Rais wa Nigeria ataka kujua jinsi taasisi feki ilivyoanzishwa ndani ya ofisi yake

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Nigeria, Bola Tinubu, ameagiza kufanyika kwa uchunguzi wa tuhuma za ufisadi baada ya madai kwamba taasisi ya serikali isiyokuwepo kisheria iliundwa ndani ya ofisi yake na kupewa fedha za umma zenye thamani ya dola za Marekani 950,000.
Kwa mujibu wa Ikulu ya Nigeria, barua iliyodaiwa kutolewa na Mkuu wa Wafanyakazi wa Rais ya kuanzisha Presidential Foreign Intervention Promotion Council (PFIPC) ilikuwa ya kughushi.
Polisi wameanzisha msako dhidi ya Adeniyi Adeyemi Matthew, ambaye alikuwa akijitambulisha kama Mkurugenzi Mkuu wa PFIPC, kwa tuhuma za kughushi nyaraka, kujifanya afisa wa umma na makosa mengine yanayohusiana.
Kabla ya kutoweka, Adeyemi aliviambia vyombo vya habari vya nchini humo kuwa hana hatia na kwamba ana hofu kuhusu usalama wa maisha yake.
Aliahidi kufika mahakamani kuthibitisha kutokuwa na hatia, akisisitiza kuwa taasisi hiyo ilianzishwa kwa mujibu wa sheria. Pia aliwashutumu baadhi ya maafisa waandamizi serikalini kwa kudai rushwa wakati wa mchakato wa uteuzi wake na baadaye kujaribu kudhibiti fedha za taasisi hiyo. Ikulu imekanusha tuhuma hizo.
Adeyemi alisema PFIPC ilianzishwa mwaka 2024 kwa lengo la kuvutia uwekezaji wa kigeni nchini Nigeria, lakini hakuna rekodi yoyote inayoonesha kuwa ilifanikiwa kufanikisha uwekezaji wowote.
Taasisi hiyo ina wafanyakazi watatu pekee, ambao tayari wamehojiwa na polisi.
Jumanne, Rais Tinubu aliiagiza Tume Huru ya kupambana na vitendo vya rushwa (ICPC) kufanya uchunguzi na kuwasilisha ripoti kamili ndani ya siku 30.
Uchunguzi wa BBC News Pidgin umebaini kuwa taasisi hiyo ilikuwa imepata ofisi ndani ya Federal Secretariat, jengo kubwa la serikali linalohifadhi wizara nyingi za Nigeria katika mji mkuu, Abuja.
Pia ilifungua akaunti za benki katika Benki Kuu ya Nigeria (CBN) na iliorodheshwa katika Sheria ya Bajeti ya mwaka 2026 ikiwa na mgao wa naira bilioni 1.3, sawa na dola za Marekani 950,000.
Hata hivyo, Ofisi ya Mhasibu Mkuu wa Serikali imesema PFIPC haikuwahi kuwa na akaunti inayofanya kazi katika Benki Kuu ya Nigeria, na haijawahi kupokea fedha za umma wala kulipa mishahara.
Ikulu ya Rais imesema uchunguzi wa kisayansi uliofanywa na polisi umethibitisha kuwa saini ya Mkuu wa Wafanyakazi wa Rais, Femi Gbajabiamila, iliyokuwa kwenye barua inayodaiwa kuanzisha taasisi hiyo, ilighushiwa.
Kwa mujibu wa mashtaka yaliyowasilishwa katika Mahakama Kuu, mjini Abuja, Adeniyi Adeyemi pamoja na washtakiwa wengine wawili wanatuhumiwa kutumia nyaraka za serikali zilizoghushiwa kuanzisha na kuendesha taasisi hiyo inayodaiwa kuwapo, kufungua akaunti kadhaa za benki kwa jina lake na kutafuta kutambuliwa rasmi kwa taasisi ambayo serikali inasisitiza kuwa haipo.
Rais Bola Tinubu ameiagiza Tume Huru ya Kupambana na Vitendo vya Rushwa na Makosa Mengine Yanayohusiana (ICPC) kuchunguza tuhuma mbalimbali, zikiwemo:
- Kughushi barua za uteuzi na nyaraka rasmi za serikali;
- Kutumia madai ya uongo kutafuta utambuzi rasmi na uungwaji mkono wa kidiplomasia, ikiwemo kuwezesha upatikanaji wa visa;
- Kufungua akaunti nyingi za benki kwa kutumia nyaraka zinazodaiwa kughushiwa; na
- Kuchunguza nafasi ya mtumishi yeyote wa umma, mtu binafsi, taasisi ya kifedha au mpatanishi ambaye huenda alihusika katika kuwezesha njama hiyo.
Rais pia ameagiza wachunguzi kuchunguza mazingira yaliyoifanya taasisi inayodaiwa kuwa ya kubuniwa ionekane kuwa halali, pamoja na kubaini udhaifu katika mifumo na taratibu za serikali ambao unadaiwa kutumiwa kufanikisha mpango huo.
Kashfa hiyo imezua shinikizo kubwa kutoka kwa mashirika ya kiraia, wanasiasa wa upinzani na mawakili waandamizi, ambao wamekuwa wakitaka kufanyika kwa uchunguzi huru kuhusu suala hilo.


