Nini hutokea unapozidisha dozi ya paracetamol?

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwanafunzi huyo alipata tatizo la kushindwa kufanya kazi kwa viungo kadhaa vya mwili na akawekewa mashine ya kumsaidia kupumua ili kuokoa maisha yake.
Tukio hilo lilitokea Machi 2025, wakati Riley Lubas, mwenye umri wa miaka 20, alipokuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza chuoni. Wakati huo, alikuwa akisumbuliwa na mafua makali.
Alitumia dawa mbili za dukani, ambazo zote zilikuwa na paracetamol.
Hali yake ilizidi kuwa mbaya, akawekewa mashine za kumsaidia kuishi na kukaa hospitalini kwa wiki kadhaa. Kwa bahati nzuri, hali yake ilianza kuimarika ghafla, na akaanza tena kutembea na kuzungumza.
Chuo cha Madaktari wa Jumla cha Royal College of General Practitioners (RCGP) nchini Wales kinashauri watu kusoma kwa makini lebo na maelekezo ya dawa yoyote kabla ya kuitumia. Pia inashauriwa kushauriana na daktari kabla ya kutumia dawa yoyote.

Chanzo cha picha, SWNS
Riley alikuwa akiendelea vizuri na maisha yake ya chuo, lakini wakati wa majira ya kuchipua alipata mafua, jambo aliloliona kuwa la kawaida na lisilo na madhara makubwa.
"Katika mwaka wa kwanza, wanafunzi wengi hupata kile kinachoitwa 'freshman flu' au mafua ya kawaida. Hivyo nilitumia dawa mbili."
"Wakati huo, sikujua kwamba paracetamol ilikuwa kwenye dawa zote mbili."
Kwa mujibu wa NHS, kutumia paracetamol zaidi ya kiwango kinachopendekezwa kunaweza kusababisha madhara makubwa kwenye ini na figo.
Dalili za awali za sumu ya paracetamol zinaweza kujumuisha kichefuchefu, kutapika na maumivu ya tumbo.
Tukio hili linaonyesha umuhimu wa kukagua kwa makini viambato vilivyomo kwenye dawa mbalimbali, hasa unapokuwa unatumia zaidi ya dawa moja kwa wakati mmoja
Kutoka maumivu ya tumbo hadi kutumia mashine ya kumsaidia kupumua

Chanzo cha picha, SWNS
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Riley alipoanza kuhisi maumivu ya tumbo, aliamua kutafuta msaada wa kitabibu.
Alifanyiwa vipimo katika Hospitali ya Royal United mjini Bath, Uingereza, na kugundulika kuwa ini lake halikuwa likifanya kazi vizuri.
Wazazi wake, Chris na Kate Lubas, walipopokea taarifa kuhusu hali ya mwanao, walikimbilia hospitalini. Wanaishi naye mjini Newport, kusini-mashariki mwa Wales.
Chris, ambaye ni mkurugenzi wa kampuni, alisema awali madaktari walihisi huenda alikuwa na homa ya ini.
"Baada ya saa chache, karibu saa 7:30 usiku, nilipigiwa simu kutoka kitengo cha wagonjwa mahututi (ICU). Walisema: 'Mnahitaji kuja haraka.'"
"Kitu pekee walichoweza kutuambia wakati huo ni kwamba walikuwa wakifanya kila walichoweza kuokoa maisha yake," alisema.
Wazazi wa Riley waliambiwa kuwa hali ya mwanao ilikuwa katika hatari kubwa.
Chris aliona hali ya mwanawe ikiendelea kuwa mbaya.
Hali yake ilifikia kiwango cha hatari, na alianza kuchanganyikiwa na kuona vitu ambavyo havikuwepo.
"Siku hiyo hiyo, alipewa dawa za kumlaza hadi saa 12 jioni. Akawekewa mashine za kumsaidia kuishi na kufanyiwa uchujaji wa damu kwa mashine. Viungo vyake vingi viliacha kufanya kazi."
"Hapo ndipo wahudumu wa hospitali walipotuambia kwa mara ya kwanza jinsi hali yake ilivyokuwa imezorota," alisema.
Madaktari pia walikuwa na wasiwasi kuhusu hali ya majimaji yanayozunguka ubongo wa Riley. Mapafu na figo zake pia zilikuwa zimeacha kufanya kazi.
Chris alisema:
"Tulishangaa sana. Hatukuweza kuelewa jinsi kila kitu kilivyotokea kwa haraka kiasi hicho."
Kufikia wakati huo, hali ya Riley ilikuwa imezorota sana, hivyo alihamishiwa Hospitali ya King's College mjini London, ambayo ina kitengo maalumu cha wagonjwa mahututi kwa ajili ya kutibu wagonjwa walio katika hali mbaya.
Madaktari waliwauliza wazazi wake kiasi cha paracetamol alichokuwa amekitumia.
Baadaye waliweza kubaini dawa mbili ambazo Riley alikuwa ametumia. Hapo ndipo walipoelewa kilichokuwa kimemtokea.
Chris alisema:
"Hakukuwa na suluhisho la moja kwa moja la kutibu hali hiyo. Lakini angalau sasa tulijua chanzo."
Riley alisema nini wakati wa kupona kwake?

Chanzo cha picha, SWNS
Riley sasa amepona kabisa kutokana na tukio hilo na anafanya kazi katika baa.
Baada ya tukio hilo la kiafya kumpata mwana wao, wazazi wa Riley walitembea umbali mrefu ili kuhamasisha watu kuhusu hatari za kuzidisha dozi ya paracetamol.
Matembezi hayo ya kilomita 50, yaliyofanyika katika Rasi ya Gower, pia yalilenga kuchangisha fedha kwa ajili ya kitengo cha wagonjwa mahututi (ICU) cha Hospitali ya King's College.
"Inashangaza jinsi hali ilivyoweza kuwa mbaya kwa haraka kiasi hicho," alisema Riley.
"Nilikuwa mgonjwa kabla. Kwa hiyo nilipoanza kuhisi maumivu ya tumbo, nilidhani ni maambukizi ya tumbo."
"Sikujua kwamba maumivu hayo yalikuwa yanahusiana na ini langu."
"Ninashukuru sana kwamba hatimaye niliweza kupona na kurejea kwenye maisha yangu," alisema.
Wataalamu wanasemaje kuhusu paracetamol?

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni kutoka Ofisi ya Takwimu za Taifa ya Uingereza (ONS), mwaka 2024 kulikuwa na vifo 27 nchini Wales ambapo paracetamol ilitajwa kuwa chanzo cha kifo kwenye vyeti vya vifo.
Royal College of General Practitioners (RCGP) ni taasisi inayowakutanisha madaktari wa huduma za jumla.
Dk Will McIntosh, rais wa RCGP Wales na daktari wa huduma za jumla, alisema si jambo la kawaida kwa vijana kutumia paracetamol kupita kiasi bila kukusudia.
Hata hivyo, aliongeza kuwa mtu akitumia dawa mbili kwa wakati mmoja ambazo zote zina paracetamol, anaweza kuwa katika hatari.
McIntosh alisema shinikizo la kazi na masomo huwafanya vijana, hasa, kutumia dawa zinazouzwa bila cheti cha daktari.
"Hasa wakati wa magonjwa ya virusi, hata kama si magonjwa makubwa, ni muhimu sana kupata mapumziko ya kutosha," alisema.
McIntosh alisema wakati mwingine umuhimu wa kupumzika hupuuzwa katika jitihada za kupona haraka.
"Kwa magonjwa mengi ya aina hii, mwili unahitaji kupumzika na kupewa muda wa kupambana na ugonjwa. Aidha, dawa zinazouzwa bila cheti cha daktari zinaweza kutumika."
Alisema maduka ya dawa huwa makini sana katika kuuza dawa kwa wingi. Kwa sababu hiyo, mara nyingi kuna kikomo cha kiasi cha paracetamol kinachoweza kuuzwa kwa mtu mmoja.
Pia alisema madaktari wa huduma za jumla sasa wanafahamu zaidi hatari zinazoweza kusababishwa na kuzidisha dozi ya paracetamol kwa wazee.
Alisema hatari hiyo inaweza kuwa kubwa zaidi kwa wazee wenye uzito mdogo.
"Hali za aina hii zinapotokea, dalili zinaweza kuwa kali sana na hatari inaweza kuwa kubwa," alisema.
"Kwa hiyo, tunataka idadi ya visa kama hivi iwe ndogo sana," alisema.
Aliwashauri watu kusoma kwa makini lebo na maelekezo yaliyo kwenye dawa kabla ya kuzitumia.
Mambo ya kuzingatia unapotumia paracetamol
Kwa mujibu wa Huduma ya Taifa ya Afya ya Uingereza (NHS):
Kiwango cha juu cha paracetamol ambacho mtu mzima anaweza kutumia ni vidonge 8 vya miligramu 500 kila kimoja ndani ya saa 24.
Dawa zenye majina ya kibiashara zinaweza pia kuwa na paracetamol, hivyo soma kwa makini lebo na maelekezo yaliyo kwenye kifurushi cha dawa.
Usitumie paracetamol kwa zaidi ya siku tatu mfululizo bila kushauriana na daktari.
Unapotumia paracetamol, usitumie dawa nyingine ambazo pia zina paracetamol. Hii inajumuisha dawa nyingi zinazotumika kutibu mafua na homa.
Imetafsiriwa na Faidha Ngaga na kuhaririwa na Ambia Hirsi
































