Poland nusura ianzishe mgogoro tangu vita vya pili vya dunia, Waziri Mkuu
Waziri Mkuu Donald Tusk amesema klichofanywa na Urusi kimevuka mstari mwekundu.
Muhtasari
- Urusi yashutumu Poland kwa 'kueneza uwongo' kuhusu uvamizi wa ndege zisizo na rubani
- Israel yashambulia mji mkuu wa Yemen - vyombo vya habari vya Houthi
- Urusi inasema hakuna maeneo ya Poland yaliyolengwa kushambuliwa
- Qatar inasema 'ina haki' ya kujibu shambulizi la Israel
- Urusi yasema haitatoa maoni yoyote kuhusu Poland
- Ndege 24 za Urusi zisizo na rubani ziliingia Poland - Zelensky
- Majibu ya nchi za Magharibi hayatoshi kumfanya Putin kuogopa kutuma ndege zisizo na rubani nchini Poland
- Poland inakaribia mzozo tangu Vita vya dunia vya pili - waziri Mkuu
- Wizara ya mambo ya ndani ya Poland imesema ndege saba zisizo na rubani za Urusi ziligunduliwa
- Maandamano ya Nepal 'yaliingiliwa' Gen Z wadai, huku jeshi likishika doria mitaan
- Mwanamke aliyemng'ata ulimi mshambuliaji wake aachiwa huru baada ya miaka 61
- Wanachama wa genge la waendesha baiskeli wanaopinga Uislamu wanaendesha ulinzi katika maeneo hatari ya misaada ya Gaza
- Poland yadungua ndege zisizo na rubani za Urusi baada ya 'ukiukaji mkubwa wa anga'
- Qatar: Shambulio la Israeli ni 'ugaidi wa serikali' na tunayo haki ya kujibu
- Hamas yadai viongozi wake wamenusurika na shambulio lake mjini Doha, huku Trump akisema hajafurahi
Moja kwa moja
Na Dinah Gahamanyi
Urusi yashutumu Poland kwa 'kueneza uwongo' kuhusu uvamizi wa ndege zisizo na rubani

Chanzo cha picha, Reuters
Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi inasema Poland imekuwa ikieneza "simulizi za uwongo" kuhusu uvamizi wa ndege zisizo na rubani ili "kuzidisha mzozo wa Ukraine".
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti yake, wizara ya mambo ya nje inakariri kwamba haikuwa imepanga kulenga eneo la Poland.
"Ukweli huu halisi unaondoa kabisa simulizi za uongo zilizoenezwa tena na Poland ili kuzidisha mzozo wa Ukraine," wizara hiyo inasema.
Inaongeza kuwa Katibu Mkuu wa Nato Mark Rutte "hakuweza kujibu swali kama kulikuwa na ushahidi wowote" wa shambulio lililopangwa.
Wakati huo huo, waziri wa Poland Tomasz Siemoniak aliishutumu Urusi kwa kueneza habari potofu kuhusu uvamizi wa ndege zisizo na rubani. Alichapisha kwenye X, kwamba Urusi imezindua "kampeni kubwa ya upotoshaji" na kwamba "ilikuwa ikiikashifu Poland."
Poland imeungwa mkono kikamilifu na washirika wake wa Nato, ambao wamelaani uvamizi wa ndege zisizo na rubani katika eneo la Poland.
Soma zaidi:
Habari za hivi punde, Israel yashambulia mji mkuu wa Yemen - vyombo vya habari vya Houthi

Chanzo cha picha, Reuters
Israel imefanya takriban mashambulizi sita ya anga kwenye mji mkuu wa Yemen, Sanaa, vyasema vyombo vya habari vyenye kuhusishwa na Houthi.
Kundi la waasi linaloungwa mkono na Iran limedhibiti sehemu kubwa ya kaskazini-magharibi mwa Yemen tangu mwaka 2014.
Tangu kuanza kwa vita vya Israel dhidi ya Hamas huko Gaza mwezi Oktoba 2023, Wahouthi wamekuwa wakirusha makombora mara kwa mara dhidi ya Israel na kushambulia meli za kibiashara katika Bahari ya Shamu na Ghuba ya Aden, wakisema wanafanya kazi kwa mshikamano na Wapalestina huko Gaza.
Israel na Marekani hapo awali zimefanya mashambulizi ya anga kujibu.
Soma zaidi:
Urusi inasema hakuna maeneo ya Poland yaliyolengwa kushambuliwa

Chanzo cha picha, EPA
Wizara ya ulinzi ya Urusi inasema haikupanga kushambulia maeneo yoyote nchini Poland, baada ya Warsaw kusema ndege 19 zisizo na rubani za Urusi ziliingia kwenye anga yake wakati wa mashambulizi ya usiku magharibi mwa Ukraine.
Katika taarifa za kila siku kuhusu vita vya Ukraine, imesema: "Hakuna maeneo ya Poland yaliopangwa kulengwa.
"Masafa ya juu zaidi ya ndege za UAV zilizotumika katika shambulizi [huko Ukraine] hayazidi kilomita 700 [maili 435].
"Hata hivyo, tuko tayari kufanya mazungumzo na wizara ya ulinzi ya Poland kuhusu suala hilo."
Soma zaidi:
Qatar inasema 'ina haki' ya kujibu shambulizi la Israel

Chanzo cha picha, Reuters
Qatar imezungumza na timu yake ya kisheria juu ya namna ya kumuwajibisha Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu kwa kuhusika na uvunjaji wa sheria za kimataifa.
Hapo jana, katika mkutano na waandishi wa habari, waziri mkuu wa Qatar alielezea shambulizi hilo kama "kitendo cha kigaidi cha serikali kilichofanywa chini ya Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu" na "ukiukaji wa uhuru".
"Nchi ya Qatar ina haki ya kujibu mashambulizi ya Israel na itachukua hatua madhubuti dhidi ya ukiukaji wowote wa kizembe au uchokozi unaotishia usalama wake na utulivu wa kikanda," taarifa ilisema.
Iliongeza kuwa wanaahidi kuchukua "hatua zote muhimu kujibu".
Iliendelea kusema kuwa "Qatar itaanza mapitio ya kina ya sera na taratibu za kuzuia vitendo hivyo na kuzuia kujirudia."
Soma zaidi:
Habari za hivi punde, Urusi yasema haitatoa maoni yoyote kuhusu Poland
Kremlin imetoa maoni yake ya kwanza kuhusu Poland ... ikisema haitatoa maoni.
"Hatungependa kutoa maoni juu ya hili," alisema msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov kwenye mkutano wake wa kila siku na waandishi wa habari.
"Hili si la kwetu kufanya hivyo. Ni suala la wizara ya ulinzi [ya Urusi]."
Alipoulizwa kuhusu tuhuma zinazotolewa Moscow, Peskov anajibu: "Uongozi wa Umoja wa Ulaya na Nato unaituhumu Urusi kwa uchochezi kila siku, kwa kawaida bila kuunga mkono jambo hili."
Ndege 24 za Urusi zisizo na rubani ziliingia Poland - Zelensky

Chanzo cha picha, EPA
Maelezo ya picha, Rais Volodymir Zelensky Katika taarifa nyingine kutoka kwa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, kiongozi huyo anasema kuvuka kwa mpaka na kuingia Poland kwa ndege isiyo na rubani ya Urusi kulitokea saa 00:50 kwa saa za huko (23:50 BST).
Anaandika kwenye X kwamba "angalau ndege zisizo na rubani mbili za Urusi ambazo ziliingia katika eneo la Poland wakati wa usiku zilitumia anga ya Belarusi".
Hii "inaweza kuwa kubwa kuliko takwimu iliyotangazwa hapo awali", anasema. Kama ukumbusho, Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk amesema jeshi la Poland lilirekodi mashambulizi 19 ya ndege zisizo na rubani katika anga ya nchi hiyo usiku kucha.
Ndege zisizo na rubani "inavyoonekana" zilikuwa zikikaribia kushambulia Poland na vile vile Ukraine, anaongeza.
Anasema data iliyopatikana inaonyesha kuwa kulikuwa na angalau dazeni mbili za ndege zisizo na rubani za Urusi ambazo zingeweza kuingia kwenye anga ya Poland. Ukraine inafanya kazi katika kuthibitisha hili, anaongeza.
Majibu ya nchi za Magharibi hayatoshi kumfanya Putin kuogopa kutuma ndege zisizo na rubani nchini Poland

Chanzo cha picha, EPA
Maelezo ya picha, Rais Vladmiri Putin Huu ni mfano mwingine wa sera ya Magharibi ya iliofeli.
Kwa miaka mingi, majibu ya nchi za Magharibi kwa mashambulizi ya Urusi nchini Ukraine yamekuwa yakidhibitiwa na hofu ya kuichokoza Moscow kufanya kitu kikali na cha ukatili zaidi.
Hofu hizi - pamoja na vikwazo vya kifedha - vimezuia washirika wa Ukraine kuipatia silaha nyingi na bora zaidi, achilia mbali kupeleka wanajeshi wa ardhini.
Lakini Kremlin haina wasiwasi kama huo. Imeweka uchumi wa Urusi kwenye msingi wa vita, na haiogopi kuongezeka kwa kuzidisha mashambulio ya anga dhidi ya Ukraine, kuwalenga raia, au kuwashirikisha wanajeshi wa Korea Kaskazini.
Majibu tuliyoyaona kutoka kwa nchi za Magharibi hadi sasa hayatoshi kumfanya Putin aogope matokeo iwapo ataamua kutuma ndege zisizo na rubani nchini Poland.
Poland inakaribia mzozo tangu Vita vya dunia vya pili - waziri Mkuu

Chanzo cha picha, EPA
Maelezo ya picha, Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk anasema Poland iko karibu zaidi kuanzisha mzozo kuliko wakati wowote tangu Vita vya Pili vya Dunia.
"Sina sababu ya kudai kwamba tuko ukingoni mwa vita, kwasababu mstari mwekundu umevukwa, na ni hatari zaidi kuliko hapo awali," mawaziri wakuu wa Poland wameliambia bunge.
"Hali hii inatuleta karibu zaidi na mgogoro tangu Vita vya Pili vya Dunia".
Habari za hivi punde, Wizara ya mambo ya ndani ya Poland imesema ndege saba zisizo na rubani za Urusi ziligunduliwa
Mamlaka nchini Poland imepata ndege saba zisizo na rubani na mabaki ya kitu kisichojulikana katika maeneo kote nchini kufuatia uvamizi wa anga ya Poland usiku kucha, msemaji wa wizara ya mambo ya ndani anasema.
Karolina Galecka anauambia mkutano wa waandishi wa habari kwamba ndege tano zisizo na rubani na mabaki ya kitu kisichojulikana zilipatikana katika maeneo tofauti katika jimbo la Lublin, mashariki mwa Poland, ambayo inapakana na Belarus na Ukraine.
Anasema ndege zake mbili zisizo na rubani ziligunduliwa katikati na kaskazini mwa Poland, mbali zaidi na mipaka: Moja iligunduliwa katika shamba huko Mniszków, katika mkoa wa Łódź katikati mwa Poland, karibu kilomita 250 (maili 155) kutoka mpaka wa Belarusi.
Nyingine iligunduliwa karibu na jiji la Elbląg kaskazini mwa Poland
Maandamano ya Nepal 'yaliingiliwa' Gen Z wadai, huku jeshi likishika doria mitaani

Chanzo cha picha, Getty Images
Jeshi la Nepal limeshika doria katika mitaa ya mji mkuu Kathmandu, baada ya taifa hilo la kukabiliwa na machafuko mabaya zaidi kuwahi kutokea kwa miongo kadhaa.
Maandamano ya kupinga ufisadi na upendeleo serikalini yaligeuka na kuwa vurugu siku ya Jumanne.
Waziri mkuu alijiuzulu huku nyumba za wanasiasa zikiharibiwa, majengo ya serikali yakichomwa moto na bunge lilivamiwa na kuchomwa moto.
Lakini makundi ya vijana wa "Gen Z" yanayoongoza maandamano hayo yamejitenga na uharibifu huo, yakisema maandamano hayo "yalitekwa nyara na watu waliohisi wamepata "fursa" ya kufanya uharibifu.
Leo mitaa ya Kathmandu inaonekana kuwa tulivu, lakini moshi bado unafuka kutoka kwenye majengo yaliyochomwa moto huku magari yaliyoungua yakitapa barabarani.
Amri ya kutotoka nje imetangazwa kote nchini hadi Alhamisi asubuhi, jeshi lilisema, likionya kuwa hatua kali itachukuliwa dhidi ya mtu yeyote atakayejihusisha na ghasia hizo zilizosababisha uharibifu mkubwa.
Watu 27 wamekamatwa kwa kuhujihusisha na vurugu na uporaji. Silaha 31 pia zilichukuliwa kutoka mikononi mwa raia, iliongeza.
Jeshi linajaribu kudhibiti hali tete,baada ya Waziri Mkuu KP Sharma Oli kujiuzulu na kuacha ombwe la uongozi.
Mwanamke aliyemng'ata ulimi mshambuliaji wake aachiwa huru baada ya miaka 61

Chanzo cha picha, News1
Maelezo ya picha, Kesi ya Bi Choi imenukuliwa katika vitabu vya sheria nchini Korea Kusini kuwa mfano halisi wa mahakama kushindwa kutambua kujitetea wakati mwathiriwa anakabiliwa na ukatili wa kingono. Mwanamke mmoja nchini Korea Kusini ameachiliwa huru baada ya mahakama kusikiliza upya kesi dhidi yake miongo kadhaa baada ya kuhukumiwa kifungo gerezani kwa kumng'ata ulimi mwanamume aliyemshambulia kingono.
Choi Mal-ja alikuwa na umri wa miaka 18 alipopatikana na hatia ya kumdhuru vibaya mshambuliaji wake na kuhukumiwa kifungo cha miezi 10 jela.
Mshambuliaji wake, ambaye alikuwa na umri wa miaka 21, alipokea kifungo chepesi cha miezi sita.
Kesi dhidi ya Choi ilianza kusikilizwa tena katika mji wa Busan mwezi Julai kufuatia kampeni ya muda mrefu iliyolenga kusafisha jina lake.
Katika kikao chao cha kwanza, waendesha mashtaka walimuomba msamaha na, katika hali isiyo ya kawaida, wakaiomba mahakama kufuta hukumu hiyo.
"Singeweza kuacha kesi hii iendelee bila kujibiwa... [nilitaka] kuwatetea waathiriwa wengine ambao wamejipata katika hali kama yangu," Bi Choi alisema baada ya kuachiliwa.
Kesi ya Bi Choi imetajwa katika vitabu vya sheria nchini Korea Kusini kama mfano halisi wa mahakama kushindwa kubaini maana ya kujitetea wakati mtu anapokabiliwa na unyanyasaji wa kingono.
Kulingana na rekodi za mahakama, mshambuliaji huyo alikuwa amembamiza chini Bi Choi katika jaribio la kumbaka mahali huko Gimhae.
Alifanikiwa kujiokoa baada ya kung'ata na kukata takriban 1.5cm (0.59in) ya ulimi wake.
Mwanamume huyo alitaka kufidiwa jeraha alilopata katika kisa hicho na hata kuvunja nyumba ya Bi Choi wakati mmoja, vyombo vya habari vya Korea Kusini viliripoti.
Katika mojawapo ya maamuzi yenye utata zaidi nchini Korea Kusini kuhusu unyanyasaji wa kingono, mwanamume huyo alipewa kifungo cha miezi sita, baada ya kupatikana na hati aya kupitia njia ambayo hakustahili kupitia na kumtishia.
Hakuwahi kushtakiwa kwa jaribio la ubakaji. Bi Choi alipata adhabu kali zaidi kwa kumsababishia jeraha baya mwilini, huku mahakama ikisema wakati wa tukio hilo ikisema kuwa alivuka "mipaka ifaayo" ya kujilinda.
Wanachama wa genge la waendesha baiskeli wanaopinga Uislamu wanaendesha ulinzi katika maeneo hatari ya misaada ya Gaza

Kampuni inayolinda maeneo ambayo misaada inasambazwa huko Gaza imekuwa ikiwatumia wanachama wa genge la waendesha baiskeli la Marekani wenye historia ya chuki dhidi ya Uislamu kuendesha usalama wao wenye silaha, uchunguzi wa BBC umegundua.
BBC News imethibitisha utambulisho wa wanachama 10 wa Klabu ya Pikipiki ya Infidels wanaofanya kazi huko Gaza la UG Solutions - mkandarasi binafsi anayetoa ulinzi katika maeneo ya Gaza Humanitarian Foundation, ambapo mamia ya raia waliokuwa wakitafuta chakula wameuawa katika matukio ya fujo na milio ya risasi.
Tunaweza kufichua kwamba wanachama saba wa genge hilo wako katika nyadhifa za juu za kusimamia maeneo kwenye operesheni yenye utata ya usaidizi inayoungwa mkono na Israel na Rais wa Marekani Donald Trump.
UG Solutions (UGS) ilitetea sifa za wafanyakazi wake kwa kazi hiyo, ikisema haichunguzi watu kwa "mapenzi ya kibinafsi au ushirika ambao hauhusiani na utendakazi wa kazi".
Wakfu wa Misaada ya Kibinadamu wa Gaza (GHF) ulisema una "sera ya kutostahimili chuki yoyote, upendeleo wa kibaguzi au mienendo".
Genge hilo kwa sasa linaandaa matamshi ya chuki dhidi ya Uislamu kwenye ukurasa wake wa Facebook na hapo awali limekuwa na nyama choma ya nguruwe "kukaidi" mwezi mtukufu wa Kiislamu wa Ramadhani.
Soma zaidi:
Poland yadungua ndege zisizo na rubani za Urusi baada ya 'ukiukaji mkubwa wa anga'

Chanzo cha picha, Reuters
Taarifa ya jeshi la Poland imesema kuwa anga la nchi hiyo lilikiukwa mara kandhaa na ‘’vitu vinavyofanana na ndege zisizokuwa na rubani’’
Hii ilitokea wakati wa shambulio la hivi punde la Urusi kote Ukraine, ambapo shambulio la anga lilianza kabla ya usiku wa manane, na maonyo ya angalau droni 100 angani - na Urusi ikitayarisha makombora na kuyarusha.
Msemaji kutoka serikali ya Poland amesema mkutano wa dharura utafanyika saa nane alfajiri kwa saa za eneo na kuwa Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk tayari anakutana na mawaziri wanaohusika na usalama wa serikali kuhusu shambulio hilo.
Kisha, Waukraine walipoingia kwenye makazi chini ya ardhi, njia za mahandaki ambazo walitazama zilianza kuripoti ndege kadhaa zisizo na rubani zikivuka hadi Poland.
Walianza kuandika kwa lugha ya Kipoland, wakiwaonya watu huko kujificha. "Chelm – kwenye makazi!" , "Zamosc - ndani ya malazi!"
Hii inahisi kama kuongezeka kwa mashambulizi ya Moscow - kujaribu majibu ya Magharibi. Kwa sababu inaonekana ndege zake zisizo na rubani hazikuingia Poland tu.
Ziliingia ndani vya kutosha hata kusababisha uwanja wa ndege wa Warsaw kufungwa.
Na hii inatokea huku mashambulizi ya angani dhidi ya Ukraine yamekuwa makubwa zaidi na ya mara kwa mara.
Wikendi iliyopita, kombora la Urusi liligonga jengo kuu la serikali Poland. Kabla ya hapo, majengo ya EU na Baraza la Uingereza huko Kyiv yaliharibiwa.
Ndege zisizo na rubani za Urusi zimewahi kuvuka mpaka wa magharibi mwa Ukraine hapo awali. Kombora la Kirusi hata lilitua msituni mara moja, lakini halikulipuka.
Mnamo mwaka 2022, wanakijiji wawili waliuawa karibu na mpaka, inaonekana baada ya ulinzi wa anga wa Ukraine kuangusha kombora. Kwa hivyo jeshi la anga la Poland sasa lipo vitani.
Lakini hawajawahi kupiga kitu chochote hapo awali. Kwa hivyo hili ni eneo jipya kwa Poland na kwa Nato.
Unaweza pia kusoma:
Qatar: Shambulio la Israeli ni 'ugaidi wa serikali' na tunayo haki ya kujibu

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim Al Thani Waziri mkuu na Waziri wa mambo ya jje wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim Al Thani ametangaza kwamba Qatar imekabiliwa na shambulio la "uhaini" la Israeli ambalo linaweza tu kuelezewa kama "ugaidi wa serikali."
Katika mkutano na waandishi wa habari mjini Doha, Al Thani alisisitiza kuwa nchi yake haitavumilia ukiukwaji wowote wa mamlaka yake na uadilifu wa eneo na itakabiliana kwa uthabiti na tisho lolote kwa usalama wake. Alithibitisha kuwa Qatar inayo haki ya kujibu "shambulio la wazi" na itachukua hatua zote muhimu kukabiliana nalo.
Waziri huyo alifichua kuwa Marekani iliifahamisha Qatar kuhusu shambulizi hilo dakika kumi baada ya kutokea, akibainisha kuwa Israel ilitumia silaha ambazo hazikugunduliwa na rada.
Alikitaja kile kilichotokea "jaribio la kuyumbisha usalama na utulivu wa kikanda," akiongeza kuwa "Waziri mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu anaongoza eneo hilo kwa kiwango kisichoweza kurekebishwa," na kwamba hatua hii imevuka viwango vyote vya maadili.
Al Thani alibainisha kuwa shambulio hilo limekuja licha ya mazungumzo yanayoendelea katika siku za hivi karibuni kwa ombi la Marekani kujadili mipango ya amani, ikiishutumu Israel kwa kujaribu kuhujumu juhudi hizo. Aliongeza, "Je, jumuiya ya kimataifa inahitaji ujumbe wa wazi zaidi kuhusu nani ni mnyanyasaji katika eneo hilo?"
Waziri huyo alisisitiza kuwa Qatar haijaacha juhudi zozote za kusimamisha vita huko Gaza, lakini baada ya shambulio la hivi karibuni, haoni uwezekano mkubwa wa kupatikana kwa makubaliano ya amani.
Aliongeza, "Diplomasia ya Qatar imejengwa juu ya misingi ya utulivu na suluhu za kisiasa, na hakuna kitendo cha uadui kitakachotuzuia kuendelea na jukumu letu la upatanishi na kujitahidi kuleta utulivu wa kikanda."
Unaweza pia kusoma:
Hamas yadai viongozi wa Hamas wamenusurika na shambulio lake mjini Doha, huku Trump akisema hajafurahi

Chanzo cha picha, Reuters
Hamas imedai imesema kuwa viongozi wake waliolengwa na shambulizi la anga la Israel wamenusurika , lakini watu sita wameuawa katika shambulio hilo.
Wakati huo huo Rais wa Marekani Donald Trump amesema "hajafurahishwa" na mashambulizi ya anga ya Israel huko Qatar, na kuongeza shinikizo la kimataifa baada ya kuongezeka kwa vita vya Israel dhidi ya Hamas.
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema mashambulizi hayo yalikuwa "halali kabisa" kwa sababu uyaliwalenga viongozi wakuu wa Hamas ambao walipanga shambulio la tarehe 7 Oktoba 2023 dhidi ya Israeli, ambalo lilianzisha vita vya Gaza.
Kundi la wapiganaji wa Palestina limesema wanachama wake watano waliuawa katika shambulio la anga la Israel katika mji mkuu wa Qatar, lakini lilidai kuwa jaribio la kuua timu yake ya mazungumzo "lilifeli".
Qatar ililaani shambulizi hilo la Israel, na kuliita la "uoga" na "ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa".
Qatar ni mshirika mkuu wa Marekani katika eneo ambalo ni eneo la kituo kikuu cha anga cha Marekani.
Alipoulizwa kuhusu mashambulizi ya Israel dhidi ya Qatar, Trump alisema: "Sawa, sifurahishwi... sijafurahishwa na hali nzima. Sio hali nzuri.
"Lakini nitasema hivi, tunataka mateka warejeshwe, lakini hatujafurahishwa na jinsi ilivyoshuka leo," aliambia vyombo vya habari.
Hamas ilisema timu ya mazungumzo ilikuwa inakutana kujadili pendekezo la hivi punde la Marekani la kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza katika makazi ya watu huko Doha wakati liliharibiwa vibaya na mfululizo wa milipuko.
Wizara ya mambo ya ndani ya nchi hiyo ya Ghuba imesema mwanajeshi mmoja wa kikosi chake cha Usalama wa Ndani aliuawa na wengine kujeruhiwa, bila kutaja majeruhi wowote wa Hamas.
Qatar imekuwa mwenyeji wa ofisi ya kisiasa ya Hamas tangu 2012, na imehudumu pamoja na Marekani na Misri kama mpatanishi katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya kundi hilo na Israel.
Unaweza pia kusoma:
Hujambo na karibu kwa matangazo haya ya mubashara tukikuletea habari za kikanda na kimataifa.
