Je, historia inaweza kuandikwa upya? Guardiola, Man City na mashtaka 115

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Katika misimu 10, Pep Guardiola ameiongoza Manchester City kutwaa mataji 17 makubwa - na 20 kwa jumla.
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Iwapo, kama inavyotarajiwa, Pep Guardiola ataondoka Manchester City mwishoni mwa msimu huu, atafanya hivyo akiwa mmoja wa makocha wenye mafanikio na ushawishi mkubwa katika historia ya Premier League.

City wamekuwa na nguvu kubwa katika mechi za Uingereza katika misimu yake 10 ya uongozi, muda ambao walishinda Ligi ya Premia mara sita (pamoja na rekodi nne mfululizo), pamoja na Ligi ya Mabingwa na Treble ya kihistoria.

Lakini ni kwa kiwango gani orodha isiyo na kifani ya zaidi ya mashtaka 100 ya madai ya ukiukaji wa sheria za fedha za Ligi Kuu ya Uingereza inaweka kivuli kwa muda wa Guardiola kuongoza?

Huku City wakiwa wamekana kufanya makosa kila mara, jibu litakuwa wazi tu wakati matokeo ya kesi hiyo yatakapofichuliwa.

Tume huru bado haijachapisha uamuzi takriban mwaka mmoja na nusu baada ya kikao cha nidhamu kukamilika.

Ikiwa sakata hiyo imekuwa na jukumu katika muda wa kuondoka kwa Guardiola, na kama alitaka kuondoka City kabla ya matokeo kujulikana, haijulikani.

Lakini hadi wakati huo, ni jambo lisiloepukika kwamba maswali yataulizwa kuhusu jinsi gani hasa City walivyofanikisha enzi ya kubeba kombe ambayo imekuwa ikifurahia tangu kuchukuliwa kwa klabu hiyo na bilionea wa kifalme wa Abu Dhabi Sheikh Mansour - naibu waziri mkuu wa Falme za Kiarabu - mwaka 2008.

Je, ni mashtaka gani?

.
Maelezo ya picha, Mhariri wa michezo wa BBC Dan Roan anaelezea mashtaka ya Manchester City

Mashtaka hayo 115 yanahusiana zaidi na msururu wa madai ya ukiukaji wa sheria za kifedha ya ManCity kati ya 2009 na 2018.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Ingawa hakuna pendekezo lolote kwamba Guardiola alikuwa anafahamu kuhusu kosa lolote, kuna mwingiliano wa miaka miwili na uongozi wake katika Uwanja wa Etihad, ulioanza majira ya joto ya 2016.

Mashtaka yanahusiana na:

Madai ya kushindwa kutoa taarifa sahihi za fedha, ikijumuisha maelezo ya malipo ya wachezaji na meneja, kuanzia misimu ya 2009-10 hadi 2017-18.

Madai ya kushindwa kuzingatia sheria za Uefa za fedha (FFP) kuanzia 2013-14 hadi 2017-18.

Madai ya ukiukaji wa kanuni za faida na uendelevu za Ligi Kuu (PSR) kuanzia 2015-16 hadi 2017-18.

City pia wanakabiliwa na mashtaka mengi kwamba walishindwa kushirikiana na uchunguzi wa Ligi Kuu kati ya Desemba 2018 na Februari 2023.

Kama meneja, Guardiola hajahusishwa na mchakato wa kisheria. Lakini hajaweza kudai kuwa mashtaka haya yanahusu tu kipindi kabla ya kuwasili kwake.

Mashtaka hayo yanafikiriwa kuhusishwa na madai yaliyotolewa kwa mara ya kwanza mnamo 2018 na chombo cha habari cha Ujerumani Der Spiegel, ambacho kilichapisha barua pepe za ndani za Man City zilizovuja.

Imedai kuwa nyaraka hizo zilionyesha kuwa klabu hiyo imeongeza mapato ya udhamini kutoka kwa shirika la ndege la serikali la Etihad na kampuni ya simu inayodhibitiwa na serikali ya Etisalat, kwa kuficha uwekezaji wa moja kwa moja kutoka kwa kampuni yake ya Mansour ya Abu Dhabi United Group (ADUG) kama mapato ya udhamini, kwa kuingiza fedha kupitia akaunti za kampuni hizo.

Hii, ilidaiwa, ilikuwa njia ya kuzunguka sheria za FFP zilizoanzishwa na Uefa mnamo 2011, na PSR iliyoletwa na Ligi Kuu mnamo 2012, mifumo miwili sawa ya udhibiti wa matumizi iliyoundwa kupunguza hasara za vilabu. Hatahivyo City na makampuni yalikanusha makosa.

Hapo ndipo yalifuata madai mengine ya kuripoti vibaya taarifa za kifedha zilizohusu hati ambazo zilidai kuonyesha malipo ya siri ya 'nje ya vitabu' kwa meneja wa zamani Roberto Mancini kupitia ada za ushauri kutoka kwa kilabu huko Abu Dhabi, na kuwapa wachezaji pesa zaidi kuliko ilivyokuwa kupitia akaunti rasmi ili matumizi yaliyorekodiwa yawe chini ya ilivyokuwa. Mancini alikana kosa lolote.

Kwa kifupi, City wanatuhumiwa kwa kupindua sheria za Ligi Kuu ambazo vilabu vilikubali kufuata, na kupotosha ushindani kwa misimu mingi.

City - ambao wamekuwa wakikana kuwa ni mali ya serikali - walisema barua pepe hizo zilipatikana kinyume cha sheria na ni "jaribio la kuharibu sifa ya klabu", wakisisitiza kuwa hawana hatia.

Hukumu hiyo itamaanisha nini?

Iwapo City itaondolewa mashtaka makubwa zaidi, urithi wa Guardiola utaonekana kuwa salama.

Lakini iwapo klabu hiyo itagundulika kuwa imekiuka sheria za kifedha, wengi watahitimisha kwamba makosa hayo yalisaidia City kutumia pesa nyingi kununua wachezaji bora, na kuweka misingi ambayo Guardiola aliijenga ili kupata mafanikio mengi, na kufikia kilele cha ushindi wa Treble wa 2023.

Mnamo 2024, Jose Mourinho alisisitiza kuwa alishinda mataji yake matatu ya Ligi ya Premia akiwa na Chelsea "kwa haki na safi", baada ya kuulizwa kuhusu Guardiola kufanya ishara ya vidole sita baada ya mechi, kuashiria kunyakua mataji aliyokuwa ameshinda.

Mourinho pia alitania kwamba huenda bado akatunukiwa medali ya washindi wa Ligi Kuu ya Uingereza, ikiwa City ingeishia kupokonywa mataji kama adhabu. Akiwa meneja wa Manchester United, Mourinho alikuwa amemaliza wa pili kwa City msimu wa 2017-18.

Iwapo City ingepatikana na hatia, huenda kukawa na marejeo mengi kutoka kwa mashabiki pinzani kwa mataji ambayo Guardiola alishinda kwa pointi moja pekee (zaidi ya Liverpool 2019 na 2022) na pointi mbili (zaidi ya Arsenal mwaka 2024).

Bila shaka, kama City ingepatikana na hatia, itakuwa vigumu kujua kama Guardiola angeshinda kidogo - na kiasi gani - ikiwa klabu ingezingatia sheria.

Lakini huo ndio ukubwa na uzito wa mashtaka, katika tukio kama hilo, wakosoaji bila shaka watabisha kwamba mafanikio yake mengi yametiwa doa, hata yale yaliyotokea baada ya kipindi kinachohusiana na kesi hiyo.

Mnamo 2019, huku City ikichunguzwa na Uefa, Guardiola aliulizwa moja kwa moja na BBC Sport ikiwa urithi wake unaweza kuathiriwa na mzozo huo.

"Hapana, hapana kabisa," alijibu.

Hata hivyo, mwenyekiti wa City Khaldoon al-Mubarak amekiri kufadhaishwa na mafanikio ya klabu hiyo uwanjani yakiambatana na ukumbusho wa mara kwa mara wa mashtaka yanayofunguliwa dhidi yao.

Klabu nyingine ya Ligi Kuu ni onyo. Sasa kuna shaka kuhusu mataji mbalimbali ambayo Chelsea ilishinda miaka ya 2010, baada ya klabu hiyo kubainika kufanya orodha ya malipo ya siri kwa mawakala kuhusu uhamisho, kati ya 2011 na 2018.

Guardiola amesema nini?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Pep Guardiola

Huko nyuma mwaka wa 2019, wakati City ikichunguzwa na Uefa, na kufuatia madai kuhusu malipo kwa Mancini, Guardiola alijibu kwa hasira alipoulizwa wakati wa mkutano na waandishi wa habari kufuatia fainali ya Kombe la FA ikiwa aliwahi kupokea malipo kama hayo.

Guardiola alijibu: "Kusema kweli, unadhani ninastahili kuwa na swali la aina hii, siku tuliposhinda Treble [ya nyumbani], nilipokea pesa? Je, unanishutumu kwa kupokea pesa?"

Mwandishi wa habari aliyehusika alieleza kuwa hapo awali aliwauliza City, lakini kutokana na kukosekana kwa jibu, aliona hana chaguo ila kumhoji meneja huyo.

Guardiola amekuwa akiwaunga mkono mabosi wake hadharani, hata wakati, mnamo 2020, City ilipewa marufuku ya miaka miwili ya kushiriki mashindano ya Uropa na Uefa kwa madai ya ukiukaji wa FFP, adhabu ambayo hatimaye ilibatilishwa na Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS).

Miaka miwili baadaye, Guardiola alisema angeondoka City ikiwa angehisi uongozi wa klabu hiyo umewahi kumdanganya. "Wanaeleza na ninawaamini," alisema.

"Baadhi wanaamini kuwa utetezi wake kwa wamiliki wa City haukuwa sahihi, lakini ni vigumu kufikiri kwamba wafanyakazi wengi wangefanya kazi tofauti kama wangewekwa katika nafasi sawa," anasema Jotischky.

Mnamo 2023, baada ya klabu yake kushtakiwa na Ligi ya Premia, Guardiola aliwashutumu wapinzani wa City kwa kuhukumu mapema kesi hiyo.

"Wazo langu la kwanza ni kwamba tayari tunahukumiwa," alisema. "Ni sawa na Uefa, tayari tulikuwa tumehukumiwa. Klabu ilithibitisha kuwa hatukuwa na hatia kabisa."

Pia aliitaka Ligi Kuu kuharakisha kushughulikia kesi hiyo, akitaka hukumu itolewe "leo mchana" au "kesho".

Kitendo cha City kushutumiwa kwa kushindwa kutoa ushirikiano katika uchunguzi wa ligi hakikuonekana kumtatiza.

Ilionekana kuwa Guardiola pia alisema: "Mwishowe, najua kwa hakika kwamba tulichoshinda tulishinda uwanjani. Hatuna shaka yoyote."

Mnamo 2024, baada ya kusaini nyongeza ya kandarasi ya miaka miwili, aliapa kusalia City, hata kama wangeshushwa daraja kama adhabu. "Watu wanasema 'nini kitatokea ikiwa tutashuka daraja?' Nitakuwa hapa," alidai.