Timu 4 zinazoshiriki kombe la dunia kwa mara ya kwanza

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 3

Kombe la Dunia la FIFA 2026 linaloanza Juni 11 - Julai 19, 2026 linatarajiwa kuwa moja ya matukio makubwa zaidi katika historia ya soka duniani. Mashindano haya yatakuwa na muundo mpana zaidi na yatatoa nafasi kwa mataifa zaidi kushiriki kuliko hapo awali, jambo linalofungua mlango kwa simulizi mpya za kihistoria kutoka sehemu mbalimbali za dunia.

Katika toleo hili, mashabiki wa soka watashuhudia mataifa kadhaa yakijitokeza kwa mara ya kwanza au kurudi baada ya miaka mingi ya kusubiri.

Baadhi ya timu hizi zimepitia safari ndefu ya changamoto, zikiwemo kushindwa mara kadhaa katika hatua za mchujo, lakini hatimaye zimefanikiwa kuvunja vikwazo hivyo na kufuzu kushiriki katika jukwaa kubwa zaidi la soka duniani.

DRC na Haiti zinarudi kwenye mashindano haya baada ya miaka 52, zikicheza mara ya mwisho fainali za mwaka 1974, Huku Iraq ikirejea baada ya miaka 40, mara ya mwisho ilicheza mwaka 1986. Lakini hizi nne zitagusa nyasi za kombe la dunia kwa mara ya kwanza tangu zizaliwe.

1. Cape Verde (Afrika)

Cape Verde imeandika historia kubwa kwa kufuzu Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza, ikiwa ni mafanikio makubwa kwa taifa hili la visiwa vidogo vya Atlantiki. Ushindi huu umeifanya Cape Verde kuwa moja ya hadithi kubwa za soka barani Afrika.

Nchi hii, yenye idadi ndogo ya watu chini ya 600,000, imeonyesha kwamba ukubwa wa taifa hauzuii mafanikio ya michezo. Ushindi wao dhidi ya timu zilizozoeleka kama Cameroon umeonesha mabadiliko makubwa ya kiwango cha soka lao.

Safari yao imejengwa juu ya nidhamu, mbinu bora za kiufundi, na wachezaji wengi wanaocheza ligi za Ulaya, jambo lililosaidia kuimarisha ushindani wao kimataifa.

2. Curaçao (Amerika Kusini)

Curaçao imeingia kwenye historia kama nchi yenye idadi ndogo zaidi ya watu kuwahi kufuzu Kombe la Dunia, ikiwa na wakazi wapatao zaidi ya 150,000 pekee. Hii ni rekodi mpya katika historia ya mashindano hayo.

Mafanikio haya yamekuja baada ya juhudi ndefu ndani ya ukanda wa CONCACAF, ambapo Curaçao ilifanikiwa kuvuka hatua ngumu za mchujo na kuwashangaza wengi waliodhani hawawezi kufika mbali.

Ushiriki wao umeleta furaha kubwa Amerika Kusini, na umeonyesha kwamba hata mataifa madogo yanaweza kufikia kilele cha soka la dunia iwapo yatakuwa na mipango sahihi na nidhamu ya hali ya juu.

3. Jordan (Asia)

Jordan, wanaojulikana kama "The Chivalrous Ones", hatimaye wamefanikiwa kufuzu Kombe la Dunia baada ya karibu miaka 40 ya majaribio katika mchujo huko Asia. Hii ni hatua kubwa katika historia ya soka la nchi hiyo.

Kabla ya kufuzu kwao, Jordan walikuwa wamekaribia mafanikio mara kadhaa, ikiwa ni pamoja na kuwa washindi wa pili katika Kombe la Asia na Kombe la Arab Cup, lakini bado walikosa tiketi ya Kombe la Dunia.

Safari yao ya mafanikio inaonyesha uvumilivu na maendeleo ya muda mrefu ya soka lao, na sasa wanakwenda kushiriki kwenye jukwaa kubwa zaidi duniani wakiwa na matumaini makubwa.

4. Uzbekistan (Asia)

Uzbekistan ni moja ya mataifa mapya kabisa katika Kombe la Dunia 2026, na pia ni timu ya kwanza kutoka Asia ya Kati kufanikiwa kufuzu mashindano hayo.

Baada ya miaka zaidi ya 30 ya changamoto tangu kupata uhuru, na majaribio saba yaliyogonga mwamba, ikitolewa mara zote katika hatua za mchujo, hatimaye "White Wolves" wamefanikiwa kuvunja mwiko huo.

Ushiriki wao unawakilisha mafanikio makubwa kwa eneo lote la Asia ya Kati, na ni ishara ya maendeleo ya soka lao kimataifa, hasa baada ya vipigo vya maumivu katika hatua za mwisho za mchujo wa bara la Asia.