Kila mtu anataka kupungua uzito, lakini mafuta kidogo sana mwilini yana hatari zake

.
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Mafuta, kwa kiasi fulani, yametumika kupotosha kwa miaka mingi.

Utamaduni wa lishe unatuambia tunapaswa kuyaondoa; baadhi ya makampuni ya chakula hutuuzia bidhaa zenye mafuta kidogo, na majukwaa ya kuinua uzito yanashiriki ushauri wa jinsi ya kupunguza asilimia ya mafuta mwilini.

Kuangalia kwa haraka mitandao ya kijamii ndiko kunakohitajika ili kupata vidokezo vya jinsi ya "kupata mwili uliojaa misuli." Aina hii ya mwili wenye misuli ina sifa kubwa.

Mwaka huu, wataalamu wana wasiwasi kuhusu kuibuka tena kwa mwelekeo wa kuwa mwembamba sana, unaoendeshwa katika baadhi ya matukio na umaarufu wa dawa za kupunguza uzito.

Hata hivyo, ingawa mafuta mengi husababisha matatizo ya kiafya na yanaweza kusababisha unene kupita kiasi, kuwa na mafuta kidogo sana si jambo zuri kwetu pia.

Kama wataalamu wengi walivyoeleza, lengo la kuondoa mafuta mwilini mwetu linaweza kuwa na madhara, iwe ni kwa mtazamo wa kibiolojia au wa kijamii.

"Tunapaswa kuyapenda mafuta yetu," ananiambia Elif Oral, daktari bingwa wa mfumo wa homoni (endocrinologist) na profesa wa tiba katika Chuo Kikuu cha Michigan. "Yanatimiza jukumu muhimu sana la kibiolojia."

Basi, tunahitaji kiasi gani cha mafuta hasa? Na kwa nini kuwa na kiwango kidogo sana cha mafuta mwilini ni hatari kwetu?

.

Kwa nini mafuta ya mwili ni muhimu?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kwa ujumla, kuna aina mbili tofauti za mafuta: mafuta yanayotokana na chakula na mafuta ya mwili.

Mafuta ya chakula ni yale tunayopata kupitia ulaji, huku mafuta ya mwili yakiwa ni njia ya asili ya kuhifadhi nishati ambayo hatuihitaji kwa wakati huo.

Tunapokula, mafuta, wanga, na protini vilivyomo kwenye chakula huvunjwa na kuwa viambato rahisi zaidi ambavyo mwili unaweza kuvitumia kama chanzo cha nishati.

Wanga hubadilishwa kuwa glukosi, protini kuwa asidi za amino, na mafuta kuwa asidi za mafuta.

Ikiwa mara kwa mara tutakula kalori nyingi kuliko tunazotumia, seli za mafuta zinazojulikana kama adipocytes huhifadhi virutubisho hivyo vya ziada katika mfumo wa lipidi. Hali hii husababisha seli za mafuta kuongezeka ukubwa.

Hata hivyo, leo tunajua kuwa mafuta ya mwili mbali na kuwa eneo rahisi tu la kuhifadhia vitu ni kiungo kinachofanya kazi kikamilifu na kina jukumu la kudhibiti shughuli mbalimbali za mwili.

Kama ilivyo katika hadithi ya Goldilocks na Dubu Watatu, jambo la msingi ni kupata uwiano sahihi: kuwa na mafuta mengi mno au machache mno mwilini kunaweza kuathiri afya vibaya.

.

Tunahitaji kiasi gani cha mafuta mwilini?

Ni vigumu kwa kushangaza kupima asilimia ya mafuta mwilini mwako, ingawa tutalizungumzia hili zaidi baadaye. Zaidi ya hayo, hakuna kiwango cha asilimia kilichowekwa kimataifa ambacho kila mtu anapaswa kukifikia; mahitaji hutofautiana kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine.

Hata hivyo, kama mwongozo wa jumla, wanaume watu wazima wenye afya njema kwa kawaida huwa na kati ya asilimia 10 na 20 ya mafuta mwilini. Kwa wanawake watu wazima wenye afya njema, asilimia hiyo kwa kawaida huwa kati ya 20 na 29. Watu wenye tatizo la unene uliopitiliza (obesity) huwa na asilimia ya mafuta mwilini inayozidi 30.

Kuhusu kiasi kinachofaa zaidi, Ryden anasema, "ni vigumu sana kubainisha kiwango kamili. Kinaweza kutofautiana kulingana na watu, jinsia, na makundi ya kijamii au asili."

Miongoni mwa wanariadha, kiasi cha kawaida cha mafuta mwilini huwa cha chini zaidi.

.

Jinsi ya kupima mafuta mwilini

Kuna njia kadhaa za kupima kiasi cha mafuta mwilini.

Vipimo vya kina zaidi hupatikana kwa kutumia mashine za skani ya mwili mzima aina ya DEXA, ambazo zinaweza kutofautisha kati ya mafuta ya mwili, misuli, na mifupa. Hata hivyo, njia hii inahitaji vifaa maalum na inaweza kuwa na gharama kubwa.

Njia moja maarufu ya kufanyia vipimo nyumbani ni kupima unene wa mikunjo ya ngozi. Hii huhusisha kupima unene wa tabaka la mafuta lililo chini ya ngozi kwa kubana eneo hilo kwa kutumia kifaa maalum cha kupimia (calipers).

Hata hivyo, kifaa hiki kinaweza kupima unene wa mikunjo ya mafuta katika sehemu fulani tu za mwili. Mafuta ya ndani (visceral fat) hayawezi kupimwa moja kwa moja kwa njia hii.

Lakini vipimo vya mikunjo ya ngozi si sahihi sana na vinaweza kutoa takwimu zinazoonyesha viwango vya chini kuliko uhalisia.

Chaguo jingine la kufanya hivi nyumbani ni kutumia mizani ya kidijitali ya kisasa (smart scale). Mizani hizi hufanya kazi kwa kupitisha mkondo wa umeme wenye nguvu ndogo mwilini ili kukadiria kiasi cha mafuta.

Hata hivyo, matokeo ya vipimo hivi huathiriwa na kiasi cha maji mwilini, hivyo hayachukuliwi kuwa sahihi kwa kupima viwango vya mafuta. Pia, haziwezi kuonyesha mahali ambapo mafuta yamehifadhiwa au kutofautisha kati ya mafuta ya ndani na aina nyingine za mafuta.