Onyo la uhaba wa chakula kutokana na shambulizi la mji wa Odesa Ukraine
Katika picha zilizochapishwa mtandaoni na jeshi la Ukraine, wazima moto wanaonekana wakikanyaga vifusi vya kile kilichokuwa kituo cha biashara na ghala la chakula
Moja kwa moja
Tembo wa Zimbabwe waua watu 60 mwaka huu- maafisa

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Tembo hao wanatembea katika makundi mengi, kulingana na Nick Mangwana Tembo wa Zimbabwe wameua watu 60 kufikia sasa mwaka huu, kulingana na msemaji wa serikali. Akiandika kwenye Twitter, Nick Mangwana, alisema ni mada ya kusikitisha.
"Suala la Migogoro ya Binadamu/Wanyamapori limekuwa la kusisimua sana. Mwaka huu pekee Wazimbabwe 60 wamepoteza maisha kutokana na tembo na 50 kujeruhiwa. Mwaka 2021, 72 walipoteza maisha.
Zimbabwe itafanya Mkutano wa Tembo mwezi huu." Katika wilaya moja, Bubi, tembo "wamekula kila kitu mashambani na sasa wanahamia makazi," aliandika.
Pia aliongeza kuwa wanaingia kwenye migogoro na binadamu, na kusababisha tembo waliojeruhiwa ambao wanakuwa "wakali na wasioweza kudhibitiwa".
Inakadiriwa kuwa kuna tembo 100,000 nchini Zimbabwe, na idadi hiyo inaongezeka. Mtaalamu mmoja wa wanyamapori, T
inashe Farawo, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba huenda hali ikawa mbaya zaidi.
"Tishio huenda likaongezeka tunapoelekea msimu wa kiangazi wakati mifugo itakuwa ikienda kutafuta maji na chakula," AFP inamnukuu akisema.
Ruka X ujumbeRuhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya njeMkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe
Watu 14 wafariki,wakiwemo watoto, katika shambulio la DR Congo

Chanzo cha picha, AFP
Watu 14 wamefariki, wakiwemo watoto, katika shambulio lililotokea katika jimbo la Ituri mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Tukio hilo lililotokea Jumatatu karibu na mji wa Fataki lilikuwa kwenye kambi ya watu waliopoteza makazi yao.
Washukiwa wa wanamgambo kutoka kundi la Codeco wamelaumiwa na vyanzo vya ndani. Pia walilaumiwa kwa shambulio kwenye mgodi wa dhahabu huko Djugu katika jimbo hilo hilo siku ya Jumapili, ambalo lilisababisha vifo vya makumi ya watu.

Mfanyikazi wa zamani wa Meta nchini Kenya awasilisha kesi mahakamani

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Meta inasema inahitaji washirika kutoa mishahara na marupurupu mazuri Nchini Kenya mfanyakazi wa zamani wa kampuni mama ya Facebook, Meta, amewasilisha kesi mahakamani akidai kuwa mazingira duni ya kazi yanakiuka katiba ya nchi.
Ombi la Daniel Motaung linasema wafanyakazi wa ndani, ambao husimamia machapisho ya Facebook, wanapata malipo yasiyo ya kawaida na kupokea usaidizi duni wa afya ya akili baada ya kutazama maudhui yanayoathiri mawazo.
Bw Motuang anasema kazi hiyo ya kudhibiti imemsababishia msongo wa mawazo unaotokana na kiwewe.
Alifukuzwa kazi baada ya kujaribu kuwashawishi makumi ya wenzake kuunda muungano wa kutetea maslahi yao.
Kesi hiyo inataka fidia ya fedha na ukaguzi huru wa haki za binadamu katika ofisi ya Bw Motaung.
Pia inataka mahakama iamuru kwamba haki za muungano zilindwe.
Msemaji wa Meta alisema ilihitaji washirika wake kutoa malipo, faida na usaidizi unaoongoza katika tasnia.
Kampuni Sama,inayotoa huduma za nje, hapo awali ilikanusha madai ya kuwadhulumu wafanyikazi wake.
Serikali ya Tanzania imetoa ruzuku ya bilioni 100 kwenye mafuta ili kupunguza bei ya bidhaa hiyo

Chanzo cha picha, Bunge
Serikali ya Tanzania imetoa ruzuku ya bilioni 100 kwenye mafuta ili kupunguza bei ya bidhaa hiyo kuanzia June 1, 2022.
Akiongea Bungeni wakati wa kutoa mkakati wa kukabiliana na kupanda kwa bei ya mafuta, Waziri wa Nishati January Makamba anasema "Ruzuku hii (Shilingi Bilioni 100) inatolewa kwa kupunguza matumizi ya Serikali katika kipindi kilichobaki cha mwaka 2021/22.
Anaongeza kuwa Kutolewa kwa ruzuku hii hakutagusa miradi ya maendeleo ambayo inaendelea. Hatua hii imekuja baada ya Bunge la Tanzania wiki iliyopita kumpa Waziri huyo muda wa siku tano kuhakikisha anakuja na mkakati wa kupunguza bei ya mafuta ili kupunguza mzigo kwa wananchi.
Mbali na hatua hiyo Waziri huyo pia ameelezea mipango mingine ya kukabiliana na kupanda kwa bei ya mafuta ikiwemo kuruhusu watu wenye uwezo wa kuleta mafuta kufanya hivyo na kuwa na hifadhi ya mafuta ya kimakakati ambayo itawezesha kupata unafuu wa mafuta na mpango wa Ushirikiano wa kujenga maghala makubwa ya mafuta kwa ajili ya kuuza nje ya nchi.
Bei za mafuta zinaweza kupungua zaidi kuanzia Agasti 2022.
- Mzozo Ukraine: Je dunia inategemea vipi mafuta na gesi ya Urusi?
- Mzozo wa Ukraine: Kwa kiasi gani dunia inategemea mafuta na gesi ya Urusi?
Makombora yashambulia kituo cha biashara Odesa

Chanzo cha picha, Reuters
Makombora yaliyotumiwa yanaweza kuwa ya enzi za Usoviet lakini uharibifu uliofanyika bado ni mkubwa.
Katika picha zilizochapishwa mtandaoni na jeshi la Ukraine, wazima moto wanaonekana wakikanyaga vifusi vya kile kilichokuwa kituo cha biashara na ghala.
Moshi mnene na mweusi ulisambaa katika mji huo wa bandari lakini kwasababu ya amri ya kutotoka nje mitaa ilikuwa tupu wakati makombora yalipopigwa usiku.
Mamlaka inasema mtu mmoja alifariki na wengine watano kupelekwa hospitalini.
Mashambulizi hayo yalitokea Jumatatu jioni, siku hiyo hiyo ambayo rais wa Baraza la Ulaya alikuwa katika mji huo.
Charles Michel alisema ameona maghala yaliyojaa nafaka, ngano na mahindi huko Odesa ambayo yalikuwa tayari kusafirishwa nje ya nchi lakini yamezuiwa.
Tishio la usalama wa chakula duniani ni jambo lililosisitizwa na Rais Zelensky wa Ukraine katika hotuba yake ya usiku.
Alisema kuwa bila Ukraine kusafirisha nje, nchi kadhaa ...walikuwa "tayari wana uhaba wa chakula" na kwamba hali inaweza "kuwa, kusema ukweli, ya kutisha".
Unaweza pia kusoma
KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
Kim Jong Un ampongeza rais Putin kwa Siku ya Ushindi

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Korea Kaskazini iliunga mkono hadharani uvamizi wa Moscow nchini Ukraine Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un ametuma salamu za pongezi kwa Rais Vladimir Putin baada ya kusherehekea Siku Ushindi ya Urusi, akielezea "mshikamano thabiti" wa nchi yake na Moscow, shirika la habari la Korea Kaskazini KCNA limeripoti.
Katika barua yake iliyotumwa tarehe 9 Mei, Kim anasema "Mshikamano madhubuti wa muda mrefu kwa sababu ya watu wa Urusi kung'oa vitisho vya kisiasa na kijeshi na usaliti wa vikosi vya adui".
Kiongozi wa Korea Kaskazini pia ameelezea imani yake kwamba uhusiano wa kimkakati na wa jadi wa urafiki kati ya nchi hizo mbili utakuwa kwa kasi".
Hivi karibuni Korea Kaskazini imeangazia uhusiano wake wa karibu na Urusi, na kuunga mkono hadharani Moscow juu ya uvamizi wake nchini Ukraine.
Mwezi Februari, ililaumu mzozo wa Ukraine juu ya "sera ya kivita" ya Marekani na Magharibi.
Mbwa atunukiwa tuzo ya heshima ya rais kwa kugundua mabomu Ukraine

Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa Ukraine Vladimir Zelensky amemtunukia tuzo ya heshima ya Rais mbwa aliyepewa jina Pattern kwa huduma zake tangu uvamivi wa Urusi.
Mbwa huyo mwenye umri wa miaka miwili na nusu amekuwa shujaa wa kitaifa nchini Ukraine, ishara ya upinzani wa Ukraine dhidi ya Urusi. Mbali na kubaini marundo zaidi ya 200 ya nyaya zinazohusishwa na vipulizi, mwezi April alitajwa kugundua mabomu zaidi ya 90.
Rais Zelensky alisema: "Ninataka kuwatunuku mashujaa hawa wa Kiukreni ambao tayari wanasafisha ardhi yetu."Rais Zelensky alisema katika hafla ya Jumapili huko Kyiv kwamba mbwa huyo sio tu anasaidia kubaini vilipuzi, lakini pia hufundisha watoto wetu kanuni muhimu za usalama katika maeneo ambayo kuna hatari.Sherehe ya tuzo hiyo pia ilihudhuriwa pia na Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau, ambaye aliwasili Ukraine siku ya Jumapili. Justin Trudeau alitangaza kwamba Canada itatoa silaha zaidi na vifaa kwa Ukraine.Rais Zelensky alikabidhi medali kwa mbwa huyo na mmiliki wake My Hello Ilyo. Mbwa huyo mdogo kiumbo amekuwa maarfu nchini chini ya kitengo cha usalama tangu uvamizi wa Urusi,
Rais wa zamani wa Nigeria Goodluck Jonathan kuwania tena urais

Chanzo cha picha, AFP
Rais wa zamani wa Nigeria Goodluck Jonathan amejitosa tena kuwania kurejea madarakani katika uchaguzi wa mwaka ujao baada ya kuhama chama cha siasa, BBC inaelewa. Bw Jonathan amejiunga na chama tawala cha All Progressives Congress (APC) ambacho kilimshinda mwaka 2015 baada ya kukaa madarakani kwa miaka mitano.
Kundi la wafuasi lilinunua fomu ya uteuzi kwa niaba yake siku ya Jumatatu, na kuendeleza mtindo wa wanaotaka kutumia washirika kununua fomu hiyo. Uamuzi wake wa kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho cha kuwania urais akiwa na chama cha APC umewashangaza sana Wanigeria wengi, hasa wale wa chama chake cha zamani, People’s Democratic Party (PDP).
Kwa muda wa miezi kadhaa, uvumi ulikuwa umezagaa kuhusu kujithusisha kwake kwa siri katika chama tawala lakini si Bw Jonathan wala washirika wake walikuwa wametoa maoni yao.
Haijabainika kwa nini Bw Jonathan aliamua kubadili vyama, lakini kumekuwa na fununu kwamba amekuwa hana furaha kufuatia kushindwa kwake kwenye uchaguzi wa 2015, ambapo inasemekana alihisi kusalitiwa na washirika wakuu ndani ya chama.
Anastahiki muhula mmoja zaidi iwapo atashinda katika uchaguzi wa mwaka ujao jambo ambalo linaweza kumaanisha mamlaka kurejea katika eneo la kaskazini mwa Nigeria katika mpangilio ambao haujaandikwa, wenye utata ambao unabadilisha mamlaka kati ya kaskazini na kusini.
Bw Jonathan anatoka kusini mwa Nigeria. Yeyote atakayepata uteuzi wa APC kwa uchaguzi atatarajia ushindani mkali kutoka kwa PDP. Wagombea wake kama vile Peter Obi, Makamu wa Rais wa zamani Atiku Abubakar na gavana wa jimbo la Rivers Nyesom Wike ni maarufu sana, haswa kusini mwa Nigeria.
Askari Magereza aliyemsaidia 'mpenzi' wake mtuhumiwa kutoroka jela ajiua

Chanzo cha picha, Lauderdale
Askari magereza wa kike ambaye alitoroka na mshukiwa wa mauaji kutoka jela ya Alabama, Marekani amefariki dunia baada ya kujipiga risasi wawili hao wakikamatwa, polisi wanasema.
Vicky White, 58, alifariki hospitalini baada ya yeye na Casey White (hawana uhusiano wa kindugu), 38, kukamatwa huko Indiana kufuatia msako wa polisi.
Wawili hao walikuwa walitoroka katika gereza la Kaunti ya Lauderdale tarehe 29 Aprili. Inaaminika kuwa walikuwa wapenzi. Kulingana na maafisa, walionekana mara ya mwisho alipokuwa akimsafirisha kwa kisingizo cha uongo cha matatizo ya afya ya akili.
Ilikuwa siku ya mwisho ya Bi White kazini kabla ya kustaafu. Alikuwa ameuza nyumba yake hivi majuzi na akawaambia wenzake kwamba alipanga kutumia wakati mwingi ufukweni.
Ofisi ya Wachunguzi wa Kaunti ya Vanderburgh ilithibitisha kwamba Vicky White alifariki katika hospitali ya eneo hilo baada ya kujipiga risasi wakati wa kukamatwa. Taarifa zaidi kuhusu kifo chake zinatarajiwa kutolewa leo Jumanne kufuatia uchunguzi wa maiti yake.
Sherifu wa Kaunti ya Lauderdale Rick Singleton alisema hapo awali kwamba gari la wapenzi hao hao lilipinduka wakiwa kwenye harakati za kutoroka baada ya msako wa polisi huko Evansville, Indiana, ambapo Casey White alijisalimisha. "Tumemkamata mtu hatari mtaani leo. Hataona mwanga wa jua tena," alisema.
Casey White alikuwa anatumikia miaka 75 jela kwa makosa mengine mbalimbali ikiwemo ya wizi aliyoyafanya mwaka 2015.
Hujambo, karibu katika taarifa zetu za moja kwa moja leo 10.05.2022
