Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Marekani na Iran zaanza mazungumzo kuhusu makubaliano ya awali ya amani Uswizi
Mazungumzo ya Marekani na Iran yanaanza nchini Uswizi huku Tehran ikisema imefunga mlango wa bahari wa Hormuz
Muhtasari
- Chama cha Waziri Mkuu Ethiopia chashinda uchaguzi mkuu Ethiopia
- Ghana kupokea mabaki ya urithi wa kihistoria 2,000
- Marekani na Iran zaanza mazungumzo kuhusu makubaliano ya awali ya amani Uswizi
- Taiwan kufanya mazoezi ya kujitayarisha na vita
- Israel yasema imewauawajumbe wawili wa Hamas
- Uuzaji wa mafuta wasitishwa Crimea
- Mfalme Charles kufichua kwa mara ya kwanza kiwango cha kodi anacholipa
- Sina sababu ya kuamini Waziri Mkuu Starmer atajiuzulu - Waziri
- Mpatanishi Mkuu wa Marekani na Iran awasili Uswisi
- Dunia yasherehekea Siku ya Baba huku mjadala wa malezi ukiongezeka
- Shambulio la Israel chanzo cha kifo cha mwanaharakati wa uhifadhi Lebanon
- Ziara hii haimaanishi kuanza kwa awamu ya pili ya mazungumzo - Iran
- Mashambulizi ya Israel yawaua watu sita Gaza, akiwemo mpiga picha wa Al Jazeera
- Kombe la Dunia 2026: Curaçao waweka historia, wapata sare ya kwanza dhidi ya Ecuador
- Mazungumzo ya Marekani na Iran kuanza Uswisi
Moja kwa moja
Na Asha Juma
Chama cha Waziri Mkuu Ethiopia chashinda uchaguzi mkuu Ethiopia
Chama tawala cha Prosperity Party kinachoongozwa na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, kimeshinda uchaguzi mkuu wa nchi hiyo kwa wingi wa kura, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Ethiopia ilitangaza Jumapili.
Kwa mujibu wa tume hiyo, Prosperity Party kimepata viti 438 kati ya 547 vya bunge la taifa katika uchaguzi ulioghubikwa na migogoro ya kiusalama na tuhuma za ukandamizaji.
Huu ni ushindi wa pili wa uchaguzi kwa Abiy Ahmed, ambaye aliingia madarakani mwezi Aprili 2018, kufuatia maandamano makubwa ya kupinga serikali dhidi ya chama tawala cha wakati huo, Ethiopian People's Revolutionary Democratic Front (EPRDF), muungano uliotawala nchi hiyo tangu mwaka 1991.
Mamilioni ya watu katika jimbo la kaskazini la Tigray, ambalo bado linaendelea kuathiriwa na madhara ya vita vya miaka miwili, hawakuweza kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa saba wa nchi hiyo.
Serikali ya shirikisho na viongozi wa Tigray wamekuwa wakituhumiana kwa kukiuka makubaliano yaliyomaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 2020 hadi 2022.
Vilevile, maeneo mengi ya uchaguzi katika mikoa ya Oromia na Amhara, ambayo ndiyo yenye idadi kubwa zaidi ya watu nchini humo, hayakuweza kushiriki uchaguzi kutokana na mapigano yanayoendelea kati ya waasi wenye silaha na vikosi vya serikali.
Tume ya Uchaguzi ilisema kuwa, "Licha ya kuwepo kwa changamoto katika majimbo machache, uchaguzi ulikuwa wa mafanikio."
Maeneo ambayo hayakuweza kufanya uchaguzi tarehe 1 Juni 2026 yatafanya uchaguzi wa marudio, ingawa tume bado haijatangaza tarehe ya uchaguzi huo.
Chama cha Prosperity Party, ambacho kimeshinda viti 438 bungeni, kinatarajiwa kuunda serikali mpya mwanzoni mwa mwezi Oktoba, huku Abiy Ahmed akitarajiwa kuendelea kuwa kiongozi wake.
Ghana kupokea mabaki ya urithi wa kihistoria 2,000
Serikali ya Ghana imekaribisha uamuzi wa Ujerumani na Uholanzi wa kurejesha takribani mabaki ya urithi wa kihistoria 2,000 yaliyochukuliwa kutoka taifa hilo la Afrika Magharibi wakati wa enzi za ukoloni na biashara ya utumwa kupitia Bahari ya Atlantiki.
Tangazo hilo limetolewa wakati wa mkutano wa Next Steps Conference, wa mashauriano wa ngazi ya juu uliofanyika mjini Accra, ambapo mabalozi wa nchi hizo mbili za Ulaya waliwasilisha orodha ya mabaki hayo kwa Rais wa Ghana, John Dramani Mahama, kabla ya kurejeshwa kwake nchini.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ghana, Samuel Okudzeto Ablakwa, alisema serikali ya Ujerumani imekamilisha utambuzi wa vitu vya kihistoria vilivyochukuliwa kutoka eneo la jadi la Kpando na imejitolea kuvirejesha vyote nchini Ghana.
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Denmark aliomba radhi kwa nafasi ya nchi yake katika biashara ya utumwa wa Waafrika kupitia Atlantiki na kuahidi kusaidia juhudi za kuhifadhi majumba ya kihistoria yaliyojengwa na Denmark katika pwani ya Ghana. Alisema hatua hiyo inalenga kuzuia kufutwa kwa historia, kuhimiza ukweli kujulikana na kuhakikisha makosa hayo hayajirudii.
Hatua hizi za kidiplomasia zinatajwa kuwa mafanikio makubwa katika juhudi za Ghana za kushinikiza kurejeshwa kwa urithi wa kitamaduni uliochukuliwa wakati wa ukoloni na kuondoa athari za mifumo ya kikoloni katika taasisi za kitamaduni duniani.
Katika miaka ya hivi karibuni, nchi kadhaa za Afrika zimefanikiwa kushinikiza kurejeshwa kwa baadhi ya vitu vya kihistoria vilivyochukuliwa wakati wa ukoloni, ingawa baadhi ya vitu hivyo vimerudishwa kwa mkopo wa muda tu.
Mwaka 2022, Ujerumani ilikuwa nchi ya kwanza kurejesha sanamu za shaba za Benin kwa Nigeria kama sehemu ya juhudi za kukabiliana na kile ilichokiita "historia yake mbaya ya kikoloni”.
Sanamu hizo zilichukuliwa mwaka 1897 na wanajeshi wa Uingereza kutoka Ufalme wa Benin, uliokuwa katika eneo ambalo sasa ni Jimbo la Edo nchini Nigeria, na nyingi ziliuzwa katika minada ya London kabla ya kusambazwa katika makusanyo mbalimbali duniani.
Marekani na Iran zaanza mazungumzo kuhusu makubaliano ya awali ya amani Uswizi
Maafisa wa Marekani na Iran wamewasili Uswizi kwa mazungumzo ya moja kwa moja baada ya kusaini makubaliano ya awali ya kumaliza vita wiki iliyopita.
Makubaliano hayo yanajumuisha ahadi ya kufikia makubaliano ya mwisho ndani ya siku 60, pamoja na kusitisha mapigano katika maeneo yote ya mzozo, ikiwemo Lebanon, na kufunguliwa tena kwa Mlango-Bahari wa Hormuz.
Hata hivyo, mapigano yanayoendelea kati ya Israel na Hezbollah inayoungwa mkono na Iran nchini Lebanon yaliifanya Iran kutangaza Jumamosi kwamba imefunga njia hiyo muhimu ya usafirishaji wa majini, ingawa takwimu za ufuatiliaji zinaonyesha kuwa meli zimeendelea kupita katika eneo hilo.
Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, alisema kuwa Marekani ina matumaini ya kupiga hatua katika suala la nyuklia na hali ya Lebanon, huku Tehran ikisema kuwa itasisitiza upande mwingine kutekeleza ahadi zake.
Vance aliungana na wenzake nchini Uswisi Jared Kushner, mkwe wa Rais wa Marekani Donald Trump, pamoja na mjumbe maalum Steve Witkoff.
Kwa upande wa Iran, Spika wa Bunge Mohammad Bagher Ghalibaf na Waziri wa Mambo ya Nje Abbas Araghchi waliwasili nchini Uswisi Jumamosi usiku.
Taiwan kufanya mazoezi ya kujitayarisha na vita
Jeshi la Taiwan litafanya mazoezi ya kujitayarisha na mapambano kwa siku tano kuanzia wiki hii, Wizara ya Ulinzi ilisema Jumapili.
Hatua hiyo ni sehemu ya mpango wa kisasa wa kuboresha mafunzo ya kijeshi kwa kuelekeza zaidi mazoezi kwenye mazingira halisi yanayofanana na vita badala ya maonyesho ya kawaida yaliyopangwa.
Taiwan, ambayo China inaidai kuwa sehemu ya himaya yake licha ya pingamizi kutoka serikali ya Taipei, inasema majeshi ya China mara kwa mara hufanya shughuli za kijeshi angani na baharini karibu na kisiwa hicho ili kuishinikiza ikubali mamlaka ya Beijing.
Jeshi la Taiwan limeanza kuandaa baadhi ya mazoezi yake kwa kuzingatia uwezekano wa China kubadili ghafla moja ya mazoezi yake ya kawaida kuzunguka kisiwa hicho na kuyageuza kuwa shambulio halisi.
Mazoezi hayo, yaliyopewa jina la “Mazoezi ya Utayari wa Haraka wa Vita”, yataanza Jumatatu na kumalizika Ijumaa. Wizara ya Ulinzi ilisema ni sehemu ya mpango wa mafunzo ya kila mwaka ya operesheni za pamoja za vikosi vya ulinzi.
"Lengo kuu ni kuvifundisha vikosi katika ngazi zote kuzoea taratibu za mapambano na mazingira ya uwanja wa vita wakati wa hatua ya utayari wa kupelekwa vitani," wizara hiyo ilisema.
Aidha, mazoezi hayo yanatarajiwa kuimarisha uwezo wa kubadilika haraka kutoka hali ya amani kwenda hali ya vita pamoja na kuharakisha upelekaji wa vikosi muhimu, yakihusisha wanajeshi halisi, katika maeneo halisi, kwa wakati halisi, kwa kutumia vifaa halisi na kupitia utekelezaji halisi.
Taiwan mara kwa mara hufanya mazoezi ya kijeshi. Mapema mwezi huu ilijaribu mfumo wake mpya wa kurusha makombora wa HIMARS uliotengenezwa Marekani, ambao pia umetumika kwa kiasi kikubwa na Ukraine, katika Mlango wa Bahari wa Taiwan.
Michezo mikubwa ya kivita ya kila mwaka ya Taiwan, inayojulikana kama Han Kuang, inatarajiwa kufanyika mwezi Agosti.
Soma zaidi:
Israel yasema imewaua wajumbe wawili wa Hamas
Jeshi la Israel limesema siku ya Jumapili kuwa limewaua Hussein Qadra na Mohammed Farra, ambao lilidai kuwa walikuwa wajumbe wa vikosi vya kijeshi vya Hamas na Islamic Jihad.
Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na jeshi hilo kwenye mtandao wa X, Qadra, ambaye alikuwa akiongoza mtandao huo pamoja na Farra, alifanya kazi chini ya uongozi wa Hamas na alisaidia kuwezesha uhamishaji wa zaidi ya sarafu za shekeli milioni 500 Kwenda kwa Hamas.
Soma Zaidi:
Uuzaji wa mafuta wasitishwa Crimea
Mamlaka zinazoungwa mkono na Urusi zimesitisha uuzaji wa mafuta kwa wananchi katika eneo la Crimea linalokaliwa kimabavu na Urusi, wakati Ukraine ikiendelea na mashambulizi yake dhidi ya eneo hilo.
Uuzaji wa mafuta ulikuwa tayari umepunguzwa kutokana na uhaba uliosababishwa na uharibifu wa hivi karibuni wa Ukraine dhidi ya njia za usambazaji katika maeneo yanayokaliwa na Urusi.
Gavana wa Crimea, Sergey Aksyonov, alisema watu binafsi na kampuni watazuiwa kununua mafuta katika vituo vya mafuta, na mafuta yatauzwa tu kwa taasisi za serikali zinazohusika na kuhakikisha "utendaji na usalama" wa Crimea.
Awali, Aksyonov alisema watu wanne waliuawa na wengine 28 kujeruhiwa baada ya shambulio la ndege isiyo na rubani yani droni ya Ukraine kulenga kituo cha kuhifadhi mafuta mjini Kerch usiku kucha.
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, aliliita shambulio hilo "jibu la haki kwa mashambulizi ya kikatili ya Urusi."
Crimea, ambayo Urusi ilidhibiti kinyume na sheria mwaka 2014, limekuwa eneo linalokumbwa na changamoto kubwa za usafirishaji na uhaba wa bidhaa.
Zelensky alisema Kyiv pia ilishambulia kituo cha usafirishaji wa mafuta katika eneo la Krasnodar nchini Urusi, ambalo liko karibu na Crimea upande wa pili wa Mlango wa Kerch. Mamlaka za eneo hilo zilisema mtu mmoja aliuawa kwenye kivuko cha abiria.
Rais huyo alisema pia vituo vya kijeshi vya usafirishaji wa vifaa na mifumo ya rada vililengwa, bila kutaja maeneo husika.
"Urusi inaelewa nguvu pekee, na nguvu zetu za masafa marefu bila shaka zinafanya kazi kwaajili ya amani," alisema katika taarifa iliyowekwa kwenye mtandao wa X.
Zelensky aliongeza kuwa watu wasiopungua saba waliuawa katika mashambulizi ya Urusi mwishoni mwa wiki, huku zaidi ya watu 30, wakiwemo watoto, wakijeruhiwa.
Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilisema ndege zisizo na rubani 239 za Ukraine zilidunguliwa usiku kucha.
Pande zote mbili zimeongeza mashambulizi katika miezi ya hivi karibuni huku juhudi za kufikia usitishaji mapigano zikikwama, zaidi ya miaka minne tangu Urusi ianzishe uvamizi wake mkubwa nchini Ukraine.
Ukraine imeelekeza mashambulizi yake kwenye miundombinu ya nishati na vituo vya mafuta, ikisema maeneo hayo yanawezesha uwezo wa vita wa Urusi.
Wiki iliyopita, mabaki ya mafuta meusi yaliripotiwa kunyesha mjini Moscow baada ya Ukraine kushambulia kiwanda kikubwa cha kusafisha mafuta, shambulio lililoelezwa kuwa kubwa zaidi la aina hiyo tangu kuanza kwa vita. Moscow iliahidi kulipiza kisasi.
Crimea imekuwa ikikabiliwa na matatizo makubwa ya usafirishaji na uhaba wa bidhaa. Eneo hilo lina umuhimu mkubwa wa kimkakati kwasababu vikosi vya Urusi hulitumia kama msingi wa kuanzisha mashambulizi dhidi ya maeneo mengine ya Ukraine.
Pia ni eneo maarufu la mapumziko ya majira ya joto kwa Warusi, baadhi yao wakiripoti kupata changamoto ya kupata mafuta ya magari yao ili waweze kurejea nyumbani.
Pia unaweza kusoma:
Mfalme Charles kufichua kwa mara ya kwanza kiwango cha kodi anacholipa
Kwa mara ya kwanza, Mfalme Charles wa Uingereza anatarajia kufichua kiasi cha kodi anacholipa kama mfalme siku ya Alhamisi Juni 25 2026, msemaji wa familia ya kifalme alisema hayo siku ya Jumapili, huku Kasri la Buckingham likijaribu kuimarisha uwajibikaji na uwazi zaidi kwa wananchi.
Kwa mujibu wa sheria, Charles halazimiki kulipa kodi ya mapato, kodi ya faida ya mtaji au kodi ya urithi kwa mali alizorithi kutoka kwa Malkia Elizabeth II.
Hata hivyo, kwa hiari yake, Charles amekubali kulipa kodi ya mapato na kodi ya faida ya mtaji pale anapouza mali zake binafsi.
• Maelezo hayo yatachapishwa kama sehemu ya hesabu za mwaka za familia ya kifalme zitakazotolewa Alhamisi Juni 25 2026.
• Mbali na pauni milioni 132 (sawa na dola milioni 175) alizopokea kutoka serikalini katika mwaka wa kodi wa 2025/26 kwaajili ya kugharamia majukumu ya kifalme, Charles pia hupata mapato binafsi kutoka kwenye ardhi na mashamba yake binafsi pamoja na uwekezaji mbalimbali.
• Msemaji wa Kasri la Buckingham alisema hatua hiyo inalenga “kukuza uelewa mpana zaidi kuhusu uwajibikaji wetu”.
• Kasri lilisema Charles alikuwa akitoa taarifa kuhusu kodi alizokuwa analipa alipokuwa Mwanamfalme wa Wales, na ana nia ya kuendelea kufanya hivyo katika miaka ijayo akiwa mfalme.
• Mwaka jana, Kamati ya Bunge la Uingereza ya Hesabu za Umma ilianzisha uchunguzi kuhusu utaratibu wa makaazi ya kifalme yanayotolewa kwa baadhi ya wanafamilia wa familia ya kifalme.
(Kwa kiwango cha ubadilishaji kilichotumiwa, dola 1 ya Marekani ni sawa na pauni 0.7557 za Uingereza.)
Sina sababu ya kuamini Waziri Mkuu Starmer atajiuzulu - Waziri
Waziri wa Biashara wa Uingereza, Peter Kyle, amesema siku ya Jumapili kuwa hana sababu yoyote ya kuamini kwamba Waziri Mkuu Keir Starmer anapanga kutangaza kujiuzulu siku ya Jumatatu.
Akizungumza na kituo cha taarifa za habari cha Sky News, Kyle alisema alikuwa na mazungumzo ya wazi na ya moja kwa moja na Starmer siku ya Ijumaa.
Gazeti la Observer la Uingereza liliripoti kuwa Starmer anatarajiwa kujiuzulu Jumatatu na kuweka wazi ratiba ya kuondoka kwake madarakani.
Hata hivyo, chanzo kutoka serikalini kilisema kuwa Waziri Mkuu bado anaendelea kuzingatia majukumu yake ya kuiongoza serikali.
Alipoulizwa kuhusu taarifa zinazoeleza kuwa Starmer anajiandaa kujiuzulu, "Sina sababu yoyote ya kuamini kuwa taarifa hizo ni za kweli. Ninaona uvumi mwingi unaendelea kusambaa," Kyle alisema.
"Leo, kama ilivyo tu kwa kila siku nyingine niliyomfahamu Keir, bado yupo kazini akifanya kazi kwa bidii. Wakati huohuo, anajaribu kupata nafasi ya kutafakari hali halisi ya kisiasa, changamoto zilizopo mbele yetu, pamoja na fursa zilizopo," Kyle aliongeza.
Kyle alikataa kueleza kwa undani mazungumzo yake ya Ijumaa na Starmer, isipokuwa kusema tu yalikuwa marefu na kwamba:
"Hakuwahi hata mara moja kuzungumzia maslahi yake binafsi. Kila mara alikuwa akizungumzia maslahi ya nchi."
Shinikizo dhidi ya nafasi ya Starmer limekuwa likiongezeka kwa miezi kadhaa, na liliongezeka zaidi siku ya Ijumaa baada ya mpinzani wake mkuu ndani ya chama, Andy Burnham, kushinda kiti cha ubunge ambacho kingemwezesha kuanzisha rasmi mchakato wa kumpinga Starmer katika uongozi wa chama.
Kwa mujibu wa ripoti ya Observer, Starmer alikuwa akijadili suala hilo na mke wake katika makaazi rasmi ya Chequers, kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho.
Viongozi waandamizi wa Chama cha Labour wanatarajia kuwa atatoa tamko la wazi kuhusu mustakabali wake mapema Jumatatu.
Soma Pia:
Mpatanishi Mkuu wa Marekani na Iran awasili Uswisi
Ofisi ya Waziri Mkuu wa Pakistani Shehbaz Sharif imetangaza kuwasili kwake nchini Uswisi kuhudhuria mazungumzo kati ya Iran na Marekani.
Jenerali wa Jeshi Asim Munir, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Pakistani na Vikosi vya Wanajeshi, pia anaandamana na Bw. Sharif katika safari hii.
Pakistan imekuwa mpatanishi mkuu katika mazungumzo kati ya Iran na Marekani katika miezi ya hivi karibuni.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistani hapo awali ilikuwa imesema kwamba wawakilishi kutoka Marekani na Iran, pamoja na wapatanishi kutoka Pakistan na Qatar, pia watahudhuria mkutano huo.
Dunia yasherehekea Siku ya Baba huku mjadala wa malezi ukiongezeka
Dunia leo inaungana kuadhimisha Siku ya Baba, siku maalum inayotambua na kuenzi mchango wa baba katika malezi ya watoto, ustawi wa familia na maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Maadhimisho haya, yanayofanyika kila Jumapili ya tatu ya mwezi Juni, yamekuwa fursa muhimu ya kuonyesha shukrani kwa baba, kutafakari nafasi yao katika maisha ya watoto, pamoja na kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili katika kutimiza majukumu yao ya kifamilia na kijamii.
Wengi hutumia siku hii kuwatakia heri baba zao, kuwapatia zawadi au kutumia muda pamoja nao kama njia ya kuonyesha shukrani kwa mchango wao.
Katika baadhi ya familia, siku hii pia hutumika kuwakumbuka kina baba waliofariki dunia au wale ambao wamekuwa na mchango mkubwa katika maisha ya watoto wao licha ya changamoto mbalimbali.
Hata hivyo, baadhi ya baba wanakabiliwa na changamoto za kiuchumi, majukumu ya kazi na mabadiliko ya kijamii yanayoathiri uwezo wao wa kutumia muda wa kutosha na familia zao.
Maadhimisho ya Siku ya Baba mwaka huu yanakuja wakati ambapo mijadala kuhusu usawa wa majukumu ya malezi kati ya wazazi inaendelea kushika kasi katika sehemu mbalimbali duniani.
Kwa wengi, siku hii si tu ya kusherehekea, bali pia ya kutafakari namna ya kuimarisha mahusiano ya kifamilia na kuhakikisha watoto wanapata malezi bora kutoka kwa wazazi wote wawili.
Pia unaweza kusoma:
Shambulio la Israel chanzo cha kifo cha mwanaharakati wa uhifadhi Lebanon
Mwanaharakati wa mazingira wa Lebanon, Mona Khalil, ambaye kazi yake ilisaidia kubadilisha sehemu ya pwani ya kusini mwa Lebanon kuwa moja ya maeneo muhimu zaidi ya mashariki ya Bahari ya Mediterania kwa viota vya kasa wa baharini walio hatarini kutoweka, amefariki baada ya kujeruhiwa katika shambulio la Israel.
Khalil, mwenye umri wa miaka 76, alijeruhiwa wakati nyumba yake iliyopo ufukweni mwa Mansouri, karibu na mji wa kusini wa Tyre, iliposhambuliwa wakati wa mashambulizi ya Israel kusini mwa Lebanon wiki mbili zilizopita.
Alifariki siku ya Ijumaa baada ya kukaa hospitalini kwa siku kadhaa, kulingana na shirika moja la mazingira la eneo hilo.
Kifo chake kilitokea wakati mashambulizi ya anga ya Israel yalipoongezeka kusini mwa Lebanon, hali inayozua wasiwasi kuhusu uwezekano wa kuongezeka tena kwa ghasia licha ya juhudi za kidiplomasia za kudumisha amani tete ya kikanda.
BBC imewasiliana na jeshi la Israel kwa ajili ya maoni.
Soma zaidi:
Ziara hii haimaanishi kuanza kwa awamu ya pili ya mazungumzo - Iran
Shirika la habari la Iran IRNA linaripoti kuwa ujumbe wa Iran uliowasili Uswisi umepangwa kufuatilia “jinsi ya kutekeleza ahadi zilizomo katika makubaliano ya maelewano kati ya Iran na Marekani.”
Kabla ya ujumbe huo kuondoka Iran, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Ismail Baghaei, alisisitiza kuwa ziara hii haimaanishi kuanza kwa awamu ya pili ya mazungumzo ya kufikia makubaliano ya mwisho, bali lengo lake kuu ni “kudai utekelezaji wa ahadi za upande wa pili.”
“Uelewa au makubaliano yoyote hupimwa katika hatua ya utekelezaji, na kwa kuzingatia uzoefu wa upande wa pili katika kuvunja ahadi zake, lazima tuwe thabiti na makini sana katika kudai haki zetu katika hatua ya utekelezaji,” Baghaei alisema.
Soma zaidi:
Mashambulizi ya Israel yawaua watu sita Gaza, akiwemo mpiga picha wa Al Jazeera
Mashambulizi ya Israel huko Gaza yameua takriban watu sita, akiwemo mpiga picha wa Al Jazeera na mtoto mmoja, kwa mujibu wa maafisa wa afya na waokoaji.
Al Jazeera ilisema “inalaani vikali uhalifu huu wa kikatili wa kulenga na kumuua” mwandishi wake Ahmed Wishah, ambaye aliuawa katika shambulio la bomu lililolenga nyumba moja katikati ya Gaza siku ya Jumamosi.
Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilidai kuwa Wishah alikuwa “gaidi katika kitengo cha kijeshi cha Hamas ambaye alihudumu kama mpiga risasi wa kuvizia”.
Wizara ya Afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas, ambayo takwimu zake zinachukuliwa kuwa za kuaminika na Umoja wa Mataifa, inasema jeshi la Israel limeua watu 1,007 tangu makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas yalipoanza Oktoba iliyopita.
Al Jazeera ilisema kifo cha Wishah siku ya Jumamosi “kinawakilisha ukiukaji mpya na mkubwa wa sheria zote za kimataifa na kanuni, na kinaonyesha sera inayoendelea ya kuwanyima sauti waandishi wa habari na kunyamazisha ukweli”.
IDF ilisema Wishah katika miezi ya hivi karibuni alikuwa akipanga mashambulizi ya kuvizia dhidi ya wanajeshi wa Israel, bila kutoa ushahidi.
Watu wengine wawili waliuawa pamoja na Wishah katika shambulio hilo lililolenga nyumba katika kambi ya wakimbizi ya Bureij, kwa mujibu wa hospitali ya eneo hilo na shirika la ulinzi wa kiraia linaloendeshwa na Hamas, ambalo hufanya kazi za uokoaji.
IDF pia ilidai kuwa wawili hao waliouawa walikuwa sehemu ya Hamas.
Ndugu yake Wishah, Mohamed, ambaye pia alikuwa mwandishi wa Al Jazeera, aliuawa katika shambulio la Israel mwezi Aprili. IDF ilidai kuwa alishirikiana na Hamas katika makao makuu ya uzalishaji wa makombora na silaha ya kundi hilo, bila kutoa maelezo zaidi.
Soma zaidi:
Kombe la Dunia 2026: Curaçao waweka historia, wapata sare ya kwanza dhidi ya Ecuador
Timu ya taifa ya Curacao walipata pointi yao ya kwanza kabisa katika Kombe la Dunia baada ya uchezaji wa kuvutia kutoka kwa kipa Eloy Room aliyefanikisha kuizuia timu ya taifa ya Ecuador iliyopoteza nafasi nyingi.
Kipa wa Miami FC, Room, aliweka rekodi kwa kuokoa jumla ya mipira 15, akizuia mashambulizi ya Wamarekani Kusini katika Kundi E.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 37 alionyesha kiwango cha juu sana cha uchezaji, akilingana na rekodi ya kipa wa Marekani Tim Howard ya kuokoa mara nyingi zaidi katika mechi ya Kombe la Dunia.
Howard aliokoa mara 15 dhidi ya timu ya taifa ya Ubelgiji mnamo mwaka 2014 katika mechi iliyokwenda hadi muda wa ziada (na pia kuruhusu mabao mawili katika kipigo cha 2-1) — lakini Room aliwezesha timu ya kocha Dick Advocaat kupata sare ya kihistoria.
Alianza kuokoa baada ya dakika tatu tu, na wengi wanasema kuwa ndiye aliyekuwa mchezaji bora zaidi wa usiku huo, na kumfuatilia kwa karibu mchezaji Enner Valencia aliyemzuia kufunga kwa karibu kabisa na lango.
Baada ya hapo, John Yeboah naye alinyimwa nafasi ya kufunga, kabla ya Room kuokoa tena shuti la Valencia katika jumla ya mara sita za kuokoa katika kipindi cha kwanza.
Kipindi cha pili kilikuwa na kasi zaidi baada ya mapumziko, huku kipa Room akifanya kazi ya ziada ya kuokoa mipira ya hatari iliolenga lango ya Moisés Caicedo, Pedro Vite, Kevin Rodríguez, Nilson Angulo, Gonzalo Plata na wachezaji wengine.
Curaçao nao walipata nafasi nzuri sana karibu na dakika ya 60, lakini shuti la Leandro Bacuna lilizuiliwa, kabla ya Liviana Comenencia naye kujaribu bahati yake na mpira kuokolewa.
Ecuador watajilaumu kwa kupoteza nafasi zao za wazi za kufunga, baada ya kupiga mashuti 27 kwa jumla bila mafanikio.
Sasa wanapaswa kuishinda Ujerumani, ambao ni vinara wa kundi, katika mchezo wao wa mwisho ili kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele kwenye hatua ya mtoano, baada ya kuanza vibaya kwa kupoteza dhidi ya Ivory Coast kwenye mchezo wao wa ufunguzi.
Kwa upande mwingine, Curacao—ambao walichapwa mabao 7-1 na Ujerumani kwenye mchezo wao wa kwanza—bado wana nafasi ya kusonga mbele hadi hatua ya 32 bora iwapo wataifunga Ivory Coast katika mechi yao ya mwisho ya hatua ya makundi.
Soma zaidi:
Mazungumzo ya Marekani na Iran kuanza Uswisi huku Tehran ikidai kufunga Mlango-Bahari wa Hormuz
Mazungumzo ya Marekani na Iran kuanza Uswisi huku Tehran ikidai kufunga Mlango-Bahari wa Hormuz
Mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Marekani na Iran yanatarajiwa kuanza nchini Uswisi licha ya jeshi la Iran kusema kuwa limefunga tena Mlango-Bahari wa Hormuz kufuatia mashambulizi ya Israel kusini mwa Lebanon.
Jeshi la Marekani limepinga madai hayo, likisema kuwa "usafiri wa meli unaendelea kama kawaida". Iran ilisema kuwa Mlango-Bahari wa Hormuz ulifungwa kujibu mashambulizi mabaya ya Israel nchini Lebanon, ambayo Tehran ilisema yalikiuka makubaliano yake na Marekani ya kumaliza vita.
Jumamosi jioni, Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, aliondoka Washington kuelekea Uswisi kwa ajili ya mazungumzo hayo.
Ujumbe wa Iran unaojumuisha Spika wa Bunge, Mohammad Bagher Ghalibaf, na Waziri wa Mambo ya Nje, Abbas Araghchi, tayari umewasili.
Duru mpya ya mazungumzo inatarajiwa kuanza Jumapili. Vance alisema ana matumaini ya kupiga hatua “kuhusu suala la nyuklia” na pia “suala la usitishaji mapigano nchini Lebanon”.
Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kupanda ndege yake, aliulizwa kuhusu mapigano kati ya Israel na Hezbollah pamoja na mashambulizi ya anga ya Israel kusini mwa Lebanon.
"Hali kwa kweli inaendelea kuimarika zaidi huko, na mambo yanaanza kutulia kidogo," Vance alisema.
"Hili ni jambo ambalo tutalazimika kuendelea kulisimamia ili kuhakikisha kwamba Israel na Lebanon zote mbili ziko salama na zenye usalama. Hilo ndilo lengo kuu — kufanya eneo lote liwe salama na utulivu," Vance aliongeza.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei, alisema kuwa nchi yake itakuwa "ikisisitiza upande mwingine kutimiza ahadi zake."
Soma zaidi:
Hujambo na karibu katika matangazo yetu Mubashara.