Jinsi matiti makubwa yanavyoweza kuathiri afya yako

Chanzo cha picha, Getty
"Nilikuwa nikitembea nikiwa nimeinama mabega, ili tu kuficha matiti yangu makubwa. Nakumbuka hilo kwa sababu nilikuwa naona aibu sana."
Raquel, mhadhiri wa chuo kikuu kutoka Argentina, aliamua kufanyiwa upasuaji wa kupunguza ukubwa wa matiti yake mwaka wa 2010.
Kwa sasa akiwa na umri wa miaka 52, anasema matokeo ya upasuaji huo yamempa hisia ya uhuru ambayo hajawahi kuhisi hapo awali.
Ingawa matiti makubwa huchukuliwa kuwa ya kuvutia katika sehemu nyingi duniani, ukweli wa kuishi na matiti makubwa unaweza kuwa mgumu, na kusababisha changamoto kubwa kwa afya na ubora wa maisha ya wanawake.
Matiti makubwa yamehusishwa na dalili mbalimbali, zikiwemo maumivu ya muda mrefu ya mgongo, maumivu ya kichwa, mkao usio sahihi, kufa ganzi na matatizo ya usingizi, pamoja na changamoto za afya ya akili.
Takwimu za hivi karibuni kutoka Jumuiya ya Kimataifa ya Upasuaji wa Plastiki ya Urembo (ISAPS) zinaonyesha kuwa jumla ya upasuaji 652,676 wa kupunguza ukubwa wa matiti ulifanyika duniani kote mwaka 2024.
Idadi kubwa zaidi ya upasuaji huo ilirekodiwa nchini Brazil (115,647), ikifuatiwa na Marekani (67,478), Ufaransa (38,780), Ujerumani (32,068), Uturuki (25,334) na India (22,400).

Chanzo cha picha, Raquel
Raquel anasema amekuwa akisumbuliwa na maumivu ya muda mrefu ya mgongo kutokana na kuwa na matiti makubwa tangu alipokuwa kijana.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Lakini nchini Argentina, anasema, mara nyingi kuwa na matiti makubwa kulionekana kama jambo nzuri.
"Watu wengi, hata wanawake, wanakuambia kwamba una bahati sana," anaelezea.
"Sikuwa na bahati. Niliteseka sana. Niliteseka nilipokuwa kijana, hata pia nilipokuwa mwanamke na mama."
Anasema bado anasumbuliwa na maumivu ya mgongo kutokana na namna alivyokuwa akitembea ili kujaribu kuficha mwili wake.
Raquel, ambaye ni mtu anayependa mazoezi, anasema alipenda kufanya yoga, Pilates na mazoezi ya viungo. Lakini hatimaye, uzito wa matiti yake ulimzuia kufanya mazoezi.
Dkt. Nora Nugent, rais wa Chama cha Madaktari wa Upasuaji wa Plastiki ya Urembo cha Uingereza, anasema kuzuiwa kufanya harakati za kawaida na ugumu wa kufanya mazoezi ni miongoni mwa malalamiko yanayojitokeza mara nyingi kutoka kwa wagonjwa wanaotafuta upasuaji wa kupunguza ukubwa wa matiti.
"Kwa upande wa utendaji wa mwili, matiti makubwa huwa na uzito, hivyo huvuta mwili kuelekea mbele na kuweka shinikizo la mara kwa mara kwenye mgongo na shingo,"
"Pia hufanya mazoezi yasiwe ya rahisi na kufanya iwe vigumu sana kupata sidiria inayokutosha vizuri na kutoa usaidizi unaohitajika."
Raquel anasema alilazimika kuvaa "sidiria mbili au tatu" kwa wakati mmoja ili kupata usaidizi wa kutosha kwa matiti yake.
Kupata sidiria inayomtosha pia kulimuwekea mzigo wa ziada kifedha.
"Nchini Argentina, sidiria za wanawake wenye matiti makubwa zilikuwa ghali sana," anasema.
"Nilijihisi huru"

Chanzo cha picha, Raquel
Nchini Uingereza, Nugent anasema wagonjwa wake wengi huondolewa kati ya gramu 500 na 800 za tishu kutoka kila titi, ingawa amewahi kushuhudia visa ambavyo kiasi kikubwa zaidi kiliondolewa.
"Wakati mwingine si kiasi kikubwa ukizingatia uzito wa mwili kwa ujumla, lakini ni kiasi kikubwa kwa eneo dogo," anaeleza.
Kwa Raquel, madaktari waliondoa jumla ya kilo 2.5 za tishu kutoka kwenye matiti yake.
"Baada ya upasuaji, nakumbuka nilivyohisi nilipolazimika kuinama kuchukua kitu sakafuni, nikajiambia, 'Wow, ni kama nimepata mwili mwingine.' Nilijihisi huru sana."
Nguvu ya sidiria inayotoshea vizuri
Profesa Joanna Wakefield-Scurr alipokwenda kwa daktari wake kutokana na maumivu ya muda mrefu ya matiti, aliambiwa kwamba alichohitaji ni sidiria inayomtoshea vizuri.
Akiwa mtaalamu wa biomekanika, aliamua kufanya utafiti kuhusu kile kinachofanya sidiria iwe nzuri na inayofaa.
"Nilitambua kwamba kwa kweli nilijua machache sana kuhusu kwa nini tunahitaji sidiria, faida zake ni zipi na inapaswa kufanya kazi vipi," anasema Wakefield-Scurr.
"Badala yake, sidiria ilionekana zaidi kama nyenzo ya mitindo kuliko kitu chenye kazi maalumu, kinachotoa manufaa ya kiafya. Hilo lilinikatisha tamaa sana."
Hali hiyo ilimhamasisha kuanzisha kikundi cha utafiti wa afya ya matiti katika Chuo Kikuu cha Portsmouth nchini Uingereza mwaka wa 2005.
Timu yake ilibaini madhara manne makuu ya kuvaa sidiria isiyotoshea vizuri; maumivu, kunyooshwa kwa ngozi na kuharibika kwa tishu, mabadiliko katika namna mtu anavyopumua na muda kati ya mapigo ya moyo, pamoja na kikwazo katika kuendelea kufanya shughuli za kimwili.
"Ikiwa una matiti mazito na yanatikisika juu na chini, hilo linaweza kubadilisha upumuaji wako na namna unavyopumua. Pia hubadilisha nguvu unayoweka chini unapokanyaga. Kwa namna fulani, linaathiri jinsi mwili wako mzima unavyofanya kazi."

Chanzo cha picha, UEFA/UEFA via Getty Images
Kupitia miaka ya utafiti na majaribio, kikundi hicho pia kiligundua kuwa suluhisho la kupunguza maumivu ya matiti linahusiana zaidi na kupunguza mwendo wa matiti kuliko ukubwa wa mwendo wenyewe.
Timu hiyo tayari imefanya kazi na wanamichezo wa kiwango cha juu, akiwemo Lionesses, timu ya taifa ya wanawake ya soka ya England, pamoja na baadhi ya wachezaji bora wa gofu wanawake duniani, ili kutengeneza sidiria inayofaa zaidi kwa mahitaji yao.
"Tunaona mashirika kama Shirikisho la Soka la England (FA) na World Rugby yakiwekeza fedha katika mipango ya afya ya wanamichezo wanawakena hilo limeanza kutokea katika kipindi cha miaka mitano iliyopita pekee," anasema Wakefield-Scurr.
"Ni jambo jipya kwa kiasi fulani, lakini ni vizuri kuona mabadiliko haya."
"Wagonjwa wanataka kuishi maisha bora"
Raquel alilazimika kukabiliana na namna jamii inavyoiona na kuielewa changamoto ya kuwa na matiti makubwa.
Anasema alihisi kuhukumiwa na watu waliomzunguka baada ya kufanyiwa upasuaji wa kupunguza ukubwa wa matiti yake, na kwamba kulikuwa na dhana potofu kuhusu sababu iliyomfanya aamue kufanyiwa upasuaji huo.
"Nadhani watu wengi walifikiri kwamba ilikuwa zaidi kuhusu mwonekano kuliko suala la afya," anasema Raquel.
"Nakumbuka nilipofanyiwa upasuaji, mwanamke mmoja aliniambia, Sasa unapaswa kwenda kuondoa tumbo lako na kufanyiwa liposuction.'"
Licha ya maoni hayo, Raquel anasema hajutii uamuzi wake.
"Nina furaha sana, na sasa kwa kuwa nimefikia kipindi cha ukomo wa hedhi, sijui ningekabilianaje na maisha nikiwa na matiti makubwa. Siwezi kufikiria tena kuishi na mwili huo."
Nugent anasema kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa wanaotafuta upasuaji wa kupunguza ukubwa wa matiti kunaweza kuonyesha kuongezeka kwa umuhimu wa kujitunza kiafya.
"Kwa hakika kuna ongezeko, si miongoni mwa wanawake pekee bali pia kwa wagonjwa kwa ujumla wanaotaka kuishi maisha bora,"



































