Jinsi FIFA inavyovuna mabilioni ya dola katika kila Kombe la Dunia

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Richard Sheehan
- Nafasi, The Conversation
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 9
Katika Kombe la Dunia, mfungaji bora hutunukiwa tuzo ya Kiatu cha Dhahabu, huku kipa bora akipokea tuzo ya Glovu za Dhahabu.
Hata hivyo, mashindano hayo pia yamekuwa chanzo kikubwa cha mapato kwa FIFA, ambayo huingiza mabilioni ya dola kupitia mauzo ya tiketi na shughuli nyingine za kibiashara.
Kwa Kombe la Dunia la 2026, bei za tiketi zimepanda kwa kiwango kikubwa kiasi kwamba hata Rais wa Marekani Donald Trump amesema hatanunua tiketi hizo licha ya kuwa mshirika wa karibu wa Rais wa FIFA, Gianni Infantino.
Hatua hiyo imezua hofu kuwa mashabiki wengi wa kawaida huenda wakazuiwa kushuhudia michuano hiyo kutokana na gharama kubwa.
Katika Kombe la Dunia la 2022 nchini Qatar, tiketi za daraja la kwanza kwa mechi za hatua ya makundi ziligharimu takriban dola 220 za Marekani, huku wakazi wa Qatar wakipata baadhi ya tiketi kwa dola 11 pekee.
Kwa fainali, tiketi za daraja la kwanza ziligharimu karibu dola 1,600.
Kuanzia 2026, FIFA imeanzisha mfumo wa bei zinazobadilika kulingana na mahitaji ya soko. Mfumo huo unamaanisha kuwa bei za tiketi zinaweza kubadilika muda wowote kulingana na kiwango cha mahitaji.
Tiketi za daraja la kwanza ambazo zilianza kuuzwa kwa karibu dola 600 mwaka 2025 sasa zinauzwa kwa zaidi ya dola 1,000 katika mechi nyingi.
Kwa mechi ya ufunguzi mjini Mexico City, tiketi za daraja la kwanza zimevuka dola 2,500, huku hata tiketi za daraja la chini zaidi zikigharimu zaidi ya dola 1,000.
Kwa upande wa fainali, tiketi za daraja la kwanza zilianza kwa zaidi ya dola 6,000 lakini kufikia Mei zilikuwa zimepanda hadi zaidi ya dola 32,000.
FIFA yakaribia kuvunja rekodi ya mapato

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa mujibu wa profesa mstaafu wa masuala ya fedha na mwandishi wa kitabu Keeping Score: The Economics of Big Time Sports, amefanya makadirio yanayoonyesha kuwa ongezeko la mapato yatokanayo na mauzo ya tiketi linaweza kuifanya FIFA kuvuka kiwango cha dola bilioni 15 katika Kombe la Dunia la 2026. Hilo lingekuwa rekodi mpya kwa shirikisho hilo la soka duniani na kiwango kikubwa zaidi kuliko lengo lake la awali la dola bilioni 11.
Mkakati wa FIFA wa kutumia mfumo wa bei zinazobadilika unaweza kuwa njia ya kurejesha sehemu ya mapato ambayo kwa kawaida huwanufaisha wauzaji wa tiketi katika soko la pili. Hata hivyo, hatua hiyo huenda isikubalike kwa mashabiki wengi wanaotarajia kununua tiketi.
Aidha, bado haijulikani wazi jinsi FIFA itakavyotumia mabilioni ya dola ya ziada yatakayopatikana.
Hii ni kwa sababu dhamira yake ya kutumia soka kuleta mabadiliko chanya katika jamii imekuwa ikitiliwa shaka kutokana na historia ya tuhuma za rushwa, ufisadi na ukosefu wa uwazi katika uendeshaji wake.
FIFA hufanyaje kazi?
Ni muhimu kuangalia bei za tiketi katika muktadha mpana wa hali ya kifedha ya FIFA na malengo yake ya jumla.
FIFA ni taasisi isiyo ya kibiashara iliyosajiliwa nchini Uswizi kama shirika la hisani.
Dhamira yake si kuandaa mashindano kama Kombe la Dunia pekee, bali pia kuendeleza mchezo wa soka na kuongeza upatikanaji wake katika maeneo mbalimbali duniani.
FIFA huendesha shughuli zake kwa mzunguko wa bajeti wa miaka minne, ambapo sehemu kubwa ya mapato yake hupatikana katika mwaka wa mwisho wa mzunguko huo, wakati Kombe la Dunia linapofanyika.
Mlinganisho wa kihistoria unaonyesha jinsi mapato hayo yalivyokua kwa miaka.
Kombe la Dunia la mwaka 1994 nchini Marekani, ambalo wengi huliona kuwa mojawapo ya mashindano yaliyofanikiwa zaidi, lilizalisha faida halisi ya dola milioni 700 kutokana na bajeti ya dola milioni 550. Mafanikio hayo yalichangiwa kwa kiasi kikubwa na mauzo ya tiketi na mikataba ya udhamini iliyovuka matarajio.
Viwanja vikubwa na mahudhurio makubwa ya mashabiki pia vilisaidia kufanikisha malengo ya maendeleo ya FIFA, ikiwemo kuzinduliwa kwa Major League Soccer nchini Marekani.
Kufikia mwaka 2022, mapato ya FIFA yalikuwa yameongezeka kwa kiwango kikubwa.
Mapato ya kipindi cha miaka minne kilichojumuisha Kombe la Dunia la 2022 yalitarajiwa kufikia dola bilioni 6.44, lakini hatimaye yalifikia dola bilioni 7.57. Sehemu kubwa ya ongezeko hilo ilitokana na haki za matangazo na shughuli za masoko.
Ingawa makadirio ya mapato ya tiketi yalionekana kuwa ya kawaida kutokana na ukubwa mdogo wa viwanja nchini Qatar, mapato halisi yalivuka matarajio kwa kiasi kikubwa, jambo linaloaminika kusababishwa na makadirio ya tahadhari yaliyowekwa na FIFA.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa upande wa matumizi, gharama ziliendana kwa karibu na bajeti iliyopangwa, huku dola bilioni 2.8 zikitengwa kwa programu za maendeleo katika kipindi cha 2019 hadi 2022.
Licha ya matumizi hayo, akiba ya FIFA iliongezeka kutoka dola bilioni 2.81 hadi dola bilioni 3.89 kutokana na mafanikio ya Kombe la Dunia la 2022.
Ikielekea Kombe la Dunia la 2026, FIFA ilikadiria kuwa mapato yake yangeongezeka kwa dola bilioni 4.36 ikilinganishwa na kipindi cha 2019 hadi 2022 na kufikia dola bilioni 11.
Ongezeko hilo lilitarajiwa kuchangiwa hasa na mauzo ya tiketi, ambayo yalikadiriwa kuongezeka kwa dola bilioni 2.59, pamoja na haki za matangazo ambazo zilitarajiwa kuongezeka kwa dola milioni 890.
Wakati huo huo, gharama zilitarajiwa kuongezeka kwa dola bilioni 4.57, hali ambayo ingeacha ziada ya takribani dola milioni 100, sawa na kiwango kidogo cha ziada kilichorekodiwa katika mzunguko uliotangulia.
Hata hivyo, mwaka 2024 FIFA ilirekebisha makadirio yake na kuongeza matarajio ya mapato kwa kipindi cha 2023 hadi 2026 kutoka dola bilioni 11 hadi dola bilioni 13.
Jinsi FIFA inavyoathiri mahitaji ya tiketi
Historia ya FIFA inaonyesha mwenendo unaojirudia mara kwa mara: makadirio ya mapato yaliyowekwa kwa tahadhari, udhibiti mkali wa matumizi, na ongezeko la mapato linalozidi matarajio kupitia mauzo ya tiketi na leseni za kibiashara.
Matokeo yake huwa ni mapato makubwa zaidi kuliko yaliyotarajiwa pamoja na kuongezeka kwa akiba ya shirika hilo.
Kwa mujibu wa makadirio yangu, mapato yatokanayo na haki za matangazo na shughuli za masoko mwaka huu yanaelekea kufikia viwango vilivyowekwa kwenye bajeti. Aidha, kwa kuzingatia historia ya FIFA, matumizi yake halisi kwa kawaida huendana kwa karibu na makadirio ya bajeti.
Hata hivyo, mauzo ya tiketi yanasalia kuwa chanzo kikuu cha mapato na wakati huo huo chanzo kikubwa cha mjadala.
Upanuzi wa Kombe la Dunia la 2026 unamaanisha kuongezeka kwa idadi ya timu, mechi na mashabiki, hali ambayo imeongeza kwa kiasi kikubwa mahitaji ya tiketi.
Licha ya kutumia viwanja vikubwa zaidi kuliko vilivyotumika katika Kombe lolote la Dunia tangu mwaka 1994, mahitaji ya tiketi yamezidi kwa mbali idadi ya nafasi zilizopo.
Zaidi ya maombi milioni 500 ya tiketi yaliwasilishwa kupitia mfumo wa bahati nasibu, huku nafasi zilizokuwepo zikiwa takribani milioni 7.1 pekee.
Tofauti hiyo kubwa kati ya mahitaji na upatikanaji imeipa FIFA uwezo mkubwa wa kupanga bei za tiketi.
Katika juhudi za kupunguza ukosoaji, FIFA ilianzisha tiketi maalumu za mashabiki zenye thamani ya dola 60 za Marekani, ambazo zilisambazwa kupitia vyama vya soka vya kitaifa.
Hata hivyo, tiketi hizo zinawakilisha sehemu ndogo sana ya tiketi zote zilizotolewa, zikiwa chini ya tiketi 600 kwa kila mechi. Kutokana na idadi hiyo kuwa ndogo, hatua hiyo haijatosha kupunguza malalamiko ya mashabiki kuhusu gharama kubwa za tiketi.

Chanzo cha picha, EPA
Tiketi nyingi ziliuzwa kwa awamu kupitia mfumo wa bei zinazobadilika kulingana na mahitaji ya soko, ambapo bei ziliongezeka kwa kiasi kikubwa kadri awamu zilivyoendelea. Sehemu kubwa ya mauzo ilifanyika katika awamu za mwisho, wakati bei zilikuwa juu zaidi.
Mipango ya upangaji wa viti viwanjani pia inaonyesha kuwa tiketi nyingi ziliwekwa katika madaraja ya juu zaidi ya bei.
Wakati huo huo, FIFA itanufaika pia na mapato yatokanayo na mauzo ya tiketi katika soko la kuuza upya, ambalo linasimamiwa na shirika lenyewe.
Mambo hayo matatu yanatarajiwa kuongeza mapato ya tiketi kwa kiwango kikubwa zaidi kuliko makadirio ya bajeti ya FIFA.
Kwa kuzingatia mwenendo huo, ninakadiria kuwa mapato yatokanayo na mauzo ya tiketi na huduma za wageni maalumu yatafikia angalau dola bilioni 7.44, zaidi ya mara mbili ya kiwango kilichowekwa kwenye bajeti ya FIFA. Makadirio hayo yanazingatia uwezo wa viwanja, bei za tiketi katika awamu mbalimbali za mauzo, mgawanyo wa viti kwa madaraja tofauti na shughuli zinazoendelea za kuuza upya tiketi.
Katika Kombe la Dunia la 2022, mapato ya wastani ya tiketi na huduma za wageni maalumu yalikuwa dola milioni 14.5 kwa kila mechi.
Kwa upande wa Kombe la Dunia la 2026, bajeti ya FIFA ya dola bilioni 3.1 inaashiria wastani wa mapato ya takribani dola milioni 30 kwa kila mechi kutokana na tiketi na huduma hizo.
Hata hivyo, kwa kuzingatia ukubwa wa viwanja vya mwaka 2026 na ongezeko kubwa la bei za tiketi, makadirio hayo yanaonekana kuwa ya chini kuliko kiwango halisi kinachoweza kupatikana.
Kwa msingi huo, haitashangaza ikiwa mapato ya mwisho yatokanayo na tiketi na huduma za wageni maalumu yatakaribia dola bilioni 9.
Kwa jumla, ninatabiri kuwa mapato yote ya FIFA katika Kombe la Dunia la 2026 yatafikia kati ya dola bilioni 14 na dola bilioni 19.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mabilioni hayo yanaenda wapi?
Mashabiki wa soka, iwe kwa kununua tiketi au kufuatilia mechi kupitia vyombo vya habari, ndio chanzo kikuu cha mapato ya FIFA.
Kwa upande wake, FIFA inasema fedha hizo hutumika kuandaa Kombe la Dunia kwa kiwango cha juu, kuendeleza mchezo wa soka na kuongeza upatikanaji wake katika maeneo mbalimbali duniani.
Hata hivyo, kadiri mapato yanavyoendelea kuongezeka, swali linaibuka kuhusu sababu za FIFA kuendelea kukusanya akiba inayozidi dola bilioni 4, kiwango ambacho ni zaidi ya nusu ya matumizi yake yote katika kipindi cha 2019 hadi 2022.
Kwa hakika, takwimu zinaonyesha kuwa shirika hilo limepunguza kwa uwiano sehemu ya fedha zilizokuwa zikielekezwa kwenye baadhi ya vipaumbele vyake vya msingi.
Katika kipindi cha 2023 hadi 2026, bajeti ya mashindano iliongezeka kutoka dola bilioni 2.45 hadi dola bilioni 5.62, sawa na ongezeko la takribani asilimia 130.
Kwa upande mwingine, bajeti ya maendeleo ya soka iliongezeka kwa asilimia 44 pekee, huku sehemu yake katika mapato yaliyopangwa ikishuka kutoka asilimia 44 hadi asilimia 36.
FIFA inaweza kutetea msimamo wake kwa kusema kuwa ongezeko la mapato ni muhimu ili kugharamia mashindano yajayo na kufadhili maendeleo ya soka duniani. Hata hivyo, maelezo yaliyomo katika bajeti yake ya kipindi cha 2027 hadi 2030 yanaonyesha kuwa hilo si jambo pekee linaloeleza mwelekeo wa matumizi ya fedha za shirika hilo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Hata hivyo, ongezeko kubwa la mapato limeibua maswali kuhusu namna fedha hizo zinavyotumika.
Takwimu zinaonyesha kuwa bajeti ya mashindano imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 130 katika miaka ya karibuni, wakati fedha zinazotengwa kwa maendeleo ya soka zimeongezeka kwa kiwango kidogo zaidi.
Wakosoaji pia wanaeleza kuwa historia ya FIFA imewahi kugubikwa na tuhuma za rushwa, ufisadi na ukosefu wa uwazi katika matumizi ya fedha.
Ingawa FIFA imeanzisha programu mbalimbali za maendeleo, ikiwemo FIFA Foundation, wachambuzi wengi wanaamini swali muhimu zaidi si kiasi cha fedha kinachoingizwa, bali ni kama fedha hizo zinatumika ipasavyo kufikia malengo ya kuendeleza soka na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
FIFA imekuwa ikieleza dhamira yake kwa kauli kama "kuendeleza mchezo, kuufikisha duniani kote na kujenga mustakabali bora."
Hata hivyo, kwa mtazamo wa mwandishi wa makala haya, bajeti zake zinaonyesha kuwa kipaumbele chake kikuu kwa sasa ni kuendesha mashindano makubwa na kuongeza mapato kuliko katika kupanua uwekezaji wa moja kwa moja katika maendeleo ya mchezo duniani.
Ukubwa wa mapato ya FIFA
Tukipiga hesabu kwa haraka kwa kukitumia makadirio ya mapato ya FIFA ya dola bilioni 14 na bajeti za sasa za klabu kubwa za Tanzania
Yanga hutumia takribani shilingi bilioni 33.7 kwa msimu. Nayo Simba hutumia takribani shilingi bilioni 29.6 kwa msimu.
Kwa wastani, klabu kubwa Tanzania hutumia karibu shilingi bilioni 30 kwa mwaka.
Dola bilioni 14 ni zaidi ya shilingi trilioni 36 za Tanzania (kwa makadirio ya kawaida ya ubadilishaji fedha).
Hivyo shilingi trilioni 36 kwa kuigawanya dhidi ya shilingi bilioni 14 inakupa miaka 1,200.
Kama mapato ya Kombe la Dunia yanaweza kuendesha Simba au Yanga kwa zaidi ya miaka 1,000, swali si ukubwa wa fedha za FIFA bali ni kiasi gani cha fedha hizo kinachorejea kusaidia maendeleo ya kandanda barani Afrika.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid












