Waridi wa BBC: 'Kilio cha watoto kilichonisukuma kupaza sauti'

.
    • Author, Halima Nyanza
    • Nafasi, BBC Swahili
    • Akiripoti kutoka, Dar es Salaam
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

"Ni hadithi ndefu lakini kwa ufupi inatokana na maisha ambayo nimekuwa nayo, japo hayajanihusu mimi moja kwa moja. Ni maisha yaliyopo katika jamii ninayoishi ambako vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vinafanyika."

Hivyo ndivyo Agnes Suleiman Kahamba, mwanzilishi wa taasisi isiyo ya kiserikali ya Tupaze Sauti, alivyoanza kusimulia kilichomsukuma kujitosa katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake, vijana na watoto.

Agnes anasema alikulia akishuhudia matukio ya ukatili yaliyowaathiri watoto waliomzunguka, hali iliyomgusa na kumjengea hamasa ya kutafuta suluhisho kwa waathirika.

"Nakumbuka nilipokuwa nakaribia kufanya mtihani wangu wa darasa la saba, usiku wakati najisomea nilikuwa nasikia katika nyumba ya jirani wazazi wakigombana na hata kupigana. Wakati mwingine walikuwa wakimpiga mtoto wao ambaye tulikuwa tunasoma naye. Kilikuwa kipindi cha mitihani, hivyo huyo binti alikuwa akipitia ukatili akiwa bado mdogo. Maisha hayo yalimfanya aathirike kisaikolojia. Hayo yote ni mambo yaliyokuwa yakiniumiza kila wakati," anasema.

Akiwa msomi wa masuala ya ustawi wa jamii, Agnes anasema taasisi yake imejikita zaidi katika maeneo ya vijijini ambako hukutana na waathirika wengi wa unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake, vijana na watoto.

Kupitia ushirikiano na viongozi wa serikali za mitaa na wadau wengine, taasisi hiyo hutoa elimu kwa waathirika na kuwasaidia kujikwamua katika changamoto zinazowakabili.

Anasema Tupaze Sauti pia hutoa msaada wa kisheria na huduma za ushauri nasaha kwa lengo la kuwasaidia waathirika kurejea katika maisha yao ya kawaida.

"Tunataka kuwasaidia waathirika kuwakomboa kifikra, kimawazo na kisaikolojia," anasema.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Licha ya mafanikio hayo, Agnes anakiri kukutana na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa shughuli zake, ingawa anasema zimekuwa chache kutokana na ushirikiano mzuri kati ya taasisi yake na serikali.

Hata hivyo, anabainisha kuwa baadhi ya mila na desturi katika maeneo wanayofanyia kazi zimekuwa kikwazo katika jitihada za kuwalinda wanawake na watoto dhidi ya ukatili.

Anasema kazi zao huwashirikisha pia wanasheria, askari wa polisi kupitia Dawati la Jinsia, wataalamu wa afya pamoja na wataalamu wa maendeleo ya jamii.

Akizungumzia baadhi ya changamoto hizo, Agnes anataja mila zinazohusisha kuwafundisha watoto wa kike masuala ya ndoa wakiwa bado na umri mdogo katika baadhi ya maeneo ya kusini mwa Tanzania.

"Katika eneo hili, baadhi ya watoto wa kike wenye umri wa miaka 13 hadi 15 huingizwa kwenye mafunzo ya unyago wakiwa bado wadogo, kuanzia darasa la tano hadi la saba. Baada ya hapo wanatafuta wanaume ili kujaribu kile walichojifunza. Sasa unaona akiingia hapo wakati mwingine anaweza kupata magonjwa au mimba katika umri mdogo na hivyo kukatisha elimu yake. Hapo tunaona ndoto zake zimeishia hapo," anasema akiashiria uzoefu alioupata wakati wa utekelezaji wa mradi katika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma.

Kwa mujibu wa Agnes, kupitia shughuli za Tupaze Sauti, imefanikiwa kuwasaidia zaidi ya wanafunzi 100 kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya, Afisa Elimu, Jeshi la Polisi kupitia Dawati la Jinsia pamoja na wadau wengine wa maendeleo.

Tukio la ukeketaji

Katika kazi yake hiyo, Agnes anasema anakumbuka tukio ambalo kamwe hatalisahau.

"Miongoni mwa matukio ambayo siwezi kuyasahau ni niliyoyashuhudia mkoani Mara, ambako mabinti wanane walifanyiwa ukeketaji kwa kutumia kifaa kilekile. Hali hiyo iliwaweka watoto hao katika hatari kubwa ya maambukizi ya magonjwa na kuwaacha wakipitia maumivu makali," anasema Agnes.

Mbali na mila, Agnes Suleiman Kahamba anasema watoto wengi katika kaya maskini na maeneo ya vijijini wanashindwa kupata haki yao ya elimu kwa wakati muafaka, na pengine hata kuikosa kabisa, kutokana na uwezo duni wa wazazi wao.

Anatoa mfano wa kijana mmoja ambaye hadi anatimiza miaka tisa hakuwa amepata fursa ya kupata elimu. Hata hivyo, kutokana na mapenzi yake kwa shule, alikuwa akienda maeneo ya shule karibu na darasa na kusikiliza wenzake walivyokuwa wakifundishwa.

"…..Nilienda kwenye hiyo shule kwa ajili ya kutoa misaada, ndipo nilipokutana na kijana hiyo, nilimuita nikamuhoji ndipo aliponielezea kwamba wazazi wake hawataki asome kutokana na gharama zilizopo ikiwemo sare za shule, viatu, begi la kuwekea vitabu . Natamani sana kusoma ndio maana nakuja hapa kusikiliza wenzangu wanavyofundishwa."

Kwa masikitiko na sauti ya kulia, Agnes anasema jambo hilo lilimuumiza sana, kuona mtoto huyo akishindwa kufikia ndoto zake.

Hali hiyo ilimfanya Agnes kurejea tena katika eneo hilo akiwa amejipanga kumsaidia mtoto huyo, baada ya kukusanya michango ya fedha kwa ajili ya kumnunulia vifaa vya kujikimu katika masomo yake pamoja na fedha za malipo mengine.

Anasema kwa sasa mtoto huyo yuko darasa la tatu na anasoma vizuri.

Agnes anasema changamoto bado ni nyingi katika kuwazuia watoto wa vijijini kupata elimu, hivyo kupitia taasisi yake ya Tupaze Sauti, ameweka nguvu katika kushughulikia suala hilo.

.

"Huu ni wito"

.

Akizungumzia mafanikio yake, Agnes anasema ni mengi kupitia kazi yake hiyo na kwamba anajivunia kuisaidia jamii.

Anasema huo ni wito na kwamba hawalipwi.

Anasema kutambulika kwake na kupewa tuzo mbalimbali pia ni faraja kwake, kwani ni ishara kwamba jamii imeona juhudi zake.

Miongoni mwa tuzo hizo ni Top Young Women Entrepreneur 2026, inayolenga kutambua mchango wa wanawake vijana katika ujasiriamali na shughuli mbalimbali za biashara.

Anasema tuzo hiyo ina maana kubwa kwake:

"... kuwepo katika orodha ya wanawake 100 Tanzania wenye ushawishi, hicho ni kitu kikubwa kwangu. Inamaana nafanya kazi kubwa na jamii inaona, inanipa Motisha kubwa sana."

Agnes, ambaye pia ni mwigizaji, amezungumzia nguvu ya mitandao ya kijamii katika kufikisha ujumbe kwa vijana na walengwa wengine, iwapo itatumika vizuri.