Kijiji ambacho watu husafiri kilomita 45 kuchaji simu zao

.
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Kwa Kulsooma, msichana mwenye umri wa miaka 19 kutoka Kijiji cha Vandiji iliyopo kwenye milima ya Himalaya, wilaya ya Kupwara Kashmir, suala la utandawazi na Maisha ya kisasa, ni mambo anayoyasikia, kwani maisha yake ni sawa na ya watu wa kale.

Vizazi vitano vya Kijiji cha Vandiji hawajahi kuwa na nguvu za umeme, na kizazi cha sasa kinakuwa pia kwa kutumia mwanga wa stovu au jiko la mafuta na mishumaa.

Kijiji hicho kimekuwa kikisubiria kupata umeme kwa miongo kadhaa ila hawajafanikiwa hadi kufikia sasa.

Watu wa kale wanaoishi nyakati za sasa

Sio tu njia pekee ndiyo mbovu kufika katika Kijiji hicho, ila Maisha ya wakaazi hao pia ni magumu.

Baada ya kufanya kazi mchana kutwa, jioni ikifika, changamoto mpya zinawakabili.

"Wanawake hapa wana wasiwasi sana kwa sababu mchana wanakumbwa na moshi kutoka kwenye majiko wanayopikia, na usiku moshi kutoka kwenye taa au mishumaa wanayotumia kusomea huwasababishia maumivu," anasema Kulsooma.

Anaelezea kuwa anapoondoka kijijini hapo, mara moja yeye huhisi kama si sehemu ya ustaarabu wa kisasa wa binadamu.

"Tunapokwenda sokoni Kupwara, tunajihisi duni tunapoona watu wakiwa na simu zao za kisasa. Tunapotembelea nyumba za ndugu,tunaona vifaa vya umeme vya kisasa. Inatufanya tuhisi kama, sisi ni watu wa kale wanaoishi katika nyakati za kisasa."

.

Kutokana na ukosefu wa barabara na umeme, wakaazi wa eneo hilo huishi kwa kukwea milima.

Wilaya ya Kupwara ipo kilomita 75 kaskazini mwa Srinagar. Kijiji cha Vandiji kipo kilomita 45 kutoka mji wa Kupwara, na inaweza kufikia kwa kutumia usafiri wa gari.

Ila watu hukwea millima hadi kufikia makazi yao. Na katika safari hii tulikutana na Bashir Ahmed Mir, ambaye alikuwa amebeba vyombo vya nyumbani begani.

Anatuelezea kuwa "huwa tunabeba vyombo vya nyumbani na bidhaa nyingine kutoka Kupwara na usiku tunakutana barabarani tukiwa na tochi, hakuna barabara, hakuna umeme, nikama serikali haijui Kijiji cha Vandiji kiko wapi"

Wakaazi wa eneo hilo huteremeka na kukwea milima kueleka mji wa Kupwara kuchaji simu zao ili waweze kuzungumza na jamaa zao, iwapo kuna dharura.

Ila huduma ya mtandao wa mawasiliano kwa njia ya simu ni duni sana.

"Nilipata mshutuko wa moyo kutokana na moshi wa jiko"

Ukosefu wa umeme umewaathiri pakubwa kiafya wakazi wa Kijiji hicho.

Abdul Rashid Malik, amekuwa akipokea matibabu kwa miaka miwili sasa. Anaugua ugonjwa wa moyo kutokana na kifua chake kuathirika.

"tunachoma kuni nyingi kila siku, haiharibu tu nyumba yetu bali pia afya yetu. Nilianza na kukohoa, kisha daktari akaniambia nina maambukizi ya kifua na baadaye ikabainika moshi unaathiri moyo wangu"

Abdul aliongezea kuwa "iwapo kungekuwa na umeme hakuna mmoja wetu angekuwa mgonjwa. Kuanzia kwa mababu zangu hadi babangu, hakuna ambaye amewahi kuona umeme. Tumeishi Maisha yetu sote gizani na sasa tunao watoto wadogo, hatujui nini kitawatokea huko mbeleni."

Watu wengi katika Kijiji hiki cha takriban watu 500, wanaugua magonjwa tofauti ya kifua, koo,macho yanayosababishwa na moshi kutoka taa ya mafuta au koroboi.

Kasmiir

Lakini mbona Kijiji hiki hakina umeme hadi kufikia sasa?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Maafisa husika wanasema kutounganisha umeme katika Kijiji hicho kunatokana na hali mbaya ya barabara.

"Vandiji ipo kilomita elfu 12 juu ya bahari, na barabara zake ni hatari. Umeme unaweza kuunganishwa ila ni vigumu kusafirisha vifaa vya kujenga miundo mbinu za umeme eneo hilo." Alisema Mohamed Shafi Wani mhandisi mkuu katika idara ya umeme.

Ila ngoja ngoja ya wakaazi hao inaweza kuisha mwaka huu

"Tayari tumesafirisha vifaa hitajika, na mpango wetu ni kuunganisha umeme katika Kijiji hicho mwishoni mwa mwaka huu" Mohammed Shafi Wani aliiambia BBC.

Tulipofika nyumbani kwa Riaz Ahmed Lone, baada ya giza kuingia, binti yake mwenye umri wa miaka 11, Asifa Jan, alikuwa akisoma somo la teknolojia ya habari, huku Riaz akiwasha tochi kwa ajili ya mwanga.

Riaz alituambia "Mustakabali wa watoto wetu uko hatarini. Leo, watu duniani kote wameunganishwa na simu za mkononi, lakini sisi bado tunaishi gizani. Unawezaje kupiga simu ikiwa hakuna umeme?"

Mohammad Sultan, mkuu wa kijiji cha Vandiji, amekuwa akiwasiliana na maafisa wa serikali kwa miaka mingi, lakini umeme bado haujafika kijijini humo.

"Nimechoka kwenda kutoka ofisi moja hadi nyingine kwa miaka mingi kuhusu suala hili. Sasa nguzo za umeme zimewekwa kijijini, lakini bado hakuna nyaya za umeme wala maandalizi mengine ya kuziunganisha," anasema Sultan.