Kiongozi wa upinzani wa Zambia ahojiwa na polisi - ripoti
Shirika la utangazaji la Zambia ZNBC linaripoti kuwa kiongozi wa upinzani wa nchini hiyo, Brian Mundubile, ambaye alikuwa amejificha baada ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais wa hivi karibuni, amekabidhiwa kwa polisi.
Matokeo rasmi ya uchaguzi wa tarehe 13 Agosti yalionyesha kuwa Rais aliyeko madarakani, Hakainde Hichilema, alishinda kwa kupata asilimia 60 ya kura dhidi ya asilimia 38 alizopata Mundubile.
Siku moja baada ya uchaguzi, vikosi vya usalama vilivamia eneo moja jijini Lusaka lililohusishwa na Mundubile, na kusababisha kifo cha waziri wa zamani wa serikali na kuwakamata wanasiasa wengine kadhaa.
Mamlaka ziliishutumu upinzani kwa kupanga uasi wa kutumia silaha, madai ambayo upinzani uliyakataa. Kufuatia uvamizi huo, Mundubile alihamia "eneo salama chini ya ulinzi wa shirika la kimataifa la haki za binadamu kutokana na vitisho dhidi yake," chama chake cha NRPUP kilisema.
ZNBC inaripoti kuwa kiongozi huyo wa upinzani, pamoja na mgombea mwenza wake Makebi Zulu, walikuwa wakilindwa na Umoja wa Mataifa jijini Lusaka.
Shirika hilo linaongeza kuwa wawili hao sasa wanahojiwa na "maafisa wa vyombo vya dola" mbele ya mawakili wao kufuatia wito wa kuitwa kwa ajili ya mahojiano kuhusu "madai ya vitendo ambavyo polisi wanasema vina uwezo wa kutishia usalama wa taifa".
Upinzani haukuweza kuwasilisha kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi mahakamani kwa sababu mahakama zilikuwa zimefungwa na mamlaka siku ya Jumatatu, ambayo ilikuwa siku ya mwisho ya kuweza kufungua kesi hiyo.