Walowezi wa Israel wazuia familia ya Wapalestina kurejea nyumbani

Chanzo cha picha, Reuters
Zaidi ya walowezi 100 wa Israel wameshambulia kijiji cha Jalud katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, na kuzuia familia ya Kipalestina kurejea nyumbani huku wakikabiliana na wanajeshi wa Israel, kwa mujibu wa mashahidi.
Nyumba mbili za familia ya Tubasi katika kijiji hicho zilichukuliwa na walowezi wiki kadhaa zilizopita, wakati mashambulizi ya walowezi na unyakuzi wa ardhi yakiongezeka, hali ambayo imezua lawama kutoka kwa jumuiya ya kimataifa.
Familia hiyo ilikuwa imehifadhiwa sehemu nyingine ndani ya kijiji hicho, kilicho kaskazini mwa mji wa Ramallah, hadi jeshi la Israel lilipokubali kuisindikiza kurejea nyumbani usiku wa Jumatatu na kuipa ulinzi dhidi ya walowezi.
Hata hivyo, mashahidi walisema kuwa dakika chache baada ya familia hiyo kufika nyumbani, kundi la walowezi zaidi ya 100 lilifika eneo hilo.
Walowezi hao walichoma nyumba hizo moto, wakaziba barabara za kuingia eneo hilo na kuwarushia mawe maafisa wa Israel. Jeshi la Israel limesema maafisa wake watatu walijeruhiwa katika vurugu hizo.
"Kutokana na ghasia hizo, operesheni ya kuirejesha familia hiyo nyumbani haikukamilika," jeshi la Israel lilisema katika taarifa.
Kwa mujibu wa mashahidi, wanajeshi waliwaelekeza wanafamilia hao kupanda juu ya paa la nyumba walipoingia walowezi, kabla ya kuwaondoa eneo hilo wakati makabiliano yalipozidi kuwa makali.
Tukio hilo limeibua tena maswali kuhusu uwezo wa jeshi la Israel kudhibiti walowezi wanaopata ujasiri zaidi chini ya serikali ya mrengo wa kulia ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, ambayo imesimamia upanuzi wa makazi na vituo vya walowezi katika Ukingo wa Magharibi.
Soma Zaidi Hapa:
Walowezi wa Israel wananyakua ardhi za Wapalestina wakati huu wa vita



















