Kwa nini Iran ina wasiwasi kuhusu kuimarika kwa uhusiano kati ya Israel na UAE?

Chanzo cha picha, TABNAK
Ziara ya hivi karibuni ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, jijini Abu Dhabi imeibua mashaka makubwa zaidi Tehran dhidi ya Falme za Kiarabu (UAE).
Maafisa na vyombo vya habari vya Iran vilielezea mkutano huo kama ushahidi wa hivi karibuni wa ushirikiano wa kiusalama unaozidi kuimarika kati ya Israel na UAE dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Hofu hizi, pamoja na mtazamo wa kuichukulia UAE kama tishio la kiusalama, zimeongezeka tangu vita vya hivi karibuni ambapo Iran ililenga mara kwa mara maslahi ya Marekani yaliyoko UAE, pamoja na miundombinu ya nishati ya nchi hiyo.
Hata hivyo, mvutano huo unavuka mipaka ya vita hivyo. Uhusiano wa UAE na Israel, ukaribu wake na Iran pamoja na Mlango-bahari wa Hormuz wenye umuhimu wa kimkakati, mzozo wa muda mrefu kuhusu visiwa vitatu katika Ghuba, na uhusiano wake mpana wa kiuchumi na Iran, vyote vimeunda uhusiano tata ambapo kutokuaminiana sana kunakinzana na uhalisia wa kutegemeana kiuchumi.
Kwa nini ziara ya Netanyahu iliikasirisha Tehran?
Baada ya Waziri Mkuu wa Israel kutembelea Abu Dhabi mnamo Septemba 27 na kukutana na Rais Mohammed bin Zayed Al Nahyan, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Ismail Baghaei, alizitahadharisha nchi za eneo hilo kuwa matumizi ya maeneo yao na Israel kulenga Iran yanaweza kusababisha "madhara makubwa sana".
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, Meja Jenerali Mohsen Rezaei, alizungumza kwa uwazi zaidi. Alisema: "Kama vile kuwa mwenyeji wa kambi za kijeshi za Marekani hakukuwaletea usalama, vivyo hivyo kuwa mwenyeji wa 'mchinjaji wa Gaza' hakutaleta matokeo mazuri."
Katika ujumbe kwenye mtandao wa X, Rezaei pia alizitaka nchi za eneo hilo kuacha kile alichokiita "madai yasiyo na msingi" kuhusu "visiwa vitatu vya Ghuba ambavyo ni mali ya Iran."
Kutajwa kwa visiwa hivyo katika onyo hilo hakukuwa kwa bahati mbaya. Siku chache tu kabla ya hapo, Falme za Kiarabu (UAE) zilikuwa zimerejelea madai yake kuhusu visiwa vya Ghuba vinavyodhibitiwa na Iran vya Abu Musa, Greater Tunb, na Lesser Tunb, katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Tehran ilisisitiza tena kwamba mamlaka yake juu ya visiwa hivi "haiwezi kujadiliwa".
Magazeti ya Iran yalikwenda mbali zaidi.
Kichwa cha habari katika gazeti la "Vatan-e Emrooz" kilisomeka: "Wakati mashekhe wa Imarati wanapofanya kazi kama vibaraka wa Trump na Bibi," na kulielezea taifa hilo jirani la Ghuba kama "kampuni ya Kizayuni ya Imarati."
Vyombo vingine vya habari pia vilionyesha Abu Dhabi kama mhusika anayewezesha uratibu wa usalama unaoongozwa na Israel dhidi ya Iran, na kukisia kuwa mkutano huo unaweza kupelekea kuundwa kwa ushirikiano mpana zaidi wa usalama katika eneo hilo.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Kwa nini Tehran inalenga Falme za Kiarabu (UAE)?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ufafanuzi wa kina kuhusu matukio na masuala muhimu zaidi, ili kukusaidia kuelewa mabadiliko makubwa yanayokuzunguka na athari zake katika maisha yako.
Sababu ya moja kwa moja inaweza kuwa jiografia. UAE iko ng'ambo ya Ghuba mkabala na Iran, na inapakana na Lango la Hormuz njia muhimu sana ya kimataifa ya usafirishaji wa nishati ambayo kwa sasa iko katikati ya mzozo kati ya Marekani na Iran.
Pia, Abu Dhabi ina miundombinu mikubwa ya kijeshi ya nchi za Magharibi, huku UAE ikiwa imejenga bandari na njia mbadala nje ya Lango la Hormuz, hasa huko Fujairah.
Kwa Tehran, hali hii inaleta changamoto kubwa ya kiusalama.
Wakati wa mzozo huo, maafisa wa Iran walizishutumu mara kwa mara nchi za Ghuba kwa kuruhusu Marekani na Israel kutumia ardhi, anga, au vituo vyao vya kijeshi.
Katika moja ya kauli zake, Baghaei alisema kuwa "maeneo ya jirani kwenye pwani ya kusini ya Ghuba ya Uajemi" yalitumiwa kupanga na kuandaa mashambulizi dhidi ya Iran.
Kufuatia hayo, Iran ilianzisha mfululizo wa mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani (droni) dhidi ya maeneo mbalimbali nchini UAE, ikilenga sio tu kambi za Marekani, bali pia miundombinu ya kiraia na ile ya nishati.
Maafisa wa Iran walielezea mashambulizi hayo kama hatua ya kulipiza kisasi dhidi ya vituo vya kijeshi vilivyohusika katika mashambulizi dhidi ya Iran, huku mamlaka za UAE na serikali nyingine zikipinga hoja hizo za Tehran.
Hivyo, mzozo huo umezidisha mashaka ya Iran kwamba UAE sio tu inahifadhi vikosi vya Marekani, bali inazidi kuingizwa katika mtandao wa usalama wa Marekani na Israel.
Ni ipi nafasi ya visiwa vya Ghuba na 'makubaliano ya Abraham'?
Mgogoro kuhusu visiwa hivyo vitatu ulianza miongo kadhaa kabla ya kuanzishwa kwa uhusiano wa sasa kati ya Israel na UAE.
Kwa Iran, visiwa hivi vinawakilisha suala la mamlaka ya taifa lisiloweza kujadiliwa na ni kipengele muhimu cha msimamo wake wa kimkakati katika eneo la Ghuba.
UAE inasisitiza kuwa visiwa hivyo ni eneo la UAE linalokaliwa kimabavu na Iran, na imetoa wito mara kwa mara wa kufanyika mazungumzo au usuluhishi wa kimataifa.
Katika muktadha huu, imepata uungwaji mkono kamili wa kisiasa kutoka kwa mataifa makubwa ya Kiarabu, ikiwemo Saudi Arabia.
Hata hivyo, Tehran imeeleza mara kwa mara kuwa visiwa hivyo ni "sehemu isiyotenganishwa ya eneo la Iran".
Ali Akbar Velayati, mshauri wa masuala ya kimataifa wa Kiongozi Mkuu wa Iran, aliandika katika ujumbe kwenye mtandao wa X mnamo Oktoba 3: "Nchi ambayo maisha yake ya kisiasa hayajafikisha hata nusu karne inatoa madai kutoka kwenye jukwaa la Umoja wa Mataifa kuhusu visiwa ambavyo vimeandikwa kama vya Iran katika nyaraka za kihistoria na ramani za karne nyingi zilizopita."
Pia alisisitiza tena kuwa visiwa hivyo ni vya Iran na kuikosoa UAE kwa kumkaribisha Netanyahu.
Hisia ya kutishiwa iliongezeka sana kutokana na Makubaliano ya Abraham yaliyotiwa saini mwaka 2020.
Makubaliano hayo yalipotiwa saini, yalisababisha wimbi la kulaaniwa vikali na Kiongozi Mkuu wa wakati huo, Ali Khamenei, ambaye aliishutumu Abu Dhabi kwa kusaliti "ulimwengu wa Kiislamu, ulimwengu wa Kiarabu, nchi za eneo hilo, na kadhia ya Palestina."
Alisema UAE iliwasaidia Waisraeli "kupata ngome katika eneo hilo".
Miaka sita baadaye, msimamo huu umerudi na kuwa msingi wa mjadala wa sasa kuhusu "Israel ya pili".
Licha ya changamoto zote zinazokabili makubaliano hayo, hasa baada ya vita vya Gaza mwaka 2023, mchakato wa kuhalalisha uhusiano kati ya Waarabu na Israel ulionekana mjini Tehran kama mfano hatari.
Utata unaozunguka makubaliano hayo umepata uzito zaidi wa kisiasa kwani sasa unaingiliana na ushindani mpana zaidi kuhusu usalama wa Ghuba.
Tovuti ya "Pars Today", inayohusishwa na serikali ya Iran, ilieleza kuwa uhusiano huo umepita mipaka ya uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi na kufikia ushirikiano wa "usalama, ujasusi na kijeshi". Katika ripoti iliyochapishwa tarehe 1 Oktoba, tovuti hiyo ilidai kuwepo kwa uratibu wa kijasusi kati ya Israel na Abu Dhabi wakati wa mzozo wa mwaka 2026, madai ambayo pia yamewahi kutolewa hadharani na wabunge pamoja na wachambuzi.
Wakati utegemezi wa kiuchumi unapoleta changamoto ya kimkakati
Hapa ndipo penye utata katika uhusiano huo. Iran na Falme za Kiarabu (UAE) ni mahasimu wa kiusalama, lakini pia ni washirika wakubwa wa kibiashara.
Kwa muda mrefu, Dubai imekuwa lango muhimu la kibiashara kwa bidhaa zinazoingizwa Iran, bidhaa zinazouzwa tena (re-exports), na miamala muhimu ya kifedha, hasa kutokana na vikwazo vikali vya kimataifa.
Ripoti ya shirika la habari la Tasnim mwishoni mwa mwezi Mei ilinukuu utafiti uliokadiria thamani ya biashara isiyo rasmi kati ya Iran na UAE kuwa takriban dola bilioni 16.
Ripoti hiyo iliongeza kuwa sehemu kubwa ya bidhaa muhimu zinazoingizwa Iran hupitia njia za UAE.
Uhusiano huu wa kiuchumi umedumu licha ya miaka mingi ya mvutano wa kisiasa.
Hata hivyo, vita vilivuruga uhusiano huo kwa kiasi kikubwa. Mwezi Agosti, UAE ilitangaza kusimamisha shughuli zote za kibiashara, kifedha, na nyinginezo na Iran hadi hapo itakapotoa taarifa nyingine, huku mvutano wa kikanda ukizidi kuongezeka.
Hii ina maana kwamba changamoto ya kimkakati inayolikabili Tehran imezidi kuwa kubwa.
Ingawa watu wenye msimamo mkali nchini Iran wanaielezea Abu Dhabi kama "kituo cha uadui" au "Israeli ya pili", hasa pale viongozi wa Israel wanapokaribishwa huko, UAE bado iko karibu kijiografia, ni muhimu kiuchumi, na inashiriki kikamilifu katika mfumo wa biashara wa kikanda ambao Iran yenyewe inautegemea sana.
Hali hii inaweza kuelezea kwa nini kauli za Iran zinatishia Abu Dhabi huku wakati huo huo zikiitaka ijiepushe na Washington pamoja na Israel.
Mkakati mpana wa Iran hauhusu tu ziara ya hivi karibuni ya Netanyahu, bali pia iwapo UAE inakuwa sehemu ya kudumu ya mfumo wa usalama unaoongozwa na Israel, mfumo ambao Tehran imetumia miaka mingi kujaribu kuuvunja, na jinsi inavyoweza kupinga mabadiliko haya bila kuathiri maslahi yake yenyewe ya kiuchumi na kidiplomasia.
































