Watu wanne wafariki dunia katika maandamano ya kupinga ongezeko la bei ya mafuta Kenya

Waziri wa nishati wa Kenya Opiyo Wandayi awarai wakenya kuwa na subira akiwaahidi kuwa serikali inashughulikia suala la mafuta, huku upinzani ukimtaka ajiuzulu.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Lizzy Masinga & Asha Juma & Mariam Mjahid

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo ya moja kwa moja. Usiku mwema.

  2. Watu wanne wafariki dunia katika maandamano ya kupinga ongezeko la bei ya mafuta Kenya

    G

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Waziri wa usalama wa ndani Kenya Kipchumba Murkomen amethibitisha kuwa watu wanne wameuawa katika mgomo wa usafiri ulioambatana na maandamano yaliyogeuka vurugu sehemu nyingi nchini hiyo.

    Kwa mujibu wa wizara yake watu 30 wamejeruhiwa, na watu 348 wamekamatwa kufikia sasa.

    Wakati huo huo, Waziri Murkomen amesema uvunjifu wa amani, uharibifu wa mali ya umma na uporaji hautasaidia bei ya mafuta kushuka.

    Waziri huyo pia amedai kuwa aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua amechochea vurugu kupitia kauli zake za kisiasa.

    Murkomen amewaambia wanahabari kuwa uchunguzi umeanzishwa kubaini waliochochea ghasia hizo.

    ''Uchunguzi umeanzishwa ili ibainike kama waliohusika katika maandamano ni wezi au la'', anasema Murkomen.

    Kwasasa, kuna baadhi ya barabara jijini Nairobi zimefungwa kutokana na hali kuwa tete.

    Soma zaidi:

  3. Samia aunda Tume ya kuchunguza ghasia za uchaguzi mkuu 2025

    Jaji Chande akimkabidhi ripoti ya tume kwa Rais Samia

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Jaji Chande akimkabidhi ripoti ya tume kwa Rais Samia

    Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameunda Tume ya Uchunguzi wa Kijinai kuchunguza matukio ya ghasia yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

    Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi, hatua hiyo inalenga kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani yaliyojitokeza wakati na baada ya uchaguzi huo.

    Taarifa hiyo ambayo imetumwa kwa vyombo vya habari, imeeleza kuwa tume hiyo imeundwa kwa mujibu wa mamlaka yaliyotolewa chini ya Sheria ya Tume za Uchunguzi, Sura ya 32.

    Shabani Ally Lila, Jaji wa Mahakama ya Rufani, ameteuliwa kuwa Kamishna na Mwenyekiti wa Tume hiyo.

    Wajumbe wengine walioteuliwa kuwa makamishna ni pamoja na Gad John Mjemmas, Awadh Mohamed Bawazir na Aishieli Nelson Sumari, ambao wote ni majaji wastaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

    Uamuzi wa kuundwa kwa tume hiyo, ni utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya uchunguzi wa matukio hayo iliyoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu Othman Chande iliyotaka uchunguzi wa kijinai ufanywe na tume maalum ya kijinai.

    Katika pendekezo hilo, Jaji Chande alisema tume hiyo itakuwa na jukumu la kupeleleza zaidi ili kushughulikia tuhuma zilizobainishwa katika taarifa ua Tume.

    Haya yanajiri siku chache baada ya bunge la Ulaya kuahirisha ziara yao Tanzania wakisema kuwa serikali ya Tanzania haijaonyesha ushirikiano.

    Kundi hilo lilikuwa limenuia kuja Tanzania ili kutathmini matukio ya baada ya uchaguzi yaliyosababisha vifo vya watu kadhaa.

    Soma zaidi:

  4. Marekani na Israel inajiandaa kushambulia upya Iran - Gazeti la New York Times

    f

    Chanzo cha picha, ATTA KENARE / AFP via Getty Images

    Gazeti la The New York Times limeripoti, likinukuu maafisa wawili wa Mashariki ya Kati ambao hawakutajwa majina, kwamba Marekani na Israel wanajiandaa kwa uwezekano wa mashambulizi mapya dhidi ya Iran, ambayo huenda yakaanza mapema wiki ijayo.

    Kwa mujibu wa maafisa hao wawili waliozungumza kwa sharti la kutotajwa majina, maandalizi ya Marekani na Israel yanatajwa kuwa makubwa zaidi ya kijeshi kuwahi kufanyika tangu kusitishwa kwa mapigano.

    Waziri wa Ulinzi wa Marekani aliliambia Bunge la Congress wiki hii kuwa Pentagon ina mipango ya hali mbalimbali, ikiwemo kuhamisha vituo vya kijeshi, kuongeza au kupanua vita endapo itahitajika, pamoja na kupunguza na kuondoa majeshi katika eneo hilo.

    The New York Times imenukuu maafisa wa Marekani wakisema kuwa iwapo Rais Donald Trump ataamua kushambulia, chaguo mojawapo ni mashambulizi makali ya anga dhidi ya vituo vya kijeshi na miundombinu ya Iran, na chaguo jingine ni operesheni ya ardhini yenye lengo la kuondoa akiba ya urani iliyoboreshwa ya Iran, ambayo inaaminika ilizikwa chini ya vifusi kufuatia mashambulizi ya awali dhidi ya vituo vya nyuklia katika vita vya siku 12.

    Wakati huo huo, afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Israel amenukuliwa na kituo cha televisheni cha Channel 12 akisema kuwa Israel inajiandaa kwa uwezekano wa kurejea kwa vita na Iran “wakati wowote.”

    Soma zaidi:

  5. Urusi na Belarus zafanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi ya nyuklia

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Urusi na Belarus leo zimefanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi ya nyuklia.

    Kwa mujibu wa Wizara ya Ulinzi ya Belarus, mazoezi hayo yamelenga kujifunza “usafirishaji wa silaha za nyuklia na maandalizi ya matumizi yake.”

    Wizara hiyo imesisitiza kuwa mafunzo hayo yalipangwa mapema na “hayalengi nchi zozote wala hayatoi tishio kwa usalama wa kikanda.” Jeshi la anga na vitengo vya makombora vilishiriki katika mazoezi hayo.

    Hii si mara ya kwanza kwa nchi hizo kufanya mazoezi ya pamoja ya nyuklia, kwani kwa miaka miwili iliyopita zimekuwa zikifanya mazoezi kama hayo kila mwaka.

    Mwaka jana, Urusi ilipeleka kombora la Oreshnik nchini Belarus, kombora lake la kisasa la mwendo wa kasi mkubwa (hypersonic) linaloweza kubeba kichwa cha nyuklia, hatua iliyoongeza mvutano na muungano wa nchi za Magharibi.

    “Wakati wa mazoezi, imepangwa kujifunza masuala yanayohusiana na usafirishaji wa silaha za nyuklia na maandalizi ya matumizi yake kwa ushirikiano na upande wa Urusi,” imesema Wizara ya Ulinzi ya Belarus.

    Kumalizika kwa muda wa mkataba wa New START, baadhi ya vizuizi vya silaha za nyuklia kati ya Marekani na Urusi vilikoma kufanya kazi.

    Mkataba wa New START, ambao ni makubaliano ya kupunguza silaha za nyuklia kati ya Marekani na Urusi uliosainiwa mwaka 2010, uliendelea kutumika hadi takriban miezi mitatu iliyopita (Februari).

    Belarus ni nchi isiyo na pwani iliyoko Ulaya Mashariki, inayoongozwa kwa zaidi ya miaka 30 na Alexander Lukashenko, mshirika wa karibu wa Vladimir Putin, na inategemea sana Moscow kiuchumi na kijeshi.

    Belarus inapakana na Ukraine upande wa kusini na nchi za NATO za Poland, Lithuania na Latvia upande wa kaskazini na magharibi.

    Nchi hiyo pia inahifadhi silaha za nyuklia za kimkakati za Urusi.

    Soma pia:

  6. Polisi Kenya wasema maandamano ya kupinga ongezeko la bei za mafuta yalikiuka sheria

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Nairobi, Issah Mohamud, amesema maandamano yaliyoshuhudiwa sambamba na mgomo wa sekta ya usafiri yalikiuka sheria kwa kuwa hayakutanguliwa na taarifa rasmi kwa polisi.

    Akizungumza na wanahabari, Mohamud amesema maandamano hayo hayakuwa ya amani, akidai waandamanaji waliweka vizuizi barabarani na kuvuruga shughuli za kawaida za wananchi.

    “Maandamano hayakuwa ya amani, waliweka vizuizi barabarani na kusumbua raia na abiria wengine. Hali hii ilitatiza biashara na kulemaza uchumi kwa sababu imeathiri familia nyingi,” amesema Issah Mohamud.

    Ameongeza kuwa polisi walifanikiwa kurejesha utulivu katika maeneo yaliyoathirika, licha ya baadhi ya waandamanaji kudai kuwa walikuwa wakilalamikia kile walichokiita dhuluma.

    “Ninawarai Wakenya wote kutokubali kurubuniwa na wanasiasa au upande wowote,” ameongeza.

    Aidha, amesema watu 225 wamekamatwa kufuatia matukio hayo na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani.

    Soma zaidi:

  7. Takriban wamarekani sita waambukizwa na Ebola katika mlipuko uliozuka DR Congo

    n

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Takriban Wamarekani sita wameambukizwa na virusi vya Ebola wakati wa mlipuko unaoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, vyanzo vimeiambia CBS News, mshirika wa BBC nchini Marekani.

    Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza mlipuko huo kuwa dharura ya kimataifa, huku wizara ya afya ya DR Congo ikiripoti takriban visa 350 vinavyoshukiwa na vifo 91.

    Mmarekani mmoja anadaiwa kuwa na dalili za ugonjwa huo, huku wengine watatu wakitajwa kuwa wamewahi kuwa katika hatari kubwa ya maambukizi au kugusana na wagonjwa. Bado haijafahamika iwapo yeyote kati yao ameambukizwa.

    Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa vya Marekani (CDC) vimesema vinasaidia katika “kuondolewa kwa usalama kwa idadi ndogo ya Wamarekani walioathirika moja kwa moja,” lakini havijathibitisha idadi kamili.

    Kipindi hiki cha Ebola kinasababishwa na virusi vya Bundibugyo, ambavyo havina dawa wala chanjo zilizoidhinishwa.

    Pia kuna visa viwili vilivyothibitishwa na kifo kimoja nchini Uganda, kwa mujibu wa CDC.

    Serikali ya Marekani inaripotiwa kupanga usafiri wa kundi hilo dogo la Wamarekani walioko DR Congo ili kupelekwa katika eneo salama la karantini, kwa mujibu wa chanzo kimoja kilichonukuliwa na kituo cha habari za afya STAT.

    Chanzo hicho kinaongeza kuwa kundi hilo linaweza kupelekwa katika kambi ya kijeshi ya Marekani nchini Ujerumani, ingawa taarifa hiyo bado haijathibitishwa rasmi.

  8. Mgomo wa usafiri watatiza biashara ya chakula mpakani Taveta na kusababisha kupanda kwa bei

    F

    Mfanyabiashara wa usafirishaji mboga katika mpaka wa Kenya na Tanzania eneo la Taveta, Abdi Suleiman, amesema mgomo unaoendelea umeathiri pakubwa usambazaji wa bidhaa za chakula kutoka Tanzania kuelekea Kenya, hali inayosababisha upungufu wa bidhaa katika migahawa na maduka.

    Suleiman ameiambia BBC kuwa tangu asubuhi hajaweza kusafirisha bidhaa kama kawaida kutoka mji wa mpakani wa Tanzania wa Holili kuelekea Taveta, akieleza kuwa changamoto hiyo imewaathiri sana wafanyabiashara wadogo.

    “Tunachukua bidhaa nyingi za chakula Holili, na mimi husafirisha chakula pekee si abiria. Ninaona jinsi mama mboga na migahawa wanavyopata shida kwa sababu walitegemea usambazaji wangu,” amesema.

    Ameongeza kuwa uhaba huo umepelekea kupanda kwa bei ya baadhi ya bidhaa katika eneo hilo.

    “Kwa mfano, kilo moja ya viazi ambayo jana iliuzwa shilingi 250 sawa na dola ($1.93), sasa inauzwa hadi shilingi 400 sawa na dola ($3.09)” amesema Abdi Suleiman.

    Soma zaidi:

  9. Abiria waliokuwa safarini kutoka Tanzania kwenda Kenya wakwama kutokana na mgomo wa usafiri

    F

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Abiria na wafanyakazi wa usafiri kati ya Tanzania na Kenya wamekumbwa na usumbufu mkubwa baada ya safari ya basi kutoka Dar es Salaam kuelekea Nairobi kukwama karibu na eneo la Kajiado kufuatia vizuizi vya barabarani vinavyohusishwa na mgomo wa usafiri Kenya.

    Kondakta wa basi linalomilikiwa na kampuni ya Tanzania (B One) linalofanya safari kati ya Dar es Salaam na Nairobi amesema walikumbwa na changamoto hiyo muda mfupi baada ya kuvuka mpaka wa Namanga, licha ya kupita kwa wakati.

    “Tumetoka Dar es Salaam Jumapili saa 5:00 usiku tukitarajia kufika Nairobi Jumatatu asubuhi, lakini baada ya kuvuka Namanga tulikumbwa na vizuizi vya barabarani na sasa tumekwama karibu na Kajiado,” amesema.

    Ameongeza kuwa abiria wengi wamekwama ndani ya basi hilo bila uhakika wa muda wa kuendelea na safari yao.

    “Abiria walikuwa wamejaa na wengi walikuwa wakisafiri kwa kazi na biashara. Sasa baadhi wamelala ndani ya basi, wengine wameenda kupumzika maeneo ya jirani, na hatujui hali itatulia lini,” ameongeza.

    Mfanyabiashara Njeri, aliyekuwa ndani ya basi hilo, ametoa wito kwa mamlaka kuchukua hatua za haraka kushughulikia changamoto za sekta ya usafiri akisema wananchi wanapata hasara.

    “Watu wengi wanasafiri kwa kazi, biashara na mahitaji ya familia. Mamlaka zinapaswa kushughulikia suala la bei ya mafuta kwa haraka kwa sababu hali hii inaathiri uchumi na maisha ya wananchi,” amesema Njeri.

    Soma zaidi:

  10. 'Mgomo wa matatu wasababisha hasara kubwa na bado utaendelea' - Albert Karagacha

    Rais wa Shirikisho la Wamiliki wa Matatu, Albert Karagacha

    Chanzo cha picha, Socials

    Maelezo ya picha, Rais wa Shirikisho la Wamiliki wa Matatu Kenya, Albert Karagacha

    Rais wa Shirikisho la Wamiliki wa Matatu, Albert Karagacha, amesema kuwa sekta hiyo imepata hasara inayokadiriwa kufikia zaidi ya shilingi milioni 500 za Kenya kufuatia mgomo unaoendelea, akisisitiza kuwa hatua hiyo itaendelea hadi bei ya mafuta itakapopunguzwa.

    Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Muungano wa RIG, Cornelius Chepsoi, amedai kuwa serikali haiwezi kuwaadhibu wananchi mara mbili kwa kuwapatia mafuta yasiyo na ubora unaotakiwa kisha kuwauzia kwa bei ya juu, hali anayodai ni ya kuwadhulumu Wakenya.

    Ameongeza kuwa anapinga madai kwamba mzozo unaoendelea Mashariki ya Kati ndio chanzo kikuu cha kupanda kwa bei ya mafuta nchini Kenya, akieleza kuwa hoja hiyo inatumika kama propaganda.

    “Kuna propaganda zinazoenezwa na serikali kuwa ongezeko la bei ya mafuta linatokana na vita Iran, lakini tunataka serikali ipunguze ushuru kwa sababu Wakenya wa kawaida wanaumia,” amesema Cornelius Chepsoi.

    Soma zaidi:

  11. Australia yatoa tahadhari ya usalama kwa raia wake walioko Kenya

    Bendera ya Australia

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Ubalozi wa Australia umetoa tahadhari ya usafiri kwa raia wake kufuatia maandamano yanayoendelea dhidi ya ongezeko la bei ya mafuta jijini Nairobi na maeneo mengine nchini Kenya.

    Kupitia ujumbe wake uliosomwa na BBC Swahili, ubalozi huo umesema: “Kuna maandamano yanayoendelea kuhusiana na usafiri Nairobi na maeneo mengine. Punguzeni safari na mfanye zile za muhimu pekee''.

    Aidha raia wa Australia wametakiwa kujiepusha na mikusanyiko, kufuatilia taarifa za vyombo vya habari vya ndani kwa taarifa za hivi karibuni, na wazingatie maelekezo ya mamlaka za eneo.”

    Taarifa hiyo imekuja wakati ambapo sehemu mbalimbali za nchi zimeripotiwa kukumbwa na usumbufu wa usafiri kufuatia maandamano ya kupinga ongezeko la bei ya mafuta na mgomo wa sekta ya usafiri.

    Soma zaidi:

  12. Maandamano ya kupinga ongezeko la bei ya mafuta yashika kasi Kenya, mgomo wa usafiri ukiendelea

    f

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Maandamano ya kupinga ongezeko la bei ya mafuta yashuhudiwa katika baadhi ya sehemu nchini Kenya

    Ghasia zimeripotiwa katika maeneo mbalimbali nchini Kenya huku maandamano dhidi ya ongezeko la bei ya mafuta na mgomo wa usafiri wa umma ukiendelea kushika kasi.

    Katika eneo la Makavazi yaliyoko Jijini Nairobi, maafisa wa polisi wamerusha mabomu ya kuwasha ili kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wamekusanyika nje ya eneo hilo.

    Katika mji wa Meru, waandamanaji wamefunga baadhi ya barabara na kuzuia magari kupita, hali inayosababisha usumbufu mkubwa wa usafiri wa umma.

    Huko Kaunti ya Murang'a, kundi la vijana linaripotiwa kufanya vurugu na kuwashinikiza wafanyabiashara kufunga maduka yao wakati wa maandamano hayo.

    Katika mji wa Mombasa, vijana wamejaribu kuweka vizuizi barabarani katika eneo la stendi ya magari ya Lights wakitekeleza mgomo wa usafiri wa umma. Hata hivyo, polisi wamewatawanya baadhi ya wahudumu wa matatu waliokuwa wamekusanyika eneo hilo.

    Katika kaunti ya Makueni, waandamanaji wanaripotiwa kuteketeza ofisi za chama cha UDA zilizoko Wote wakilalamikia ongezeko la bei ya mafuta.

    Wakati huo huo katika kaunti ya Kisii, maafisa wa polisi wamewataka madereva wa malori kuondoa magari yaliyokuwa yakizuia barabara ya Kisii kuelekea Oyugis huku mgomo wa matatu ukiendelea kushuhudiwa eneo hilo.

    Katika eneo la Kitengela, baadhi ya waandamanaji wanadaiwa kugeuza maandamano hayo na kuanza kupora maduka yaliyokuwa yamefunguliwa. Hata hivyo, milio ya helikopta za polisi zimeanza kusikika angani huku maafisa wa usalama wakijaribu kudhibiti hali.

    Haya yakijiri Waziri wa nishati Opiyo Wandayi amewataka wakenya kuvuta subira akiwaahidi kuwa serikali inashughulia suala la mafuta.

    ''Naomba wakenya wawe na subira.Serikali inashughulikia suala la mafuta'', anasema Waziri Opiyo.

    Soma zaidi:

  13. Kiongozi wa upinzani Kenya Kalonzo Musyoka amtaka waziri wa nishati ajiuzulu

    Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka

    Chanzo cha picha, Socials/Kalonzo

    Maelezo ya picha, Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka

    Maandamano ya kupinga kuongezeka bei za mafuta nchini Kenya yakiendelea kutanuka katika kaunti mbalimbali nchini humo na kuathiri usafiri wa umma Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka amemtaka waziri wa nishati kujiuzulu.

    ''Waziri wa Nishati, Opiyo Wandayi, anapaswa kuchukua hatua muhimu zaidi katika kipindi chake cha uongozi, hatua ambayo historia na wananchi wa Kenya wataikumbuka, kupunguza mara moja bei ya mafuta na kujiuzulu, amesema Kalonzo Musyoka.

    Awali waziri wa fedha wa Kenya amesema hakukuwa na haja ya kufanya mgomo wa usafiri kwa sababu tayari serikali ilishakua hatua kudhibiti athari kali za kupanda kwa mafuta zaidi kutokana na vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

    Polisi jijini Nairobi wanaendelea kutawanya waandamanaji kwa kutumia bomu za kuwasha.

    Soma zaidi:

  14. Hakukuwa na haja ya mgomo wa usafiri wa umma – Waziri wa Fedha Kenya

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Waziri wa Fedha nchini Kenya amesema hakukuwa na haja ya kufanya mgomo wa usafiri kwa sababu tayari serikali ilishakua hatua kudhibiti athari kali za kupanda kwa mafuta zaidi kutokana na vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

    Akizungumza Jumatatu, Waziri wa Fedha John Mbadi alisema serikali inazingatia kuchukua hatua mpya za kuwalinda Wakenya kutokana na athari za kupanda kwa bei ya mafuta na kuwa Rais William Ruto anatarajiwa kuongoza mkutano wa ngazi ya juu kuhusu bei ya mafuta atakaporejea kutoka ziara rasmi nchini Azerbaijan.

    "Tunaweza tu kutumaini kwamba vita hivi vitaisha, lakini hata tunavyotarajia, lazima tufanye maamuzi fulani. Nina uhakika serikali itakaa tena mara tu Rais atakaporudi kutathmini ni nini zaidi kinachoweza kufanywa," Mbadi alisema.

    "Kwa maoni yangu, hakukuwa na haja ya kufanya mgomo wa usafiri, ingawa bei za mafuta zimepanda. Wasiwasi wangu ni kwamba tunajaribu kutatua tatizo la kimataifa kwa kutumia njia za ndani, jambo ambalo halifai," alisema.

    "Kama tungeacha bei bila kuingilia kati, dizeli leo ingekuwa inagharimu si chini ya Sh35 zaidi, na petroli ingekuwa inagharimu Sh70 zaidi."

    Mbadi ametoa matamshi hayo hata baada ya maelfu ya Wakenya kulazimika kutembea hadi kazini leo Jumatatu asubuhi baada ya mgomo wa kitaifa wa matatu kuathiri usafiri wa umma katika miji mikubwa, kupinga ongezeko kubwa la bei ya mafuta lililotangazwa wiki iliyopita.

    Soma zaidi:

  15. Mwimbaji nyimbo za Injili aliyeshambiliwa kwa petroli afariki dunia Kenya

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rachel Wandeto, mwimbaji wa nyimbo za injili ambaye alishambuliwa kwa petroli na watu wasiojulikana ameaga dunia.

    Wandeto alikuwa akipigania maisha yake katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta baada ya watu wasiojulikana kumvamia na kummwagia petroli kabla ya kumchoma moto huko Mwiki.

    Huduma ya Kitaifa ya Polisi Kenya ilitoa taarifa na kulaani shambulio hilo.

    Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Jumapili, Mei 17, Huduma ya polisi ilisema tukio hilo lilitokea Jumamosi, Mei 16, 2026 katika eneo la Mwiki katika kaunti Ndogo ya Kasarani, ambapo mwanamke mmoja anadaiwa kumwagiwa kile kinachoaminika kuwa petroli na kuchomwa moto.

    Polisi walisema mwathiriwa anapigania maisha yake katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), wakiongeza kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa shambulio hilo huenda lilihusishwa na mitazamo yake ya kisiasa.

    "Suala hili linachunguzwa na timu maalum kutoka Makao Makuu ya DCI," NPS ilisema.

    Katika ripoti ya tukio kutoka Kituo cha Polisi cha Mwiki, polisi walisema umma uliripoti kwamba mwanamke mmoja alikimbizwa katika Hospitali ya Uzima Uhai baada ya kuchomwa moto katika Barabara ya Obama, Mtaa wa 11, yapata kilomita moja kusini mwa kituo hicho.

    Maafisa waliokimbilia hospitalini walimtambua mwathiriwa kuwa Rachael Wandalo, ambaye alikuwa amepelekwa huko na mumewe, Peter Njaramba.

    Polisi walisema inadaiwa kwamba mwanamke huyo alivamiwa na kundi la wanaume watatu waliommiminia petroli na kumchoma moto.

    Ripoti hiyo ilionyesha kuwa mwathiriwa alipata takriban asilimia 70 ya majeraha ya moto na baadaye akapelekwa hospitali kuu ya Kenyatta kwa matibabu maalum. Kesi hiyo iliwekwa chini ya uchunguzi katika Kituo cha Polisi cha Mwiki.

  16. Baadhi ya shule zaahirisha masomo juu ya maandamano Kenya

    .

    Chanzo cha picha, AFP

    Baadhi ya shule za mjini Nairobi na vitongoji vyake zimeahirisha masomo siku ya leo huku usafiri wa barabarani ukiwa umetatizika kutoka na mgomo wa usafiri wa umma.

    Shule hizo zimetaja usalama wa wanafunzi kama sababu kuu ya kufuta shughuli za masomo siku ya Jumatatu, na kuwasihi wazazi kuhakikisha watoto wao wanaendelea na shughuli za msingi wakiwa nyumbani.

    Ujumbe ambao umekuwa ukisambaa mtandaoni juu ya mgomo wa usafiri umesababisha hali ya wasiwasi kwa wazazi wakihofia usalama wa watoto hasa wanaotumia usafiri kwenda shuleni au wale ambao shule zao ziko katikati ya jiji.

    Wachezaji wanagoma kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta.

    Wahudumu wa usafiri wa umma wameitisha mgomo wakipinga bei ya juu ya mafuta kuwahi kushuhudiwa nchini kenya.

    Soma zaidi:

  17. Raia wachoma magurudumu ya magari barabarani huku mgomo wa usafiri ukiendelea Kenya

    .

    Chanzo cha picha, NMG

    Wahudumu wa uchukuzi wa umma wamesema watalemaza sekta ya usafiri hadi pale mamlaka ya udhibiti bei wa mafuta EPRA itabatilisha uamuzi wa kupandisha bei ya lita moja ya mafuta ya petroli iliyopanda kwa senti 16 za dola moja ya Marekani na lita moja ya mafuta ya dizeli ambayo imeongezwa kwa senti 23 za dola moja ya Marekani.

    Kulingana na vyombo vya habari vya ndani nchini Kenya, mitaa yenye idadi kubwa kama Rongai, Kawangware, Kitengela imeshuhudia ukosefu wa usafiri wa umma, huku baadhi ya wahudumu wakiwasha moto magurudumu ya magari na kufunga barabara.

    Katika barabara ya Ngong, baadhi ya wahudumu wamefunga barabara kwa kutumia mawe na pia kuchoma moto magurudumu. Polisi wako katika eno hilo kwa sasa kudhibiti hali.

    Katika barabara kuu ya Thika, baadhi ya wenye magari wamelazimika kubadili mwendo kujilinda dhidi ya waandamanaji ambao wamewasha moto barabarani.

    Polisi wamelazimika kufyatua mabomu ya kutoa machozi katika mtaa wa Kayole ambapo wahudumu hao walikuwa wamefunga barabara.

    Abiria waliozungumza na vyombo vya habari walisema kwamba wanatakiwa kulipa shilingi elfu moja za kenya kutumia bodaboda kufika mjini Nairobi, gharama ambayo ni ya juu sana kwa wengi kumudu.

    Msemaji wa huduma ya polisi Muchiri Nyaga katika tarifa aliyochapisha usiku wa kuamkia Jumatatu hii, alisema kwamba polisi hawatakubali utovu wa usalama wa aina yoyote huku wakitambua kwamba haki ya kufanya maandamano ipo katika Katiba ya nchi.

    Katika mtaa wa Zimmerman, wahudumu hao wamewasha moto kwa magurudumu ya gari huku wakiweka mawe pia barabarani.

    Pia unaweza kusoma:

  18. Mgomo wa usafiri waanza Kenya kupinga bei ya mafuta

    d

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Raia wengi nchini Kenya wamejikuta wakipata ugumu wa kufika kwenye maeneo yao ya kazi asubuhi ya leo baada ya wamiliki wa mabasi ya abiria pamoja na waendesha bodaboda kuanza mgomo wa kushinikiza serikali kushusha bei ya mafuta.

    Waandaaji wa mgomo huo wanasema ongezeko la gharama za mafuta limeendelea kuongeza ugumu wa maisha kwa wananchi wa kawaida. Aidha, wametaka mamlaka ya udhibiti wa nishati na mafuta, EPRA, kuvunjwa wakidai imeshindwa kudhibiti bei hizo.

    Mbali na sekta ya uchukuzi wa umma, shughuli za usafirishaji wa mizigo na utalii pia zinatarajiwa kuathirika kutokana na mgomo huo unaoendelea katika maeneo mbalimbali nchini humo.

    Mgomo huo umeanza siku chache baada ya wahudumu wa usafiri wa umma kutangaza kuongeza nauli kwa asilimia 50 kufuatia bei mpya za mafuta zilizotangazwa Mei 14.

    Kwa sasa, lita moja ya petroli jijini Nairobi inauzwa kwa shilingi 214.25 huku dizeli ikiuzwa kwa shilingi 242.92.

    Soma zaidi:

  19. UAE yaripoti shambulio karibu na kituo cha nishati ya nyuklia cha Abu Dhabi

    Mashambulizi ya droni yaligonga karibu na Kituo cha Nguvu za Nyuklia cha Barakah kilichopo Abu Dhabi, maafisa walisema

    Chanzo cha picha, AFP

    Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) imesema shambulio la droni lilisababisha moto karibu na kituo chake cha nishati ya nyuklia siku ya Jumapili, na kulielezea tukio hilo kama “ongezeko hatari la mzozo.”

    Maafisa wanasema wanafanya uchunguzi kubaini chanzo cha shambulio hilo. Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo ilisema droni tatu zilivuka kuingia UAE kutoka “upande wa mpaka wa magharibi.”

    Iliongeza kuwa droni mbili zilidunguliwa, lakini moja iligonga jenereta ya umeme “nje ya eneo la ndani la uzio wa usalama” wa Kituo cha Barakah kilichopo Abu Dhabi, na kusababisha moto.

    Hakukuwa na majeruhi walioripotiwa, na pia hakukuwa na athari katika viwango vya usalama wa mionzi, mamlaka za eneo hilo zilisema.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya UAE ililaani shambulio hilo na kulielezea kama “kitendo kisichokubalika cha uchokozi,” ikisema ina haki ya kujibu vitendo vyovyote vya uhasama.

    Pia iliongeza kuwa “kulenga vituo vya nishati ya nyuklia vya amani ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa, katiba ya Umoja wa Mataifa, na misingi ya sheria za kibinadamu.”

    Wizara ya Ulinzi pia ilisema nchi hiyo “itakabiliana kwa nguvu dhidi ya majaribio yoyote ya kudhoofisha usalama wa taifa.”

    Maafisa bado hawajasema droni hizo zilipotoka. UAE hapo awali imeishutumu Iran kuwa nyuma ya mashambulio dhidi ya miundombinu yake ya nishati na uchumi tangu vita vilipoanza katika eneo hilo mwezi Februari.

    Unaweza kusoma;

  20. Taiwan haitachochea mgogoro wala kuachia mamlaka yake ya kujitawala, asema rais

    Lai Ching-te

    Chanzo cha picha, Bloomberg via Getty Images

    Taiwan haitachochea mgogoro wowote lakini pia haitaacha uhuru wake, amesema rais wake Lai Ching-te baada ya mkutano kati ya Donald Trump na Xi Jinping ambapo walijadili suala la uhuru wa Taiwan.

    Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali ya China, Xi alimwambia Trump kwamba Taiwan, kisiwa kinachojitawala lakini kinachodaiwa na Beijing, ilikuwa “suala muhimu zaidi” katika uhusiano wa pande mbili, na kwamba kushughulikia vibaya suala hilo kunaweza kusababisha mgogoro.

    Baada ya ziara yake mjini Beijing, Trump alitoa onyo kwa Taiwan, akiiambia Fox News: “Sitafuti kuona mtu yeyote akitangaza uhuru.”

    Marekani ni mshirika wa muda mrefu wa Taiwan na imefungwa kisheria kuipa kisiwa hicho njia za kujilinda.

    Katika mahojiano yake, Trump alisema kuwa sera ya Marekani kuhusu Taiwan haijabadilika, huku akiweka wazi kwamba hataki mgogoro na Beijing.

    Trump pia aliwaambia waandishi wa habari kwamba Xi alikuwa na msimamo “mkali sana” kuhusu Taiwan lakini Trump “hakutoa ahadi yoyote upande wowote”.

    Chini ya uongozi wa Lai na mtangulizi wake Tsai Ing-wen, serikali ya Taiwan kwa miaka mingi imekuwa ikisisitiza kwamba hakuna haja ya kutangaza rasmi uhuru kwa sababu tayari inaichukulia Taiwan kama taifa lenye mamlaka yake.

    Lai alirudia msimamo huo katika chapisho lake la Facebook, ambalo lilikuwa jibu lake la kwanza la moja kwa moja kuhusu mkutano huo, akisema kwamba “hakuna suala la ‘uhuru wa Taiwan’.”

    Unaweza kusoma;