Mkuu wa NATO aiambia BBC kuwa matamshi ya Trump ni kama "mabishano ya kifamilia"
Katibu Mkuu wa NATO, Mark Rutte, amesema muungano huo wa kijeshi wa mataifa ya Magharibi una nguvu zaidi kuliko wakati mwingine wowote.
Alitoa kauli hiyo katika mahojiano na BBC wakati wa mkutano wa kilele wa NATO uliofanyika mjini Ankara.
Kauli hiyo imekuja licha ya matamshi makali ya Rais wa Marekani, Donald Trump, ambaye alisema amesikitishwa na kile alichodai kuwa NATO haikuungana na Marekani katika vita vyake dhidi ya Iran.
Hata hivyo, NATO haikushirikishwa rasmi katika operesheni hiyo, ingawa baadhi ya nchi wanachama, ikiwemo Uingereza, ziliruhusu majeshi ya Marekani kutumia kambi zao kufanya mashambulizi dhidi ya maeneo ya makombora ya Iran.
Katika mahojiano hayo, mwandishi wa BBC alimwambia Rutte kuwa kuna tofauti kati ya kauli za matumaini zinazotolewa na viongozi wa NATO na matamshi ya wakati mwingine yanayoonekana kugawa yaliyotolewa na Trump.
Katika mkutano huo, Trump alirudia msimamo wake kwamba Marekani inapaswa kuichukua Greenland na pia aliitaja Hispania kuwa "mshirika mbaya". Hata hivyo, alisema viongozi waliokutana Ankara walionesha umoja na kwamba kulikuwa na "upendo mkubwa" katika kikao hicho.
Akijibu, Rutte alisema hali hiyo ni kama ilivyo katika familia.
"Ni kama familia. Kuna familia ambazo hazigombani kabisa, na nyingine huzozana mara kwa mara, lakini bado hubaki familia," alisema.
Rutte alisisitiza kuwa Trump anaendelea kuunga mkono NATO kikamilifu.
"Trump ameijitolea kabisa NATO," alisema.
Alipoulizwa ni kwa nini ana uhakika huo, ikizingatiwa kwamba Trump aliwahi kusema siku za nyuma kuwa kuiondoa Marekani ndani ya NATO ni jambo linaloweza kuzingatiwa, Rutte alijibu:
"Nina uhakika kwa asilimia 100 kwamba Trump anaunga mkono NATO. Anaelewa kuwa operesheni za kijeshi za Marekani, ikiwemo Operesheni Epic Fury dhidi ya Iran, zisingeweza kufanyika kwa kiwango hicho bila kutumia Ulaya kama jukwaa la kuendeshea operesheni za kijeshi."
Rutte alisema kuwa katika kipindi cha wiki sita kati ya mwisho wa Februari na katikati ya Aprili, kabla ya makubaliano ya kusitisha mapigano kuanza kutekelezwa, zaidi ya ndege za kijeshi 5,000 ziliondoka katika vituo vya kijeshi vya Ulaya kwa mujibu wa makubaliano ya pande mbili ya matumizi ya kambi hizo.
Akizungumzia umuhimu wa nchi za Nordic zilizo wanachama wa NATO, ambazo ziko karibu na Rasi ya Kola nchini Urusi ambako kuna vituo vikubwa vya manowari zenye silaha za nyuklia, Rutte alisema eneo hilo lina mchango muhimu katika usalama wa Marekani kwa kutoa tahadhari za mapema kuhusu vitisho vinavyoweza kutokea.
Unaweza kusoma;