Kwa upande wake, Kenya inapanga
kusoma bajeti ya $37.2 bilioni (Kes 4.84 trilioni) ambayo ni kubwa zaidi kuwahi
kuwasilishwa nchini humo. Katika mwaka wa kifedha uliopita, bajeti ya taifa
hilo ilikuwa ya dola $33 bilioni.
Sekta ambazo zinaratajiwa kunufaika
na ongezeko katika bajeti hii ni huduma za usalama wa ndani na ulinzi wa taifa,
idara ya ujasusi, pamoja na sekta za nishati, elimu, afya na maji.
Hata hivyo katika vikao vya umma na
pia mitandaoni, kumekuwa na maswali kuhusu iwapo taifa hilo kweli linahitaji
bajeti kubwa kiasi hicho.
Rwanda nayo inatarajiwa kutangaza
bajeti ya $5.4 bilioni (Rwf 7.8 bilioni), ambayo ni ongezeko la asilimia 12%
kutoka kwa bajeti ya mwaka uliopita ya $4.8 bilioni.
Bajeti hiyo inatarajiwa kuimarisha
ukuaji wa uchumi wa Rwanda, na asilimia 68% inatarajiwa kufadhiliwa na mapato
ya ndani.
Bajeti hizi zinawasilishwa wakati
wananchi wakiendelea kukabiliwa na changamoto za kupanda kwa gharama za maisha,
hususan bei ya mafuta kutokana na mzozo wa Mashariki ya Kati, pamoja na uhaba
wa ajira.
Hizi ni baadhi ya kauli za wananchi
tuliozungumza nao jijini Dodoma:
"Suala la mafuta ndio
linalotuumiza sana. Serikali inatupa ahadi ya kila siku kuwa bei itapunguzwa,
lakini hakuna mabadiliko," anasema mkazi mmoja.
Mwingine alisema: "Bajeti
inasomwa lakini matumizi sio mazuri. Hii inapunguza mzunguko wa fedha
mtaani."
Ongezeko la bei ya mafuta
limeshuhudiwa katika mataifa yote ya Afrika Mashariki, hali ambayo imesababisha
kupanda kwa nauli, chakula na gharama za kufanya biashara kwa jumla.
Wananchi watakuwa makini kuona ni
mapendekezo gani ya kikodi ambayo yatatolewa na serikali za kila nchi ili
kufadhili bajeti hizo, na yatakuwa na athari gani kwao.
Tanzania na Rwanda tayari zimesema
zitalenga mapato ya ndani zaidi kufadhili bajeti zao – na wengi wanasubiri
kuona ni maeneo gani ambayo yataguswa zaidi.
Nchini Kenya, bajeti huambatana na
mswada wa fedha unaoelezea jinsi bajeti hiyo itakavyofadhiliwa kupitia kodi,
mikopo na njia nyinginezo. Wananchi wamekuwa wakitoa maoni kuhusu mapendekezo
ya mwaka huu, ambapo baadhi yamezua mjadala kama vile ushuru wa simu za
mkononi, miamala ya fedha na mamlaka ya shirika la ukusanyaji ushuru KRA.