Makubaliano ya Hormuz yanaweza kufikiwa kesho - Marekani
Waziri wa Fedha wa Marekani, Scott Bessent, amesema makubaliano kati ya Marekani na Iran kuhusu kufungua Mlango bahari wa Hormuz yanaweza kuafikiwa hapo kesho.
Muhtasari
- Rais wa Cameroon afanya mabadiliko katika uongozi wa jeshi akiwa nje ya nchi
- Mazungumzo kuhusu Mlango wa Hormuz yamepiga hatua, makubaliano bado hayajaafikiwa - Rubio
- Makubaliano ya kufungua Mlango Bahari wa Hormuz yanaweza kuafikiwa kesho - Marekani
- Besigye bado hawezi kuzungumza - Winnie Byanyima
- Qatar : Juhudi za kidiplomasia za kupatanisha Iran na Marekani zinaendelea
- Marekani imetumia karibu makombora yake yote ya masafa marefu katika vita dhidi ya Iran - Reuters
- Zaidi ya wahamiaji 150 waokolewa baada ya boti yao kushika moto wakielekea Uingereza
- Maporomoko ya ardhi yawauwa waumini nchini Ethiopia
- Mapigano eneo la Tigray yanahatarisha maisha ya raia - Amnesty
- Bangladesh yatilia shaka hatua ya India kumruhusu Sheikh Hasina kuwahutubia wanahabari
- Afisi ya Rais wa Iran: Madai ya kujiuzulu kwa Rais Pezzekian ni uwongo mtupu
- Maandamano dhidi ya mazoezi ya kijeshi ya pamoja ya Korea Kusini na Marekani yafanyika mjini Seoul
- Chama cha muungano nchini Afrika Kusini kimefungua kesi mahakamani kupinga sheria iliyomkasirisha Trump
- EU yataka mipaka imara zaidi kufuatia wahamiaji kuvuka kuingia Ceuta
- Urusi yasema watu saba wameuawa na 40 kujeruhiwa baada ya droni ya Ukraine kushambulia ufukwe wenye watu wengi
- Ripoti za shambulio dhidi ya meli ya kibiashara karibu na Mlango Bahari wa Hormuz
- Iran: Tulikuwa tayari kushambulia Ukraine, lakini tulisitisha shambulio hilo baada ya nchi hiyo kuomba radhi
- Iran yasema inafanya mazungumzo na Oman na si Marekani
Moja kwa moja
Seif Abdalla & Beldeen Waliaula
Rais wa Cameroon afanya mabadiliko katika uongozi wa jeshi akiwa nje ya nchi

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Picha ya rais wa Cameroon, Paul Biya Paul Biya, rais wa Cameroon ambaye hajaonekana hadharani kwa takriban miezi miwili, amefanya mabadiliko katika uongozi wa jeshi la nchi hiyo huku kukiwa na wasiwasi kuhusu kuendelea kwake kukaa nje ya nchi.
Rais huyo mwenye umri wa miaka 93 amewateua maafisa wapya katika nyadhifa muhimu za jeshi na kuwapandisha vyeo makanali watano kuwa brigedia jenerali.
Mabadiliko ya aina hii si jambo geni katika utawala wa serikali ya Biya.
Wakati alipokuwa akiwania muhula wake wa nane wenye utata katika uchaguzi wa urais wa mwaka jana,Biya alifanya mabadiliko makubwa katika uongozi wa juu wa jeshi. Mwezi Juni mwaka huu pia aliwapandisha vyeo maafisa kadhaa wa jeshi na vikosi vya usalama.
Hata hivyo, mazingira ya mabadiliko ya hivi karibuni yamezua mjadala mkubwa, hasa kwenye mitandao ya kijamii.
Biya alitia saini amri za mabadiliko hayo akiwa mjini Geneva, Uswizi, ambako amekuwa akiishi tangu alipoondoka Cameroon tarehe 7 mwezi Juni kwa kile ambacho wasaidizi wake walikiita "ziara fupi ya kibinafsi."
Raia wengi wa Cameroon wamekosoa ukosefu wa taarifa kuhusu shughuli zake na kutokuwa na uhakika kuhusu muda atakaokaa nje ya nchi.
Baada ya uchaguzi wa mwaka jana, Biya aliahidi kutangaza baraza jipya la mawaziri, lakini hadi sasa hajafanya hivyo. Aidha, nafasi mpya ya Makamu wa Rais iliyobuniwa mwezi Aprili bado haijajazwa.
Soma pia:
Mazungumzo kuhusu Mlango wa Hormuz yamepiga hatua, makubaliano bado hayajaafikiwa - Rubio

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Picha ya Marco Rubio Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Marco Rubio, amesema mazungumzo kuhusu safari za meli katika Mlango bahari wa Hormuz yanayohusisha Iran na Oman yamepiga hatua, lakini makubaliano ya mwisho bado hayajaafikiwa.
"Kumekuwa na maendeleo katika mazungumzo hayo, lakini bado hayajakamilika. Tunatumaini makubaliano yataafikiwa hivi karibuni," amesema Rubio.
Mapema, Waziri wa Fedha wa Marekani amesema mazungumzo na Iran yanaendelea na kwamba makubaliano ya kufunguliwa kwa Mlango bahari wa Hormuz yanaweza kuafikiwa hapo kesho.
Kauli za maafisa wa Marekani zimekuja wakati Iran na Oman zimekuwa zikifanya mazungumzo kwa zaidi ya wiki moja kuhusu namna ya kusimamia na kuendesha shughuli za Mlango bahari wa Hormuz, ingawa maafisa wa Iran wameendelea kukanusha kuwa kuna mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani.
Soma pia:
Makubaliano ya kufungua Mlango Bahari wa Hormuz yanaweza kuafikiwa kesho - Marekani

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Waziri wa Fedha wa Marekani, Scott Besent Waziri wa Fedha wa Marekani, Scott Bessent, amesema makubaliano kati ya Marekani na Iran kuhusu kufungua Mlango bahari wa Hormuz yanaweza kuafikiwa hapo kesho.
Akizungumza na shirika la habari la CNBC, Bessent amesema kufunguliwa kwa Mlango bahari wa Hormuz kutasaidia kushusha bei za nishati duniani.
"Tunaendelea na mazungumzo na Wairani, na ninaamini kuna uwezekano kwamba leo au kesho tutaafikia makubaliano ya kufungua Mlango bahari wa Hormuz na kurejea katika hali ya kawaida kabla mzozo huu."
Kauli ya Waziri huyo imekuja wakati Iran na Oman zimekuwa zikifanya mazungumzo kwa zaidi ya wiki moja kuhusu namna ya kusimamia Mlango bahari wa Hormuz, ingawa maafisa wa Iran wamekuwa wakikanusha kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani.
Kulingana na shirika la habari la Reuters, afisa mmoja wa Iran anayeshiriki katika mazungumzo hayo amesema Tehran inataka kuwa na udhibiti wa meli zinazoingia katika Mlango bahari wa Hormuz na kupewa taarifa kuhusu meli zinazoondoka kwenye njia hiyo ya bahari.
Soma pia:
Besigye bado hawezi kuzungumza - Winnie Byanyima

Chanzo cha picha, Reuters
Winnie Byanyima, mke wa mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye, amesema kuwa mume wake anaendelea kuimarika kiafya, lakini bado ni mdhaifu sana na anaendelea kupokea matibabu katika Kitengo cha Wagonjwa Mahututi (ICU) katika hospitali ya rufaa ya Mulago, nchini Uganda.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumtembelea mume wake, Byanyima alisema Besigye kwa sasa ameacha kupata chakula kupitia mishipa, lakini hali yake ya kiafya bado ni tete.
"Nilimkuta amelala usingizi, lakini amechoka sana. Alionekana dhaifu mno. Aliendelea kulala kwa muda mrefu, na alipoweza kufungua macho bado hakuweza kuzungumza."
Byanyima aliongeza kuwa mume wake pia bado hawezi kuandika.
Mwanasiasa huyo mkongwe wa upinzani alilazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi ICU, baada ya kuanguka na kupoteza fahamu wakati wa kusikilizwa kwa kesi yake mahakamani tarehe 30 mwezi Julai.
Muda mfupi kabla ya kuanguka, Besigye alikuwa amepinga vikali uamuzi wa mahakama wa kuwateua mawakili wa serikali kumwakilisha.
Wakili wake mkuu, Erias Lukwago, alikamatwa, huku aliyekuwa Waziri wa Sheria wa Kenya, Martha Karua, ambaye pia alikuwa wakili wake akizuiwa kuingia nchini Uganda.
Byanyima pia ametoa wito kwa mamlaka za Uganda kuheshimu utawala wa sheria na haki za binadamu, ikiwemo haki ya Besigye ya kupata matibabu stahiki na kusikilizwa kwa kesi yake kwa haki.
Soma pia:
Qatar : Juhudi za kidiplomasia za kupatanisha Iran na Marekani zinaendelea

Chanzo cha picha, Getty Images
Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Qatar imesema juhudi za kidiplomasia zinaendelea ili kupata suluhu ya mzozo kati ya Marekani na Iran, huku wapatanishi wakiendelea kushauriana ili kufanikisha mazungumzo na kubadilishana mapendekezo kati ya pande hizo mbili.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Qatar, Majid Ansari, amesema kwa sasa hakuna mazungumzo ya moja kwa moja yaliyopangwa kati ya Iran na Marekani.
"Tunathibitisha kuwa juhudi za wapatanishi wa pande zote kutafuta suluhu zinaendelea," Ansari aliwaambia waandishi wa habari.
Aliongezea kuwa mazungumzo hayo yanalenga kupata "suluhu ya muda mfupi" itakayosaidia kufufua mazungumzo na kurejesha mchakato mpana wa upatanishi.
Qatar, pamoja na Pakistan, ni miongoni mwa nchi zinazoipatanisha Iran na Marekani katika juhudi za kupunguza mvutano na kufikia suluhu ya kidiplomasia.
Soma pia:
Marekani imetumia karibu makombora yake yote ya masafa marefu katika vita dhidi ya Iran - Reuters

Chanzo cha picha, Reuters
Katika taarifa iliyochapishwa na shirika la habari la Reuters, huenda Marekani inashuhudia upungufu wa makombora ya masafa marefu.
Kulingana na taarifa hiyo ya Reuters, Marekani imetumia karibu makombora yake yote ya masafa marefu yenye uwezo mkubwa wa kulenga shabaha kwa usahihi wakati wa vita vya miezi mitano dhidi ya Iran, hii ni kulingana na vyanzo vilivyoiambia Reuters.
Hali hiyo imezua wasiwasi kuhusu utayari wa jeshi la Marekani kukabiliana na migogoro mingine inayoweza kutokea baadaye.
Makombora hayo ni yale ya kurushwa kutoka ardhini kwenda ardhini yanayojulikana kama Army Tactical Missile Systems (ATACMS) na Precision Strike Missiles (PrSM). Vyanzo viwili vimesema kuwa Marekani imetumia "karibu yote" ya makombora hayo.
Hii ni mara ya kwanza kuripotiwa kwamba akiba ya Marekani ya makombora ya ATACMS na PrSM imepungua kwa kiwango kikubwa.
Makombora hayo ya masafa marefu ni sehemu muhimu ya silaha za jeshi la Marekani, kwani huwawezesha kushambulia malengo kwa usahihi wakiwa mbali. Makombora ya ATACMS yanayozalishwa na Marekani yamekuwa na mchango mkubwa katika vita vya Ukraine kwa kusaidia vikosi vya Ukraine kushambulia malengo ndani ya Urusi.
PrSM ni kizazi kipya cha makombora yenye uwezo wa juu zaidi na kinatarajiwa kuchukua nafasi ya ATACMS, ambayo yana uwezo mdogo wa kufika mbali.
Kulingana na Reuters vyanzo vyake havikufichua idadi ya makombora yaliyosalia katika akiba ya jeshi la Marekani.
Soma pia:
Zaidi ya wahamiaji 150 waokolewa baada ya boti yao kushika moto wakielekea Uingereza

Chanzo cha picha, Getty Images
Zaidi ya wahamiaji 150 wameokolewa baada ya boti waliyokuwa wakitumia kuvuka Mferejiwa English Channel kushika moto leo asubuhi, hii ni kulingana na ripoti za mamlaka ya Ufaransa.
Kulingana na mamlaka ya usalama wa baharini ya Ufaransa inayosimamia Mfereji wa English Channel na Bahari ya North sea, boti hiyo ilikuwa ikielekea Uingereza wakati injini yake ilipowaka moto.
Watu 157 wameokolewa na wamepelekwa katika bandari ya Boulogne-sur-Mer. Hadi sasa, hakuna taarifa za majeruhi au vifo.
Tukio hilo limetokea siku moja baada ya Waziri Mkuu wa Uingereza, Andy Burnham, kuahidi kuwa serikali yake itachukua hatua kali kupunguza idadi ya watu wanaowasili nchini humo kwa kutumia boti ndogo.
Maafisa wa Ufaransa walisema boti hiyo iliondoka nchini humo siku ya Jumatatu usiku.
Soma pia:
Maporomoko ya ardhi yawauwa waumini nchini Ethiopia

Chanzo cha picha, North Showa Zone Police
Maelezo ya picha, Miili ya watu 11 kati ya 14 waliofariki imezikwa katika utawa huo Mazishi ya watu 14 waliopoteza maisha yao kufuatia maporomoko ya ardhi yaliyokumba mlima wa watawa katika eneo la Amhara, kaskazini mwa Ethiopia,yamefanyika hii leo.
Watu hao walikuwa wamekusanyika katika mlima huo kwa ibada ya usiku, kabla ya maporomoko hayo ya ardhi kutokea.
Juhudi za kuwaokoa watu wengine wanaohofiwa kufunikwa na vifusi imesitishwa, baada ya sehemu ya mlima huo kuporomoka alfajiri ya Jumatatu.
Mlima huo ulio na utawa, ina chumba cha ibada kilichochongwa ndani ya mlima, ambako waumini walikuwa wamekusanyika kwa ibada maalumu.
"Ardhi iliyokuwa juu ya pango iliporomoka baada ya mvua kubwa kunyesha usiku kucha," afisa mwandamizi wa eneo hilo, Dagnachew Azbite, aliiambia BBC.
Afisa huyo alisema kuwa, watu saba walijeruhiwa, watano kati yao wakiwa katika hali mbaya.
Ibada iliyokuwa ikiendelea katika utawa wa Tsadqane Debre Mitmaq St Mary, ilijumuisha ibada ya kujitakasa kwa maji matakatifu, ambayo ni maarufu miongoni mwa Wakristo wa Kanisa la Orthodox wanaotafuta uponyaji wa kiroho kwa magonjwa sugu.
"Wengi ya waliopoteza maisha yao walikuwa wamekusanyika kupokea maji matakatifu," alisema Megabe Hadis Neka Tibeb Ababu, meneja mkuu wa jimbo la kanisa hilo, alipozungumza na shirika la habari la AP.
Kwa mujibu wa Megabe, watu 11 kati ya waliofariki wamezikwa katika utawa huo, huku miili ya wengine ikisafirishwa katika maeneo yao ya asili kwa ajili ya mazishi.
Soma pia:
Mapigano eneo la Tigray yanahatarisha maisha ya raia - Amnesty

Chanzo cha picha, AFP via Getty
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeonya kuwa mapigano yaliyoibuka upya katika eneo la Tigray nchini Ethiopia yamewaweka raia katika hatari kubwa ya kukumbwa na ukiukaji wa haki za binadamu.
Hii inajiri kufuatia mapigano mapya kuzuka kati ya jeshi la Ethiopia na vikosi vya TPLF, hali inayozua hofu ya kurejea kwa ukiukaji mkubwa wa haki za kibinadamu ulioshuhudiwa wakati wa vita vya mwaka wa 2020 hadi 2022.
Baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kumalizika miaka minne iliyopita, mapigano makali yalizuka siku ya Jumamosi asubuhi katika eneo la Shererina, karibu na mpaka wa Sudan.
Mamia ya wakazi wa Tigray wamekimbilia nchini Sudan.
Shirika la amnesty international limetoa wito kwa pande zote zinazozozana kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu, kuwalinda raia na kuruhusu misaada ya kibinadamu kuwafikia watu walioathirika na vita hivyo.
Soma pia:
Bangladesh yatilia shaka hatua ya India kumruhusu Sheikh Hasina kuwahutubia wanahabari

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Picha ya aliyekuwa waziri mkuu wa Bangladesh Sheikh Hasina Bangladesh inaitaka India kuelezea msimamo wake kuhusu hotuba ya mtandaoni inayotarajiwa kutolewa na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Bangladesh, Sheikh Hasina, ambaye yuko uhamishoni mjini New Delhi, nchini India
Bangladesh imeonya kuwa kuruhusu Waziri huyo wa zamani, kuendesha shughuli za kisiasa ilihali anatafutwa na mamlaka za Bangladesh, zinaweza kuathiri uhusiano baina ya mataifa hayo mawili.
Waziri huyo aliyeondolewa madarakani baada ya maandamano makubwa yaliyopinga utawala wake, anatarajiwa kuhutubia hafla ilioandaliwa na klabu ya waandishi wa habari wa kigeni Asia kusini, kuadhimisha miaka miwili baada ya kuanguka kwa utawala wake.
Soma pia:
Afisi ya Rais wa Iran: Madai ya kujiuzulu kwa Rais Pezzeshkian ni uwongo mtupu

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Rais Pezzekssian wa Iran Afisa mwandamizi katika ofisi ya Massoud Pezeshkian ameyataja madai kwamba Rais wa Iran amejiuzulu kuwa ni "upuuzi mtupu na uongo."
Mehdi Tabatabaei, Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Habari katika Ofisi ya Rais wa Iran, aliandika kwenye mtandao wa X: "Muungano mbovu wa watu wenye msimamo mkali waongo, wadanganyifu na wasiojali umelenga umoja mtakatifu na mshikamano wa kitaifa."
Awali, kauli zilizotolewa na Mohammad Bagher Kharrazi—mwanazuoni wa kidini aliye karibu na familia ya Kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran—kuhusu Bw. Pezeshkian zilikuwa zimepata nafasi kubwa katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii nchini Iran.
Bw. Kharrazi alisema kuwa Mojtaba Khamenei, kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, "aliandika kwamba iwapo Pezeshkian atajiuzulu tena, tutakubali kujiuzulu kwake."
Maandamano dhidi ya mazoezi ya kijeshi ya pamoja ya Korea Kusini na Marekani yafanyika mjini Seoul

Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock
Maelezo ya picha, Mkutano wa maandamano mbele ya Ubalozi wa Marekani mjini Seoul Siku ya Jumanne, tarehe 4 Agosti, wanachama wa kundi la wanaharakati wa mashirika ya kiraia mjini Seoul, mji mkuu wa Korea Kusini, waliandaa maandamano ya kupinga mbele ya Ubalozi wa Marekani jijini humo.
Waandamanaji hao, ambao ni wanachama wa kundi la "Korean Solidarity for Peace, Sovereignty and Reunification" (Mshikamano wa Korea kwa ajili ya Amani, Utawala Huru na Kuunganishwa Tena), walitoa wito wa kusitishwa kwa zoezi kubwa la kila mwaka la kijeshi la "Ulchi Freedom Shield"; zoezi ambalo huendeshwa kila mwaka na Korea Kusini pamoja na Marekani ili kuimarisha utayari wa pamoja na uratibu kati ya majeshi ya nchi hizo mbili.
Zoezi la mwaka huu limepangwa kuanza katika kipindi cha takriban wiki mbili zijazo na kudumu kwa siku 10.
Washiriki katika zoezi hilo ni pamoja na Kamandi ya Vikosi vya Pamoja, Vikosi vya Marekani nchini Korea Kusini, Kamandi ya Umoja wa Mataifa, Wakuu wa Majeshi ya Korea Kusini, pamoja na taasisi mbalimbali za serikali.
Chama cha muungano nchini Afrika Kusini kimefungua kesi mahakamani kupinga sheria iliyomkasirisha Trump

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Ramaphosa Chama cha Democratic Alliance cha Afrika Kusini, ambacho ni chama cha pili kwa ukubwa katika muungano unaounda serikali, kilifungua kesi mahakamani siku ya Jumatatu kupinga sheria ya kutaifisha ardhi; sheria ambayo Rais wa Marekani Donald Trump aliirejelea alipositisha misaada kwa nchi hiyo mwaka jana.
Kesi hiyo imezua mvutano na chama kikubwa zaidi, African National Congress, wakati nchi hiyo ikijiandaa kwa uchaguzi wa serikali za mitaa mwezi Novemba.
Sheria ya Kutaifisha Ardhi (Expropriation Act) inaruhusu serikali kuchukua ardhi kwa ajili ya maslahi ya umma—katika baadhi ya matukio bila kumlipa mmiliki fidia—ikiwa ni sehemu ya juhudi za kushughulikia athari za mfumo wa ubaguzi wa rangi (apartheid).
Imekuwa mada ya mjadala mrefu na mara nyingi wenye mvutano mkali kwa miaka mingi, na ikapitishwa kuwa sheria na Rais Cyril Ramaphosa mnamo Januari 2025. Hakuna ardhi iliyochukuliwa hadi sasa.
EU yataka mipaka imara zaidi kufuatia wahamiaji kuvuka kuingia Ceuta

Maelezo ya picha, Wahamiaji wakiingia Ceuta Rais wa Tume ya Ulaya, Ursula von der Leyen, ametoa wito wa "hatua za pamoja" kuhusu usalama wa mipaka kufuatia wimbi la vurugu la makumi ya maelfu ya wahamiaji walioingia kutoka Morocco hadi eneo la Uhispania la Ceuta wiki iliyopita.
Uhispania inakadiria kuwa takriban wahamiaji 69,500 sasa wamerejea Morocco, idadi inayozidi makadirio ya awali ya watu 50,000. Idadi rasmi ya vifo upande wa Uhispania wa mpaka ni 72, huku vifo 11 vikiripotiwa upande wa Morocco.
Siku ya Jumanne, mawaziri wa mambo ya ndani wa Umoja wa Ulaya (EU) watafanya mazungumzo ya dharura kwa njia ya video ili kujadili suala hilo.
Matukio hayo huko Ceuta yameleta mvutano katika mahusiano kati ya baadhi ya nchi wanachama 27 wa Umoja wa Ulaya.
Katika barua aliyomwandikia Waziri Mkuu wa Uhispania, Pedro Sánchez, von der Leyen alipongeza "hatua zake za haraka" katika kushughulikia mgogoro huo.
Hata hivyo, aliongeza kusema: "Kutokana na tukio hili, ni wazi kwamba tunapaswa kufanya zaidi ili kuimarisha mipaka yetu katika maeneo muhimu."
Kufuatia kuvuka kwa wahamiaji hao kwenda Ceuta, Italia ilisitisha kwa muda makubaliano ya Schengen na Uhispania.
Makubaliano ya Schengen yanaondoa ukaguzi wa mipaka na kwa sasa yanahusisha zaidi ya watu milioni 450 na nchi 29 barani Ulaya
Urusi yasema watu saba wameuawa na 40 kujeruhiwa baada ya droni ya Ukraine kushambulia ufukwe wenye watu wengi

Mamlaka za eneo hilo zimesema kuwa ndege isiyo na rubani (drone) ilianguka kwenye ufukwe wenye watu wengi kusini mwa Urusi, na kuua watu saba wakiwemo watoto watatu.
Katika picha za mitandao ya kijamii zilizothibitishwa na BBC, ndege hiyo inaonekana ikielekea kwa kasi kwenye eneo la miamba kabla ya kuanguka na kulipuka na kuwa mpira wa moto kwenye ufukwe uliopo chini, huku watalii wakishuhudia tukio hilo wakiwa ukingoni na ndani ya maji.
Gavana wa eneo la Krasnodar, Veniamin Kondratyev, alisema kuwa jumla ya watu waliojeruhiwa ilifikia 40, huku watu 17 wakipelekwa hospitalini.
Aliishutumu Ukraine kwa kufanya "shambulio la makusudi dhidi ya raia". Ukraine haijatoa tamko lolote. Pande zote mbili zinakanusha kulenga raia kwa makusudi.
Haijulikani wazi ni nini kilikuwa lengo la ndege hiyo. Baadhi ya chaneli za Telegram za Ukraine zimedai kuwa ilianguka ufukweni kutokana na vita vya kielektroniki vilivyovuruga mawimbi ya mawasiliano ya ndege hiyo. Vyombo vya habari vya Urusi vilinukuu mashuhuda kadhaa wakisema kuwa milio ya risasi ilisikika kabla ya mlipuko huo, jambo linaloashiria kuwa mifumo ya ulinzi wa anga huenda ilijaribu kuitungua ndege hiyo.
Ajali hiyo ilitokea kwenye ufukwe karibu na kijiji cha Arkhipo-Osipovka katika Bahari Nyeusi. Kutokana na hali ya hewa ya joto, ufukwe mrefu na miundombinu bora ya utalii, eneo hilo ni maarufu kwa Warusi wanaokwenda likizoni, hasa tangu vikwazo vilipopunguza uwezekano wa kusafiri nje ya nchi kwa watu wengi.
Watalii na wakazi wa Arkhipo-Osipovka waliambia vyombo vya habari vya eneo hilo kuwa hakuna ving'ora vilivyolia kabla ya shambulio hilo la ndege isiyo na rubani.
"Tulijikinga kwa kutumia viti vya kupumzikia ufukweni, na hatukuona ilipolipukia," alisema mtalii mmoja. Mtu mwingine alisema kuwa ingawa hakuona ndege hiyo ikigonga, alisikia "milio ya risasi, kama ya bunduki ya rashasha" ikifuatiwa na mlipuko.
Ripoti za shambulio dhidi ya meli ya kibiashara karibu na Mlango Bahari wa Hormuz

Chanzo cha picha, Reuters
Shirika la Uingereza la Operesheni za Biashara ya Baharini (UKMTO) limetangaza kuwa limepokea taarifa kuhusu mkasa wa baharini uliotokea maili 20 za baharini kaskazini mashariki mwa Al Khasab, Oman.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, meli ya mizigo ilitoa taarifa kupitia njia ya mawasiliano ya dharura ya VHF 16 kwamba ilikuwa imelengwa na kitu kisichotambulika.
Tovuti inayofuatilia mikasa ya ajali baharini ilisema kuwa "mamlaka zinafanya uchunguzi kuhusu tukio hilo."
Jana, meli ya kubeba mafuta katika eneo hilo iliripoti mlipuko uliotokea karibu nayo, lakini kwa mujibu wa Shirika la Operesheni za Biashara ya Baharini, wafanyakazi na sehemu ya nje ya meli hiyo hawakupata madhara.
Iran: Tulikuwa tayari kushambulia Ukraine, lakini tulisitisha shambulio hilo baada ya nchi hiyo kuomba radhi

Chanzo cha picha, YJCnews
Maelezo ya picha, Aliyekuwa kamanda wa IRGC Mohsen Rezaei Aliyekuwa kamanda wa IRGC, Mohsen Rezaei, alisema katika mahojiano mapya ya televisheni kwamba vikosi vya jeshi la Iran vilikuwa tayari kushambulia maeneo matatu nchini Ukraine baada ya Ukraine kushambulia meli ya kibiashara ya Iran katika Bahari ya Caspian, lakini uamuzi huo ulisitishwa kufuatia kile alichokiita "omba-radhi" kutoka Ukraine.
Bw. Rezaei anarejelea mazungumzo ya simu kati ya mawaziri wa mambo ya nje wa Iran na Ukraine, ambapo, kulingana na Abbas Araghchi, mwenzake wa Ukraine, Kiev ilisema kuwa hakukuwa na nia ya kushambulia meli ya kibiashara ya *Anna* katika Bahari ya Caspian na kwamba hatua hiyo ilichukuliwa kama sehemu ya vita dhidi ya Urusi, na si kama njia ya kuchochea mvutano zaidi na Tehran.
Bw. Rezaei, ambaye ni mshauri mkuu wa kijeshi wa kiongozi wa Iran, alidai katika mahojiano hayo kwamba katika siku za mwisho za vita vya siku 40, "mashambulizi sahihi zaidi ya ndege zisizo na rubani na makombora ya Iran dhidi ya kambi za Marekani"—ambayo kwa maoni yake yalisababisha "kambi ya Kuwait kuharibiwa vibaya," vikosi vya Marekani "kuondoka Erbil, Iraq," na "kuhamishwa kwa makamanda wa CENTCOM kutoka Jordan hadi Israel"—yalikuwa mambo yaliyozuia shambulio la ardhini la Marekani.
Bw. Rezaei, ambaye aliongoza Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi (Revolutionary Guard) wakati wa vita kati ya Iran na Iraq, alizungumzia mwelekeo wa sasa wa vita vya nchi hiyo na Marekani katika Lango la Bahari la Hormuz akisema: "Hatutaruhusu njia yoyote isiyo ya Iran kufunguliwa katika Lango la Bahari la Hormuz.
Hata kama Marekani italeta meli katika njia hiyo ni haramu kupitia Lango la Bahari la Hormuz, tutailenga meli hiyo."
Iran yasema inafanya mazungumzo na Oman na si Marekani, baada ya Trump kusema mazungumzo yataanza tena

Chanzo cha picha, GETTY
Maelezo ya picha, Rais Donald Trump Iran inasema inafanya mazungumzo na Oman ili kufikia "makubaliano" kuhusu njia ya muda kupitia Lango la Bahari la Hormuz, ili kuruhusu usafirishaji wa kibiashara kurejea.
Taarifa hiyo ilitolewa baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kusema kuwa mazungumzo mapya ya kumaliza uhasama na Iran yangeanza siku ya Jumatatu - na kwamba alikuwa amesitisha mashambulizi makubwa dhidi ya nchi hiyo kwa ajili ya lengo hilo.
Trump hakutaja ni nani watakaoshiriki katika mazungumzo hayo. Hata hivyo, Iran ilisema haifanyi mazungumzo na Marekani - na haina mpango wa kufanya hivyo.
Kukanusha huko kwa Tehran inaonekana kulimkasirisha rais wa Marekani, ambaye baadaye aliandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social kwamba uongozi wa Iran una "tabia ya unafiki wa hali ya juu".
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ikulu ya White House baadaye, alisisitiza kuwa mazungumzo hayo yanaendelea.
"Yanaendelea hivi sasa... hii ni fursa ya mwisho kwao kutia saini makubaliano mazuri," alisema.
Mwishoni mwa wiki, Trump alikuwa amesema kuwa "misingi" ya makubaliano ilikuwa imekubaliwa - na ingejumuisha kufunguliwa tena kwa Hormuz, njia muhimu ya maji ambayo kufungwa kwake na Iran kumesababisha bei ya mafuta kupanda kwa kasi.
Tehran imefunga njia hiyo mara kwa mara tangu Marekani na Israel zilipoanza mashambulizi dhidi ya nchi hiyo mwezi Februari.
Natumai hujambo na karibu katika habari zetu za moja kwa moja
