwa,” hii ni kulingana na serikali ya Israel.

    Wizara ya mambo ya kigeni ya Israel imesema kuwa mmoja wa wanaume hao, Saif Abu Keshek, “anashukiwa kuwa na uhusiano na shirika la kigaidi,” huku mwingine, Thiago Avila, “akishukiwa kufanya shughuli haramu.” Wawili hao bado wanazuiliwa na mamlaka za Israel.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Mvua kubwa kushuhudiwa maeneo mengi nchini Kenya

    Picha ya mama akijikinga mvua

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Picha ya mama akijikinga mvua

    Idara ya hali ya hewa nchini Kenya (KMD) imetoa ilani kuhusu uwezekano wa kushuhudia mafuriko, maporomoko ya ardhi,pamoja na mvua kubwa itakayoendelea kunyesha wiki ya kwanza ya mwezi Mei.

    Utabiri wa idara hiyo unasema maeneo mengi nchini Kenya, yataendelea kushuhudia mvua kubwa.

    Maeneo ya mashariki na magharibi mwa bonde la ufa, eneo la ziwa Victoria,pwani mwa Kenya na kaskazini mashariki mwa Kenya, ni maeneo yanayotarajiwa kushuhudia mvua kubwa.

    Kulingana na idara ya hali ya hewa, mvua hii itanyesha mara nyingi nyakati za alasiri na jioni zikiambatana na ngurumo za radi.

    Wanaoishi maeneo ambayo hushuhudia mafuriko au maporomoko ya ardhi wametakiwa kuhamia maeneo salama.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Mataifa ya Kiarabu, Marekani Kusini yalaani hatua ya Israel kuzuia msafara wa Flotilla

    Picha za meli

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelezo ya picha, Picha za meli

    Mawaziri wa mambo ya kigeni kutoka Jordan, Uhispania, Pakistan, Brazil, Bangladesh, Uturuki, Afrika Kusini, Colombia, Libya, Maldives na Malaysia wamelaani vikali kile walichokiita “shambulio la Israel” dhidi ya “Msafara wa Global Resilience Flotilla,” mpango wa kiraia wa kibinadamu uliokuwa ukipeleka msaada eneo la Gaza.

    Mawaziri hao wamesema kuwa mashambulizi yaliyolenga meli hizo pamoja na kukamatwa kinyume cha sheria kwa wanaharakati zaidi ya 100 ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.

    Taarifa hiyo ya pamoja imeeleza wasiwasi kuhusu usalama wa wanaharakati hao wakiitaka Israel kuwaachilia mara moja na kuhakikisha usalama wao.

    Aidha, mawaziri hao wametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa “kutekeleza wajibu wake wa kimaadili na kisheria katika kulinda raia, kuheshimu sheria za kimataifa, na kuhakikisha uwajibikaji katika ukiukaji huu uliotekelezwa na Israel.”

    Pia unaweza kusoma:

  6. "Kiongozi mkuu wa Iran yuko salama" - Iran

    Bendera iliyo na picha ya Mojtaba Khamenei, Kiongozi Mkuu wa Iran

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Bendera iliyo na picha ya Mojtaba Khamenei, Kiongozi Mkuu wa Iran

    Ayatollah Mohsen Qomi, ambaye ni mwanachama wa baraza la wataalamu , na pia anahudumu katika ofisi ya kiongozi mkuu wa Iran, amepuuzia madai yanayotilia shaka afya ya kiongozi mkuu wa taifa hilo, Mojtaba Khamenei.

    Qomi amesema kiongozi huyo yuko salama, na anaendelea na majukumu yake ya kitaifa, na kudai kuwa uvumi unaoenezwa unatoka kwa mataifa ya magharibi.

    “Baadhi ya watu wanauliza kuhusu hali ya afya ya Kiongozi wetu mtukufu, Ayatollah Sayyid Mojtaba Khamenei.Ni maadui wanaouliza, ‘Kwa nini haonekani hadharani? Kwa nini hatumi ujumbe wa sauti au video? Kwa nini waliomtembelea hawazungumzi?’ Wanataka kutumia maswali haya kutulazimisha kujibu ili wafanikishe malengo yao,” aliliambia shirika la habari la Fars News Agency

    Qomi aliongeza kuwa licha ya majeraha aliyopata, viongozi wa Iran kwa sasa wanaangazia kwa umakini kulinda maisha ya kiongozi huyo.

    “Kwa sasa, jambo muhimu zaidi ni kuhakikisha tunahifadhi maisha ya Kiongozi wetu, licha ya majeraha aliyoyapata, Mwenyezi Mungu amemhifadhi” alisema Qomi.

    Pia unaweza kusoma:

  7. Falme za Kiarabu yawashauri raia wake kutosafiri Iran, Lebanon na Iraq

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Umoja wa Falme za Kiarabu, UAE imetangaza marufuku ya usafiri kwa raia wa nchi hiyo kwenda Iran, Lebanon na Iraq, na kutoa wito kwa wale wote walio katika nchi hizo kurejeanyumbani haraka iwezekanavyo.

    Katika taarifa Wizara hiyo ilisema: "Kwa kuzingatia mhali ya sasa ilivyo katika eneo hilo, na ndani ya mfumo wa UAE ya kufuatilia hali za raia wake nje ya nchi na kuhakikisha usalama wao, Wizara inawahimiza watu kuzingatia maagizo na tahadhari iliyotolewa na serikali ili kulinda usalama wa raia wake."

  8. Wafanyakazi wa Meta nchini Kenya waliodai kuona wenzao wakishiriki ngono wapoteza kazi

    .

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Meta inakabiliwa na shinikizo la kueleza ni kwa nini ilifuta mkataba wake na kampuni iliyokuwa ikitumia kutoa mafunzo kwa AI, muda mfupi baada ya baadhi ya wafanyakazi wake nchini Kenya kudai kuwa walilazimika kutazama picha za utupu zilizonaswa na miwani mahiri ya Meta.

    Mnamo Februari, wafanyakazi wa kampuni hiyo, Sama, waliambia magazeti mawili ya Uswidi kuwa walishuhudia watumiaji wa miwani wakienda chooni, na kufanya ngono.

    Chini ya miezi miwili baadaye, Meta ilifuta mkataba wake na Sama, katika hatua ambayo Sama inasema itasababisha wafanyakazi 1,108 pupoteza kazi.

    Meta inasema imechukua hatua hiyo kwa sababu Sama haikukidhi viwango vyake, madai ambayo Sama anapinga.

    Shirika hilo la Kenya linadai uamuzi wa Meta ulisababishwa na hatua ya wafanyikazi hao kuzungumzia suala hilo.

    Meta haijashughulikia madai hayo lakini iliiambia BBC kwamba "imeamua kusitisha kazi yetu na Sama kwa sababu hawafikii viwango vyetu". Sama ametetea kazi yake.

    "Sama imetimiza viwango vya uendeshaji, usalama na ubora unaohitajika katika shughuli zote za wateja wetu, ikiwa ni pamoja na Meta," ilisema taarifa yake.

    "Hatujawahi kuarifiwa chohcote kuhusu utendakazi wetu, kwa hivyo tutaendelea kutetea ubora na uadilifu wa kazi yetu."

    Mwishoni mwa Februari, magazeti ya Uswidi ya Svenska Dagbladet (SvD) na Goteborgs-Posten (GP) yalichapisha uchunguzi ambao ulijumuisha visa vya wafanyikazi ambao hawakutajwa ambao walikuwa wameombwa kukagua video zilizorekodiwa na miwani tamba ya Meta.

    "Tunaona kila kitu - kuanzia sebuleni hadi watu wakiwa uchi wa mnyama," mfanyakazi mmoja aliripotiwa kusema.

    Wakati wa uchapishaji, Meta ilikiri kwamba wafanyakazi waliopewa kandasi kufanya kazi kwa niaba yao wakati mwingine wanaweza kukagua maudhui yaliyorekodiwa kwenye miwani yake mahiri endamo wataweka maudhio yao kwenye mtandao wa Meta AI.

  9. Kuunda upya silaha za Marekani baada ya vita na Iran itachukua miezi hadi miaka – Waziri wa ulinzi

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelezo ya picha, Waziri wa Ulinzi nchini Marekani Pete Hegseth

    Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegsett ametangaza katika mkutano na wajumbe wa Congress kwamba kujenga upya hifadhi za silaha za Marekani, ambazo zimepungua kufuatia vita na Iran na migogoro mingine ya kijeshi katika miaka ya hivi karibuni, inaweza kuchukua "miezi hadi miaka," kulingana na aina ya vifaa.

    Seneta Mark Kelly wa Arizona alimuuliza Bw. Hegsett kwenye sakafu ya Seneti itachukua muda gani kuchukua nafasi ya hifadhi.

    "Mashambulizi mengi haya yanatumia silaha zetu bora, na tunatumia nyingi, pamoja na viingilia.

    Huwezi kuzalisha silaha hizi mara moja," alisema.

    Seneta Kelly aliongeza kuwa ombi la bajeti lililowasilishwa linaonyesha kuwa Idara ya Ulinzi pia ina ushahidi wa suala hili na kutaka ratiba maalum ya kubadilisha mifumo hii.

    "Hilo ndilo swali linalohitaji kuulizwa," Bw. Hegst alijibu, akisisitiza kwamba kujenga upya hifadhi kunaweza kuchukua kutoka kwa miezi michache hadi miaka michache, kulingana na aina ya mfumo wa silaha.

    Pia unaweza kusoma:

  10. Mshukiwa ashtakiwa kwa jaribio la mauaji baada ya Wayahudi wawili kuchomwa kisu Uingereza

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Essa Suleiman amefunguliwa mashtaka ya jaribio la mauaji baada ya wanaume wawili wa Kiyahudi kuchomwa kisu Golders Green, kaskazini mwa London, Polisi wa Metropolitan wamesema.

    Kijana huyo mwenye umri wa miaka 45 ameshtakiwa kwa makosa mawili ya kujaribu kuua na shtaka moja la kupatikana na kifaa chenye ncha kali katika eneo la umma kuhusiana na tukio hilo la Jumatano.

    Pia ameshtakiwa kwa jaribio la mauaji kuhusiana na tukio tofauti katika mtaa wa Great Dover huko Southwark mapema siku hiyo hiyo.

    Siku ya Alhamisi, kiwango cha tishio la ugaidi nchini Uingereza kilipandishwa kufuatia shambuliwa la kisu dhdi ya wanaume wawili wa Kiyahudi.

    Serikali inasema kuwa kupandishwa kwa kiwango cha tishio hakukutokana tu na shambulio la Golders Green, bali pia kumechochewa na “ongezeko la vitisho vya kijihadi na vya mrengo mkali wa kulia.”

    Kamishna Mark Rowley atazungumza kwenye Kiamsha kinywa cha BBC asubuhi ya leo kuhusu tukio hilo. Tutakuwa tunakuletea sasisho zote za hivi punde hapa.

    Maelezo zaidi:

  11. Wanamgambo wa Mali wataka utawala wa kijeshi kuondolewa madarakani

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Wanamgambo wa Kiislamu nchini Mali wametoa wito kwa nchi hiyo kuungana ili kuiondoa serikali ya kijeshi.

    Katika taarifa ya mtandaoni, kundi la kijihadi lenye uhusiano na al-Qaeda, JNIM, lilitaka vyama vya siasa, vikosi vya jeshi, makundi ya wanaotaka kujitenga na viongozi wa kimila kuungana dhidi ya serikali.

    Hali hii inakuja wakati mzingiro mkali unaimarishwa kuzunguka mji mkuu, Bamako.

    Siku ya Jumatano, JNIM ilionya kuwa hakuna mtu atakayeruhusiwa kuingia mjini humo.

    Kuna mashaka kuhusu uimara wa serikali ya kijeshi ya Mali baada ya mashambulizi yaliyoratibiwa na wanamgambo wa kijihadi na wanaotaka kujitenga mwishoni mwa wiki yaliyosababisha jeshi kupoteza udhibiti wa maeneo kadhaa muhimu ya kimkakati.

    Soma zaidi:

  12. Tuzo ya Oscar yatoweka baada ya mshindi kuzuiwa kuingia nayo kwenye ndege

    ..

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mshindi wa tuzo ya Oscar, Pavel Talankin alizuiwa kuingia kwenye ndege na tuzo yake ya dhahabu aliyoshinda kupitia filamu yake ya Mr Nobody Against Putin katika uwanja wa ndege wa New York - na sasa haipo.

    Talankin anasema alikuwa na Tuzo yake kwenye begi lake la mkononi kwenye ndege kuelekea Ujerumani siku ya Jumatano, lakini maafisa wa usalama wa uwanja wa ndege walimzuia katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa John F Kennedy kwa sababu walisema tuzo hiyo inaweza kutumika kama silaha.

    Lakini alipotua Ujerumani, tuzo yake ya Oscar alikuwa ametoweka.

    Shirika la ndege ya Lufthansa, ambayo ilimsaidia kubeba tuzo hiyo kwenye sanduku la safari ya ndege kwa vile Talankin haikuwa na begi la kukaguliwa, ilisema timu yao inashughulikia tukio hilo kwa "haraka" ili "kupata'' tuzo hiyo.

    .

    Chanzo cha picha, Pavel Talankin

    "Tunajutia sana hali hii," shirika la ndege lilisema katika taarifa.

    "Maafisa wetu wanashughulikia suala hili kwa uangalifu wa hali ya juu, na tunafanya uchunguzi wa kina ili kuhakikisha Oscar anapatikana na kurudishwa haraka iwezekanavyo."

    BBC imewasiliana na Chuo cha Sanaa na Sayansi ya Picha na Mamlaka ya Usalama wa Usafiri nchini Marekani (TSA), inayoshughulikia usalama wa uwanja wa ndege ambayo ilimzuia Talankin kuingia kwenye ndege na tuzo yake.

  13. Kiongozi wa zamani wa Myanmar Aung San Suu Kyi ahamishiwa kifungo cha nyumbani

    Aung San Suu Kyi

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Serikali ya kijeshi ya Myanmar imesema kiongozi wa demokrasia aliyekuwa kizuizini, Aung San Suu Kyi, amehamishwa hadi kifungo cha nyumbani, na adhabu yake kupunguzwa hadi miaka kumi na nane.

    Vyombo vya habari vya serikali vimeonyesha picha ya mshindi wa Nobel Prize akizungumza na maafisa wawili waliovalia sare.

    Mwanawe, Kim Aris, aliiambia BBC kuwa ana uhakika picha iliyochapishwa haina maana kwa kuwa ina miaka minne, na hajapata uthibitisho wowote kama mama yake bado yuko hai.

    Alisema taarifa pekee inayopatikana imetoka kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, na serikali ya kijeshi haiwezi kuaminika.

    '

    Chanzo cha picha, Myanmar state TV

    Bi. Suu Kyi alikamatwa baada ya serikali yake kupinduliwa kwa mapinduzi ya kijeshi mwaka 2021, na kufikishwa mahakamani kwa mashtaka ambayo kwa kiasi kikubwa yalitupiliwa mbali kama ya kutungwa.

    Pia unaweza kusoma:

  14. Kiwango cha tishio la ugaidi chapandishwa Uingereza baada ya shambulio la London

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Kiwango cha tishio la ugaidi nchini Uingereza kimepandishwa na serikali kutoka hadi kiwango cha pili cha juu zaidi - ikimaanisha kuwa shambulio la kigaidi linaonekana kuwa na uwezekano mkubwa kutokea ndani ya miezi sita ijayo.

    Serikali inasema kuwa kupandishwa kwa kiwango cha tishio hakukutokana tu na shambulio la Golders Green, bali pia kumechochewa na “ongezeko la vitisho vya kijihadi na vya mrengo mkali wa kulia.”

    Waziri Mkuu Keir Starmer amesema serikali sasa inazingatia kuanzisha hatua mpya, ikiwa ni pamoja na mamlaka makubwa zaidi ya “kufunga mashirika ya misaada yanayochochea chuki dhidi ya Wayahudi” na “kuzuia wahubiri wa chuki kuingia nchini humo”, pamoja na kuharakisha utoaji wa hukumu ya mashambulizi ya chuki dhidi ya Wayahudi “ili kuwe na kizuizi madhubuti.”

    “Serikali hii itafanya kila lililo ndani ya uwezo wetu kuondoa chuki hii. Tutaimarisha usalama wetu na kulinda jamii yetu ya Kiyahudi. Lakini pia ninatoa wito kwa kila mtu mwenye nia njema nchini kufungua macho yao kuona maumivu, mateso na hofu ya Wayahudi.”Starmer alisema.

    Shambulio la Jumatano ni la hivi karibuni katika msururu wa matukio yanayolenga jamii ya Wayahudi nchini Uingereza.

    Waziri wa Mambo ya Ndani Shabana Mahmood alisema kupandishwa kwa kiwango hicho “kutakuwa chanzo cha wasiwasi kwa wengi, hasa ndani ya jamii yetu ya Kiyahudi, ambao wamepitia mengi.”

    Mkuu wa kitengo cha polisi cha kupambana na ugaidi jijini London aliwaambia waandishi wa habari kuwa Uingereza imekuwa “ikikabiliwa na tishio la ugaidi linaloongezeka taratibu kwa muda fulani.”

    Essa Suleiman, mwenye umri wa miaka 45, bado yuko chini ya ulinzi wa polisi baada ya kukamatwa kwa tuhuma za kujaribu kuwaua Shloime Rand na Moshe Shine katika shambulio la Jumatano.

    Maelezo zaidi:

  15. Marekani yamuwekea vikwazo Kabila kwa tuhuma za kuunga mkono makundi ya waasi DR Congo

    Kabila

    Chanzo cha picha, Reuters

    Marekani imemwekea vikwazo vikubwa Rais wa zamani wa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Joseph Kabila, ikimtuhumu kuyaunga mkono makundi ya waasi ya M23 na AFC.

    Washington inadai Kabila alitoa msaada wa kifedha kwa AFC, alihamasisha wanajeshi kuasi kutoka jeshi la Congo, na hata alijaribu mashambulizi ya kuvuka mipaka dhidi ya vikosi vya serikali.

    Maafisa wanasema lengo la Kabila lilikuwa kuyumbisha serikali iliyopo madarakani na kumuweka mgombea wa upinzani ili kurejesha ushawishi wa kisiasa.

    Chini ya uamuzi wa Wizara ya Fedha, mali zote za Kabila nchini Marekani zimezuiwa.

    Raia na kampuni za Marekani zimepigwa marufuku kufanya biashara naye, na taasisi yoyote anayodhibiti kwa asilimia 50 au zaidi pia imewekewa vikwazo.

    Benki na washirika wa kigeni wameonywa dhidi ya kushirikiana naye kwa njia isiyo ya moja kwa moja, huku ukiukaji ukibeba adhabu kali za makosa ya kiraia au jinai.

    Vikwazo hivyo vimekusudiwa si tu kuadhibu bali pia kulazimisha mabadiliko ya tabia, vikionesha utayari wa Washington kulenga viongozi wa zamani wanaotuhumiwa kuchochea migogoro.BBC ilitafuta maoni kutoka jopo la mawasiliano la Kabila lakini bado haijapata majibu.

    Septemba, 2025, Mahakama ya Kijeshi mjini Kinshasa ilimhukumu kifo bila kuwepo mahakamani kwa kosa la uhaini, uhalifu wa kivita na kushirikiana na M23, aliporejea nchini kutoka uhamishoni mapema mwaka huo.

    Waziri wa Fedha wa Marekani Scott Bessent alisema hatua hizo zinaimarisha makubaliano ya amani na Ustawi ya Washington, zilizosainiwa Disemba, 2025 kati ya DRC na Rwanda.

    Aliongeza kuwa Rais Donald Trump ameweka wazi kwamba wale wanaosambaza machafuko watawajibishwa.

    Vikwazo hivyo vinafuatia hatua za awali za Marekani dhidi ya jeshi la Rwanda Machi, 2026, iliyotuhumiwa kuunga mkono kutekwa kwa miji ya Goma na Bukavu na kundi la M23.

    Kigali imekanusha madai hayo, ikisisitiza kuwa hatua zake zilikuwa za kujilinda.

    Kabila, ambaye alitawala DRC kuanzia mwaka 2001 hadi alipoondoka madarakani 2019, alisimamia makabidhiano ya kwanza ya madaraka kwa amani tangu uhuru wa nchi hiyo mwaka 1960.

    Soma zaidi:

  16. Karibu katika matangazo ya moja kwa moja.